Rwanda yarejesha malori 18 ya mafuta yaliyochakachuliwa
Na Richard Makore
23rd June 2010
TRA wasema watakiona cha moto
Ewura yachunguza sampuli zake
Sakata la kuchakachua mafuta hapa nchini limeingia katika sura mpya, baada ya maroli 18 yaliyokuwa yamebeba bidhaa hiyo kurudishwa Tanzania kutoka Rwanda kwa madai kuwa shehena iliyokuwa imebebwa ilikuwa imechakachuliwa.
Nipashe ilipata taarifa kutoka vyanzo vya kuaminika kuwa malori hayo yalirejeshwa nchini wiki iliyopita, baada ya mamlaka za Rwanda kuyakataa.
Kutokana na hali hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetaka kampuni zilizosafirisha mafuta hayo kutoa maelezo.
Mamlaka hiyo imeshangazwa na hali hiyo kwa kuwa kabla mafuta hayo hayajasafirishwa kwenda Rwanda iliyakagua na kujiridhisha kuwa yalikuwa safi na kufikia viwango ndipo iliporuhusu yasafirishwe kwenda huko.
Akizungumza na Nipashe ofisini kwake jana, Mkurugenzi wa Elimu na Idara ya Walipa Kodi wa TRA, Protas Mmanda, alithibitisha kuwa mamlaka yake inayashikilia malori hayo tangu mwishoni mwa wiki.
Mmanda alisema kuwa malori 15 wanayashilikia katika ghala lao lililopo Kibaha mkoani Pwani na matatu yamekwama njiani baada ya kuharibika wakati yakirejeshwa nchini kutoka Rwanda.
Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa malori mawili yaliharibikia mkoani Dodoma na moja mpakani mwa Tanzania na Rwanda eneo la Rusumo.
Mmanda alisema kuwa ikiwa mafuta hayo yatapimwa na kuonekana yalichanganywa na mafuta ya taa, TRA itayabana makampuni yaliyoyasafirisha ili yalipe kodi ya Sh. milioni 340 pamoja na adhabu ya Dola za Marekani 10,000 (Sh.13,930,000) kwa kila kampuni itakayobainika kuhusika.
Alisema malori hayo yalikamatwa muda mrefu huko Rwanda yakitokea Tanzania, lakini akasema kama kuna matatizo yatakuwa yamesababishwa na wamiliki wa kampuni zilizoyasafirisha kutoka Dar es Salaam kwa kuwa wao waliyakagua na kuridhika kabla malori hayo kuondoka.
Mmanda alisema mafuta hayo hayakulipiwa kodi kwa kuwa yalikuwa yanasafirishwa kwenda nje na kwamba kama yamerudishwa na yakabainika kuwa yamechakachuliwa lazima wayabane makampuni husika ili yalipe mapato ya serikali.
"Kila gari linapopakia mafuta, maofisa wetu wa TRA wanakuwepo, hivyo suala la kuchakachua mafuta hapa nchini sio rahisi kwa kuwa zoezi lote lilisimamiwa kikamilifu," alisema.
Kwa upande wake, maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), walipoulizwa kuhusiana na suala hilo, walithibitisha na kuongeza kuwa wamechukua sampuli za bidhaa hiyo kwa ajili ya kwenda kuipima kama ilichakachuliwa.
Mmoja wa ofisa wa Ewura aliliambia Nipashe kuwa upimaji wa sampuli hiyo huchukua kati ya siku nne hadi saba kabla ya kutoa matokeo.
Alisema matokea hayo yatatolewa hadharani ili kila mtu aweze kuyajua kwa lengo la kupambana na tatizo hilo la kuchakachukua mafuta.
Hivi karibuni, tatizo hilo limezidi kushamiri ambapo mwezi uliopita magari ya Ikulu yaliwekewa mafuta yaliyochakachuliwa mkoani Kilimanjaro na kuyafanya yashindwe kuwaka.
CHANZO: NIPASHE