Lishe bora kwa watoto wadogo

Dr. Wansegamila

JF-Expert Member
Feb 3, 2012
2,954
8,093
Hakuna mtu asiefahamu umuhimu wa lishe bora katika maisha ya mwanadamu. Lishe bora na iliyo kamilika, ni muhimu zaidi kwa watoto kwa sababu wao wanaendelea kukua, hivyo basi wana mahitaji ya kipekee na ya tofauti ukilinganisha na watu wazima.

NINI MAANA YA LISHE BORA NA KAMILIFU?


Ili tuweze kuelewa maana ya lishe iliyo bora na kamilifu, ni muhimu tukaangalia mgawanyiko wa makundi ya vyakula.

Vyakula vimegawanyika katika makundi makubwa matano kama ifuatavyo;

–Vyakula vya wanga, hivi ni vile vyakula ambavyo vinatupatia nguvu, mifano ya vyakula hivi ni wali, ugali, mihogo, mtama na nafaka zote.

–Vyakula vya protini

-Hivi ni vyakula ambavyo kazi yake kubwa ni kujenga miili yetu.

-Kundi hili pia limegawanyika katika protini za wanyama, mfano samaki, nyama,dagaa na protini za mimea kama vile karanga, maharagwe,njegere, kunde.

–Vyakula vya mafuta

-Vyakula vya mafuta pia husaidia kuipa miili yetu nguvu; mfano wa vyakula hivi ni kama vile nyama iliyonona, mafuta ya kupikia

-Vitamini na madini

-Kundi hili la chakula husaidia kuilinda miili yetu na magonjwa mbali mbali na kuifanya iwe na kinga ya asili. Mifano ya vyakula kwenye kundi hili ni matunda na mboga za majani.

Baada ya kuona makundi hayo ya chakula, sasa tuangalie jinsi ya kuwalisha watoto kulingana na umri wao.

UMRI KUANZIA MIEZI SITA KUSHUKA CHINI


- Kwa watoto walio chini ya umri wa miezi sita, wanatakiwa wapewe maziwa ya mama tuu!! Mtoto asipewe kitu kingine chochote kile katika umri huu(hata maji)!!

- Hii ni muhimu sana, kwani maziwa ya mama yana kila aina ya kirutubisho ambacho mtoto huyu anahitaji katika umri huu, na hakuna mbadala wake! Hata kama mama anakwenda kazini, basi anaweza kumkamulia mtoto maziwa na yakahifadhiwa vizuri, kwenye chombo kisafi.

Maziwa ya mama yakikamuliwa, yana uwezo wa kukaa hadi masaa 6 bila kuharibika(hata yasipohifadhiwa kwenye friji); na yakihifadhiwa kwenye friji, basi yanaweza kukaa hata kwa masaa 24.

- Kuna tabia pia ya wazazi kuwapa watoto chini ya miezi 6 maji; Hii pia si sahihi hata kidogo, kwani maziwa ya mama yana kiasi cha maji cha kutosha sana! Mtoto anapoonekana kuwa ana kiu, basi anyoneshwe, na sio kupewa maji.

- Kuanza kumpa mtoto chakula cha aina nyingine ambacho si maziwa ya mama, ni hatari kwa afya ya mtoto kwa sababu tumbo lake bado halijakomaa vya kutosha, na inaweza kusababisha maambukizi kwenye tumbo, tumbo kujaa gesi na hata kuharisha.

- Kama mama hatoi maziwa ya kutosha, ajitahidi kuendelea kumpa ziwa mtoto, kwani kadri mtoto anavyovuta ndivyo ambavyo maziwa yanazidi kutengenezwa kwa wingi zaidi, na mama akipunguza/akiacha kumpa mtoto ziwa basi maziwa yanakuwa yanatengenezwa kwa kiasi kidogo sana.

- Pia mama ajitahidi kunywa maji sana(angalau lita tatu au zaidi kwa siku), na vyakula vya majimaji vya kutosha ili maziwa yatengenezwe kwa wingi.

- Madaktari huwa hatushauri sana maziwa ya formula, kwani hayafikii ubora wa maziwa ya mama. Lakini, pale inapobidi, kutokana na maisha tunayoishi sasa mama anaweza asipate maziwa ya kutosha, na kama ana uwezo basi anaweza akamnunulia mtoto wake maziwa ya formula, ili kuongezea.

KUANZIA UMRI WA MIEZI SITA MPAKA MIAKA MIWILI


- Katika umri huu, mtoto anatakiwa aendelee kunyonya maziwa ya mama, lakini pia aanze kuongezewa chakula kingine huku mama akiendelea kupunguza kumnyonyesha kidogo kidogo, na kufikia miaka miwili, ni umri sahihi wa mtoto kuachishwa kabisa ziwa.

- Katika umri huu, ndio wazazi wengi huanza kuumia vichwa juu ya nini watoto wao wapewe, na hapa ndio makosa mengi juu ya lishe ya mtoto hufanyika, na kupelekea mtoto kutokupenda kula, na kupungua uzito.

- Naomba niongelee kwa namna ya kipekee, juu ya kinachoitwa “uji wa lishe” kwani ndio imekuwa ‘habari ya mjini’ kwa kina mama wengi wenye watoto wadogo. Na kwa bahati mbaya sana, hata baadhi ya wahudumu wa afya wamekuwa wakiupigia debe uji huo, na hata kuwauzia kinamama hawa mara wahudhuriapo kliniki.

Uji huo ambao huwa ni mchanganyiko maalumu wa vitu lukuki mfano unga wa mahindi, ulezi, soya, ngano, mchele, karanga, n.k. ndio ambao utakuta mtoto anapewa kuanzia asubuhi, mchana, jioni hadi usiku!!! Na inategemewa kwamba mtoto huyo aupende na kuunywa mchanganyiko huo, kila siku, day in, day out!!

-Leo naomba niwaambie kuwa huo unaoitwa uji wa lishe, hauna lishe yoyote, na kitaalamu haufai kumpa mtoto wako!! Nitasema kwa nini,

Kwanza, mchanganyiko huo wa vitu lukuki, kila kitu huiva katika joto lake ambalo ni tofauti na kitu kingine ndani ya mchanganyiko huo(mfano, karanga zinaiva haraka zaidi kuliko unga wa mahindi, ulezi unaiva haraka zaidi kuliko mchele, n.k.);

Kiasi kwamba utahitajika labda uchemshe zaidi na kuharibu virutubisho katika component nyingine ya mchanganyiko huo, au mtoto atakula baadhi ya vitu vikiwa vibichi!!!

-Pili, vitu hivyo pia vinadumu bila kuharibika kwa muda tofauti tofauti (kwa mfano, karanga huharibika mapema sana, ndani ya wiki moja tuu baada ya kuhifadhiwa), hivyo basi utakuwa unamlisha mtoto wako baadhi ya vitu vilivyooza!!!

- Tatu, kitaalamu mchanganyiko wote huo una vitu viwili tuu vikubwa; Protini na wanga!! Sasa kwa nini uchanganye vitu vyote hivo, ambavyo kiafya vina virutubisho vilivyo karibu sawa?

- Kama una uwezo wa kupata aina zote hizo za vitu (ulezi,unga wa mahindi, unga wa mchele); basi ni vyema ukawa kwa mfano na unga wako wa ulezi labdahalafu na unga wako wa mahindi(uhifadhi tofauti bila kuchanganya), halafu uwe na karanga zako ambazo unanunua labda kila wiki(kwa sababu zinaharibika mapema zaidi), na zenyewe ziwe tofauti.

Halafu uwe unambadilishia mtoto wako, kwa mfano leo asubuhi unampa uji wa ulezi, ukishaupika unasagia huko karanga zako halafu unampa; halafu labda kesho asubuhi unampa uji wa mahindi. Huu ni mfano tuu nimetoa, kwa wenye uwezo wa kupata hivi vitu wanaweza kufanya hivyo, LAKINI mtoto anawezam kusihi vizuri tuu bila huo unaoitwa uji wa lishe, kwa kula chakula cha familia kama ambavyo nitaeleza hapa chini.

-Kama nilivyodokeza, mtoto wa umri kuanzia miezi 6 hadi miaka miwili, anatakiwa ale chakula ambacho familia pia inatumia, lakini kiwe kimefanywa kuwa laini ili aweze kutafuna kwa urahisi. Pia mtoto anatakiwa ale angalau mara tano hadi sita kwa siku,pamoja na maziwa ya mama.

Kwa mfano asubuhi kabisa baada tuu ya kuamka mtoto anaweza kupewa maziwa na vipande vya mkate vilivyolowekwa kwenye maziwa, saa nne akapewa ndizi laini zilizochanganywa na mchuzi wa nyama/maharage, na kipande cha tunda. Mchana anaweza kupewa ugali na mchuzi wa mbogamboga/dagaa/samaki(pamoja na familia), jioni labda akapewa uji kidogo, na usiku akala wali na mchuzi wa maharage/nyama(pamoja na familia) na kipande cha tunda.

Mpangilio huu wa chakula ukiongezewa na maziwa ya mama hasa wakati wa usiku, unatosha kabisa kumfanya mtoto awe na afya bora, na aweze kupenda kula, kwani anakuwa na aina tofauti ya vyakula, na sio uji kuanzia asubuhi hadi usiku.

-Pia mtoto apewe maji ya kutosha

KUANZIA MIAKA MITATU HADI MITANO


-Katika umri huu, tunategemea mtoto awe ameacha kabisa kunyonya, na anakula chakula cha familia (ambacho ni mara tatu kwa siku), kujumlisha milo midogo(snacks) miwili—Jumla ya milo mitano kwa siku.

-Katika umri huu pia, bado wanahitaji protini nyingi kwani miili yao inaendelea kukua na wanahitaji protini kwa ajili ya kujenga miili yao. Pia wanahitaji sana vyakula vya wanga, kwani katika umri huu wanakuwa na michezo mingi na wanatumia nguvu nyingi.
 
Back
Top Bottom