Maaskofu walipuka

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,268
33,040
Waonya kukithiri kwa ubinafsi wa viongozi
headline_bullet.jpg
Watahadharisha utasababisha machafuko
headline_bullet.jpg
Watamani Azimio la Arusha lirejeshwe



Pengosomaxmas.jpg

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo, akiongoza sala ya Krismas katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam jana.


Viongozi wa madhehebu ya dini ya Kikristo nchini, wameonya tabia ya ubinafsi na ya kujilimbikizia mali inayofanywa na baadhi ya viongozi wa umma nchini na kutahadharisha kwamba kama hali hiyo itaachwa iendelee inaweza kuliingiza taifa katika machafuko.

Pia viongozi hao wametaka Azimio la Arusha kuhusu maadili ya viongozi kurejeshwa haraka ili kufanikisha vita dhidi ya rushwa na ufisadi miongoni mwa watendaji serikalini.

Walitoa onyo hilo wakati wakihubiri ibada ya sikukuu ya Krismasi ambapo kitaifa ilifanyika katika Kanisa la Mtakatifu Theresia mjini Tabora jana.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tabora, Mhashamu Paul Ruzoka, amewataka viongozi wa umma nchini, kuacha tabia ya tamaa na kujilimbikizia mali kwa sababu tabia hyo inaweza kuliingiza taifa katika machafuko.

Alisema tabia hiyo imekuwa ikiwafanya wananchi wakate tamaa, kwa sababu inawasababisha viongozi wenye tamaa kushindwa kufuata maadili ya utumishi wa umma na hivyo kugeuka kama maadui wao kwa kuwa wanashindwa kutenda haki.

Askofu Ruzoka, alisema ni vyema sasa wakarejea katika misingi ya maadili aliyoianzisha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ambayo ilijenga taifa lenye umoja na usawa na kuwafanya Watanzania kujiona kama watu kutoka sehemu moja.
Hata hivyo, alilaumu kuondolewa kwa Azimio la Arusha ambalo alisema uwepo wake ungesaidia kuimarika kwa maadili ya viongozi na

kupunguza tamaa na ushindani wa viongozi kumiliki mali na kuwasahau wananchi.
Askofu Ruzoka, pia aliwataka viongozi kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sera ya Kilimo Kwanza nchini, hauiathiri wananchi na kuwaacha bila ya kuwa na ardhi.

Alisema sera hiyo sasa inahimiza uwepo wa wawekezaji na hivyo kuwepo kwa hatari ya Watanzania kuwa watumwa katika ardhi yao au kutumikishwa katika mfumo wa manamba, na kuhoji: "Wakishachukua ardhi kuna nini tena kitakachobakia?.”
Aliwataka viongozi kuamka na kuanza kuwawezesha Watanzania ili watekeleze sera ya Kilimo Kwanza kwa vitendo na kujikwamua kiuchumi.

Alisema dhana ya Kilimo Kwanza msingi wake ni ardhi na kama ardhi haitakuwepo basi ni vigumu kutekelezeka na kuwasaidia Watanzania kuboresha maisha yao.

Akizungumzia athari za kutokuwepo kwa Azimio la Arusha, alisema ni pamoja na kuwepo kwa mbio za utajiri baina ya viongozi, kutofuatwa kwa maadili ya uongozi, kutokuwa na miiko, kuongezeka kwa posho katika vikao vingi na kuibuka kwa suala la mrahaba katika kazi mbalimbali za kiserikali na kukithiri kwa tamaa.

Akitoa mfano alisema ardhi ni rasilimali muhimu na inaweza kumuondoa mtu yeyote katika umaskini, hivyo kutoa mfano wa Mwalimu Nyerere, alipotembelea wilaya ya Urambo, alimkuta mkulima mmoja aliyepata Sh. 82,000 kwa mauzo ya tumbaku ambapo ni sawa na paundi 4,800.

Alisema kipato hicho kwa wakati huo kilikuwa ni sawa na mara 20 kwa mshahara wa Rais, ambacho kilimshawishi Mwalimu kutamani kuacha urais, lakini alisema alilazimika kuendelea kuwatumikia wananchi.

Alisema ni muhimu basi viongozi wa umma wakaendelea kufuata falsafa za Mwalimu Nyerere, kwa sababu zimelenga kuleta umoja wa kitaifa, haki, usawa, amani na utulivu huku akiamini kwamba pale ambapo pamekosewa, ni vyema kujisahihisha.

Alisisitiza kwamba hata Biblia Takatifu katika kitabu cha Yakobo, kinasisitiza kwamba "Tunda la uadilifu hupandwa katika amani" hivyo alionya kama misingi ya haki ikipuuzwa, amani hutoweka na uadilifu utabaki katika masimulizi pekee.

Alimsifu hayati Mwalimu Nyerere, kutokana na tabia yake ya kuiasa jamii na yeye mwenyewe kuishi sawa na misingi aliyoiamini kitu ambacho kilimfanya aishi bila ya kuwa na tamaa ya kujitajirisha, na kueleza kuwa kilikuwa mtihani mkubwa sana kwa viongozi wa zama hizo.

Ibada ya Krismas ilifanyika katika Kanisa la Mtakatifu Theresia mjini hapa, ambalo lina umri wa miaka 133 toka lilipojengwa na wamisionari wa kizungu.

Kwa upande wao, Mchungaji Michael Hafidh wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar, Askofu Dickson Kaganga wa Kanisa la TAG Kariakoo na Askofu wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Augustine Ndeliakyama Shao wametaka Azimio la Arusha kuhusu maadili ya viongozi

kurejeshwa haraka ili kufanikisha vita dhidi ya rushwa na ufisadi miongoni mwa watendaji serikalini.
Walitoa tamko hilo kwa nyakati tofauti wakati wa maadhimisho ya mkesha wa ibada ya Krismasi ambao ulifanyika katika makanisa mbalimbali mjini Zanzibar jana.

Askofu Kaganga alisema wakati huu wa kuelekea katika mjadala wa Katiba mpya, serikali lazima ifikirie kurejesha Azimio la Arusha litakalowabana vigogo wanaojihusisha na ufisadi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema kutokana na kushamiri kwa vitendo vya rushwa na ufisadi, huduma za jamii zimeendelea kudorora huku baadhi ya viongozi wakijilimbikizia mali kutokana na kuweka mbele maslahi binafsi badala ya taifa.

Askofu huyo alisema pamoja na Tanzania kuwa na rasilimali kama za madini na bahari bado wananchi wake wameendelea kuishi katika mazingira ya umaskini kutokana na usimamizi mbovu wa rasilimali za taifa.

Alisema misingi ya maadili ya viongozi iliyowekwa na Baba wa taifa Mwalimu Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Sheikhe Abeid Karume imetupwa na kubakia historia. “Leo hii kuna viongozi wanamiliki mali za kutisha bila kueleweka chanzo cha kipato chao.”alisema Askofu Kaganga.

Alisema kwamba ndani ya azimio la Arusha yamo mambo mazuri ambayo yanaweza kusaidia taifa ikiwemo suala la viongozi kutojishirikisha na biashara wakiwa katika utumishi wa serikali.

Hata hivyo, alisema katika kuelekea mjadala wa katiba mpya ni jambo la busara kwa Watanzania kujiepusha na vitendo vya udini na ukabila ili kulinda misingi ya umoja wa kitaifa.

Naye Mchungaji Hafidh wa Kanisa Aglikana Dayosisi ya Zanzibar, alisema Watanzania imefika wakati kupambana kwa vitendo katika kupiga vita vitendo vya ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi wake.

“Katika Azimio la Arusha yapo mambo lazima yarejeshwe haraka kwa maslahi ya taifa kama suala la maadili kwa viongozi wetu wa serikali na hatua hiyo itasaidia kuondoa wimbi la ufisadi nchini,” alisema Mchungaji Hafidh.

Alisema katika kusheherekea sikukuu ya Krismasi, ni vizuri kwa serikali kutafutia ufumbuzi migomo na maadamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu kwa malengo ya kudumisha umoja wa Watanzania.

Upande wake, Askofu Shao alisema rushwa na ufisadi utaondoka Tanzania iwapo viongozi wote wa serikali watakuwa tayari kukemea vitendo hivyo.

“Ni lazima kuwe na nguvu za ziada kutoka kwa viongozi wa ngazi zote kukemea na kuwawajibisha wala rushwa hususani kwenye taasisi za uongozi.”alisema askofu Shao katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Shangani mjini Zanzibar.
Alisema Watanzania hivi sasa wanaishi katika hali ngumu ya maisha kutokana na tatizo la mfumuko wa bei unaoendelea kujitokeza na kuwaumiza wananchi wengi masikini.

“Wimbo kwamba Tanzania ni kisiwa cha amani kwa sababu hakuna vita ya silaha ni mwavuli wa siasa wa kuficha shida na maovu ya serikali zetu.” alisema Askofu Shao.

Hata hivyo, alisema wakati Watanzania wameweka matumaini ya kuwa na maisha bora kupitia taasisi zilizokabidhiwa dhamana ya maendeleo ya nchi bahati mbaya taasisi hizo ndio zinaongoza kwa vitendo vya ufisadi na rushwa.

“Mwananchi akimbilie wapi kama haki imekuwa ni bidhaa katika mahakama zetu.” alisema Askofu Shao.
Alisema kutokana kushamiri kwa vitendo vya rushwa sekta ya elimu Tanzania imeendelea kuanguka na kushika nafasi ya mwisho katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aliongeza kuwa tatizo la kununua mitihani limekuwa likichangia kwa kiwango kikubwa kuanguka kwa ubora wa elimu hapa nchini.
Aidha, alisema tatizo la mikopo ya elimu ya juu limekuwa giza kuu kwa taifa kutokana na watoto wengi wanaonufaika na mikopo hiyo kuwa ni wa viongozi na kuwaacha wanyonge.

Askofu Shao alisema mikopo ya elimu ya juu imekuwa ikiwanufaisha watoto wa viongozi wa serikali wakiwemo makatibu wakuu, mawaziri na wafanyabiashara na kuwanyima wananchi wanyonge.

“Mkulima anayeishi chini ya Sh. 1,000 kwa siku hapati mkopo, tunapenda kuwaasa wahusika katika hili watende haki,” alisema.
Kuhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa alisema vimeleta mwanga wa kufichua maovu na udhaifu wa serikali.

Hata hivyo, alisema migogoro inayoendeleea kujitokeza katika vyama vya siasa inatokana na ubinafsi na uchu wa madaraka wa viongozi wa vyama hivyo.

Sikukuu ya Krismas Zanzibar imefanyika ikiwa imezorota tofauti na miaka ya nyuma kutokana na hali ngumu ya maisha baada ya soko la ndani la vyakula kuathiriwa na mfumuko mkubwa wa bei kuanzia Januari, mwaka huu.
Hata hivyo, zimefanyika katika mazingira ya amani na utulivu ambapo askari polisi walionekana kuimarisha doria katika makanisa mbalimbali ya Zanzibar.

ASKOFU LAISER ALILIA AMANI


Wilayani Monduli mkoani Arusha, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk. Thomas Laiser, ameonya kuwa amani iliyopo nchini ikitoweka hakuna Mtanzania atakayenusurika.

Kutokana na hali hiyo amewataka Watanzania kujihadhari na mambo yanayoweza kuondoa amani ambayo taifa imejipatia katika kipindi cha miaka 50 tangu kupata uhuru.

Alisema iwapo amani iliyopo itatoweka kwa sababu ya malumbano yoyote yale, hakuna Mtanzania atakayenusurika, hivyo, wanapaswa kumwomba Mungu asaidie katika hilo.

Alisema hayo katika mahubiri yake wakati wa ibada ya misa ya Krismasi iliyofanyika katika Usharika wa Monduli jana.
“Leo hii tunapoadhimisha Krimasi yetu ya mwaka huu, miaka 50 baada ya uhuru, Kristo mleta amani atuletee amani kati yetu…yapo mambo

ndugu zangu ambayo yatatuondolea amani hii aliyotuletea Yesu aliyezaliwa,” alisema.
Alibainisha kuwa Watanzania kwa miaka mingi wamekuwa na umoja na wamekuwa wamoja licha ya kuwepo kwa makabila mengi na lugha nyingi lakini wameunganishwa na lugha moja ya taifa ambayo ni Kiswahili.

“Tunazo imani zetu, tupo Waislamu, Wakristo na wafuatao imani za dini za asili, hivyo Wakristo wapende wasipende Waislamu watakuwepo na
Waislamu wapende wasipende Wakristo watakuwepo,” alisema na kuhoji,“ malumbano ya nini?”

“Sisi ni taifa moja lenye amani ambalo mfano wake haupo katika Bara la Afrika…tuheshimiane, tushikamane, tupendane na tusaidiane, kwani amani

yetu ikitoweka kwa sababu ya malumbano yoyote yale hakuna kati yetu atakayenusurika.
Akizungumzia dhana ya kutafuta ukweli, alitaka watu kuiga mfano wa Mamajusi wa Mashariki ambao hawakuwa tu watu wema, watakatifu au wenye

hekima bali walikuwa pia watu waliokazana kutafuta ukweli kuhusu kuzaliwa kwa Yesu wakiongozwa na nyota.
Alisema, “Biblia inasema, Mamajusi wa Mashariki walifika Yerusalemu wakisema yuko wapi yeye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi, maana tuliona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.”

Alisema haishangazi kujua kwa nini hawa watu wa Mungu Mamajusi wa Mashariki walitafiti kujua ukweli huu wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Ulimwengu wote ulikuwa na matazamio ya kuja kwa Masiha, hivyo ilikuwa ni lazima watafiti kujua ni yeye au ni mwingine. Kutokana na hali

hiyo, Watanzania hawana budi kutafuta ukweli wa jambo kabla ya kulizungumza ili kuepuka kuwa wazushi.
“Ulimi wa kuropoka mambo katika familia, kwa jirani, mahali pa kazi, kanisani na hata katika nchi mara nyingi ndugu umeleta madhara makubwa…jambo lisilo kweli likasemekana ni kweli baadaye ni vigumu kulifanya hilo lionekane sio kweli,” alisema na kunukuu kitabu cha

Mithali 12:19 inayosema, “Mdomo wa kweli utathibitishwa milele bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.”

PENGO NA DAWA ZA KULEVYA


Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewaasa Watanzania kuyasikiliza na kuyafuata maagizo ya Mwenyezi Mungu anayoyatoa kupitia kwa manabii wake ili waondokane na maisha ya shida na mifarakano wanayoendelea

kukumbana nayo; huku akiitaka serikali ichukue hatua madhubuti kudhibiti biashara haramu ya dawa za kulevya.
Kardinali Pengo, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa mahubiri kwenye Ibada ya Misa kusherehekea kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph.

Alisema Mwenyezi Mungu anaendelea kuwaongoza wanadamu kuishi maisha ya kumpendeza kupitia kwa manabii wake na kwamba wanaposhindwa kuwasikiliza wanayoyasema na kuyaonya ni sawa na kumuona Mwenyezi Mungu ni muongo kama alivyofanya shetani pale alipowadanganya Adamu na Hawa.

“Ni mambo mengi mabaya yaliyotokea na yanayoendelea kutokea katika jamii yetu ambapo manabii wameyasemea; kwa mfano walisema kuhusu biashara ya dawa za kulevya kuwa zinahatarisha maisha ya wananchi wetu, lakini badala ya kusikilizwa ikasemwa kuwa manabii hawa nao wanashiriki kwenye biashara hiyo,” alisema.

Alisema kitendo kama hicho hakiisaidii jamii badala yake kinaendelea kuiweka katika mazingira yenye matatizo na shida mbalimbali za kimaisha kama zinazoendelea kutokea katika nchi yetu, ikiwa ni matokeo ya kutofanyia kazi maelekezo anayoyatoa Mwenyezi Mungu.

Kardinali Pengo alisema sherehe ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo inaashiria mwanzo wa maisha mapya na alitoa rai kwa wananchi wote kuangalia hatua walizopiga kwa mwaka mzima tangu Krismas ya mwaka jana na endapo kutakuwa na mapungufu yaliyojitokeza waitumie Krismasi hii kumgeukia Muumba.

Suala la dawa za kulevya limekuwa ni tatizo ambalo viongozi wengi wa dini wamekuwa wakilipigia kelele wakiitaka serikali iwachukulie hatua watu wote wanaohusika na biashara hiyo kwa hoja kwamba inahatarisha maisha ya wananchi na hasa vijana.
Hata hivyo, suala hilo lilileta sintofahamu kubwa pale Rais Jakaya Kikwete, alipowatuhumu baadhi ya viongozi wa dini kuhusika na biashara hiyo

kwenye sherehe za kupewa daraja la Uaskofu na kusimikwa kwa Mhashamu John Ndimbo, kuwa Askofu mzalendo wa pili wa Jimbo la Mbinga.
Kwenye sherehe hizo zilizofanyika Juni 5, mwaka huu, Rais Kikwete, aliwataka viongozi wa dini kuacha kushiriki kwenye biashara ya kuuza dawa za kulevya, kauli ambayo ilipingwa vikali na viongozi wa dini wakiitaka serikali yake iwachukulie hatua za kisheria viongozi hao wanaojihusisha na biashara.

Viongozi hao walisema kwamba kauli ya Rais iliashiria kuwajua viongozi wa dini wanaojihusisha na biashara hiyo na hivyo wakashangaa kwa nini haiwakamati kwa kuwa kufanya biashara hiyo ni kosa la jinai na sheria haiangalii mtu.

DK. MALASUSA


Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa na Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa, amewataka Wakristo wote nchini kusherehekea sikukuu cha Krismasi kitakatifu ikiwemo kusaidia waliopatwa na janga la mafuriko badala ya kufanya mambo yasiyompendeza Mungu.

Aidha, aliwataka Watanzania wote waliopateza ndugu zao na waliopatwa na janga la mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam mapema wiki iliyopita kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu kuelekea mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka mpya wa 2012.
Dk. Malasusa alisema mwaka 2011 umekuwa na majanga mengi ya kitaifa ikiwemo lile la kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders ambalo mzee

mmoja wa kanisa hilo alipoteza maisha na mafuriko yaliyotokea na kusababisha baadhi ya Watanzania kupoteza maisha na makazi.
"Wakristo wenzangu nitumie nafasi hii kutoa pole kwa wenzetu waliopatwa na shida na janga la mafuriko yaliyotokea wiki iliyopita wawe na subira katika kipindi hiki kigumu...Wakristo watumie nafasi hii kuwasaidia wenzetu wanaohitaji msaada wetu na waache kusheherekea siku hii

kwa kutenda yale ambayo hayampendezi Mungu katika maadhimisho ya kuzaliwa Yesu Kristo," alisema.
Alisema Yesu Kristo alizaliwa katika hali duni na umaskini na kwamba Mungu habagui maskini wala matajiri hivyo Watanzania wote watumie nafasi hiyo kutafakari maadhimisho ya sikukuu ya Krismas.

"Tudumishe amani na kuomba kwa ajili ya majanga yanayotokea hapa nchini ili yasiweze kutokea tena," alisema askofu Malasusa.
Imeandikwa na Lucas Raphael, Tabora, Raphael Kibiriti na Hellen Mwango (Dar), John Ngunge (Monduli) na Mwinyi Sadallah (Zanzibar).

CHANZO: NIPASHE

 
Maaskofu waonya posho mpya,ufisadi
Monday, 26 December 2011 11:47
Mwananchi

WASEMA TUSIPOKUWA MAKINI TUNAUZA UHURU WETU
MAASKOFU nchini jana walitumia ibaada ya Krismasi, kuzungumzia mambo kadhaa ya kitaifa yakiwamo nyongeza ya posho za wabunge na mchakato wa katiba mpya na kuonya kuwa Watanzania wasipokuwa makini watauza uhuru wao.Wakihubiri kwa nyakati tofauti katika makanisa mbalimbali viongozi hao wa kidini walisema Tanzania ambayo sasa imefikisha miaka 50 ya uhuru wake, inahitaji viongozi wenye maono na mwelekeo thabiti katika maslahi ya taifa badala ya ya kuwa lelemama na wabinafsi.

Askofu Paulo Ruzoka wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tabora alisema wingi wa posho wanazojilimbikizia wabunge na watumishi wengine wa umma, ni maslahi binafsi ambayo kimsingi ni hatari kwa mustakabali wa taifa hasa ikizingatiwa kuwa zinaligawa taifa katika makundi ya walionacho na walala hoi.

"Kujilimbikizia posho ni kupuuza dhana ya utawala bora, lakini pia ni ubinafsi na hii ni hatari kwa taifa. Tunapaswa kufanya uamuzi mgumu wa kuleta mabadiliko ya kifikra na mtazamo kwa faida ya nchi yetu,"alisema.

Askofu Ruzoka alisema hayo alipokuwa akihubiri katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Tereza, mjini Tabora. "Tunaweza kutunza uhuru wetu kama tu tutaweka mbele maslahi ya kitaifa na si viongozi kuweka maslahi binafsi," alisema.


"Sikukuu hii ya Noeli inakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika. Maana yake ni kwamba tumeshaadhimisha Noel 50 tangu uhuru. Ni lazima tujiulize miaka hii 50 ya uhuru, imetufikisha wapi,"alisema.

Akizungumzia mchakato wa katiba mpya, Askofu Ruzoka alisema ni vema ukawa wa wazi ili kila mwananchi ashiriki na kujua mambo mbalimbali yanayoendelea."Mchakato wa katiba lazima uwe wazi ili suala la ardhi lijulikane kwa kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa Mtanzania. Kama tutaendelea kuwapa wawekezaji ardhi yetu, hatutakuwa watumwa,"alihoji.

Askofu Ruzoka alisisitiza kuwa sera ya kilimo inaonyesha kuwanufaisha wawekezaji badala ya Watanzania, jambo linaowafawanya wazalendo kurudi katika maisha ya manamba kwenye mashamba ya wawekezaji hao.

Mang'ana naye akerwa na nyongeza ya posho
Askofu Mkuu Kanisa la Menonite Tanzania (KMT), Dayosisi ya Mashariki Jimbo la Upanga jijini Dar es Salaam, Steven Mang'ana, amesema nyongeza ya posho za wabunge inaongeza chuki baina yao na wananachi.
"Watunga sheria na wawakilishi wa wananchi, wanafanya madudu kujipandishia posho. Kwani huko Dodoma hakuna walimu wala wanafunzi ambao maisha kwao pia ni magumu kama ilivyoelezwa na Spika Makinda),"alihoji Askofu Mang'ana.
Katika mahubiri yake jana katika ibada ya Krismasi, Askofu huyo aliwataka Wakristo nchini, kuwaombea viongozi ili waondokane na roho za ubinafsi.
Mokiwa: Nchi inayumba

Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Valentino Mokiwa, amesema nchi inayumba kutokana na kukosa viongozi wenye maadili, wanaojua matatizo ya wananchi kwa kuwa wengi wao, walisoma nje na hawana uzoefu wa mazingira ya Tanzania.

Akizungumza katika ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Alban jijini Dar es Salaam jana, kiongozihuyo wa kidini alisema nchi inaelekea kubaya kutokana na matabaka ya wenye nacho na wasiokuwa nacho kuzidi kuongezeka.

"Hali hiyo ikiachwa, inaweza kusababisha uhusiano mbaya katika taifa kwa sababu wengi wao wanatengwa na kupewa wanaoonekana kuwa wamesomea nje. Lakini hawa waliosoma nje wakirudi nchini, hufanya mambo ambayo hayalingani na mazingira ya Tanzania," alisema.

Akizungumzia maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru Askofu Mokiwa alisema ni aibu kuona taifa linaadhimisha miaka 50 katika hali ngumu ya uchumi huku mfumuko wa ukiwa umefikia asilimia 19.5.

Mokiwa alisema Serikali ilikuwa haina sababu ya kutumia fedha nyingi katika maadhimisho hayo na Jeshi la Wananchi kuonyesha nguvu na uwezo wake, badala yake ingetumia fedha hizo kulipa madeni ya walimu na kujenga vyumba madarasa ili kutoa huduma bora za elimu.

"Kwanza siku hizi hatuna adui hata mmoja, watu wote tunazungumza nao, sasa hizi zana za kijeshi ni za nini,"alihoji.

Alisema alishangaa kuona zana hizo za kivita na kesho yake magazeti yakiwa yamepambwa na picha za vifaa hivyo na za makomandoo wakivunja mawe kwa kichwa mambo ambayo alisema hayamsaidii mtoto wa Tanzania.
"Hivi picha ya komanda anapasua jiwe inasaidia nini, nani anataka kutazama vitu kama hivyo,inasaidia vipi upatikanaji wa elimu bora na huduma nzuri za afya," alisistiza.

Chengula alia na ufisadi
Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Evarist Chengula, amesema uchu wa madaraka na maovu kwa baadhi ya viongozi serikalini, ndiyo chanzo cha kutoweka kwa amani na haki miongoni mwa mwananchi.

Aliyasema hayo jana wakati akiongoza misa takatifu katika ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima, Jimbo la Mbeya.

Askofu Chengula alisema amani na haki vinatoweka kwa kasi nchini na katika bara la Afrika kutokana na baadhi ya watawala kunga'ang'ania madaraka kwa kipindi kirefu, lengo likiwa ni kulinda maovu wanayoyafanya wakiwa madarakani.

"Baadhi ya watawala hawataki kuachia madaraka kutokana na dhambi wazifanyazo wanapokuwepo madarakani na wanaogopa kusutwa na wananchi,"alisema askofu Chengula.

Alisema kamwe amani haiwezi kuwepo kama viongozi hawawatendei haki wananchi na kuwatumikia kwa misingi iliyothabiti na uadilifu.


Pengo ahimiza mapambano dawa za kulevya
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinari Pengo, amesisitiza kuwa taifa linahitaji kuongeza kasi katika vita dhidi ya dawa ya kulevya na kuna kila sababu kuamini kuwa wanaopinga vita hiyo wanaongozwa na roho ya mapepo.

Akizungumza katika ibada ya Krismasi katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jana, Kardinali Pengo alisema madhara ya dawa za kulevya kwa vijana, yanatambulika na kwamba jamii inapaswa kuunganisha nguvu katika vita hiyo.
"Hata manabii wamesema dawa za kulevya ni maafa kwa taifa letu. Kwa nini wawepo wanaosema ni wongo kwa sababu tu wanashughulika nayo kama hakuna pepo wa shetani hapo," alihoji Kardinari Pengo.

Askofu Noeyewa awaasa Watanzania

Askofu Wilson Noeyewa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKK) nchini Sudan ya Kusini, amewataka Watanzania kudumisha upendo na amani. Alisema hayo jana katika Ibada ya Krisma iliyofanyika kwenye Usharika wa Moshi mjini, Dayosisi ya Kaskazini.

Askofu Noeye alisema madhara ya kukosekana kwa upendo katika jamii ni vita na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kama ilivyokuwa nchini mwake Sudan.

Kabla ya Sudan Kusini kupata uhuru wake, nilifanya kazi ya kuhubiri katika mazingira magumu sana, kwa hiyo nawaasa Watanzania mpendane kwa sababu mkihubiri na mkalishika kwa dhati neno upendo, hata utukufu wa Mungu mtauona,"alisema.

Wakati huo huo, Askofu Issack Amani wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, alikemea biashara ya kusafirisha binadamu inayoanza kushamiri nchini akisema ni kinyume na utu na mapenzi ya Mungu.

Askofu huyo alitoa kauli hiyo jana mjini Moshi katika Kanisa la Kristu Mfalme, wakati akihubiri kwenye ibada ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristu, Krismasi.

Katika mahubiri yake askofu huyo alitoa wito kwa familia zilizotengana kurudisha mahusiano ili kudumisha upendo ambao umekuwa ukihubiriwa katika Biblia.

Malasusa ahimiza uwajibikaji

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa, amewataka wananchi kufanya kazi katika misingi ya kumwogopa Mungu ili kuliletea taifa maendeleo.Alitoa kauli hiyo jana wakati wa ibada ya Krismas iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front jijini Dar es Salaam.Alisema kama kila mtu ataogopa kutenda maovu katika uwajibikaji wake wa kila siku, hakutakuwa na manung'uniko.

"Ninapokumbuka maneno ya Mungu ya kupendana na kufanya kazi kwa kumwogopa, ni dhahiri napatwa na wasiwasi kwani ukiangalia katika maofisi mengi sidhani kama wanafanya hivyo," alisema Malasusa.
Askofu Malasusa alisema kutoaminiana kumeibua wimbi la viongozi na watu mbalimbali kwenda kutibiwa nje wakihofia kuhujumiwa maisha yao na hili linatokana na matendo yao kwa wananchi.
"Huwezi amini kwani nimesikia siku hizi kuna baadhi ya akina dada wanaamua kwenda nje ya nchi kujifungua kwa madai hapa nchini wanaweza kusababishiwa vifo ama vitendo viovu vya watoto wao," alisema Malasusa.

Habari hii imeandaliwa na Boniface Meena, Daniel Mjema,Moshi, Ibrahim Yamola, Keneth Goliama, James Magai, Joseph Zablon, Godfrey Kahango, Mbeya, Daniel Rutoryo



 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom