Magufuli aibua maswali

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
RAIS John Magufuli wiki hii anatimiza siku 100 akiwa madarakani; akijitambulisha kama mtu anayejali watu wa hali ya chini, mchukia rushwa na ufisadi, jasiri huku wapinzani wake wakidai kwamba bado hajaonyesha dira hasa ya aina ya mageuzi anayotaka kuyafanya.

Katika kipindi hicho cha siku 100 tu, Serikali ya Magufuli imetambulisha msamiati mpya katika lugha ya Kiswahili; “Kutumbua Majipu” ukimaanisha vitendo vya kupambana na rushwa, utendaji mbovu serikalini na matendo mengine yasiyoendana na maadili.

Magufuli aliyeapishwa kuwa Rais Novemba 6 mwaka jana, alichukua nafasi ya mtangulizi wake, Jakaya Kikwete, baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana –unaoelezwa kuwa mgumu zaidi katika historia ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini.

Na ingawa siku 100 zinazotumika kupima utendaji wa serikali yoyote duniani ni chache, Magufuli tayari ameonyesha kwamba serikali yake itakuwa tofauti na ile ya mtangulizi wake; na pengine watangulizi wake wote wengine kutokana na aina yake ya uongozi.

Hajaogopa Urais

Magufuli ni Rais ambaye hakutarajiwa na wengi kuchukua nafasi hiyo. Hadi kufikia mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wa mwaka jana, hakuna mtu aliyedhani kwamba anaweza kuwania nafasi hiyo; achilia mbali kupita na kushinda.

Ndiyo maana, aliposhinda, wengi walitaraji kuwa pengine angetulia kidogo na kusoma mazingira kabla ya kuanza kuchukua uamuzi mgumu wa baadhi ya masuala – mara kwa mara. Hata hivyo, Magufuli ameonyesha kwamba urais haujampa kifungo chochote na ametekeleza majukumu yake – kwa kunukuu maneno ya mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam “Utadhani alikuwa rais aliyekuwa likizo na kurejea ofisini kuendelea na shughul zake. Hakuna ugeni kabisa”.

Katika wiki zake za kwanza madarakani, Magufuli alitembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari (TPA) na kutoa maagizo na maelekezo yaliyogusa baadhi ya watu ambao miongoni mwao walihusishwa na CCM au vigogo ndani ya serikali na chama tawala.

Hajasafiri nje

Mtangulizi wa Magufuli, Kikwete, alikuwa akilaumiwa kwa kupenda safari za nje ya nchi. Wakati wa hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge na hata wakati wa kampeni za kuomba kuchaguliwa na Watanzania kuwa rais wao, Magufuli alieleza namna anavyokerwa na viongozi wanaosafiri kwenda nje ya nchi na kuacha majukumu yao ya hapa nchini.

Katika mojawapo ya kauli zake za kukumbukwa, Magufuli alizungumza bungeni kuwa wako viongozi hapa nchini ambao wanasafiri nchi za nje mara nyingi kuliko muda wanaotumia kuwatembelea wazazi wao.

Katika siku zake 100 za kwanza madarakani, Magufuli hajasafiri nje ya nchi hata mara moja. Kulikuwa na mikutano mikubwa miwili ambayo kwa kawaida Rais wa Tanzania angehudhuria lakini yeye hakwenda.

Mikutano hiyo ni ule wa baina ya viongozi wa Afrika na China uliofanyika nchini Afrika Kusini na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika Ethiopia ambayo yote aliwakilishwana Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Serikali yake imebana safari zisizo za lazima za viongozi na yeye mwenyewe ameonyesha mifano. Kuna mifano ya watumishi wa serikali waliozuiwa katika viwanja vya ndege hapa nchini wakati wakiwa katika harakati za kuondoka nchini bila kibali cha serikali.

Kipenzi cha tabaka la chini

Kwenye siku 100 za kwanza, Magufuli amewakuna wananchi. Hii ni kutokana na kauli zake, hatua ambazo amechukua dhidi ya watu walioonekana kuwa hawagusiki na pia tabia yake ya kusimama kuzungumza na wananchi kila anapopata nafasi.

Kwa wananchi wa kawaida, hawaelewi inakuwaje mtu ambaye kakamatwa na pembe za ndovu, asifungwe kwa sababu ushahidi haujakamalika na hiyo ndiyo lugha ambayo Rais Magufuli amekuwa akiitumia wakati anazungumza na wananchi.

Katika mikutano yake na wananchi anayoifanya wakati anaposimamishwa, Magufuli mara nyingi huwa anazungumzia masuala na kero zinazowakabili wananchi wa eneo husika na mara nyingi huwa ni kero ambazo zinawagusa wananchi wa maeneo mengi.

“ Huyu ndiye Rais tuliyekuwa tukimtaka. Siyo rais anakuja kuzungumza na wananchi na kuzungumza mambo yasiyowahusu. Kama watu shida yenu ni maji yeye atazungumzia maji. Kama mna shida ya mifugo au barabara, yeye atazungumzia. Ndiyo maana wananchi wanapenda,” alisema Rashid Saria ambaye alikuwa mmoja wa wananchi wa Arusha waliomsimamisha Magufuli azungumze nao wakati akiwa njiani kwenda Monduli kwenye mahafali ya Chuo cha Kijeshi.

Kuongeza mapato

Wakati Magufuli akichukua wadhifa wa urais, serikali ilikuwa ikikusanya kiasi cha kati ya shilingi bilioni 850 hadi bilioni 900 kwa mwezi. Tangu aingie madarakani, wastani wa ukusanyaji mapato umeongezeka na kuwa shilingi bilioni 1,200 (trilioni 1.2).

Kiwango hicho tayari ni rekodi katika historia ya ukusanyaji mapato hapa nchini na sifa hiyo ni kubwa kwa sababu amefanikisha hilo katika kipindi cha siku 100 tu tangu aingie madarakani.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamishina Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, kuna uwezekano wa kiwango hicho kuongezeka kwa kadri mianya ya ukwepaji kodi itakavyozidi kuzibwa, viwanda na mashirika yasiyofanya kazi kuanza kuzalisha na mikakati mipya ya ukusanyaji kodi kupitishwa.

Rais wa mitandao ya kijamii

Katika historia ya Tanzania, hakuna Rais ambaye amekumbana na nguvu ya mitandao ya kijamii kuliko Magufuli. Pengine yeye ndiye rais ambaye ameanza kufuatiliwa na mitandao hiyo kuanzia katika siku yake ya kwanza hadi atakapomaliza.

Mara alipoanza tu urais wake, mitandao ya kijamii iliibua picha zake za video zikimuonyesha akizungumza na marafiki zake na kudai kuwa yeye hawezi kuwa Rais wa Tanzania kwa sababu watu watamchukia kwa hatua atakazochukua.

Wakati alipovaa magwanda ya kijeshi akiwa njiani kuelekea Monduli, picha za Magufuli zilianza kuenea kupitia mitandao ya kijamii muda uleule wa tukio na kuzua mijadala mbalimbali ya kijamii. Kwa bahati nzuri, hadi sasa, hakuna tukio lolote baya lililotokea katika siku zake 100 za urais ambalo mitandao ililidaka mapema.

Kwa kifupi, taarifa ya Magufuli ambayo zamani ingechukua siku nzima kuwafikia wananchi au kuwafanya wasubiri hadi usiku kusikiliza taarifa ya habari, sasa kinasambaa katika muda uleule na kwa kasi ambayo watangulizi wake, ukiondoa Kikwete katika Awamu yake ya Pili ya Uongozi, hawakuwahi kukutana nayo.

Raia Mwema
 
Back
Top Bottom