Mafisadi wameigeuza nchi yetu shamba la bibi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,794
287,947
Uongozi umeigeuza nchi yetu shamba la bibi

Joseph Mihangwa Julai 23, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

“DUNIA ni jukwaa (la michezo ya kuigiza) ambapo kila mmoja hucheza nafasi yake kwa zamu…” (William Shakespeare katika Mfanyabiashara wa Venice).

Utawala wa nchi ni jukwaa la mchezo wa kuigiza ambapo kila mtawala huingia na kutoka kwa zamu (kupokezana vijiti?) baada ya kuigiza sehemu yake; lakini nchi na watu ni wa kudumu .

Chini ya utawala mzuri au mbaya wanaonufaika au kuathirika ni nchi na wananchi. Ndiyo maana, kwa kutambua hili, Serikali na watawala wamewekewa mipaka ya kikatiba. Mfano, hapa kwetu, Katiba inatamka wazi kwamba, “… Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba” (ibara 8 (1) (a) ) ; na pia kwamba, “Serikali itawajibika kwa wananchi “ (Ibara 8 (1) (c)) .

Tanzania imeshuhudia wachezaji wanne jukwaani tangu uhuru, kila mmoja na staili na mbinu zake za kuigiza na kutumbuiza, kuanzia na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (1961-1985), aliyeingia na kaulimbiu ya “Uhuru”, kisha “Uhuru na Umoja”, “Uhuru na Kazi”, na hatimaye “Uhuru ni Kazi”, kila kaulimbiu ikiwakilisha agenda ya kipindi fulani katika miaka 24 ya utawala wake. Kwa Nyerere dira ya maendeleo ilikuwa ni “Ujamaa na Kujitegemea” .

Serikali ya awamu hii ya ilisisitiza uadilifu na uwajibikaji wa viongozi, usawa na uchumi kuwa mikononi mwa wananchi kwa mujibu wa “Azimio la Arusha” la 1967. Awamu hii iliweza kujenga umoja wa kitaifa imara na kuleta hali ya amani na utulivu inayodumu hadi leo, japo sasa kwa kusuasua. Kwa sababu hii Tanzania ilisifika na kuheshimika kimataifa.

Awamu ya pili, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi ilidumu kutoka 1985-1995. Yeye aliingia kwa staili ya pekee akijielewa udhaifu wake kwa kujilinganisha na “kichuguu mbele ya Mlima Kilimanjaro” (Nyerere), au “manowari ya kivita na mtumbwi”, na aliahidi kupambana na rushwa, ufisadi na ubadhirifu serikalini.

Kwa kuzingatia ahadi yake hiyo, wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam walimkabidhi “fagio la chuma” aweze kufagia uchafu huo, lakini hadi aking’atuka mwaka 1995, si rushwa, wala ufisadi wa aina yoyote alioweza kuufagia, badala yake uliongezeka kwa mwendo wa kuruka.

Awamu hiyo haikuwa na dira ya maendeleo wala kaulimbiu, badala yake wananchi walimtungia kauli mbiu ya utani kwa kumwita “Mzee Ruksa”. Ni chini ya awamu hii Azimio la Arusha lilifutwa kwa Azimio la Zanzibar (1992), na ubinafsisha wa uchumi wa nchi na mali za taifa usiojali ukatia fora, maadili ya taifa na uwajibikaji miongoni mwa viongozi ukatoweka na kwa kila kitu kuwa ni “ruksa” kwa nguvu ya mtu.

Kuna kipindi Mwalimu alikerwa na udhaifu huu na kulalamika kwamba “Ikulu imegeuzwa pango la wafanyabiashara na walanguzi”. Na kuhusu ubinafsishaji usiojali, Mwalimu alihofia na kuonya juu ya uwezekano wa kubinafsisha kila kitu ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kubinafsisha hata magereza.

Awamu ya pili itakumbukwa kama chimbuko na mwanzo wa kuweka uchumi wa taifa mikononi mwa wageni, kuibuka kwa matabaka ya kijamii na udini, kupanuka kwa ufa kati ya matajiri na masikini, kufa kwa moyo wa uzalendo na maadili ya taifa. Ni kipindi hiki Tanzania iligeuzwa “shamba la Bibi” kwa maana ya yote “ruksa” kupora atakacho bila ya hofu ya kuhojiwa au kuwajibishwa.

Serikali ya Awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin William Mkapa (1995-2005), iliahidi kuendesha mambo yake chini ya kaulimbiu ya “Uwazi na Ukweli”, na akaahidi kutokomeza ufisadi uliokithiri tangu awamu ya pili. Kuonyesha kwamba alikuwa mwanaume wa shoka, haraka haraka aliunda Tume ya kubainisha mianya ya rushwa na jinsi ya kutokomeza janga hilo nchini chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba ambayo ilifanya kazi nzuri na kukabidhi taarifa yake.

Na kama ilivyokuwa kwa Rais Mwinyi na “Fagio la Chuma”, hadi aking’atuka mwaka 2005, Mkapa hakuzungumza lolote tena juu ya ufisadi, wala kuifanyia kazi taarifa ya Tume hiyo.

Rais Mkapa alijiwekea utaratibu wa kulihutubia taifa kwa njia ya Redio kila mwisho wa mwezi, bila shaka kwa kutimiza matakwa ya ibara ya 18(2) ya Katiba kwamba, “Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi”. Utaratibu huu ulirithiwa na Serikali ya awamu ya nne ingawa sasa unaonekana kuachwa taratibu.

Ni utaratibu mzuri, lakini umma ulianza kuhoji aina ya taarifa zilizokuwa zikitolewa kwa wananchi, na mara nyingine viongozi hao wamejikuta kwamba umma unaelewa mengi ya muhimu kwa taifa kuliko walivyofikiri, na huenda ni kwa sababu hii utaratibu huu sasa unasuasua.

Awamu ya tatu imeondoka madarakani ikaacha ufisadi umeota mizizi bila ya ubavu wa kukemea. Ufisadi huo ni pamoja na ule uliogunduliwa hivi karibuni wa mamilioni ya fedha ya Benki Kuu (EPA), IPTL, TANESCO, Ununuzi wa ndege ya Rais, Kiwira Coal Mines, kashfa ya rada, mikataba mibovu ya madini, TICTS, uuzaji wa mali za umma kwa bei ya kutupa, kama vile hoteli Kilimanjaro, Hotel 77, Shirika la Simu – TTCL, Benki ya NBC na misamaha ya kodi.

Inasemekana NBC na mali zake lukuki iliuzwa kwa makaburu wa Afrika Kusini kwa Sh. 15bn tu, ambapo walilipa Sh. 12bn pekee ambazo hata hivyo inasemekana hazionekani katika vitabu vya serikali.

Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha pia kuwa jumla ya Sh. 7.3bn zilifujwa Wizara ya Ujenzi pekee mwaka 2002, ambapo mwaka 2004 Sh. 40bn zilitafunwa katika Wizara mbali mbali.

Kwa upande wa Serikali za Mitaa, jumla ya Sh. 31bn zililiwa mwaka 1997, Sh. 97bn mwaka 1999, ambapo mwaka 2000 Sh. 57bn zilitoweka kwa kutaja matukio machache tu. Waliojaribu kuhoji juu ya vitendo hivi walipata jibu la mwaka kwa kuitwa “wavivu wa kufikiri”, “wenye wivu”, “wapinzani’ na hata kuambiwa kwa umasikini wao “wale nyasi”.

Hata hivyo, awamu ya tatu itakumbukwa kwa kudhibiti na kusimamia vizuri misaada ya wahisani kutoka nje na kuweza kurejesha imani ya wafadhili hao kwa Serikali yetu. Fedha hizo zimeweza kutumika vizuri kwa maendeleo kama vile ujenzi wa shule, barabara na miundombinu mingine nchini.

Awamu ya nne ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, imeingia madarakani (2005) na kurithi gharika la matatizo na migogoro iliyoasisiwa na awamu mbili zilizotangulia. Kikwete, maarufu kama JK, kama alivyokuwa Rais John F. Kennedy wa Marekani (maarufu JFK), ni mwenye mvuto na mcheshi. Mke wa JK, Salma, kama alivyokuwa mke wa JFK, Jackie, ni maarufu (celebrity). Hawa wawili, JK na Salma, kama walivyokuwa JFK na Jackie, ni kama wacheza sinema wenye mvuto wa pekee.

Pamoja na mvuto na ucheshi wake, JK alionya toka mwanzo kwamba watu (hasa wasaidizi wake) wasidanganyike na tabasamu lake kwani ana “msimamo usioyumba kwenye masuala ya utawala na uongozi wa nchi”, na akasikika akisema, kama alivyozoea kusema JFK, “Usiulize nchi yako itafanya nini, uliza utafanya nini kuisaidia nchi yako”

Kwa mwanzo huo, wananchi wengi walianza kusema “Nyerere amefufuka”, na wakadiriki kumpa jina la “Tumaini Lililopotea”. Yeye aliingia kwa kauli mbiu ya “Ari mpya, Nguvu mpya, Kasi mpya”. JK amechukua madaraka katikati ya utamaduni uliojengeka wa kutowajibika, ufisadi, rushwa, usiri katika kuendesha serikali, uporaji wa rasilimali unaofanywa na wageni na demokrasia legelege.

Ameingia wakati jamii tayari ikiwa imegawanyika kitabaka, kati ya walala hoi na matajiri wachache ambao ndio wameendelea kushika hatamu za siasa (Chama) na uchumi wa nchi na kutishia umoja wa kitaifa, amani na utulivu.

Ni bahati mbaya kwamba (na hili hatuoni haya kulisema) idadi kubwa ya viongozi wetu wamechaguliwa kwa nguvu ya fedha (rushwa) si kwa lengo la kutumikia bali kwa lengo la kutumikiwa na kujinufaisha kisiasa na kiuchumi.

Katiba ya nchi (Ibara 9(c) ) inamtaka JK kuhakikisha kwamba “ Shughuli za Seriakli zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla, na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine”. Iko wapi “kasi mpya” ya kuzuia utajiri wa nchi yetu kuendelea kuporwa na “wawekezaji” matapeli, wakishirikiana na wazalendo (wengine viongozi) waliouasi umma na sera za nchi?

Mbona anafumbia macho ufisadi na mafisadi waliochokwa na umma kama vile anataka kuwaambia “Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa baba yenu ameona vema kuwapa ule (ulaji) ufalme”? Wananchi wanapenda kuona mijadala kuhusu IPTL, Richmond, EPA, Kiwira na kashfa zingine inafikia mwisho kwa hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya wahusika kwa “Nguvu na Kasi Mpya”.

Au tuelewe kwamba hachukui hatua dhidi yao kwa sababu “Ari” inakosekana; au kwamba “roho inatamani (kuchukua hatua),lakini mwili ni dhaifu”? Kwa nini? Uko wapi msimamo usioyumba wa mtu ambaye ni “Tumaini la Watanzania lilipotea”?

Tunadhani Rais bado angali anasumbuliwa na jinamizi la “mitandao” ya uchaguzi uliopita, linalomfunga mikono na miguu kutenda. Ni mtu mwema mno na mwepesi kulipa fadhila na mwenye kumwonea haya mtu aliyewahi kumwamini hata kama ataharibu.

Mfano ni Baraza kubwa la Mawaziri 63 alilounda kwanza kama kielelezo jinsi alivyokuwa njia panda nani amchukue na nani amuwache kati ya wanamtandao wake.

Tumejionea jinsi baadhi ya wateule wananvyoharibu kazi kisha kuwapa pole “kwa ajali ya siasa”, badala ya kuchukua hatua sawia. Haya yote yanafanya kauli yake ya “msimamo usio yumbika” ipoteze nguvu na ari ya kutenda.

Tena, ibara ya 9(d) inamtaka JK kuhakikisha kwamba “Maendeleo ya uchumi wa taifa yanakuzwa na kupangwa kwa ulinganifu na kwa pamoja”, na 9(c) kwamba, “ Matumizi ya utajiri wa taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umasikini, ujinga na maradhi”.

Tunauliza, iko wapi mipango ya pamoja wakati tumeshinikizwa na kukubali bila kuhoji sera za Benki ya Dunia (WB) na IMF, zinazoitaka Serikali kujiondoa katika kupanga na kusimamia uchumi wa nchi na kuacha nguvu ya soko ifanye kazi? Kama ni kupanga kwa pamoja ili kuondosha umasikini, Mtanzania gani mwenye uchungu wa nchi yake angekubali Kilimo kipangiwe asilimia sita tu (460bn/=) ya bajeti ya trilioni 7.216/= mwaka 2008/2009?

Kwamba, (Ibara 9(k) inamtaka kuhakikisha kwamba “Nchi inatawaliwa kwa kufuata misingi ya demokrasia na Ujamaa”. Uko wapi Ujamaa, wakati Azimio la Zanzibar (1992) lilikwishaua kila kitu? Nani asiyejua kwamba tunaimba ujamaa huku tukicheza kibepari? Tumekosa dira, kisiasa na kiuchumi. Na kwa nahodha asiyejua bandari aendayo, hakuna upepo ulio mwafaka kwake.

0713-526972

jmihangwa@yahoo.com
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom