Elections 2010 Madiwani wa CCM 40 wawasha moto mkali

Mamboleo

Member
Oct 15, 2008
69
38
Umeibuka mgogoro mkubwa kati ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara na kamati za siasa za wilaya tatu za mkoa huo na kusababisha zaidi ya madiwani wateule 40 wa chama hicho kutishia kukihama chama chao.

Mgogoro huo uliibuka juzi baada ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mara chini ya Uenyekiti wa Makongoro Nyerere kudaiwa kukata majina ya watu wanaotajwa kukubalika waliojitokeza kugombea nafasi za uenyekiti wa halmashauri za Musoma Vijijini, Rorya na Bunda na kupendekezwa na kamati za wilaya.

Habari zilizopatikana jana mjini Musoma na kuthibitishwa na baadhi ya viongozi wa CCM wa wilaya hizo, zinadai kuwa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mara kwa kutumia ushawishi wa mmoja wa viongozi wa CCM mkoa wa Mara ilikata majina ya wagombea hao wanaodaiwa wanakubalika kutokana na chuki.

Kutokana na maamuzi hayo, madiwani hao wateule na wagombea wao waliandamana hadi makao makuu ya chama ili kurudisha kadi zao na kujiunga na vyama vya upinzani, lakini wakati walipowasili katika ofisi hizo za mkoa walikuta zimefungwa.

Madiwani waliofanya maandamano ni kutoka Rorya wakiongozwa na Charles Ochere anayetetea nafasi hiyo kwa kipindi cha pili akiongozana na madiwani wengine 15, Magina Magesa anayegombea Musoma Vijijini aliyeongozana na madiwani 17 pamoja na kiongozi mmoja wa CCM wilaya ya Bunda akimwakilisha Joseph Marimbe anayegombea Halmashauri ya Bunda akiongozana na madiwani 16 wakiwemo ambao wameomba nafasi za viti maalum ingawa majina yao hayajarejeshwa kupinga maamuzi ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mara.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Rorya, Gerald Samuel, alisema kitendo kilichofanywa na Kamati ya Siasa ya Mkoa kwa kukubali mawazo ya mtu mmoja yanalenga kuua chama hicho mkoani Mara. “Nakwambia kamati ya siasa ya mkoa kusikiliza mtu mmoja kwa vile ndiye mwenye pesa sasa chama kimekufa kwani kuna hatari ya kupoteza madiwani karibu wote jimboni kwetu na halmashauri ikaongozwa na wapinzani kama walivyofanya Musoma Mjini,” alisema Samuel.

Alisema kamati ya siasa iliteua majina ya wana-CCM watatu ili kupata baraka za Kamati ya Siasa ya Mkoa na kurejeshwa kwa madiwani wa CCM kwa ajili ya kupigiwa kura, lakini alisema inasikitisha kuona kikao cha mkoa kikitekwa na mtu mmoja na kubatilisha maamuzi ya wilaya.

Mmoja wa madiwani ambaye ni miongoni wa waliokatwa majina yao, Ochere, alisema ili kurudisha heshima ya CCM Mkoa wa Mara, ni vema kamati ya CCM ya mkoa ikajiuzulu kwa madai imekuwa ikipitisha maamuzi kwa maslahi ya mtu binafsi.

Mbunge wa Rorya, Lameck Airo, alisema endapo maamuzi ya Kamati ya Siasa ya Mkoa hayatatenguliwa, yuko tayari kuungana na madiwani hao kurudisha kadi yake na kubaki kuwa mwanancha wa kawaida.

“Haiwezekani huyu mtu ndiye aliyetuletea mgogoro katika makao makuu wa wilaya na leo tena ndiye anayesema na kusikilizwa wakati wanajua kauli zake za kutanguliza pesa ndizo zimekigharimu chama Jimbo la Musoma…sasa hasira zake anaonekana kuzihamishia sehemu nyingine…hivi kamati ya siasa ya wilaya ambayo hata DC (mkuu wa wilaya) alikuwemo leo mapendekezo yake yanatupwa?” alihoji.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Musoma, Ferouz Banno, alithibitisha kupata malalamiko kutoka kwa madiwani hao baada ya kumalizika kikao cha Kamati ya Siasa ya mkoa huku wakitishia kufanya maandamano ya kurejesha kadi.

Hata hivyo, alisema aliwaomba kusitisha uamuzi huo na kwamba angefanya mawasiliano na uongozi wa CCM taifa baada ya uongozi wa mkoa kuonekana kutotenda haki.
“Ni kweli wamekuja kwangu kwa nia ya kurejesha kadi zao ili kata zao zitangazwe kuwa wazi, nimewaomba wasitishe zoezi hilo kwani kama uongozi wa mkoa umenunuliwa na mtu mmoja basi uongozi wa taifa utachukua hatua kwa kuzingatia maamuzi ya kamati za siasa ya wilaya…lakini sijui kama wamenielewa kwa vile walionekana kuchukizwa na kitendo kile wakidai ni chuki na fitina za kigogo mmoja ndani chama,” alisema Banno.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya Musoma Vijijini, Bwire Nyabukika, alisema kitendo kilichofanywa na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mara kinapaswa kulaaniwa vikali kwani kinaweza kusababisha CCM kupoteza imani kwa wananchi kwa vile kimeshindwa kuzingatia maoni ya wilaya.

“Nimesikitishwa kweli na kamati ya mkoa. Watu wazima wanakaa na kubadili maamuzi ya kamati za wilaya kwa maslahi yao badala ya kuangalia maslahi ya chama hapa ndipo tutajua huyo aliyenunua kamati hiyo kama kweli anaweza kununua hata uongozi wa taifa na chama kikafa,” alisema Nyabukika.

Akizungumzia suala hilo Makongoro Nyerere alisema maamuzi hayo yalitokana na Kamati ya Siasa ya Mkoa kugawanyika.
“Wewe ndugu yangu ulitegemea mimi nifanye nini kwa kamati ile ya siasa au ulitaka tena nipigwe kama walivyowahi kutaka kunipiga huko nyuma. Hata chama makao makuu wanajua CCM Mara inaendeshwa na nani,” alisema Nyerere kwa njia ya simu.
“Ndugu yangu we niache tu hata taifa wanajua ni nani mwenye maamuzi na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mara,” alisema na kuongeza:

“Mimi kuwa mwenyekiti sina kura za kutosha kwa kuwatendea haki wana-CCM wenzangu, la msingi nawaomba hao madiwani waache kukurupuka kwa kutaka kukiadhibu chama kwani zipo ngazi za kufuata kama hawajatendewa haki.”

Hata hivyo, aliwaomba wana-CCM hao kuacha kukihama chama hicho na kujiunga na upinzani badala yake wasubiri maamuzi ya ngazi ya taifa kwa hatua zitakazochukuliwa.
Katibu wa CCM, Yusuf Makamba, alisema kuwa tayari amepata taarifa hizo kwa njia zisizo rasmi na kwamba ofisi yake inasubiri taarifa rasmi ili chama kiweze kuchukua hatua.
“Tayari nimesikia malalamiko hayo, lakini sijayapata rasmi, lakini bwana wewe kazi yako si kuandika… sasa nenda kaandike kama ulivyo sikia huko,” alisema Makamba alipoulizwa na NIPASHE.


CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom