Madini: tukiwachekea nyani, tutavuna mabua

Madini: tukiwachekea nyani, tutavuna mabua

Chillah

JF-Expert Member
Joined
Oct 12, 2016
Posts
9,532
Reaction score
10,894
Madini: tukiwachekea nyani, tutavuna mabua
By ezekiel kamwaga

Madini: tukiwachekea nyani, tutavuna mabua

MIAKA minne iliyopita, mimi na waandishi wengine wawili, Paul Maregesi (Mtanzania) na Flora Mallya (Star TV) tulibahatika kutembelea nchi ya Thailand kwa ufadhili wa Wizara ya Nishati na Madini.

Safari yetu iliandaliwa na wizara, baada ya kuona juhudi za vyombo vya habari mbalimbali nchini katika kuandika habari zinazohusu rasilimali asili za taifa, na lengo haswa lilikuwa kuongeza elimu zaidi kwa vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusu sekta ya madini na gesi.

Tulisafiri na Naibu Waziri wa Nishati na Madini wa wakati ule, Steven Masele, pamoja na wataalamu wa gesi, madini na mafuta kutoka serikalini na wadau wengine binafsi.

Kwa muda wa wiki tatu tulitembelea maeneo mbalimbali nchini Thailand yanayojishughulisha na uchimbaji (extraction industry) na tulitumia hata helikopta kutembelea visima ndani ya bahari, kuona jinsi gesi inavyochimbwa na kusafirishwa nchi kavu. Kwetu kweli ilikuwa ni maajabu.

Kati ya vitu muhimu tulivyojifunza wakati wa safari ile ni jinsi watu wa Thailand wanavyofaidika na rasilimali za nchi yao, kwa maana kwamba mikataba ya uchimbaji huwa inaandaliwa kwa uangalifu na ustadi mkubwa, kuhakikisha kuwa wageni hawafaidiki zaidi ya taifa ambalo uchumi wake upo vizuri, kwa vile sekta ya madini imesaidia sana kuinua hali ile.

Tulichokigundua kule Thailand ni kwamba ingawaje kampuni zinazojishughulisha na uchimbaji zinatoka Canada kwa asilimia 98, wataalamu walioajiriwa na kampuni hizo wengi wao ni raia wa Thailand.

Mfano ni wa kampuni moja ya Canada tuliyoikuta kule kusini mwa Thailand, ambayo ina wafanyakazi karibu 400 nchini humo, lakini ni wafanyakazi wanne tu kati yao ndio walikuwa wametoka Canada, na wote waliobakia walikuwa ni raia wa Thailand ambao wameandaliwa vilivyo kuhakikisha nchi yao inafaidika kwa kile kinachojulikana kama ‘win win situation’.

Wanafanyaje hawa wa- Thailand kufanikisha hilo? Ni kwamba kuanzia ngazi ya chekechea, watoto huanza kufundishwa gesi ni kitu gani, na umuhimu wake katika maendeleo ya nchi yao.

Wakati watoto chekechea wanajifunza kusoma na kuandika, maneno yanayotumiwa ni yale yanayomlenga mtoto huyo kuanza kujua gesi au mafuta ni kitu gani, na akianza shule ya msingi, elimu kuhusu gesi na mafuta inatafutiwa nafasi katika mitaala ya shule za huko.

Wanafunzi wanaoingia shule za sekondari huko Thailand huelimishwa zaidi kuhusu gesi, na wanapoingia katika vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu kuna kozi nyingi za elimu ya gesi na mafuta zinazotolewa.

Wapo wanaosomea utaalamu wa uchimbaji, wengine biashara na masoko, wengine kuhusu mikataba ya madini na gesi, wengine kodi na tozo za kimataifa na wengine wanasomea elimu ya rasilimali watu katika sekta hiyo.

Pamoja na kwamba mikataba ya mafuta na gesi huko Thailand bado ni ya siri kama ilivyo hapa Tanzania, mikataba hiyo inaandaliwa kitaalamu kabisa na wataalamu kutoka Thailand, kuhakikisha kuwa nchi yao haiingizwi mkenge na makampuni ya kigeni.

Kwa kifupi ni kwamba, pamoja na kwamba ni kampuni za kigeni zinazochimba mafuta na gesi huko Thailand, ukweli ni kwamba kampuni hizo zinawatumia wataalamu kutoka Thailand ambao wamesoma vizuri, na si rahisi nchi yao kudanganywa na kukosa mapato stahiki katika biashara hiyo.

Baada ya kutembelea visima vya mafuta maeneo mmbalimbali tulipata bahati pia kushiriki maonyesho ya kimataifa ya madini mjini Bangkok ambapo wataalamu kutoka Mamlaka ya Ukaguzi wa Madini (TMAA) walikuwapo pia.

Waziri Masele na sisi tulishangazwa na kampuni kubwa za kutoka India ambazo zilikuwa zinatangaza Tanzanite kama vile ilikuwa inazalishwa huko Mashariki ya Mbali.

Nakumbuka kulikuwa na mchimbaji mmoja kutoka Arusha ninayemkumbuka kwa jina moja la Askofu aliyekuwa anashiriki katika maonyesho hayo ya madini akiwa ameleta Tanzanite yake kutoka Arusha.

Zaidi ya kampuni 10 tulizotembelea mabanda yake ya Tanzanite katika maonyesho yale yalikuwa ni ya kigeni, na hali ile ikatufanya tuone jinsi nchi yetu ilivyo nyuma katika biashara za kimataifa.

Ni katika muktadha huu nimekuwa nikitafakari ni jinsi gani nchi yetu inaweza kufaidika na rasilimali zake kama madini, gesi na baadaye mafuta (utafiti unaendelea kwa mafanikio makubwa) ili kuhakikisha kuwa kampuni za kigeni hazituachii mahandaki, kama zilivyofanya kule Buzwagi na Buliyanhulu baada ya kuchota dhahabu walivyotaka kwa kutumia mikataba mibovu.

Sijui Wizara ya Nishati na Madini ina mikakati gani itakayoifanya kushirikiana na ile ya Elimu na Ufundi, kuhakikisha kuwa kwa miaka ijayo taifa linakuwa na wataalamu wengi katika sekta hiyo, ili nchi ifaidike na rasilimali zake kwa kutumia elimu ya vijana wetu katika uchimbaji wa rasilimali hiyo.

Nalisema hili kwa sababu ningefurahi sana kama ningesikia kila mwaka kuna kongamano la wanafunzi wa sekondari waliochujwa kutoka shule mbalimbali nchini ambao wanaandaliwa katika ngazi tofauti, ili taifa lisiendelee kudanganywa na kampuni za kigeni katika biashara hii.

Kwa vipindi tofauti nimetembea maeneo mbalimbali nchini kuangalia ubora wa elimu ya sekondari, na hasa zile za kata, na nimegundua kuwa nchi hii ina vijana wenye uwezo mkubwa wa akili, na kama wataandaliwa vilivyo wanaweza kuja kulisaidia sana taifa siku zijazo.

Kama kweli tupo makini na uchimbaji wa mafuta, madini na gesi ni lazima tuanze kuwekeza kwa vijana katika ngazi mbalimbali, ili waje kulisaidia taifa na hivyo kuharakisha maendeleo katika ngazi mbalimbali.

Kampuni za kigeni ziwatumie wataalamu wa nchini wanaolipwa mishahara na marupurupu mazuri, ili kuhakikisha kuwa nchi haidanganywi katika biashara hii.

Naona kuna umuhimu kwa sasa kuanzisha somo linalohusu rasilimali za taifa ili lifundishwe kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, kuanza kujenga hamasa miongoni mwa wanafunzi wetu, waanze kujenga uelewa na kusomea taaluma hiyo kwa undani zaidi katika vyuo vikuu baadaye.

Ripoti za Kamati mbili alizounda Rais John Magufuli hivi karibuni zimegundua mambo ya hovyo hovyo ambayo yamefanyika yakilifanya taifa kupotoza matrilioni ya shilingi kwa sababu tu wahusika waliosaini mikataba ya uchimbaji, hawakuwa na utaalamu wa kutosha au walisikumwa na maslahi binafsi.

Kinachopaswa kufanyika kwa sasa ni kwanza kujenga uzalendo miongoni mwa kizazi cha sasa, ili kione uchungu na rasilimali za taifa na hivyo kujiwekea mikakati ya kuzilinda ili ziinufaishe nchi na si wawekezaji kama ilivyo kwa sasa ambapo nchi hainufaiki vilivyo na mikataba ya uchimbaji wa madini, na hata ile ya gesi.

Miaka michache iliyopita mimi pamoja na waandishi wenzangu Richard Mgamba na Joseph Mwamunyange tulitembelea migodi ya dhahabu ya Tulawaka, Bulyanhulu na Buzwagi na tulishangazwa na jinsi shughuli za uchimbaji zilivyokuwa zinaendeshwa kule.

Baadhi ya maswali tuliyouliza wakati huo ni pale tulipokuta mchanga (Makinikia) ukipakiwa katika makontena na tukajibiwa kuwa usafirishwaji huo ulikuwa halali kwani ulikuwepo kwenye mkataba kati ya serikali na Barrick wakati huo.

Lakini sisi kama vyombo vya habari kuna vitu bado hatujavichungunza kwa upande wa wawekezaji ili kuujulisha umma pia, na baadhi ya mambo hayo ni gharama za uwekezaji katika uchimbaji ambazo kwa kawaida ni ghali sana.

Mfano, tairi moja tuu ya mashine zinazochimba dhahabu mwaka ule wa 2012 tuliambiwa inagharimu jumla ya shilingi 30,000,000/- na inaweza tu kutumika kwa muda wa mwaka mmoja. Mashine hiyo inahitaji tairi nne na zote zinagharimu 120 milioni.

Ni muda muafaka kwa sasa kwa vyombo vya habari kuanza kuandika gharama kuhusu uwekezaji katika sekta ya madini, mafuta na gesi, ili wananchi waweze kuelewa jinsi biashara hii inavyoendeshwa duniani, na hili linapaswa kufadhiliwa kwa pamoja na serikali na makampuni husika.

Natamani nchi hii siku moja iwe na miradi na taasisi mbalimbali ambazo zitakuwa zimejengwa kwa faida iliyopatikana kwenye mafuta, madini na gesi, na kama hatuwezi kufika hapo, tutakuwa tunamchekea nyani, hivyo tusubiri kuvuna mabua.

www.raiamwema.co.tz/2017/07/19/tukiwachekea-nyani-tutavuna-mabua/
 
Back
Top Bottom