Mabadiliko 2012 ni muhimu sana | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mabadiliko 2012 ni muhimu sana

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Jan 2, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jan 2, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,616
  Trophy Points: 280
  Na Daniel Mwaijega
  NIANZE kwa kuwatakia heri ya Mwaka Mpya wasomaji wote wa safu hii nikiamini Mungu kwa upendo wake amewawezesha kuingia mwaka huu wa 2012 mkiwa na afya njema na amani tele.

  Nawashukuru kwa kuniunga mkono kupitia usomaji wenu na maoni ambayo mmekuwa mkiyatoa kila inapochapishwa safu hii. Mwaka jana nilipata ushirikiano mzuri sana kutoka kwenu ambao umekuwa changamoto katika kuboresha na kuendelea kuandika, nikijua kuna wasomaji wanaofuatilia pamoja na kunipa maoni ya aina mbalimbali, ikiwemo kunikosoa mlioona sijawagusa, au nilipopotoka.

  Nawashukuru mlinipongeza na kunikosoa, lakini zaidi kwa changamoto za kunisahihisha kwani hizo zimekuwa msingi wa kuboresha safu hii na kujitahidi kuwa makini zaidi ninapoandika kwa kuelewa kuwa kuna watu makini wanafuatilia kwa umakini mada zangu, tena wa kada mbalimbali.

  Najua wasomaji wangu wote ni watu makini ambao wamejenga mapenzi na heshima kwangu, ndiyo maana mnaacha mambo yenu muhimu kufutilia safu hii kila Jumapili, nawashukuru sana.

  Nasema haya kwa vile naona mmetoa mchango mkubwa kwangu kupitia usomaji wenu na tunapoingia mwaka mpya, ni wajibu wangu kuwa karibu nanyi ili niboreshe zaidi safu hii kwa manufaa ya jamii ya Watanzania na taifa letu kwa ujumla.
  Mwaka jana tumevuka matukio mbalimbali ya kitaifa na kijamii ambayo kwa ujumla yalikuwa na mvuto wa aina yake katika taifa letu, lakini zaidi hekaheka za kimaisha kutokana na mfumuko wa bei na uchumi wanachi kuendelea kushuka.

  Hii ni chanamoto kubwa kwa Watanzania ambayo inawafanya wengi kutojua cha kufanya na wanakoelekea.
  Kibaya zaidi, hoja za viongozi wetu wa kitaifa katika kulipatia ufumbuzi jambo hili ambalo limejaa siasa nyingi ambazo hazitusaidii wala kututoa katika dhiki hii licha ya nchi yetu kutostahili kuwa masikini kutokana na utajiri wa mali asili tulizonazo ambazo zinawanufaisha wachache.

  Inasikitisha kuwa watanzania wenzetu wachache, tena ambao tumewachagua kuwa viongozi wetu na kuwapa dhamana ya kusimamia uzalishaji rasilimali zetu, wametugeuka na kuanza kuchumia matumboni yao na kutengeneza pengo kubwa la kipato miongoni mwa Watanzania.

  Sasa hivi tumejenga pengo kubwa kati ya matajiri na masikini huku kundi dogo la matajiri likiendelea kujitengenezea mazingira ya kuwa wenye haki kumiliki uchumi na hata nguvu za kisiasa.

  Hili ni kero kubwa na ni hatari kwa uhuru na amani ya nchi yetu, kwa sababu ukweli kutokana na hali ngumu ya maisha, kukua kwa kundi la vijana wasio na ajira, uhusiano baina ya wananchi na viongozi wao ni kidogo kwa vile wengi wanaona kuwa waliowachagua wamewaacha solemba wakila kuku kwa mrija na kutembelea magari ya kifari huku wakitanua mirija yao kwa kuwekeza katika maeneo mbalimbali, wakati wao hata mlo mmoja kwa siku wanaupata kwa taabu.


  Kibaya zaidi kinachosikitisha na ambacho kimewakatisha tamaa wananchi walio wengi, ni kitendo cha Bunge kugeuzwa mgodi wa wabunge. Bunge ni chombo cha wananchi na wabungeni ni wawakilishi wa wananchi waliochaguliwa kwa mapenzi makubwa ili kuwatetea, lakini Bunge la safari hii, limegeuka ‘Bunge la Posho’ kutokana na kupigania posho za wabunge bila hofu wakati hali za wananchi ni mbaya.

  Wabunge wa safari hii walianza kudai nyongeza za vipato vyao na wakaendelea hadi kufikia kudai nyongeza za viwango vya posho za vikao vya Bunge, kisha kujiongezea kwa siri baada ya kusikia kelele za wananchi walipojadili suala hilo bungeni.

  Sijaona mantiki ya wabunge wetu tena wote hata wa kutoka chama cha upinzani cha Chadema wanaopiga kelele usiku na mchana kudai haki kwa mbinu mbalimbali ikiwamo kuandama, kugomea vikao vya Bunge kuonyesha kukubaliana na baadhi maamuzi kwa kile wanachokiita maslahi ya Taifa na wananchi, lakini katika hili, wengi wao wametekewa na kelele zao zimezibwa na gundi nzito (Super Glue) ya posho isipokuwa wachache tu wanaojali uzalendo wa kweli.

  Kwa mazingira hayo ni dhahiri kuwa wananchi wameachwa jangwani bila msaada wa chakula wala maji hata maturubai ya kuwahifadhi, hivyo kuwafanya watafute njia za kujikoa na kupigania maisha yao.

  Nawauliza waheshimiwa wabunge na viongozi wetu tunalipeleka wapi taifa letu? Nani kati yenu ana uhakika wa Tanzania bora na yenye mshikamano huko mbele? Inasikitisha kuwa hata sasa wanasiasa wanaendelea kupanga mikakati ya kuwatumia Watanzania wanyonge kwa kauli zao kijanja kuweka mazingira ya kupata uongozi wa taifa hili wakati wanatumia ujanja kufisadi mali zetu?

  Fikiria vita vya Urais wa mwaka 2015 inavyoshika kasi ndani ya CCM. Hii inaonyesha wazi kuwa wanasiasa wetu hawana mpango wowote madhubuti wa kuliendeleza taifa hili bali kulimaliza na Watanzania wasipokuwa makini, na mfumo wa utawala ukikubali kulaghaiwa, tutatawaliwa na magenge ya wadhalimu ambayo yataibomoa nchi yetu.

  Unapoona watu wanaanza kugombea urais mara baada ya uchaguzi kumalizika, tena waziwazi na kwa vita kama iliyopo sasa, ni dhahiri kuwa hakuna wenye mapenzi na masilahi ya taifa bali ubinafsi na ufisadi tu! Lakini kinachonisikitisha zaidi ni unafiki uliopo ndani ya mifumo ya nchi yetu.

  Wanasiasa wamejaa unafiki na baadhi ya viongozi wa dini wamekumbwa na unafiki huo, mpaka sisi wanahabari. Katika hali hii nani atasimama kulitetea taifa letu kwa haki?
  Je njaa inatufanya tuvunje maadili ya kazi na wajibu wetu kwa taifa?
  Je, ni halali mbele za Mungu wetu kudanganya kuwa baadhi ya watu ni chaguo la Mungu wakati mazingira yanaonyesha wazi kuwa wamejipanga kupigania nafasi hizi kwa njia zote hata kwa kuwadhulu wanaoona tishio kwa malengo yao?

  Mimi ni miongoni mwa wanaopiga na unafiki wa aina hiyo wa baadhi ya viongozi wangu wa kiroho, nawapinga wazi kwa sababu wanataka kutuingiza kwenye matatizo na kuondoa heshima ya uongozi wa kiroho.

  Pia tunaridhika upesi na mazingira yanayotuzunguka. Hata kama umeme hakuna tunaishi, dhahabu yetu inaliwa na wajanja kwa mgongo wa uwekezaji tunakubali kwa imani kwamba kuna siku Mungu atafanya maajabu. Acha sasa tuishi kwa matumaini!

  Watanzania tunataka kuendelea kuishi kwa amani, lakini viongozi wetu watusaidie kukabiliana na mazingira magumu ya maisha yanayosababishwa na uzembe na udhalimu au ufisadi uliokithiri katika nyanja mbalimbali za utendeaji na utumishi wa umma.
  Kuna watu ambao walilazimika kuingiza michezo michafu katika siasa za uchaguzi kwa ajili ya kutengeneza mitandao ya kulinda masilahi yao na kujenga mazingira ya uongozi katika uchaguzi wa mwaka 2015.

  Je,hali hii itaendelea mpaka lini? Siasa na uchaguzi wa Tanzania utaendelea kuwalinda na kuwanufaisha watu hao mpaka lini?
  Udhalimu haupo kwenye madini tu bali pia katika biashara ya hoteli, ambapo wawekezaji wanakuja kujenga hoteli kubwa za kitalii chini ya mfumo huo huo wa msamaha kwa kipindi fulani, ukibaki mwaka mmoja huku wakiwa wamejipatia faidia kibao, wanaziuza kwa wawekezaji wengine na kubadilisha majina.

  Wawekezaji wapya wakifanikiwa kabla hazijaanza kuingia kwenye kodi, wanaziuza kwa wengine ambao pia hubadilisha majina! Jamani hili si tatizo la watendaji na sheria zetu? Inakuwaje mwekezaji ahamishe umiliki akiwa amechuma, wakati huko nyuma hakuwahi kusema biashara ni mbaya na hata mrithi naye anapewa nafuu wakati amewekeza kidogo tu!

  Hili ni jambo linalotakiwa kuangaliwa kwa kina, watendaji wetu wanatakiwa kubadilika na kuanza kulitumikia taifa na Watanzania badala ya kundi la watu wachache.

  Sheria hafifu za uwekezaji zilizua mjadala mzito katika Bunge la Tisa chini ya Spika Samuel Sitta na kufikia mwafaka kwamba zibadilishwe, lakini sina hakika baada ya Bunge hilo lakini sina imani kama Bunge la Kumi linaweza kutuokoa kutokana na wabunge kukazania kuboresha masilahi yao ili waendelee kuneemeka na kukuza mitaji ya ubunge wa 2015.

  Ila ni muhimu sheria zote mbovu zikiwamo za ukandamizaji wa haki za binadamu, zikiwemo zinazoubana uhuru wa kupata habari, zibadilishwe kwa sababu hapa ndipo ulipojificha ufisadi wa rasilimali na ukandamizaji kwa vile sheria hizo zinawalinda na kuna watendaji wananufaika nazo, hivyo hawatakuwa tayari zibadilishwe kama hakuna nguvu na msukumo wa kutosha.

  Mwaka jana tumetimiza miaka 50 tangu nchi yetu ipate uhuru. Nadhani Rais Jakaya Kikiwete anapenda kuandika historia ya pekee katika maendeleo ya taifa letu. Kwa namna gani? Je, ana watu wa kumsaidia, au ni genge la wanafiki na yeye anawavumilia tu? Nyerere alimwambia Mzee Ruksa( Ali Hassan Mwinyi): “Punguza upole, ongeza ukali kidooogo”.

  Daniel Mwaijega ni Mhariri wa Mwananchi Jumapili.
  0713 704 898/0688 182 088

  Chanzo. Mabadiliko 2012 ni muhimu sana
   
Loading...