Mabadiliko na Tanzania ninayoihitaji

Shayu

Platinum Member
May 24, 2011
608
1,655
Kila taifa linapaswa kuwa na misingi na linapaswa kuwa na vitu ambavyo wanaamini ndivyo vinavyowaunganisha pamoja kama taifa. Taifa lolote bila ya kuwa na uelewa mpana kwanini wako pamoja na misingi yao ni nini, Ni vigumu kuendelea.

Kama nyumba inavyojengwa ambayo ni lazima iwe na msingi ili iwe imara ndio taifa linavyopaswa kuwa na misingi. Pasipo misingi hii hakuna taifa ambalo litaweza kuwa imara lenye mpangilio na endelevu. Nitajaribu kadiri ya uwezo wangu na kwa lugha rahisi sana kuelezea misingi hii ili kila mmoja aweze kunielewa. Na mtakaponielewa tutakuwa na ufahamu mpana wa kwanini tuko taifa. Na pengine tutaweza kuweka dira yetu kama taifa sawa sawa. Na Baadae yetu kama taifa itakuwa na mwangaza Zaidi kuliko ilivyo sasa.

Taifa lolote lile lazima liwe na maono ni lazima ijulikane ni aina gani ya jamii na taifa watu wanapaswa kulijenga.
Mioyo yao na akili zao lazima zitengenezwe na maono haya. Kila kitu tunachokiona katika dunia hakikutokana na kitu kinachooneka bali kilitokana na wazo kwanza na wazo likifanyika kitu halisi. Kwahiyo mifumo ya kijamii hujengwa na ubora wake unategemea sana busara, maono, maarifa na uwezo wa kiongozi .

Taifa lolote lililo ratibiwa vizuri linategemea busara ya viongozi ili sehemu zake zinazounda taifa ziwe na mahusiano mazuri na amani katika kufanya kazi zake. Bila ya hivyo hakuna taifa litakalojengeka na kuwa bora.

Kitu kikubwa ambacho taifa lolote linalo kwaajili ya maendeleo yake ni watu ambao wanaishi katika ardhi au sehemu ya ardhi katika dunia ambayo ina mtawala wake, au pengine watawala wake kulingana na aina ya tawala tulizonazo kwa sasa za kidemokrasia katika dunia za kupishana kutawala. Na kitu cha pili ni ardhi ambayo watu huitumia katika kulima,kujenga na mambo mengine ambayo hufanyika juu ya ardhi kama kufuga.

Ni dhahiri kabisa maendeleo ya kwanza kabisa binadamu kuanza kuyapata yalitokana na kilimo. Na ugunduzi wa kwanza ulitokana na changamoto za binadamu kutaka kuzalisha Zaidi kupitia kilimo. Kwahiyo kilimo kina nafasi kubwa sana katika historia ya maendeleo ya binadamu.

Watu wameumbwa na akili na kadiri binadamu anavyotumia akili yake kukabiliana na changamoto ambazo anakumbana nazo katika dunia ndivyo anavyokuwa kiakili.

Maendeleo ni matokeo ya akili isiyochoka kufikiri katika kukabiliana na changamoto zinazokabili dunia. Maendeleo tuliyonayo kwa sasa katika dunia ni zao la akili za binadamu. Vitu vyote hivi tunavyoviona kwa macho yetu ambavyo tunavitumia kwaajili ya matumizi yetu ya kila siku mwanzo havikuwepo, vimeumbwa na binadamu. Ni zao la fikra zetu. Hapo mwanzo ilikuwa vigumu mtu kuamini kwamba binadamu anaweza kusafiri angani kwa ndege au ardhini kwa motokaa lakini akili ya binadamu imeweza hili. Na binadamu wote wana akili sawa , kama iliwezekana kwa wazungu tunaweza kufanya mambo makubwa Zaidi kama tukitumia akili zetu vyema. Ni jinsi tu tunavyoelekeza mawazo yetu.

Mawazo yetu tunaelekeza wapi? Je ni kwenye vitu vyenye manufaa na tija kwetu ? kila kitu kinategemea mwelekeo wa mawazo yetu. Ni wakati sasa wa kufikiri kuhusu jambo hili. Binadamu na taifa ni zao la fikra zake hakuna Zaidi ya hilo sisi ni zao la fikra zetu. Kama tutakuwa na uwezo wa kufikiri sawa sawa tutajenga taifa hili vyema. Mikono yetu , macho yetu na miguu yetu ni nyezo tu ambazo akili hutumia kufikisha malengo yake iwe malengo hasi au chanya.

Watu wameumbwa na akili na uwezo wa kujenga taswira kwenye akili ili kuweza kubuni na kugundua vitu ambavyo vitawasaidia kujiletea maendeleo na kurahisisha maisha ya binadamu hapa duniani.
Lakini maendeleo yao inategemea sana kama watu hao ambao wanaishi kwenye taifa hilo wanajitambua na kama wameratibiwa vizuri na kupangwa vizuri katika mahusiano yao. Nikisema wanajitambua nazungumzia mtu mmoja mmoja na kwa pamoja, kama wanajitambua kama taifa na kama wanajitambua wao wenyewe. Hili ni la muhimu na la kwanza. Kujitambua kwa watu wetu kwa taifa lao. Kujua kwanini wako taifa na malengo yao nini. Nitachanganua kadiri ya uwezo wangu ili kuweka picha vizuri kwa mtakao nisoma.

Familia ni sehemu ndogo ya taifa lakini ni muhimu sana. Familia katika udogo wake ndio inayounganisha taifa na jamii. Na misingi ya taifa lolote lazima ianzie huko. Maadili ya taifa lazima yaanzie katika familia. Kama tukishindwa huko chini, hatutaweza kufanikiwa katika ngazi ya taifa.

Kwasababu malezi ya raia huanzia katika ngazi ya familia. Maendeleo yetu yanategemea sana vijana wetu wanalelewaje. Na hili ni jukumu la wazazi. Kutawala familia zao katika misingi iliyobora. Serikali inasehemu yake. Lakini msaada mkubwa katika kutawala nchi unategemea sana utawala katika familia.

Kama tunataka kujenga raia waliobora hatunabudi kuangalia familia zetu kwa umakini mkubwa. Na kuratibu watu wetu katika ngazi za chini. Lakini familia pia inategemea mahusiano yake yakoje katika jamii kwa sababu familia inaunganishwa na jamii. Na kuna mambo ambayo yanawaunganisha pamoja kama jamii katika ngazi ya chini ambayo ni maslahi ya pamoja yaliyowaunganisha.

Maslahi haya hawawezi kuyapata kama hawako pamoja au kama hawana umoja. Kwa mfano shule, huduma za maji na umeme, hospitali na miundo mbinu. Mambo haya yote jamii haiwezi kukabiliana nayo kama hawana umoja. Na ni muhimu kufahamu kwamba tusipojali familia zetu hatutaweza kujali jamii zetu wala taifa letu. Huu ndio msingi ambao tunapaswa kuujenga na kiongozi yeyote mwenye akili atautizama kwa umakini mkubwa.
Kuna uhusiano mkubwa kati ya nidhamu kwenye familia na katika taifa. Wakati umefika sasa sisi kwa sisi kuelewana na kutambua kilicho bora na chenye maslahi kwetu ndani ya familia zetu na katika taifa letu.
Tusipowapanga watu wetu katika ngazi ya chini hatutaweza kupata maendeleo. Maendeleo yatakuja kirahisi ikiwa tutawapanga watu wetu vyema.

Kuna familia, kuna jamii inayozunguka familia na kuna taifa. Mahusiano ya vitu hivi vitatu ni muhimu sana. Na lengo letu ni kujenga raia wanaowajibika na hatutaweza kujenga raia wanaowajibika kama tutapuuzia malezi katika familia.

Adabu na heshima ni muhimu kwa taifa lolote. Kunapotoweka adabu na heshima hatutaweza kujenga taifa la maana. Na hatutaweza kujenga taifa kama tutakuwa na ubinafsi na tusipokuwa tayari kujitolea.
Hatuwezi kujenga taifa hili kwa nguvu, tunahitaji watu waelewe kwanini sisi ni taifa na malengo yetu ni nini kama taifa. Wajue faida ya kuishi katika taifa. Tunatafuta kujenga taifa bora la watu wenye furaha na upendo na wenye mashirikiano. Wajue hapa ni nyumbani kwao na hawana sehemu nyingine ya kuishi. Kujenga taifa la watu wenye nidhamu na dira.

Huu ndio mwelekeo ambao tunapaswa kuujenga kama taifa. Tunapaswa kujenga mahusiano yetu. Kuleta upya umoja wa taifa hili na uwajibikaji wa pamoja. Ni Muda muafaka kuacha ubinafsi na kuangalia maslahi mapana ya taifa. Tukijua kwamba tunakuwa bora Zaidi tukiwa wamoja. Kujenga upya heshima na adabu ambayo imetoweka kwa kasi katika taifa letu.

Nguvu pekee haiwezi kuondoa hii kitu inahitajika busara na maarifa kujenga taifa hili na kuleta watu wake pamoja. Nidhamu haiwezi kuletwa na nguvu peke yake. Watu wetu wanapaswa kuelimishwa ili wajitambue kwamba tunajenga taifa hili kwaajili yao na kwaajili ya vizazi vijavyo. Na tunatumaini kwamba tutajenga Tanzania bora kwaajili ya vizazi vijavyo. Tanzania ya watu wanaoelewana na wenye malengo mamoja.

Watu ambao wanajitolea wenyewe bila kusukumwa ni watu ambao wanauwezo wa kufanya vizuri Zaidi kuliko wale wa kusukumwa. Tanzania haina watumwa wa kusukumwa tuko huru, tunahitaji kujitolea wenyewe nafsi zetu bila kusukumwa kwa faida ya taifa letu. Tuna uwezo wa kufanya mambo mazuri kwa pamoja. Tuuzike ubinafsi wetu na tuje pamoja kama taifa.

Ni tumaini langu kwamba tuna uwezo wa kujenga taifa la watu wanaopendana na kuheshimiana lakini pia la watu wanaowajibika kwa taifa lao. Na wanaowajibika kila mmoja kwa mwenzake. Hii ndio Tanzania ninayowaza na ambayo niko tayari kuijenga. Inayonifanya usiku na mchana nisilale nikitaka kuona watu wa Tanzania wakiboreka kiakili na katika mahusiano yao.

Tanzania ambayo watu watakuwa tayari kulipa kodi kwasababu wanajua umuhimu wake katika maendeleo ya nchi na viongozi wanaowajibika kwa raia kikamilifu. Tanzania ambayo mahakama itatimiza wajibu wake kwa kutenda kwa haki na kwa mujibu wa sheria na bunge linalowajibika na lenye heshima. Tanzania ambayo kila mtu atatimiza wajibu wake na kujua umuhimu wa taifa lake. Tanzania ambayo kila mtu ataheshimiwa na kuthaminiwa.
Tanzania ambayo familia zitakuwa zimeimarika na heshima ya wazee ikarudi. Vijana wakaishi kama vijana kwa adabu na nidhamu na ndoa zikaheshimiwa na watu. Tanzania ambayo watu wanaheshimu majirani zao, kuwapenda na kuwa na uhusiano mwema.

Tanzania ambayo tutaunda taasisi ambazo zitawahudumia kwa moyo mmoja raia wa nchi hii. Tunahitajika kubadilisha tabia za watu wetu ili kujenga taifa hili. Sio tu katika serikali watu wote tunapaswa kubadilika tumepinda. Tunapita njia ambayo si sahihi.

Tunapambana na utandawazi lakini hatupaswi kufanya utandawazi kutumeza ni lazima tusimamie misingi. Na misingi hii ndio haswa chimbuko la ukuaji wa taifa lolote lile pamoja na amani.
 
Back
Top Bottom