Lowassa, Membe, Pinda, Sumaye na ombwe la falsafa!

Lowassa, Membe, Pinda, Sumaye na ombwe la falsafa!

Mzee Kipara

Member
Joined
Jan 3, 2011
Posts
83
Reaction score
43
NIANZE kwa kuweka bayana mapema kabisa kwamba sikubaliani na wale wote wanaoamini ya kuwa muda haujawadia kwa Watanzania kuanza kutafakari kuhusu mtu anayefaa kuwa rais wao mpya ajaye. Au wale wanaowabeza na kuwakatisha tamaa wanaotangaza mapema nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani, na kuanza mapema kampeni zisizo rasmi kuusaka.

Mimi naamini, kwa nchi kama yetu ambayo uelewa wa wananchi ni mdogo na kuna matatizo ya mawasiliano kati ya vijiji (wanakoishi Watanzania wengi) na mijini (wanakoishi Watanzania wachache), tunahitaji muda mrefu wa kuwapima wanaotaka kutuongoza. Na hatuwezi kuwajua na kuwapima kungali mapema kama wenyewe hawajatangaza mapema nia ya kugombea.

Ndiyo maana leo hii katika Marekani japo uchaguzi wao wa rais ni mwaka keshokutwa (2016), tayari mijadala na kampeni zisizo rasmi zimeshaanza katika miji mbalimbali ya taifa hilo kubwa duniani. Majuzi, kwa mfano, nilisisimshwa na shinikizo analolipata Seneta Elizabeth Warren kujitokeza kuchuana na Hillary Clinton kuwania tiketi ya urais ya Democrat katika uchaguzi huo wa 2016. Yaelekea Marekani nayo sasa ina kiu ya kuwa na rais mwanamke!

Nilisisimshwa pia na kauli ya Rais wa sasa, Barack Obama ya kumponda Hillary Clinton kwa kuutaka urais mwaka 2016. Obama alihoji ni kwa nini mama huyo afanye jaribio la pili la kuusaka urais.

Kauli yake hiyo, hata hivyo, ililenga katika kumpigia debe makamu wake, Joe Biden, kuwa ndiye anayefaa kuwa rais mpya wa Marekani 2016. Kwa hakika, Obama aliwaambia Wamarekani kuwa kama Democrat itamteua Joe Biden kuwania urais , basi, atakuwa ‘super candidate' kwenye kampeni za 2016! Sasa hiyo ni Marekani ambayo uchaguzi wake ni 2016, sembuse sisi Tanzania ambao uchaguzi wetu ni mwaka kesho tu?

Kwa hiyo, nasema ni lojiki kwetu kwa wote wanaoutaka urais kujitokeza sasa, na ni lojiki pia Watanzania wote kuwajadili watu hao tena na tena na tena hadi hapo tutakapoishiwa kabisa cha kusema juu yao! Maana, hatupaswi kuuchukulia urais kama nafasi iliyo wazi Ikulu ambayo mtu yeyote, kwa hila na ujanjaujanja, anaweza kuijaza. Tukichukulia hivyo, basi kuna hatari ya kweli kwamba mwakani tutapata rais wa hovyo kabisa kuliko baadhi ya wengine tuliokwishawapata mpaka sasa.

Ni kwa msingi huo nilisoma na kusisimshwa hivi karibuni na makala mbili za Profesa Kitila Mkumbo alizoziandika katika gazeti hili la Raia Mwema kuhusu sifa stahiki za rais anayetufaa mwaka 2015. Nakubaliana kabisa na Profesa kuhusu sifa alizozitaja – awe na falsafa, awe mwazi na mkweli katika vipaumbele, uwezo mkubwa wa kifikra, historia nzuri ya maisha, uzoefu, bidii, weledi, uadilifu, umakini nk.

Namshukuru Profesa Mkumbo kwa kutupiga darasa maridhawa la somo la uraia; hususan sifa za rais tunayemhitaji mwakani. Hata hivyo, nikiri ya kwamba jaribio langu la kutumia sifa hizo alizoziorodhesha katika kuwapima watu waliokwishatangaza mpaka sasa nia ya kuwania urais (na hata wale ambao hawajatangaza rasmi lakini tunajua kuwa wanautaka), liliniacha na hofu kubwa!

Msingi wa hofu yangu ni kwamba wote waliokwishajitokeza mpaka sasa, wakiwemo ambao tayari wameshaunda mitandao ya kampeni na mitandao hiyo imeshaanza kufanya kazi, hawana hata asilimia 60 tu ya sifa hizo zote!
Tunaweza kubishana kuhusu hizo sifa nyingine, lakini nina hakika hatuwezi kubishana kuhusu sifa ya falsafa. Wote waliokwishajitokeza kutangaza nia ya kuutaka urais 2015, hawana sifa hiyo.

Sina hakika ni kwa nini Profesa Mkumbo aliiorodhesha sifa ya falsafa kuwa ya kwanza katika orodha yake kabla ya nyingine, lakini kama alitaka kuonyesha ya kuwa ndiyo sifa kuu (sifa mama) – basi nakubaliana naye mia kwa mia.
Ndiyo maana sikuhangaika kuwapima wataka urais wetu kwa vigezo vya sifa hizo nyingine za Profesa Mkumbo; bali hiyo moja tu kuu - sifa ya falsafa. Maana; kama hawana sifa hiyo, hizo nyingine zote hata kama wanazo ni bure tu – haziwezi kutuondoa kwenye umasikini na wala haziwezi kuliingiza taifa letu kwenye kundi la nchi duniani zinazoendelea kikweli kweli.

Hebu tukumbushane alichokieleza Profesa Mkumbo kuhusu sifa hiyo ya falsafa. Aliandika hivi: "Sifa ya kwanza ya kikazi, ni ya kifalsafa. Mgombea yeyote wa urais yatupasa tumpime kuhusu mwelekeo wake wa kifalsafa.
"Inatupasa tumjue anaamini nini kuhusu maendeleo? Yaani kwake yeye maendeleo maana yake ni nini, na ana maono na dira gani katika kufikia maendeleo hayo?

Hivyo ndivyo alivyoandika Profesa Mkumbo (Raia Mwema Na.368). Sasa, natujiulize: Ni nani kati ya wawania urais wetu ambaye mpaka sasa tunaijua wazi wazi falsafa yake anayoiamini ama kwa yeye mwenyewe kuitangaza hadharani au hata kwa sisi wenyewe kumpima matendo yake na uongozi wake? Ni Edward Lowassa? Ni January Makamba? Ni Frederick Sumaye? Ni Samuel Sitta? Ni Mizengo Pinda? Ni William Ngeleja? Ni Stephen Wassira? Ni Bernard Membe?

Kwa hakika, unaweza kujiuliza swali hilo hilo hata kwa upande wa vyama vya Upinzani: Ni Freeman Mbowe? Ni Dk. Slaa? Ni Profesa Lipumba? Ni Seif Shariff Hamad? Ni Augustine Mrema? Ni John Cheyo? Ni James Mbatia? Ni Tundu Lissu? Nathubutu kusema ya kwamba, wote hao - wakiwemo hata wale ambao walishawania urais katika chaguzi zilizopita, hawaeleweki falsafa zao ni zipi.

Wote, kama alivyosema Profesa, huishia au waliishia tu katika kujisifu kuwa wakichaguliwa urais watajenga hiki na kile au watafanya hiki na kile. Kwangu mimi, hayo ni mapungufu makubwa; maana hayo ni mambo ya kawaida kabisa ambayo mgombea urais yeyote, popote pale duniani, huyaahidi.

Na hilo linanikumbusha kuwa hata Rais wa sasa, Jakaya Kikwete, alikuwa hivyo hivyo alipogombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 2005. Hakuwa na falsafa bali kauli mbiu ya kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya. Watu wakatania: kasi mpya kuelekea wapi? Kuzimu? Leo hii, sijui Kikwete atajigamba kuwa amelisukuma taifa hatua ngapi mbele, na kuelekea wapi; maana hata falsafa yenyewe hakuwanayo na hanayo!

Vivyo hivyo hawa wataka urais wetu wa sasa. Nao hawana falsafa. Hatujui wakiupata urais watatupeleka wapi kama jamii na kama taifa. Kujinadi tu kuwa utajenga shule nyingi za sekondari za kata au utakomesha watoto kukalia matofali au utaongeza ajira au utaboresha kilimo, havitoshi kukupa urais kama hatujui falsafa yako ni ipi.

Kusema kweli, tangu alipoondoka madarakani Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, hatujawahi kupata rais mwingine aliyeiweka wazi falsafa yake anayoiamini bila woga, na aliyeipigania ifuatwe; hata kama kwa kufanya hivyo atakosana na baadhi ya Watanzania wakiwemo maswahiba na marafiki zake. Si Mwinyi, si Mkapa na wala si huyu wa sasa Jakaya Kikwete. Wote hao waliwazuga tu Watanzania ya kwamba siasa ya chama cha CCM haijabadilika – yaani ni ile ile ya Ujamaa na Kujitegemea lakini walivyoiendesha nchi au wanavyoiendesha nchi, ni kinyume chake!

Kwa hiyo, kama hawa akina Lowassa, Membe, Pinda, Makamba, Sitta, Ngeleja nk nao watakuja kujitetea (huko mbele ya safari) kuwa wanayo falsafa yao, na falsafa yao ni falsafa ya CCM, tuwakatalie; maana CCM ya sasa inajulikana kuwa imepoteza mwelekeo – imekuwa sasa ni bendera kufuata upepo tu!

Ndugu zangu, nisisitize tena kwamba tunahitaji kufahamu wataka urais wetu wana mtazamo gani wao wenyewe wa kifalsafa na kiitikadi? Tunataka kujua wakitwaa nchi watajenga jamii na taifa linalofuata mwelekeo gani? Je, wataka urais wetu ni wa mrengo wa kulia moja kwa moja au wa mrengo wa kushoto moja kwa moja? Ni wa mrengo wa kati (centrist) au ni waumini wa mrengo wa kati kushoto (centre left) au kati kulia (centre right)? Au ni wababaishaji tu wa bendera kufuata upepo?

Ni kiri kwamba maisha yangu yote ya uandishi wa habari (takriban miaka 30) sijapata kumwelewa Edward Lowassa kama ni wa mrengo wa kulia au kushoto au wa kati au wa kati kushoto au kati kulia! Vivyo hivyo kwa wawania urais wote niliowaorodhesha mwanzoni kabisa mwa tafakuri hii.

Kama wana falsafa yoyote wanayoifuata na kuiamini, basi, imebakia ndani ya mioyo yao tu; maana hawajapata kuitangaza hadharani au kwa kuandika vitabu au makala. Na sisi wananchi wala hatujaiona (kama wanayo) katika utendaji wao kwenye maisha yao ya utumishi wa umma!

Kwa maneno mengine, ama kwa sababu ya woga tu au kwa sababu ya kukosa ujasiri, wameamua kujificha ndani ya hiyo inayodaiwa kuwa falsafa ya chama chao; hata kama kiukweli haipo au haitekelezwi au hawaiamini.
Wanafanya hivyo, kwa sababu ya kuogopa kukaripiwa na vyama vyao na kuzuiwa kuwania uongozi! Lakini huo ni woga, na Tanzania haimhitaji rais mwoga.

Muwania urais aliye jasiri ni lazima aweke wazi falsafa yake anayoiamini na atakayoijenga akitwaa dola; hata kama si ile inayofuatwa na chama chake. Awe tayari kukosolewa kwa kuamini katika falsafa hiyo, na awe tayari kuitetea hata kama kwa kufanya hivyo anahatarisha kupoteza mvuto wa kisiasa alionao kwa sasa.

Hiyo maana yake ni kwamba kama akiutwaa urais, mtu wa sampuli hiyo atakisuka upya chama chake ili kifuate falsafa hiyo anayoiamini, na ambayo kwayo ndiyo iliyompa ushindi na kumuingiza Ikulu. Je, kina Lowassa wetu na kina Membe wetu na kina Pinda wetu na kina Sumaye wetu wana ujasiri huo? Jibu unalo mwenyewe!

Kabla sijahitimisha safu yangu, niseme kwamba nawapongeza kina Profesa Mkumbo, Zitto Kabwe na Samson Mwigamba kwa jinsi walivyojitahidi kuishawishi CHADEMA ijijenge upya na kuwa na falsafa inayoeleweka; ingawa sikubaliani na uamuzi wao wa kujitoa na kuanzisha chama kipya cha ACT. Nilitaraji kwamba wangebaki humo humo CHADEMA na kupambana humo humo ndani kuiuza na kuipigania falsafa yao wanayoiamini na kuleta mageuzi. Na nina hakika wangelifanikiwa; maana si siri kwamba CHADEMA kimekuwa dhaifu na itakuwa vigumu mno kushinda uchaguzi mwakani. Na tatizo la chama hiki lipo katika uongozi na katika ombwe la kifalsafa linalokisumbua CHADEMA tangu enzi za Mzee Mtei.

Kwa hakika, kama uongozi wa CHADEMA ungelikubaliana na mawazo yao na kukisuka upya chama chao kwa kukipa sura na mwelekeo mpya wa kifalsafa , kisingeingia kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani (2015) kikiwa na sura hii hii iliyochoka ya mawazo yale yale yaliyochoka ya kina Dk. Slaa, Mbowe, Ndesamburo nk.

Kwa hakika, nitashangaa sana mwakani kama chama hiki (CHADEMA) kitampata mgombea urais anayeuzika, na atakayeitoa jasho CCM ndani ya waliomo hivi sasa kwenye chama hicho! Na pengine sipaswi kushangaa; maana Tanzania yetu hii ni nchi ya vituko kwa vyama vyote vya siasa – CCM hadi vya upinzani. Ni nchi ambayo wanaofaa urais, hawautaki, na wale wasiofaa ndiyo wanaojitokeza, na wapo tayari hata kuua kuupata!

Chanzo: Raia mwema
 
Johnson Mbwambo Toka Kina
Zitto Kabwe
Kitila Mkumbo
Samson Mwigamba
Waondoke CHADEMA Amekuwa Tofauti Kabisa Na Zamani.
Ila Hajatuambia Sasa Nani Ana Afadhali Hapo.
 
mwandishi ungemalizia tu Zitto, au mkumbo au mwigamba wanafaa kuwa wagombea urais kwa sababu wana falsafa wanayoiamini na wako tayari kuipigania hata kwa njia haramu
 
Kinachoniuma sana sana ni mke wa rais kutaka kutuchagulia rais wa 2015 eti Membe awe rais jamani watanzania ebu tuwe makini katika hili na tushikamane kukataa sehemu takatifu (Ikulu) kuwa sehemu ya familia.
 
Mzee Kipara kumbe Upara siyo busara eee!! Wewe kaa na mikaratasi yako, ila sisi kwa kuwa tuko makini tunakusaidia wewe upate katiba bora ili uandike kwa uhuru zaidi - Ni juzi juzi tu wewe na wenzako mmebokolewa virungu vya ugoko lakini bado hujui ni nini hasa kiini cha tatizo hilo na mengine mengi tu yanayofanana na hayoi!!
 
mwandishi ungemalizia tu Zitto, au mkumbo au mwigamba wanafaa kuwa wagombea urais kwa sababu wana falsafa wanayoiamini na wako tayari kuipigania hata kwa njia haramu

hakuna asiye jua gazeti la Raiamwema Lipo Upande Wa Zitto.
 
Mzee Kipara kumbe Upara siyo busara eee!! Wewe kaa na mikaratasi yako, ila sisi kwa kuwa tuko makini tunakusaidi wewe upate katiba bora ili uandike kwa uhuru zaidi - Ni juzi juzi tu wewe na wenzako mmebokolewa virungu vya ugoko lakini bado hujui ni nini hasa kiini cha tatizo hilo na mengine mengi tu yanayofanana na hayoi!!

Hii siyo makala yangu mkuu, ni makala iliyoandikwa na Johnson Mbwambo kwenye gazeti la raia mwema. Mimi nimepost tu baada ya kuona kuwa alichoandika kina-make sense.
 
Hii siyo makala yangu mkuu, ni makala iliyoandikwa na Johnson Mbwambo kwenye gazeti la raia mwema. Mimi nimepost tu baada ya kuona kuwa alichoandika kina-make sense.
najua siyo yako, ila namfikishia ujumbe huyo jamaa - najua atachungulia tu humu!!
 
Back
Top Bottom