Mahakama ya Kangaroo imeshamuhukumu Abdul Nondo

Mahakama ya Kangaroo imeshamuhukumu Abdul Nondo

justin mwanshinga

Senior Member
Joined
May 22, 2014
Posts
179
Reaction score
621
MAHAKAMA YA KANGAROO IMESHAMHUKUMU ABDUL NONDO

Mahakama ya Kangaroo (Kangaroo Court) ni msamiati wenye maana ya mabaraza ya uamuzi au mikutano yenye kutoa hukumu kwenye mashauri mbalimbali, pasipo kuheshimu misingi ya sheria na haki. Kwamba watu wanakaa kikao na kutoa hukumu kwa mtu au watu bila kutimiza viwango vya kisheria katika utoaji haki.

Msamiati huo pia hubeba tafsiri ya uwepo wa mahakama halali kisheria yenye mamlaka kwenye nchi, lakini hakimu au jaji kwa makusudi kabisa anaamua kuendesha kesi nje ya sheria za mahakama na wajibu wa maadili ya mahakama. Mahakama ya Kangaroo pia huonekana kupitia hukumu zenye kukandamiza haki kwa makusudi.

Kauli kali zenye kuhukumu kabla ya kufika mahakamani ambazo hutamkwa na watawala au amri za kisiasa zenye kutolewa na viongozi wa nchi ni miongoni mwa masuala yenye kusababisha uwepo wa Mahakama ya Kangaroo. Matamshi yenye kumtia mtu hatiani kwanza kisha vyombo vya sheria ndiyo vianze kuchukua hatua, ni kipimo chenye kuthibitisha uwepo wa Mahakama ya Kangaroo.

Mfano wa Mahakama ya Kangaroo ni kama Baraza la Mapinduzi ya Watu wa Cambodia, lililoketi Agosti 19, 1979 na kumhukumu kifungo cha maisha jela aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Pol Pot na ndugu yake, Leng San. Umoja wa Mataifa ulikataa hukumu hiyo kwa sababu baraza husika halikutimiza vigezo vya kimahakama.

Msingi wa mahakama ni ule mchakato kabla ya hukumu. Ukweli wa pande mbili unasikilizwa kwa uhuru usio na vipengele. Ushahidi unatolewa na shahidi anavumiliwa kipindi akieleza kile alichonacho kuhusiana na shauri husika. Mawakili wanaachiwa uga mpana wa kuhoji ili kurahisisha haki ionekane. Mwisho jaji au hakimu anahukumu baada ya vipimo vya kisheria.

Mchakato wa mahakama umewekwa kwenye nchi ili kulinda haki za watu dhidi ya haki za kisheria. Kwamba mtu hata aonekane mkosefu kiasi gani kwenye macho ya wengine, hususan watawala, hahukumiwi kwa matakwa ya watu, bali anapimwa dhidi ya haki za kisheria. Huo ndiyo utaratibu wa nchi kama ulivyowekewa mwongozo na Katiba ya nchi.

Kwa kurejea tafsiri ya Mahakama ya Kangaroo ni kuwa maoni yoyote yenye kuhukumu watu wengine ni kosa, maana ni uthibitisho wa uwepo Mahakama ya Kangaroo. Na kwa vile kwenye mitandao ya kijamii kumekuwa na maoni mengi yenye kuhukumu wengine, ni wazi kuwa mitandaoni kuna mahakimu na majaji wengi siku hizi.

Viongozi wengi wa kisiasa wamekuwa wakitoa amri na matamshi yenye kuhukumu. Huo ni uthibitisho kwamba Mahakama ya Kangaroo inapatikana sana kwenye majukwaa ya kisiasa. Inapaswa kufahamika kwamba Mahakama ya Kangaroo ni kielelezo cha nchi kuwa na watu wasioheshimu haki za kisheria ambazo zimewekwa mahsusi ili kulinda haki za watu.

Kadhalika ni kipimo kuwa watu wengi hupenda watendewe haki lakini wao wenyewe hawaheshimu haki za wengine. Vilevile viongozi ni wepesi kusisitiza kuchukuliwa kwa hatua za kisheria lakini katika nafasi zao hawaziheshimu. Mahakama za Kangaroo hazipaswi kuwepo. Kila mtu ni vizuri akajisikia kutendewa haki mbele ya sheria za nchi.

KUHUSU ABDUL NONDO

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdul Nondo ambaye ni mwenyekiti wa Mtandao wa Haki za Wanafunzi Tanzania (TSNP), alidaiwa kutoweka usiku wa Machi 6, mwaka huu, kabla ya kupatikana jioni Machi 7. Inaelezwa kuwa Nondo alipokuwa kwenye mazingira aliyohisi ni yenye hatari, alituma ujumbe kwa rafiki yake.

Nondo anadaiwa kutuma ujumbe wa simu kwa Kiingereza wenye kutafsirika kwa Kiswahili "Nipo katikati ya hatari". Baada ya hapo hakupatikana tena. Jioni ya Machi 7, Nondo alipatikana au alijikuta yupo Mufindi, Iringa. Mtu aliyetoa taarifa za Nondo kupatikana Mufindi, alidai alimkuta akiwa hajielewi alipo, ndipo alimsaidia pesa ya kukodi taksi aende Kituo cha Polisi Wilaya ya Mufindi kuripoti apate msaada zaidi.

Habari za awali ni kwamba Nondo alikuwa Dar es Salaam. Ujumbe kwamba alikuwa kwenye hatari, aliutuma akiwa Dar es Salaam. Siku iliyofuata ndipo alijikuta Mufindi. Taarifa za kupotea Nondo zilisababisha mwamko mkubwa wa kuhoji hasa kwenye mitandao ya kijamii. Nondo alipatwa na madhila hayo kipindi akiwa ameahidi kuongoza wanafunzi kuandamana kushinikiza Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ajiuzulu.

Nondo alisema, wangeandamana kwa sababu ya kuwepo kwa matukio mengi ya uvunjifu wa haki za binadamu. Watu wengi wakikutwa wameuawa nchini na kukosekana majibu ya kina kuhusiana na vifo hivyo. Zaidi ni tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 16, mwaka huu, wakati polisi walipotumia risasi za moto kuzuia maandamano ya viongozi na wafuasi wa Chadema, waliokuwa wanakwenda ofisi za msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kinondoni, kushinikiza mawakala wao wapewa hati za viapo na barua za utambulisho kwa ajili ya uchaguzi mdogo Kinondoni, uliofanyika Februari 17, mwaka huu.

Akwilina alikuwa kwenye daladala wakati alipokumbwa na masahibu hayo ya kupigwa risasi. Hakuwa kabisa katika sehemu ya maandamano. Vilevile kuna wengine walikuwa kwenye maandamano na walipigwa risasi, lakini wakawekwa mahabusu bila kutibiwa wala kupewa dhamana. Kwa matukio hayo, Nondo aliona ni wakati mwafaka Mwigulu kung'oka Wizara ya Mambo ya Ndani.

Sasa basi, baada ya Nondo kuwa amepatikana na kwenda Kituo cha Polisi Mufindi, taarifa ya awali kabisa ya Kamanda wa Polisi Iringa, Juma Bwire, ilieleza watamshughulikia kama taarifa alizotoa zilikuwa uongo. Kwa hisia za Kamanda Bwire ni kwamba huwenda Nondo alitoa taarifa za kutekwa ili kuhamasisha wanafunzi wenzake kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.

Izingatiwe kuwa Nondo ndiye mlalamikaji. Aliripoti polisi ili kueleza yaliyomsibu kuanzia kutekwa Dar es Salaam mpaka kujikuta Mufindi. Polisi wanaopaswa kudhughulikia tukio hilo, kabla hata ya kufanya uchunguzi, wanaanza kwanza kutoa vitisho: "Tukimbaini anatoa taarifa za uongo ili kuhamasisha wanafunzi wavinje amani tutamshughulikia kama wahalifu wengine."

Ukiisoma kauli ya Kamanda Bwire, unaona kuwa polisi wanamtuhumu Nondo kwa nafasi ya kwanza kwamba 'alijiteka' kwa nia ovu, halafu wanazichukua tuhuma zake za kutekwa kwa nafasi ya pili. Mpaka hapo inatia shaka ikiwa kweli Nondo alitekwa, kama utafanyika uchunguzi makini, wakati wachunguzi wenyewe wanamtuhumu anayetakiwa kusaidiwa kiuchunguzi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar wa Salaam, Paul Makonda, yeye aliagiza polisi Iringa wakishamalizana na Nondo, wampeleke Dar es Salaam wamshughulikie kwa sababu hawezi kuuchafua 'mkoa wake' halafu aachwe. Hakuna namna nyingine ya kuitafsiri kauli hiyo zaidi ya kuusema ukweli kwamba Nondo ameshahukumiwa kuwa hakutekwa.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Lazaro Mambosasa ambaye ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, alisema Nondo hakutoa taarifa polisi, ila alikamatwa na polisi akiwa Mufindi, alipokuwa katikati ya shughuli zake. Mambosasa akasema Nondo hakutekwa, kwani Mufindi alikwenda kwa ajili ya kumfuata mpenzi wake.

Mambosasa akasema, uthibitisho kuwa Nondo hakutekwa ni kuwa hakuwahi kutoa taarifa popote. Wakati huohuo, taarifa ya RPC Bwire wa Iringa inakiri Nondo aliripoti polisi. Hapohapo kuna msamaria mwema aliyesema alimpa nauli Nondo ya kukodi taksi ili akaripoti polisi Mufindi, Iringa. Polisi maneno mengi yenye kukichanganya. Mambosasa yeye ameshamhukumu Nondo.

Katika mitandao ya kijamii hali ndiyo mbaya kabisa. Watoa maoni wengi wanamtuhumu Nondo kuwa alisafiri kwa basi mwenyewe kwenda Mufindi, kwa hiyo alitangaza kuwa ametekwa ili kusababisha taharuki kwa nchi, vilevile kujitafutia umaarufu kwa njia za kihalifu. Tayari Nondo ameshahukumiwa mitandaoni.

HAKI INITWA BATILI

Viongozi na watumia mitandao ya kijamii wanatakiwa kuheshimu haki za kisheria. Waache kujigeuza Mahakama za Kangaroo. Hukumu kwa watenda makosa haitolewi mitandaoni, kwenye majukwaa ya viongozi wa kisiasa wala kwa matamko ya makamanda wa polisi. Misimamo ya kisiasa isiwe sababu ya kuwazodoa au kuwapuuza wenye kustahili haki.

Inatakiwa kwanza Nondo asikilizwe. Alichokisema kifanyiwe uchunguzi. Ikiwa maelezo yake yatakosa nguvu ya kiupelelezi, ndipo tuhuma zihame, kutoka kutuhumu kutekwa hadi yeye kutuhumiwa kujipoteza kwa nia ovu. Siyo kumshambulia na kuanza kutoa ahadi za kumshughulikia.

tafakari kama Nondo kweli alitekwa. Maumivu aliyonayo kutokana na tukio hilo. Wakati akitegemea polisi na viongozi wa nchi wamsikilize, wamtendee haki na ikibidi waliomfanyia uhalifu wakamatwe, anajikuta akituhumiwa kutaka kusababisha taharuki kwa nchi kwa kutangaza alitekwa wakati haikuwa hivyo.

Wengine wanasema si kweli kwamba Nondo alitekwa, maana asingeachiwa nafasi ya kutuma ujumbe wa simu kwa rafiki yake. Wanasema kama alitekwa mbona hakuguswa hata kidogo? Watu hao wanajipa uchambuzi wa watu kutekwa. Utafikiri ipo kanuni kwamba kila mwenye kutekwa lazima anyang'anywe simu na apigwe mpaka aumizwe.

Aliyesema Nondo anauchafua mkoa wa Dar es Salaam kwa kutangaza alitekwa, maswali kwake ni je, anayechafua ni anayeteka au anayetekwa? Kwa nini watu wawe wakali kwa aliyetangaza kutekwa kuliko kusaidia kuwapata watekaji? Je, imesahaulika kuwa mwanamuziki Ibrahim Mshana 'Roma Mkatoliki' alitekwa wapi?

Roma akiwa na wenzake watatu, walitekwa Oysterbay, Dar es Salaam kwenye studio ya muziki ya Tongwe Records na walishikiliwa kwa siku tatu kabla kuachiwa na kujikuta wapo Ununio, Dar. Kada wa Chadema, Ben Saanane, alitoweka Dar es Salaam tangu Novemba 2016 na mpaka leo hajaonekana. Simu ya Ben inaonesha ilizimwa Mburahati, Dar.

Wapo watu walituhumu kuwa Ben alijipoteza mwenyewe kutafuta umaarufu. Miaka inapita, hali ni kimya, Ben haonekani. Hata Roma na wenzake pamoja na kutokeza wakiwa wamejeruhiwa, bado walisemwa walijiumiza makusudi ili kuhalalisha kwamba walitekwa. Leo Nondo anaulizwa eti mbona hakuumia hata kidogo. Mahakama za Kangaroo ni hatari sana.

Ndimi Luqman MALOTO
 
Back
Top Bottom