Magonjwa yakujitakia yamaliza watu nchini

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
MAGONJWA yasiyo ya kuambukizwa, ambayo wanasayansi wameyaweka kwenye kundi la magonjwa kujitakia kwa binadamu, yamebainika kuwa ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo vingi katika nchi zinazoendela, ikiwemo.Tanzania.

Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam, jana kwenye mkutano wa nne wa kimataifa kuhusu magonjwa ambayo hayaambukizwi, ulioandaliwa na Chama cha Wanafunzi Wanasayansi Tanzania (Tamsa).

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa kwenye mkutano huo na Dk Rufaro Chatora ilieleza kwamba uchunguzi uliofanywa mwaka 2005, umeonyesha kuwa vifo vinavyotokea kila mwaka duniani, asilimia 60 ya vifo vinasababishwa na magonjwa ya kujitakia.

“Inakadiriwa watu 58 milioni walikufa mwaka 2005 na kati yao 35 milioni, sawa na asilimia 60, walikufa kutokana na magonjwa sugu yasiyo ya kuambukizwa,” alisema Dk Chatora ambaye aliongoza ujumbe wa WHO kwenye mkutano huo.

Ofisa huyo wa WHO alisema miaka 20 iliyopita magonjwa ya kuambukiza yalikuwa yanaongoza kwa vifo.

Mtaalamu huyo alisema kwamba hali hiyo ni mbaya zaidi katika nchi masikini kusini wa nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania.

Miongoni mwa magonjwa hayo ambayo wanasayansi wanayaweka katika kundi la binadamu kujitakia, Dk Chatora aliyataja kuwa ni yale yanayotokana na matumizi ya tumbaku, pombe, kisukari, ukosefu wa mazoezi, kutokula vyakula bora na maradhi ya moyo.

Mkurugenzi wa Mafunzo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Gilbart Mliga alisema ingawa Tanzania ipo kwenye kundi la nchi zinazoathirika kwa magonjwa hayo, alisema hayatokani na umasikini wetu bali ni uzembe na kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu vyakula na mazingira.

“Mfano kuvuta sigara, hakuna asiyejua madhara yake. Angalia pia ukosefu wa kula mboga na matunda. Tanzania tuna mazingira mazuri ya kupata vitu hivyo vyote vikiwa freshi na kuhusu mazoezi, kila mtu ana fursa ya kufanya mazoezi. Hivyo tunaweza kusema ni suala tu la elimu,” alisema Dk Mliga.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wanafunzi wanaosomea sayansi kutoka vyuo vikuu mbalimbali Afrika, lengo likiwa ni kuweka nguvu ya pamoja katika kuzikomboa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara dhidi ya janga la magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Chanzo: Magonjwa yakujitakia yamaliza watu nchini
 
Back
Top Bottom