Liyumba akosa msamaha rais | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Liyumba akosa msamaha rais

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by nngu007, Apr 27, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Apr 27, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145

  Rachel Balama, Dar na Mwajuma Juma, Zanzibar

  RAIS Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 3,060 katika kuadhimisha miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, mwaka huu, lakini
  msamaha huo hautawagusa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.

  Miongoni mwa waliofungwa kwa makosa hayo, aliyekuwa Ofisa utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Amatus Liyumba aliyehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela Mei 24, mwaka jana kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi akiwa mtumishi ya umma na hadi sasa anaendelea kutumikia kifungo hicho.

  Bw. Liyumba alipatikana na hatia ya kutumia madaraka yake vibaya wakati akiwa mtumishi wa umma kwa kufanya mabadiliko katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya BoT, na kusababisha ongezeko la gharama za mradi kutoka dola za Kimarekani 73.6 milioni hadi 357.6 milioni.

  Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kutiwa saini na Waziri wa Wizara hiyo, Bw. Shamsi Vuai Nahodha, rais ametoa msamaha huo kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

  Ingawa taarifa hiyo haikumtaka moja kwa moja Bw. Liyumba, kipengele cha XIV cha aina ya wafungwa ambao hawataguswa na msamaha, ilisema: "Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao."

  Taarifa hiyo imeeleza kuwa rais ametoa msamaha kwa wafungwa wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka mitano ambao hadi siku ya msamaha watakuwa wametumiakia robo ya vifungo vyao.

  Wafungwa wenye magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu na saratani ambao wanaelekea kuwa katika siku za mwisho za maisha yao, ambao watathibitishwa na Jopo la Waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya.

  Wengine, ni wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi, ambao umri wao umethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya na wale wa kike waliofungwa gerezani wakiwa na mimba pamoja na wale walioingia na watoto wachanga wanaonyonya na wasionyonya.

  Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili ambao ulemavu wao umethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya.

  Mbali na walitumia vibaya ofisi zao, msamaha huo wa rais hautawahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha na wale wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.

  Wengine ni wale wanaotumikia kifungo kwa kupatikana na risasi au siraha, wapokea na watoa rushwa, wale wa makosa ya unyang'anyi na unyang'anyi wa kutumia siraha na wafungwa wa kunajisi, kulawiti na kubaka.

  Pia wanaotumikia kifungo kwa kosa la wizi wa magari kwa kutumia siraha, wafungwa waliowapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka 18 au zaidi hawakusamehewa.

  Wafungwa waliohukumiwa kifungo kwa makosa yanayohusu uharibifu wa miundombinu kama vile wizi wa nyaya za simu na umeme, jia za reli na transfoma pamoja na wale wanaotumikia kifungo cha pili au zaidi, pia waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa rais na bado wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

  Wengine waliokosa msamaha ni waliowahi kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi, waliopatikana na hatia ya kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao na waliofungwa kwa kupatikana na hatia ya kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.

  Msamaha huo umeenda sambambamba na maadhimisho ya miaka 47 ya Muungano wa tanganyika na Zanzibar ambazo zilifana jana katika Uwanja wa Amaan licha ya kuwepo kwa kauli za wtau na vikundi mbalimbali vikitaka kupitiwa upya kwa muundo wa muungano huo.

  Rais Jakaya Kikwete aliongoza sherehe hizo ambapo alikuwa mgeni rasmi na kupata nafasi ya kukagua gwaride la heshima la vikosi vya ulinzi na usalama vikiongozwa na Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga taifa (JKT), Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) pamoja na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).

  Mizinga 21 ilipigwa ikiwa ni heshima kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, ambaye aliingia uwanjani hapo kuanzia saa 4.15 akisindikizwa na msafara wa pikipiki akiwa katika gari la wazi la JWTZ akiwapungia mkono wananchi.

  Viongozi wa kitaifa waliohudhuria sherehe hizo ni Makamu wa Rais (Muungano Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Bw. Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

  Marais wastaafu walihudhuria sherehe hizo akiwemo ni Ali Hassan Mwinyi wa awamu ya pili (Muungano), Dkt. Salmin Amour (awamu ya sita Zanzibar).

  Wananchi mbali mbali waliohudhuria sherehe hizo walipata burudani ya halaiki ya vijana 700 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambao walionesha michoro ya ufundi kuhusu muungano pamoja na sarakasi.

  Burudani hiyo iliwafurahisha mamia ya wananchi ambao walifuria katika uwaja wa Amaan licha ya mvua kubwa katika kipindi hiki cha masika.

  Mapema baadhi ya waasisi wa Muungano walitaka kufanyika kwa marekebisho makubwa ya muundo wa Muungano ili ulete manufaa kwa wananchi wa pande mbili.

  Waziri wa kwanza wa Sheria na Katiba wa Muungano, Bw. Hassan Nassoro Moyo alisema wakati umefika kwa suala hilo kupelekwa kwa wananchi kuulizwa aina gani ya Muungano wanaoutaka ili upate ridhaa yao.

  "Muungano huu si wa hayati Nyerere wala Karume, wala si Muungano wa Moyo na wengine," alisema Bw. Moyo na kusisitiza vijana wa leo wanatakiwa kupewa elimu kuhusu Muungano.

  Alisema zile zama za kukubali jambo lolote linaloletwa na wakubwa kwa sasa zimepitwa na wakati, kwani wapo vijana ambao wanataka kufahamu ukweli wa mambo mbalimbali ikiwemo muungano.

  Kikundi kimoja kinachojiita Jumuiya na Taasisi za Kiislamu katika taarifa yake kimetaka kufanyika kwa marekebisho makubwa ya muundo na kwamba wakati umefika kuitishwa kwa kura ya maoni kwa wananchi kuulizwa kuhusu aina gani ya muungano wanaoutaka.

  Katika taarifa ambayo ilitiwa saini na Shekhe Thabit Mohamed Saleh, ilielezwa kuwa matatizo ya muungano yamekuwa yakizidi kuongezeka siku hadi siku huku kukiwa hakuna ufumbuzi wake.

  Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umetimiza miaka 47 huku ukipita katika wakati mgumu na vipindi tofauti vilivyotishia uhai wake na moja ya majaribio makubwa ya kuutikisa ni kuibuka kwa kundi la Wabunge 55 wa Jamhuri ya Muungano waliowasilisha hoja ya kutaka kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano wakimaanisha kuwepo wa Serikali Tatu.

  Hata hivyo hoja hiyo ambayo tayari ilikuwa imepitishwa na bunge iliondolewa, na kitendo hicho kukemewa vikali na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa madai kwamba Serikali tatu haikuwa sera ya Chama Cha Mapinduzi.
   
Loading...