kunguni wa ulaya
JF-Expert Member
- Mar 16, 2014
- 4,131
- 6,109
===================================================
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga amesema ni vigumu Serikali ya Tanzania, kusimamia masuala ya Watanzania wanaofukuzwa nchini Msumbiji, kwa kuwa haifahamu kati ya hao yupi ni Mtanzania na yupi si Mtanzania kwa kuwa hawana nyaraka zozote.
Akizungumza na gazeti hili jana ofisini kwake, Balozi Mahiga alisema Serikali inasita kuchukua hatua, kwa kuwa hata Serikali ya Msumbiji haijawaambia kwamba chukueni watu wenu.
Alisema kitendo cha kuingilia ni kama watu hao walikuwa ni wakimbizi, wakati watu hao walienda Msumbiji kwa hiyari yao na wametakiwa kuondoka kwa hiyari yao.
Alisema hadi sasa Serikali haifahamu kati ya hao waliofukuzwa, nani ana nyaraka za kusafiria za Tanzania na nani hana.
Pia haijulikani ni nani Mtanzania na yupi sio Mtanzania. Kwa hali hiyo, alisisitiza kuwa hao wanaosema ni Watanzania lazima wahakikiwe, kama kweli ni wenzetu maana wengi wao hawana nyaraka zozote. “Hatuna taarifa za uhakika raia wa Tanzania ni wangapi hadi sasa,” alisema balozi Mahiga.
Aliongeza kuwa maamuzi ya Serikali ya Msumbiji, hayagusi tu Watanzania, yanagusa watu wote waliokuwepo katika mji wa Monte Puez wakiwa wanajihusisha na uchimbaji wa madini.
Alisema wametimuliwa kutokana na Serikali ya kule, inataka kutengeneza utaratibu wa kuhakikisha Serikali inapata mapato kutoka maeneo ambako hao wanaofukuzwa, walikuwa wanachimba.
Alisema baadhi ya watu ambao wameamriwa kuondoka nchini humo, walikuwa wanajihusisha na biashara ya uchimbaji madini kinyume cha utaratibu.
Alisema Serikali ya Msumbiji imeshindwa kutafuta utaratibu wa kukusanya kodi na sasa inataka kupanga mipango ya kiuchumi ili ifaidishe wananchi wake, ambao ndio wanapewa kipaumbele.
Alisema wageni walioko huko walitakiwa kufuata utaratibu wa uhamiaji wa kupata kibali cha kufanya kazi nchini humo.
Waziri aliongeza kuwa ni jukumu la Serikali, kudhibiti wahamiaji haramu kama ambavyo Tanzania imekuwa inafanya mara kwa mara kuwarejesha makwao wahamiaji ambao hawana vibali vya kuishi nchini. Alisema Tanzania imewarudisha kwao raia wa nchi jirani kutokana na kuishi nchini kwa muda mrefu huku hawana vibali na ilifikia baadhi yao wakawa wanashindana katika ajira na wananchi wetu.
“Na sisi tumefanya jambo kama hili, hivyo wanachofanya Msumbiji sio jambo la ajabu, kwani hata nchi nyingine zimekuwa zinafanya,” alisema Mahiga.
Akanusha ubakaji, unyang’anyi Kuhusu madai ya Watanzania hao kubakwa na kuibiwa mali zao, balozi Mahiga alisema walipeleka ofisa wa ubalozi kutoka Maputo kwenda katika eneo hilo kuangalia hali halisi.
Alisema ofisi huyo alikanusha kuwepo kwa vitendo vya kuwabaka au kuwanyang’anya watu mali zao, kama inavyodaiwa.
Alisema katika operesheni hiyo inaongozwa na vyombo vya usalama vya Msumbiji, yawezekana kuna mapungufu ambayo yanaweza kuwa yamefanywa na ofisa mmoja au baadhi, lakini alisisitiza kuwa sio sahihi kutangaza kuwa jambo hilo, linatekelezwa kwa amri ya serikali ya Msumbuji.
Balozi Mahiga alisema yawezekana kutokana na machungu ya watu hao kuondolewa kwa nguvu wakaamua kuzusha kufanyiwa vitendo vya namna hiyo. Lakini waziri huyo alisisitiza kuwa Serikali ya Msumbiji imethibitisha kwamba hakuna vitendo vya namna hiyo ambavyo vimefanywa.
Waziri huyo alisisitiza kuwa watu ambao wameamriwa na Serikali ya Msumbiji waondoke wafanye hivyo.
“Huwezi kuendelea kukaa katika nchi ya watu wakati mmeshaambiwa kwamba hamtakiwi, hivyo watafute utaratibu wa kuondoka katika eneo hilo.”
Alisema licha ya Serikali ya Tanzania kutokuwa na taarifa ya namna watu hao walivyofika huko, lakini kupitia viongozi wa mkoa wa Mtwara wamefanya juhudi za kuzungumza na Serikali ya jimbo la Cabo Delgado ili watu wanaoondolewa wapewe muda wa kukusanya vitu vyao na kupanga safari.
Alisema katika mazungumzo yaliyofanyika, Tanzania imeiomba Msumbiji kuhakikisha inawalinda Watanzania hao na mali zao wajipange namna ya kuondoka nchini humo.
“Tunataka wale ambao wana mali kama wanaweza kuuza wauze na waweze kuondoka kwa usalama.”
Alisema vyombo vya ulinzi vya Msumbiji viendelee kuwalinda na kama kuna vitendo vya uhalifu, serikali ya Msumbiji ichuke hatua dhidi ya wahusika.
Alisema Serikali ya Msumbiji imeonesha ushirikiano katika kuwapa usalama Watanzania walioko huko na wamekubali kuongezewa muda ili watu waweze kuondoka kwa hiyari.
Alisema hakuna haja ya serikali ya Tanzania na Msumbiji kusimamia, kwani suala hilo limesimamiwa na mikoa.
Alisema idara ya uhamiaji iwe makini kuwahakiki watu wote wanaoingia kutoka Msumbiji. Alisema katika eneo hilo kulikuwa na watu kutoka nchi mbalimbali, ambao wanaweza kutumia mwanya huo kuingia nchini.
Wakati Balozi Mahiga akieleza hayo, juzi taarifa ya Polisi Mkoa wa Mtwara ilieleza kuwa idadi ya Watanzania wanaorejea nyumbani kutoka Msumbiji, imeongezeka hadi kufikia 2,420 na mmoja wao aliyetajwa kwa jina la Jackline Greyson, alifariki dunia muda mfupi baada ya kufika mkoani humo.
Wiki moja iliyopita katika mitandao ya kijamii taarifa zilienea kuwa Watanzania wanakamatwa ovyo, wanadhalilishwa kwa kubakwa na hawapewi nafasi ya kuchukua chochote na hata nyaraka zinazothibitisha wapo kihalali, walinyang’anywa.
Chanzo; Habarileo