Mabadiliko ya Uongozi ya chama cha ACTWazalendo

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
622
1,543
9cd83cfad9b6dc44869a3c61ca147c5f.jpg


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UTANGULIZI

Ndugu wanaHabari,

Tumewaiteni hapa kuwashirikisha taarifa kadhaa muhimu ambazo tungependa kupitia kwenu, ziwafikie wanachama wa ACT Wazalendo na umma wa Watanzania kwa ujumla.

Kama mnavyofahamu, mnamo tarehe 07 Mei, 2017 Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo ilikutana katika mkoa wa kichama Kahama na kufanya kikao chake cha kawaida. Katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa na kufikiwa maamuzi, Kamati Kuu ilifanya mabadiliko kadhaa ya safu ya Uongozi wa juu Makao Makuu ikiwemo kuthibitisha uteuzi wa Mshauri wa Chama wa masuala ya kisheria. Lengo kuu la mabadiliko yaliyofanywa na Kamati Kuu ni kuleta ufanisi wa utekelezaji wa kazi na majukumu ya Kamati za kisekta Makao Makuu ya Chama na mikoani.

Mabadiliko ya Uongozi yaliyofanywa yanahusu maeneo ya Wasemaji wa kisekta ambao ni wenyeviti wa Kamati za kisekta, Sekretarieti ya Kamati Kuu ambayo inaundwa na Makatibu wa Kamati za kisekta na katika nafasi mbili za Makatibu wa Chama ngazi ya Mkoa.

A. UTHIBITISHO WA UTEUZI WA MSHAURI WA CHAMA KATIKA MASUALA YA KISHERIA
Kwa dhamana aliyonayo kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 29(25)(vii), Kiongozi wa Chama aliona umuhimu wa Chama kuwa na Mshauri wa Masuala ya Sheria na akapendekeza jina la ndugu Albert Msando kuwa Mshauri wa Chama juu ya mambo ya Sheria na kuliwasilisha mbele ya Kamati Kuu. Kamati Kuu kwa kauli moja ilikubaliana na mapendekezo hayo na ikapitisha uteuzi huo kwa mujibu wa Katiba ibara ya 29(13)(ii). Uteuzi wa Ndugu Msando umeanza rasmi tarehe 08 Mei 2017.

B. MABADILIKO KATIKA SAFU YA JUU YA UONGOZI NA WASEMAJI WA KISEKTA NA SEKRETARIETI YA KAMATI KUU
Katika safu ya Makao Makuu, Kamati Kuu imefanya mabadiliko ya Kamati kadhaa ambapo imehamisha baadhi ya majukumu kutoka Kamati moja kwenda nyingine, huku ikilazimu kubadilisha pia majina ya baadhi ya Kamati.

Mabadiliko hayo yamefanywa kwa kuzingatia Ibara ya 29(16) na ibara ya 29 ibara ndogo ya (13) kifungu kidogo cha (i) cha Katiba ya ACT Wazalendo kinachoipa Kamati Kuu mamlaka ya kuunda Kamati za kudumu Makao Makuu.

Mabadiliko hayo ni kama ifuatavyo;-

1. Iliyokuwa Kamati ya MAFUNZO NA CHAGUZI sasa itajulikana kama Kamati ya KAMPENI NA CHAGUZI;

2. Iliyokuwa Kamati ya MAENDELEO YA JAMII sasa itajulikana kama Kamati ya PROGRAMU ZA KIJAMII;

3. Kamati Kuu iliunda Kamati mpya itakayojulikana kama Kamati ya OGANAIZESHENI, MAFUNZO NA WANACHAMA.

C. UTEUZI WA WASEMAJI WA KISEKTA (WENYEVITI WA KAMATI ZA MAKAO MAKUU) NA MAKATIBU WA KAMATI ZA KISEKTA (WAJUMBE WA SEKRETARIETI YA KAMATI KUU)
Mabadiliko ya Wasemaji wa kisekta ambao ni Wenyeviti wa kisekta kwa upande mmoja, na Makatibu wa Kamati hizo ambao ni wajumbe wanaounda Sekretarieti ya Kamati Kuu kwa upande wa pili, yamefanywa kwa kuzingatia Katiba Ibara ya 29 ibara ndogo ya (13) kifungu kidogo cha (iii), na (iv).

Aidha, Kamati Kuu ilifanya mabadiliko ya Makatibu wa Mikoa kwa kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ibara ya 27(5)(i). Walioteuliwa au kubadilishwa Kamati na nafasi zao mpya ni kama ifuatavyo;-

(a). Wenyeviti na Makatibu wa Kamati za Makao Makuu

i. Kamati ya Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma:
 Mwenyekiti aliyeteuliwa ni Ndugu Theopista Kumwenda ambaye awali alikuwa Mwenyekiti Kamati ya Mambo ya Nje.
 Katibu anaendelea kuwa Ndugu Ado Shaibu

ii. Kamati ya Fedha na Rasilimali:
 Mwenyekiti aliyeteuliwa ni Ndugu Mhonga Said Ruhwanya ambaye awali alikuwa Mwenyekiti Kamati iliyokuwa ya Maendeleo ya Jamii.
 Katibu anaendelea kuwa Ndugu Ally Kifu.

iii. Kamati ya Oganaizesheni, Mafunzo na Wanachama:
 Mwenyekiti aliyeteuliwa ni Ndugu Yeremia Kulwa Maganja ambaye awali alikuwa Mwenyekiti wa Bunge na Serikali za Mitaa.

iv. Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa:
 Mwenyekiti aliyeteuliwa ni Ndugu Annamarrystella J. Mallac.
 Katibu aliyeteuliwa ni Ndugu Janeth Joel Rithe ambaye awali alikuwa Katibu wa iliyokuwa Kamati ya Maendeleo ya Jamii.

v. Kamati ya Mambo ya Nje:
 Mwenyekiti aliyeteuliwa ni Ndugu Venance Msebo ambaye awali alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Rasilimali.
 Katibu anaendelea kuwa Ndugu John Patrick Mbozu.

vi. Kampeni na Chaguzi:
 Mwenyekiti ni Ndugu Samson Mwigamba ambaye awali alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.
 Katibu anaendelea kuwa Ndugu Mohammed M. Massaga.

vii. Katiba na Sheria:
 Mwenyekiti aliyeteuliwa ni Ndugu Emmanuel Thomas Msasa ambaye awali alikuwa Katibu wa Kamati hii.
 Katibu aliyeteuliwa ni Ndugu Stephen Ally Mwakibolwa.

viii. Kamati ya Utafiti na Sera:
 Mwenyekiti aliyeteuliwa ni Ndugu Emmanuel Mvula.
 Katibu aliyeteuliwa ni Ndugu Idrissa Kweweta.

ix. Kamati ya Nidhamu na Uadilifu:
 Katibu aliyeteuliwa ni Ndugu Dennis Chembo.

x. Kamati ya Ulinzi na Usalama:
 Mwenyekiti aliyeteuliwa ni Ndugu Mohamed Babu ambaye awali alikuwa Katibu wa Kamati hii.
 Katibu aliyeteuliwa ni Ndugu Nestory Mbena.

xi. Kamati ya Programu za Kijamii:
 Mwenyekiti aliyeteuliwa ni Ndugu Mwajabu Dhahabu.
 Katibu aliyeteuliwa ni Ndugu Edna Sunga aliyekuwa Mratibu wa Ngome ya Vijana Taifa.

b. Makatibu wa Mikoa
Kama nilivyodokeza hapo mwanzo, Kamati Kuu pia ilifanya mabadiliko madogo katika nafasi za Makatibu wa Mikoa. Mikoa iliyoguswa na mabadiliko ni Mwanza na Mara.
 Mwanza:
Kamati Kuu imempumzisha aliyekuwa Katibu wa Mkoa wa Mwanza Ndugu Salvatory Magafu na Nafasi yake kuchukuliwa na Ndugu Emmanuel Mashiku ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa akishikilia nafasi ya Katibu wa Mawasiliano na Uenezi Mkoa wa Mwanza.

 Mara:
Kamati Kuu imempumzisha Ndugu David Katikiro na nafasi yake kuchukuliwa na Ndugu Robert Endrew Magulu. Kabla ya uteuzi huu Ndugu Magulu alikuwa akishikilia nafasi ya Katibu wa Mawasiliano na Uenezi mkoa wa Mara.
Napenda kutumia nafasi hii kuwaagiza Kamati za Uongozi katika mikoa ya Mwanza na Mara kuziba mara moja mapengo yaliyoachwa wazi na waliokuwa Makatibu wa Mawasiliano na Uenezi kwa mujibu wa Katiba ya Chama chetu.

D. UCHAGUZI WA NDANI YA CHAMA
Ndugu waandishi wa Habari, Uchaguzi wa Ndani ya Chama unatarajiwa kuanza rasmi mwezi Julai mwaka huu kuanzia ngazi ya Tawi mpaka Mkoa. Baada ya ngazi hizo kukamilika zoezi litahamia ngazi ya Taifa na kuhitimishwa mwezi Machi mwaka 2018. Ratiba ya Uchaguzi tayari imepitishwa na Vikao vya Chama kwa ajili ya utekelezaji. Aidha maandalizi ya vifaa na nyaraka muhimu kwa ajili ya zoezi hilo ikiwemo fomu za kuomba nafasi za uongozi tayari zimekamilika na hatua za usambazaji mikoani zimekwishaanza.

Natoa rai kwa viongozi na wanachama wetu kote nchini kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hii ya kidemokrasia kuomba nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama chao pindi wakati utakapowadia kwa kila ngazi husika. Utaratibu wa uchaguzi wa ndani ya Chama cha ACT Wazalendo ni wa wazi, huru na wa kidemokrasia.

Hivyo ni haki na wajibu wa kila mwanachama kuomba kuchaguliwa na kuchagua katika nafasi yoyote ile anayodhani anaweza kukitumikia Chama kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Chama. Chama chetu kinaongozwa kwa misingi ya Uadilifu na tumejiwekea Miiko na Maadili ya Uongozi ambayo inapaswa kufuatwa na kila mmoja wetu.

Mwisho napenda kutoa onyo kwamba, Hatutamvumilia mwanachama yeyote atakayebainika kutumia hila, rushwa, ama vitendo vingine vyovyote vinavyokatazwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa ndani ya Chama kujipatia uongozi. Watakaopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi katika ngazi mbalimbali, wasitumie fursa hiyo kuwapendelea marafiki au ndugu zao. Wasimamie uchaguzi kwa haki bila kupendelea wala kumwonea yeyote. Nawatakia wanachama wote uchaguzi mwema na daima watangulize mbele maslahi ya nchi na chama chetu pindi wanapotekeleza zoezi hilo.

Ndugu waandishi wa Habari, Asanteni kwa kunisikiliza.

Dorothy Semu
Kaimu Katibu Mkuu
ACT Wazalendo.

Imetolewa leo tarehe 11 Mei, 2017.
Makao Makuu, Kijitonyama Dar es salaam.
 
Mngeitoa kama Press Release iliyo katika PDF ingeonesha ukomavu wa Chama chenu lakini kuitoa katika hiyo hali ya Copy and Paste inasababisha taarifa ikose mvuto. Hata hivyo hongereni kwa maamuzi yenu na kila la heri.
 
Back
Top Bottom