SoC02 Maeneo makuu matano (5) ya kupata wazo la biashara

Stories of Change - 2022 Competition
Jun 27, 2020
6
3
i) Kupata wazo kutokana na taaluma yako; wazo la biashara linaweza kutokana na taaluma yako. Unaweza kuangalia fursa zilizopo katika taaluma yako kwa maana ya fani ambayo ulisomea au ile ambayo unaifanyia kazi na kuamua kujiajiri au kufungua biashara ambayo inaendana na taaluma yako.

Mara nyingi inakuwa rahisi kwa mtu wa taaluma fulani kufungua biashara ambayo inaendana moja kwa moja na taaluma yake. Hii inatokana na ukweli kwamba, kufungua biashara au kufanya kitu cha ziada kinachohusiana na taaluma yako ya msingi, inakuwa ni muendelezo wa kile ambacho unakifanya kila siku.

Kama umeajiriwa katika fani husika kujiajiri kupitia fani hiyo inakuwa ni sawa na kuongeza tu masaa ya ziada kazini, inakuwia rahisi kuzifanya kazi zake zote kwa wakati mmoja. Kwa mfano, ni rahisi kwa mwalimu kufungua kituo cha masomo ya ziada, kuliko mhasibu kufanya hivyo.

Wazo la biashara ambalo linatoka katika taaluma yako linakurahisishia katika usimamizi wa biashara husika kwani unakuwa unaielewa kwa undani.

Angalia taaluma yako, angalia fursa zilizopo na hitaji la soko, unaweza kupata wazo lako la biashara hapo. Lakini kama ni muajiriwa basi unafahamu watu wanaofanya kazi kama hizo, nirahisi kujifunza na ni rahisi kuielewa biashara ambayo umeisomea, si rahisi kudanganywa na wafanyabishara wenzako na hata wafanyakazi wako.

ii) Wazo linaweza kutoka katika kipaji chako; kipaji ni uwezo wa asili wa kufanya jambo fulani. Binafsi naamini kuwa kila mtu ana kipaji chake, kipaji ni kitu fulani ambacho ukikifanya unakifanya vizuri bila kuhitaji kufundishwa sana, lakini pia anafurahia wakati wa kukifanya kuliko watu wengine.

Unaweza kugundua kuwa unakipaji gani kwanza kwa kujichunguza wewe mwenyewe, kwa kuangalia kitu ambacho kwako ni rahisi kukifanya, kinaweza kuwa ni kitu cha kawaida sana kama vile kupika, lakini kwako kikawa ni kipaji kwakuwa mbali na kuwa unapenda kupika lakini unapika chakula kitamu ambacho husifiwa na watu na ni rahisi kwako kujifunza mapishi mapya kuliko watu wengine.

Kinaweza kuwa ni kipaji cha kuongea, kufundisha, kuimba, kupangilia mavazi, kusuka na vitu vingine kama hivyo. Bila kujali ni aina gani ya kipaji ulichonacho unaweza kujiajiri kupitia hicho. Wakati mwingine unaweza usigundue kipaji chako, kwa maana kuwa ukawa na uwezo fulani ambao wewe mwenyewe huuoni lakini watu wanaokuzunguka wakawa wanauona.

iii) Unaweza pia kupata wazo lako la biashara kwa kuangalia kitu unachokipenda (hobi); Hobi ni kitu ambacho unapokifanya unapata furaha kwa kukifanya. Unaweza kuigeuza hobi yako kuwa biashara. Inawezekana unapenda kuvaa, unapenda kupika, unapenda kusikiliza muziki, unaweza kuamua kufanya biashara ambayo inaendana na hobi yako.

Kwa kufanya hivyo utakuwa umeua ndege wawili kwa jiwe moja, unafurahi huku ukipata pesa. Tofauti kati ya hobi na kipaji nikuwa kwenye hobi unaweza kuwa unapenda kitu fulani lakini huwezi kukifanya. Kwa mfano unaweza kuwa unapenda mpira lakini huwezi kuucheza, unapenda muziki lakini huwezi kuimba, unapenda mavazi lakini si mbunifu wa mavazi au huwezi kushona.

Hii ni tofauti na kipaji ambacho ni kitu unaweza kukifanya na pia inaweza kuwa unapenda kukifanya. Unapokuwa na hobi ya kitu fulani unakijua kitu husika. Kinakuwa ndani ya damu yako, haiwi rahisi mtu kukudanganya na unapokifanya unakifanya kwa uangalifu na kwa furaha.

Kitu chochote unapokifanya kwa furaha huwa kizuri. Kwa mfano mtu mwenye hobi ya kupika anapofungua mgahawa hata kama hatakuwa akipika yeye kila siku lakini hataruhusu kipikwe chakula kibaya katika mgahawa wake.

Mtu mwenye hobi ya kuvaa akifungua duka la nguo kamwe hataweka nguo za hovyo hovyo katika duka lake, hivyo hivyo kwa hobi nyingine. Jiangalie mwenyewe, angalia ni kitu gani kinakupa furaha ukikifanya, angalia kama kuna fursa ya kibiashara katika hobi yako, kama ipo itumia na wazo lako litakuwa limetoka hapo.

iv) Kupitia mazingira uliyopo; katika kutafuta wazo la biashara ni lazima ufanye utafiti. Orodhesha mambo ambayo ungependa kuyafanya na fanya utafiti kama mambo hayo yanaweza kuleta faida katika mazingira yako. Wazo la biashara linaweza kutokana na kitu ambacho kinakosekana katika mazingira uliyopo.

Kitu ambacho kina umuhimu lakini hakipatikani. Hapa namaanisha kua mazingira uliyopo yanaweza kuwa na fursa kwa kukosekana kwa kitu fulani sokoni. Angalia kitu ambacho hakipo, lakini kwa uhalisia au kwa maoni yako unaamini kilipaswa kuwepo na kukifanya kuwa biashara. Kwa mfano sehemu ina wafanyakazi wengi lakini hakuna mgahawa wa chakula, kuna shule nyingi lakini hakuna steshenari na vitu vingine vingi.

Angalia soko linahitaji nini, angalia mapungufu ya watoa huduma wengine, kwa maana kuwa hata kama bidhaa au huduma fulani inapatikana katika mazingira hayo lakini kama inapatikana kwa kiwango duni basi kwako inaweza kuwa fursa ya kibiashara na unaweza kuitumia kujiajiri kwa kutoa huduma yenye ubora zaidi.

Angalia kitu ambacho kinawalazimisha watu kusafiri umbali mrefu ili kukipata, kifanye kuwa biashara yako. Toa huduma ambayo haipatikani, wazo lako linaweza kutoka hapo. Hata kama wengine wataiga baadaye tayari utakuwa ushajitambulisha katika soko, utakuwa wakwanza na ubora wa kila atakeyeuiga utapimiwa kwako.

v) Uzoefu wako; wazo la biashara linaweza kutoka katika kitu ambacho una uzoefu nacho, inawezakana uzoefu uliupata kabla au hata wakati upo kazini. Inawezekana kabla ya kupata ajira ulikuwa umeajiriwa katika duka la nguo, hoteli, duka la vifaa vya ujenzi na katika biashara nyingine.

Unaweza ukaanzia hapo, kwakuwa tayari ulishakuwa na uzoefu na biashara husika itakuwa rahisi kwako kuweza kuifanya kwa mafanikio kuliko kuanzisha kitu kipya kabisa. Ni rahisi kufanikiwa katika biashara kama ulishakuwa na uzoefu kidogo.

hata kama uzoefu uliupata katika mazingira tofauti na uliyopo kwa wakati huu lakini kuna uwezekano mkubwa wa kufanikiwa kuliko kuanzisha kitu kingine kipya kabisa. Pamoja na namna zote hizo ambazo unaweza kuzitumia kupata wazo lako la biashara lakini ni lazima ufanye uchunguzi wa kina kabla ya kuamua nini chakufanya.

Ahsante!

Fanya utafiti! Fanya utafiti! Fanya utafiti! Hii itakusaidia kufanya maamuzi sahihi katika biashara utakayoamua kuifanya. Wazo lako ndilo litakalobeba taswira ya biashara yako nzima. Tumia muda mwingi kulifanyia utafuti na kulipima kuangalia kama linawezekana. Utafiti unakupa taarifa za awali kuhusiana na kile unachotegemea kukifanya.

Unakufungua macho na kukuandaa na hali halisi ya maisha ya biashara. Jifunze kwa wengine waliofanya kitu kama wewe, jifunze changamoto walizopitia wengine na kuona namna ambavyo unaweza kuzigeuza changamoto husika kuwa fursa. Usikurupuke tu na kuchagua njia ya kujiajiri, yapime mawazo yako yote na chagua moja bora zaidi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom