Mafisadi sasa wateka vijana

sulphadoxine

JF-Expert Member
Nov 1, 2010
2,257
645
WATUHUMIWA wakuu wa ufisadi ndani ya Chama Cha Mapinduzi, sasa ni dhahiri wamefanikiwa kuuteka uongozi wa juu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) na kuutumia kufanikisha ajenda zao.

Hali hiyo inathibitishwa na baadhi ya matukio kadhaa yaliyojitokeza wakati wa mkutano wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu za chama hicho, wiki iliyopita mjini Dodoma.


Vijana hao baadhi wamekuwa wakiwachafua viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho kwa maelekezo ya watuhumiwa wa ufisadi ambao sasa watachukuliwa hatua na chama hicho kung'olewa baada ya kushindwa kuamua kufanya hivyo kwa utashi wao kama walivyoamuriwa.

Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, tayari kwa namna fulani amefichua siri iliyopo miongoni mwa vijana hao, akisema kuwa baadhi ya vijana katika chama hicho kupitia umoja wao, walifikishwa katika kamati ya maadili kutokana na kutukana baadhi ya viongozi wa kitaifa.


Mukama alieleza hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wake jumanne wiki hii, ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam.

"Kuna vijana tuliwaita kwenye kamati ya maadili. Unajua hawa vijana wameunda kamati yao ya kutafuta maoni ya kuboresha chombo chao lakini kuna baadhi ya mikutano yao wamefanya wakatukana viongozi, kwa hiyo walihojiwa," alisema Mukama.

Mbali na majibu hayo ya Mukama taarifa zaidi zinabainisha ya kuwa tayari kwa kiasi kikubwa watuhumiwa wa ufisadi wamekwishaiteka UVCCM na hasa sehemu kubwa ya viongozi wake wakuu.

Viongozi wanaodaiwa kutekeleza ajenda za kifisadi ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Benno Malisa, mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Hussein Bashe na baadhi wenyeviti wa umoja huo ngazi ya mikoa na wilaya.



Katika mkutano huo Mukama alisema hakuna aliyesafishwa katika vikao vya chama hicho mjini Dodoma, na kwamba baadhi ya vyombo vya habari vimepotosha kwamba vimesafisha watuhumiwa wa ufisadi, wakati kinachoendelea ni mchakato wa kuwachukulia hatua.

Mukama amesema kwa sasa Kamati ya Maadili na Usalama Taifa, imepewa nguvu zaidi na kuwa Tume ambayo itakuwa na uwezo wa kuwachukulia watu hatua moja kwa moja bila kusubiri vikao vya juu.


Akirejea maamuzi ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na hotuba ya Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete, Mukama alisema Kamati ya Maadili na Usalama itawaita watuhumiwa na kuwataka wajitetee kabla ya kufanya uamuzi.

Alisema kamati hiyo inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, ikiwa na wajumbe wengine wakiwamo wawili kutoka Zanzibar na wawili kutoka Bara na yeye akiwa mjumbe mpya aliyeingizwa katikia utaratibu mpya.

“Mhusika ataitwa na kuhojiwa, badala ya kumhoji kwenye NEC ambayo ina watu wengi ambao mtu asiye na kosa anaweza kuhukumiwa kwa hisia za kisiasa ama mhalifu anaweza kupona kwa hisia.


“Kuhusu maadili tumekubaliana kutokuwa na ajizi katika kupambana na rushwa, viongozi wajitafakari na kujiwabisha wenyewe, wasipofanya hivyo chama hakitasita kuchukua hatua. Katika kufanikisha hilo, tumemua kuiongezea nguvu kamati ya maadili na kuibadilisha na kuwa tume kamili yenye watu 14 kutoka 12 na kuipa mamlaka ya kuamua bila kusubiri vikao,” alisema Mukama.


Alisema mabadiliko hayo yanalenga katika ngazi zote pamoja na kuwa Tume ya Maadili na Usalama itakuwa moja tu kitaifa na katika ngazi ya mikoa na wilaya zitaendelea kuwa Kamati ya Maadili na Usalama ambazo nazo zitakuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi moja kwa moja.


Mukama alisema CCM haikukurupuka katika uamuzi wake wa kufanya mageuzi na kujisafisha, na kwamba kila jambo litafanyika kwa umakini wa hali ya juu, ikiwa ni pamoja na utafiti uliofanyika ndani na nje ya nchi.

Kwa muda mrefu UVCCM ilikuwa ikituhumiwa kutumiwa na watuhumiwa wakuu wa ufisadi lakini yaliyojitokeza Dodoma yamedhihirisha ukweli huo.


Baadhi ya wachunguzi wa mambo wamesema Kikwete ana kazi kubwa kama atataka kukivusha chama chake kutokana na kulemewa na nguvu ya mafisadi ambao pia wanaungwa mkono na baadhi ya wenyeviti wa CCM wa mikoa.

Wengi wanatabiri kwamba chelewa chelewa ya kuwachukulia hatua watuhumiwa wa ufisadi itakigharimu vibaya chama hicho, kwa kuzidi kukijengea makundi na kuupa upinzani nguvu.
 
Back
Top Bottom