Ma-RC, ni wakati wa kwenda na kasi ya Hapa Kazi Tu

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
HAYAWI hayawi sasa yamekuwa, kwa muda mrefu watanzania walikuwa wanasubiri kuiona timu ya viongozi ambao Rais John Magufuli ataichagua kwa ajili ya kufanya nayo kazi katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano.

Kuteguliwa kwa kitendawili cha aina na sifa za viongozi ambao Rais huyo anayetimiza takribani miezi minne sasa tangu aingie madarakani Novemba mwaka jana, kulianza kuonekana mapema tangu alipoteua Baraza lake la Mawaziri.

Baada ya baraza hilo la mawaziri kuteuliwa, mambo mengi yalizungumziwa ikiwemo sifa za mawaziri hao aliowateua na namna watakavyoweza kuendana na kasi ya utendaji wa Dk Magufuli, ambayo inakwenda sambasamba na kauli mbiu ya hapa kazi tu.

Ukweli ni kwamba tangu viongozi hao wateuliwe kwa namna moja ama nyingine hadi sasa wameonesha kwa vitendo namna wanavyoendana na kasi hiyo katika kushughulikia kero za wananchi, lakini kusimamia utendaji serikalini na kupambana na vitendo vya ubadhirifu na rushwa.

Katika kuendelea kuchagua aina ya viongozi wa kufanya nao kazi, Rais Magufuli juzi aliteua wakuu wa mikoa (Ma-RC) wapya 13 na kubakiza saba wa zamani na kuhamisha wengine watano.

Katika uteuzi huo ni wazi kuwa wakuu wengi wa mikoa walioteuliwa ni wapya huku wengi wao wakipanda vyeo kutoka ngazi ya ukuu ya wilaya hadi kufikia nafasi ya RC. Wengine ni wazoefu kutokana na kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali zilizopita ikiwemo uwaziri, lakini pia wamo wanajeshi wastaafu.

Kwa ujumla, timu hiyo ya wakuu wa mikoa ni wazi kuwa imeteuliwa kwa umakini kulingana na sifa za kiutendaji za viongozi hao na hasa kilichozingatiwa ni namna watakavyotoa mchango wao katika kusimamia maendeleo ya mikoa waliyopangiwa.

Kati ya viongozi hao walioteuliwa wamo ambao utendaji wao wa kazi ulionekana na wazi na katika maeneo waliyokuwa wanayasimamia tayari mabadiliko yalishaanza kuonekana, hali ambayo kwa ilimvutia Dk Magufuli na kuamua ama kuendelea nao au kuwapandisha vyeo ili waweze kufanya vizuri zaidi katika ngazi hiyo ya juu.

Pamoja na ukweli huo, pia wamo vijana ambao wameaminiwa na Mkuu huyo wa nchi na kuwapatia nafasi hiyo nyeti ya kuongoza mkoa. Kutokana na ukweli huo ni wakati sasa wa wakuu hao wa mikoa kumuonesha kwa vitendo Dk Magufuli na watanzania kwa ujumla kwa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa uaminifu, lakini pia kuendana na kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ‘Hapa Kazi Tu’.

Nafasi ya ukuu wa mkoa ni nafasi kubwa, ambayo humwakilisha Rais kwa maana ya kumsaidia kufuatilia na kusimamia masuala ya ulinzi na usalama wa mkoa, kusimamia upatikanaji wa huduma bora katika maeneo nyeti kama vile afya, maji, elimu pamoja na miundombinu.

Aidha, kwa sasa mikoa mingi bado inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma bora, kama vile afya, miundombinu mibovu, ukosefu wa umeme, maji na maisha duni ya wananchi, hivyo tunatarajia kuwa viongozi hawa kwa kushirikiana na viongozi wengine wa mikoa watakuja na mikakati thabiti ya kukabiliana na changamoto hizo.

Ni wazi kuwa kuteuliwa kwa wakuu hawa wapya wa mikoa, wakiwemo wale wa zamani kuendelea kutumikia nyadhifa zao, wametimiza vigezo na sifa za kuaminiwa kuwa wanaweza kuchapakazi kwa ufanisi kwa manufaa ya watanzania, hivyo ni matarajio ya wengi kuwa hawatowaangusha watanzania.
 
Back
Top Bottom