Lipumba: Ufisadi ni matokeo ya utawala mbovu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Lipumba: Ufisadi ni matokeo ya utawala mbovu

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Aug 29, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Aug 29, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,691
  Likes Received: 82,608
  Trophy Points: 280
  Lipumba: Ufisadi ni matokeo ya utawala mbovu

  2008-08-29 09:31:45
  Na Dunstan Bahai

  Matukio ya rushwa, ufisadi na nyufa mbalimbali zilizojitokeza kwenye Muungano, ni matokeo ya kuwa na viongozi wasio waadilifu, hekima na busara.

  Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kwenye kongamano lililoandaliwa na chama hicho jijini Dar es Salaam likiwa na lengo la kujadili ukosefu wa uongozi na hatma ya Tanzania.

  Alisema uongozi usio adilifu na usio na dira wala kujiamini, hujenga matabaka kama ya mitandao.

  Alisema matabaka hayo ndiyo yanayojikuta yakiishikilia nchi katika nyadhifa mbalimbali na hata mmoja wao akifanya madudu ni vigumu kumuengua, kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka makubaliano yaliyomo kwenye mtandao huo.

  Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, wanamtandao hao ndiyo chanzo cha matokeo mabaya ya utawala wowote duniani kwani maamuzi yao hawawashirikishi wananchi.

  ``Katika nchi inayokabiliwa na dimbwi la umaskini, na inataka kujenga demokrasia ya kweli, uadilifu ndiyo unapaswa kuwa msingi wa siasa, msingi wa maongozi ya siasa.

  ``Kuzungumzia uongozi na uadilifu katika siasa si jambo jepesi. Hisia na mitazamo ya watu wa kawaida kuhusiana na siasa, imekuwa ya kuihusisha fani hiyo na tamaa, ubinafsi, uroho, unafiki, ulaghai, upotovu, uovu, fitina, hiyana na hata hujuma. Tena si watu wa kawaida tu bali hata baadhi ya wasomi wetu wanaonekana kuiona hivyo,`` alisema Profesa Lipumba.

  Alisema kutokana na hali hiyo, imechukua muda Watanzania kuamini kama mabadiliko yanawezekana hapa nchini ingawa alisema sasa wameamka na kuunga mkono jitihada za kuwepo kwa mabadiliko hayo.Profesa Lipumba, aliainisha mabadiliko 11 ambayo alidai Watanzania wanayahitaji.

  Mabadiliko hayo ni yale yatakayowapa uongozi wa namna bora ya kutumia neema ya rasilimali zilizopo, yatakayomhakikishia kila Mtanzania anamiliki alau milo mitatu iliyotimia kwa siku na kuongeza kipato chake kupitia kazi halali na jasho lake na kuhakikisha gharama za maisha hazipandi kiholela.

  Mengine alidai kuwa ni mabadiliko ya kupata huduma za msingi za afya zilizo bora na watoto kupata elimu bora ya msingi na sekondari, kupata maji safi na salama na miundombinu ya umeme na barabara iliyo imara na yatakayosafisha uozo wa ufisadi na rushwa na yatakayoleta uwajibikaji na utawala wa sheria.

  Profesa Lipumba, alianisha mabadiliko mengine kuwa ni ya kujenga misingi imara ya umoja, udugu na mapenzi kati ya wananchi wenye imani tofauti za kidini, wa makabila, rangi na jinsia tofauti.

  Mabadiliko mengine ni ya kutoa uhai mpya kwa Muungano na kuuimarisha uweze kukabiliana na changamoto mpya kwa kuhakikisha haki na usawa kati ya Tanganyika na Zanzibar na hivyo kuvutia nchi nyingine kujiunga.

  Mwenyekiti huyo wa CUF alisema mabadiliko mengine ni yale yatakayowapa dira na mwelekeo mpya utakaolipeleka Taifa katika jamii itakayozingatia haki sawa kwa wote na yenye uchumi imara unaotoa ajira na tija kwa wananchi wote, uongozi makini, thabiti na wenye uzalendo wa kweli kwa Taifa lao.

  Wakichangia kwenye kongamano hilo, Profesa Abdallah Safari, alisema maliasili zilizopo nchini haziwanufaishi wananchi wala Taifa kwa ujumla.Alisema hayo ni matokeo ya mikataba mibovu na kwamba upo wakati vijana watavamia kwenye migodi na maeneo mengine ya rasilimali zilizopo ili kunufaika nazo.

  Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Bw. Augustine Mrema, alisema hali kuwa mbaya nchini, ni ishara kwamba uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umefikia kikomo kwa vile umeshindwa kuwafikisha Watanzania katika maisha bora waliyoahidiwa.

  Alihoji sababu za Tanzania Bara kuing`ang`ania Zanzibar wakati ipo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo wanaweza kuungana nayo.

  Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia, aliwataka Watanzania kufikiria kwa kina hali inayoikabili nchi hivi sasa kwani ikisambaratika hakuna atakayepona na akawataka pia watafute mbadala kwa madai kwamba walioko madarakani wameshindwa kuongoza nchi.

  Mhadhiri wa Msikiti wa Idrisa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, Maalim Ali Bassaleh, alihoji taarifa zinazotolewa na serikali kwamba watu waliochota fedha katika Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wanazirejesha wakati hawakukopa wala kuwekesha amana.

  ``Hawa ni wezi. Wakamatwe na wafikishwe mahakamani,`` alisema Maalim Bassaleh.

  Awali, akielezea madhumuni ya kongamano hilo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, alisema walilazimika kuliandaa ili kutafakari na kuona nini la kufanya ili kuikwamua nchi ambayo alidai inapita katika kipindi kigumu kinachohatarisha hatma ya Watanzania.

  Kongamano hilo lilihudhuriwa na wawakilishi kutoka balozi za Ufaransa na Marekani, taasisi za kijamii, vyuo vikuu, wabunge wa Jamhuri ya Muungano, Baraza la Wawakilishi na makundi ya watu wenye ulemavu.

  SOURCE: Nipashe
   
 2. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #2
  Aug 29, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,691
  Likes Received: 82,608
  Trophy Points: 280
  Lipumba: CCM imechoka

  na Mwandishi Wetu
  Tanzania Daima~Sauti ya Watu

  CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimechoka na hakifai kuendelea kuongoza nchi kwa kukosa wa uadilifu, hali inayosababisha kukumbatia ufisadi unaochangia umaskini.

  Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alibainisha hayo jana wakati wa kongamano lililobeba mada isemayo ‘Ukosefu wa uongozi na hatima ya Tanzania' lililofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini, Dar es Salaam.

  Kongamano hilo lilikuwa chini ya uenyekiti wa Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Absalom Kibanda.

  "CCM imechoka, nasi tumeichoka ndiyo maana inaendelea kuwalisha watu takwimu, kwa sasa hatuna uongozi bali kuna mtandao wa mafisadi," alisema Profesa Lipumba katika kongamano hilo la kwanza la aina yake la kisiasa.

  Kongamano hilo lilihudhuriwa pia viongozi wa vyama vya upinzani, akiwamo Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, viongozi wa CHADEMA na wawakilishi wa mabalozi wa nchi mbalimbali.

  Pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupewa mwaliko wa kuhudhuria lakini haikuhudhuria wala kutuma mwakilishi na pia kutotoa sababu ya kutohudhuria kwake, hali iliyoibua maswali mengi kwa washiriki wa kongamano hilo.

  Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, kutokana na kupoteza mwelekeo huo kwa sasa chama hicho kimepachikwa jina la chama cha mafisadi na hivi sasa kimegawanyika katika makundi ya wazi.

  Akizungumzia kuhusu mfumko wa bei, alisema tangu mwaka 2005 wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madarakani hadi leo bei ya vyakula imekuwa ikipanda siku hadi siku kwa kasi mpya.

  Alitolea mfano wa bei ya unga wa sembe kwa mwaka huo kuwa kilo moja iliuzwa kwa sh 250, lakini sasa ni sh 770, mchele ulikuwa sh 500 na sasa sh 1,300, maharage sh 400 sasa sh 1,200, mafuta ya kula lita 20 yaliuzwa kwa sh 10,500 lakini kwa sasa ni sh 43,000.

  "Wananchi wa Kanda ya Ziwa wanaambulia kula mapanki - mifupa ya samaki iliyobakia baada ya minofu ya samaki kukatwa na kusafirishwa Ulaya - ambayo hata nayo yamepanda bei. Haya ndiyo matokeo ya uongozi wa Rais Kikwete wa kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

  "Ugumu wa maisha unawafanya watu kukosa milo mitatu na kuamua kufunga pasipo ridhaa yao...bei za vyakula zimepanda. Walau angetupa pole Watanzania kwa maisha magumu badala yake anatukejeli na kutueleza mambo mazuri, uchumi unakua na ajira zinaongezeka," alisema Profesa Lipumba.

  Aliitaka serikali pia kuhakikisha wanawake wajawazito na watoto wachanga wanapata lishe bora ili kuwajengea afya na kuimarisha miili yao.

  "Tunakumbuka mkasa wa mama mjamzito uliotokea Mwananyamala ambaye alipata matatizo kutokana na kushindwa kupatiwa huduma kutokana na kukosa vifaa, wajawazito wengi hawapati huduma bora, ni vyema serikali ikaliangalia hili", aliongeza.

  Profesa Lipumba alisema Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la uongozi ambalo kutokana na ukosefu wa maadili, rasilimali zimeshindwa kusimamiwa ipasavyo kwa lengo la kuwanufaisha Watanzania.

  Alibainisha kuwa kiwango kikubwa cha ukiukwaji wa maadili ya uongozi, ulianza kuonekana mapema katika awamu ya nne ambako katika kulinda wanamtandao ndani ya CCM, Kikwete aliunda baraza kubwa la mawaziri, lililokuwa na mawaziri 30 na naibu mawaziri 31, lengo likiwa kuhakikisha kila mwanamtandao anapata madaraka.

  Hata wale waliokosa nafasi za uwaziri na unaibu, nao walipewa ukuu wa mikoa pamoja na kuwa wabunge lengo likiwa ni hilo hilo.

  Kuhusu Mahakama ya Kadhi, alisema wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2005, CCM iliahidi endapo itaingia madarakani, itaanzisha mahakama hiyo, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea zaidi ya danadana.

  Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, suala hilo limesababisha mfarakano na mgawanyiko ndani ya CCM, kwani wabunge walio Waislamu walitaka iwepo wakati Wakristo waliipinga.

  Kuhusu mpasuko wa kisiasa kati ya CCM na CUF, alisema kamati ziliundwa katika kulizungumzia suala hilo na ilipofika katika utekelezaji, CCM ilianzisha ajenda nyingine na kukwepa kilichotakiwa kutekelezwa. "Kumbe hakukuwa na nia thabiti katika hili, unajenga nyufa katika jamii badala ya kuziziba," alisema Profesa Lipumba.

  Aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine, amemwandikia barua zaidi ya mbili Rais Kikwete kwa lengo la kuomba wakutane lakini hadi leo hajamjibu chochote.

  "Barua ya mwisho niliandika Juni, mwaka huu, nikiomba tukutane na kujadili suala hilo, lakini hadi leo hajajibu lolote," alisema Profesa Lipumba.

  Kuhusu hoja ya Zanzibar ni nchi au la, alisema ni muungano wa nchi mbili na kuwa inatakiwa kuwe na ukweli katika hilo.

  Alimshauri Rais Kikwete na watu wengine katika jamii kukisoma kitabu kilichoandikwa na Profesa Issa Shivji, kinachoelezea kuhusu Tanzania Bara na Zanzibar, ili kubaini ukweli.

  Kuhusu rada alisema ofisi ya kuchungza rushwa kubwa ya Uingereza, (SFO) ilibaini kuwa Kampuni ya BAE, ililipa dola milioni 12 katika akaunti za Uswisi za Sailesh Vithlani ambaye ni mfanyabiashara wa Mwanza na hadi sasa anaishi Uingereza na alikuwa wakala wa Serikali katika ununuzi wa rada hiyo.

  Alisema mbali na makachero wa SFO kuifahamisha serikali ya Tanzania kuhusu akaunti za mfanyabiashara huyo na uhusiano na BAE, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), waliamua kumuachia bila kumhoji mtuhumiwa huyo.

  "Baada ya mfanyabiashara huyo kuondoka, ndipo Takukuru ikajikakamua kupeleka kesi hiyo mahakamani mwaka 2007 na kujifanya kutoa wito kuwa mfanyabiashara huyo anatafutwa," alisema Profesa Lipumba.

  Akizungumzia kashfa ya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, alisema SFO iligundua akaunti yake ina zaidi ya dola milioni moja katika kisiwa cha Jersey, Uingereza, hii ilithibitisha kuwa kuna mtandao mkubwa wa rushwa unaoongozwa na maofisa wa ngazi za juu serikalini.

  Katika kuthibitisha hiyo, Chenge alidiriki kutoa kauli za kejeli kwa Watanzania, lakini Rais Kikwete aliendelea kuulinda mtandao wake wa mafisadi serikalini.

  "Licha ya Chenge kuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa muda wa miaka 10, lakini hakuonyesha juhudi zozote za kupambana na rushwa na badala yake, yeye mwenyewe leo hii hajakanusha kujilimbikizia fedha nyingi katika akaunti yake," alisema Profesa Lipumba.

  Akizungumzia kashfa ya Benki Kuu kutumia akaunti ya nje (EPA), kulipa makampuni 22 shilingi bilioni 133 kwa kutumia nyaraka za kughushi, alisema wizi huu ni wa kutisha ulioidhalilisha BoT.

  Alisema kwa sasa Rais baada ya kutumia mamlaka aliyo nayo ya kuwakamata wezi wa fedha za EPA, matokeo yake anawapa siku za kurejesha fedha hizo huku wananchi wakiendelea kuishi katika mazingira magumu ya kimaisha.

  Aliongeza kuwa kukosekana kwa uadilifu wa uongozi ndani ya CCM, kumewafanya Watanzania kuwa na tafsiri kuwa siasa ni fani ya kulaghai na kudanganya watu na ili kurudisha imani kwa wananchi imetoa misingi 12 ya jinsi kiongozi anavyotakiwa afuate ikiwamo kutokubali watu wake kukandamizwa.

  Alisema kuwapo kwa migomo ya wafanyakazi, uchumi dhaifu na kuendelea kuwapo kwa mpasuko wa kisiasa na hata kutishia umoja wa kitaifa, ni baadhi tu ya dalili kuwa uongozi ni mbovu na kuongeza kuwa imefikia wakati Watanzania wakubali kuleta mabadiliko.

  Kwa mujibu wa Lipumba, Tanzania ni moja ya nchi zinazoongoza kwa vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga na kusema kuwa hii inatokana na ukosefu wa viongozi waadilifu wenye kuwajali watu wake.

  Aliongeza kuwa kukosekana kwa uongozi bora katika nchi kumesababisha matatizo mengi ya kijamii ambayo yanalisumbua taifa hili kwa muda mrefu.

  Alitolea mfano tatizo la mauaji ya albino ambayo yamekuwa yakifanyika mikoa ya kanda ya ziwa na mikoa mingine kuwa ni usimamizi na misingi mibovu ya viongoizi kuanzia ngazi za chini.

  "Nalaani mauaji ya ndugu zetu maalbino, na serikali ya CCM imeonekana kutokulichukulia suala hili kama jambo la msingi, na wamewatenga, tatizo kubwa ni kwamba hata viongozi wa serikali wamehisiwa kuwa wanashiriki kutumia viungo hivyo kwa ajili ya kujipatia madaraka," alisema.

  Profesa huyo aliyebobea katika maeneo ya uchumi, aliyataja matukio mengine kama lile la Waziri Dk. Shukuru Kawambwa kuhamishwa kwa wizara nne tofauti ndani ya miaka miwili na nusu, wakati watuhumiwa wa EPA na Richmond wakishindwa kushughulikiwa kwa misingi ya sheria, ni vielelezo tosha kuwa taifa limekosa viongozi waadilifu wenye kufuata misingi ya haki.

  Awali akieleza madhumuni ya kongamano hilo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Seif Sharif Hamad, alisema kwa sasa Tanzania inapita katika kipindi kigumu ikiwamo mfumko wa bei, mpasuko wa kisiasa, uchumi dhaifu, mgawanyiko wa kidini pamoja na nyufa katika Muungano kuongezeka.

  Naye Mwenyekiti wa kongamano hilo, Kibanda, alieleza kusikitishwa na vitendo vya wanachama wa vyama vya upinzani wa Tanzania Bara kuhamahama vyama kila kukicha, akisema jambo hilo linachochea kudidimia kwa demokrasia ya ushindani ya vyama vingi.

  "Moja ya habari zinazokera ni hizo taarifa za kila kukicha za wanachama wa CUF, CHADEMA, TLP na NCCR kuhama vyama vyao na kujiunga na CCM, wakidhani kwa kufanya hivyo wanadhoofisha upinzani wakati ukweli wanachokifanya ni kuua ushindani wa demokrasia wa vyama vingi ambao ni msingi imara wa maendeleo," alisema Kibanda.

  Wakichangia katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, alisema uongozi wa CCM umekufa na kwamba hakuna kiongozi bora.

  Alisema kutokana na hali hiyo, ndiyo maana hadi leo uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere unasifiwa kwa utendaji wake wa uadilifu.

  Naye Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kuweka itikadi pembeni ili kuweza kuendeleza nchi kwa kuwa kwa sasa nchi haina mwelekeo wowote na wala hakuna maendeleo.

  Alisema maneno yanayotolea kwa ahadi na viongozi hayafanani na matendo yanayofanywa na viongozi hao kwa sasa.

  "Viongozi wanatakiwa kuweka itikadi pembeni na kufanya kazi kwa pamoja...angalia nchi inakwenda pabaya...ni maneno tu lakini bila ya matendo hakuna maendeleo yoyote yaliyofikiwa hadi sasa," alisema Mbatia.

  Naye Mwakilishi wa CHADEMA, Victor Kimesera, alisema kwa kuwa Tanzania imekuwa inanunua viongozi na si kuchagua viongozi bora, hivyo kila siku itakuwa inaongozwa na viongozi wabovu na nchi itazidi kuelekea pabaya.

  Alisema wananchi wasipoungana na kujua madhara ya kununua viongozi, basi hakutakuwa na maendeleo yoyote yatakayofikiwa.

  Taarifa hii imeandaliwa na Hellen Ngoromera, Asha Bani, Sauli Giliard na Deogratius Temba
   
 3. Mwiba

  Mwiba JF-Expert Member

  #3
  Aug 29, 2008
  Joined: Oct 23, 2007
  Messages: 7,606
  Likes Received: 215
  Trophy Points: 160
  Upinzani unahitaji kiongozi mshari ambae yupo tayari kwa lolote ili kuiweka sawa serikali isiyofuata madili ya Uongozi lakini kwa style hizi za akina Lipumba na Mbowe na Sefu wao naona watafoka na kutoa mapofu kama sabuni ya magadi ambayo zaidi ya kutoa mapovu basi inakukata na vidole na kukukwaruza, hawa viongozi wa upinzani hawafai kabisa katika kipindi hiki cha transit ni lazima waondoke na kuwapisha ,viongozi kama akina Oginga ambao wamewakabidhi wananchi kila kitu na wananchi wamekuwa wakifanya kweli na wamefanya kweli na imeonekana walichokifanya ,na kutoa tishio kwa serikali ya kibaki.
  Japo itaonekana Kibaki yupo madarakani lakini walichokifanya wapinzani chini ya Uongozi wa Odinga ni cha kupigiwa mfano,Odinga si kuwa hakufahamu kuwa wengine watapoteza maisha bali kilichokuwa kinaaaminika kwake ni kuwa haki haitaletwa kwenye sahani na kupewa.

  Tamaa ya akina Lipumba,Mbowe,Zito ,Basefu na kizee chao cha kilikacha Mrema wanaonekana ni wenye kusubiri labda ipo siku CCM itawapelekea madaraka na kuwambia haya ongozeni nchi sisi tumechoka.

  Hawa kwa sasa hawafai hawafai hawafai si hasha baada ya kupokea posho ya vikao vya bunge ukawaona wanachanganyika na wanaCCM kucheza na kufurahia mavuno ya posho baada ya kikao kisichokuwa na Faida kwa WaTanzania.Yaani hawa akina Lipumba na genge lake wanakuwa wasomaji wa mazungumzo baada ya habari

  Ni lini mlimuona Odinga na wenzake kuchanganyika na wa Kibaki kucheza na kufurahi hata baada ya muafaka , Odinga kila anapoonekana anakuwa ameuchuna tu hana wakati wa kucheka na hajawahi hata siku moja kumwita Kibaki Mheshimiwa ,je hawa akina Lipumba na genge lake ,kwa kweli hawaeleweki mara muheshimiwa mala wanaonekana kupongeza ,mala wanaunga mkono kwa kweli hapa tulipo hapawafai kabisa naona wakae pembeni na kusubili ili wawapishe wenye hasira na nchi hii kama Odinga na Kenya.Hacheki mtu ndipo tutaeleweka na CCM.
   
 4. N

  Ndjabu Da Dude JF-Expert Member

  #4
  Aug 29, 2008
  Joined: Aug 29, 2008
  Messages: 3,652
  Likes Received: 409
  Trophy Points: 180
  Hawa ndiyo kama yule fisi mwenye tamaa anayefuata na kunyemelea mtu anayevinjari bushi akisubiri mkono uanguke autafune, au siyo?
   
 5. Mwiba

  Mwiba JF-Expert Member

  #5
  Aug 29, 2008
  Joined: Oct 23, 2007
  Messages: 7,606
  Likes Received: 215
  Trophy Points: 160
  Haijambo hata huyo fisi akikuona umezubaa anaweza akajikaza na kukulukia akihakikisha anaondoka japo na kiganja.

  Hawa viongozi wa Upinzani tulionao hawana msimamo ,kwa maana unapokuwa mpinzani ni mwiko kuunga mkono kwani ukishafanya hayo ya kuunga mkono na kupongeza tayari unakuwa umeshapoteza sifa ya kuwa mpinzani.

  Lipumba na genge lake ni kama walowezi waliovamia wananchi wanaotaka mabadiliko lakini hutumia migongo ya wananchi hao kujipatia riziki,genge ambalo linakaa mezani na Chama tawala kupanga mikakati na kuipitisha bungeni ,hivi genge la akina Lipumba limekosa kuukwamisha japo msaada mmoja ? Inamaana wameunga mkono miswaada yote ,sasa nini faida yao kila kitu wameunga mkono hivi upinzani upo wapi ?
  Si kama mlivyosikia wameisifia hotuba ya Pinda tena wote ,nawashangaa.
   
 6. N

  Ndjabu Da Dude JF-Expert Member

  #6
  Aug 29, 2008
  Joined: Aug 29, 2008
  Messages: 3,652
  Likes Received: 409
  Trophy Points: 180
  Sasa huoni fisi akijaribu kufanya hivyo si inakuwa murder case tena mjomba, au vipi? Maana ni kwamba, jee ubavu huo fisi anao kweli? Hata kwenye tamthilia fisi (wapinzani) sifa yake kubwa ni ile ya woga tu siku zote dhidi ya binadamu (CCM), au unasemaje?
   
 7. Liz Senior

  Liz Senior JF-Expert Member

  #7
  Aug 30, 2008
  Joined: Apr 19, 2007
  Messages: 485
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Kuna wakati mwingine mimi huwa nashindwa kuelewa, pengine ni ufinyu wangu wa ueledi naomba nisamehewe kwa hilo. Hivi tunapowapiga mawe hawa viongozi wa upinzani wanapofanya mambo km haya..nikimaanisha kuanzisha mijadala na kueleza kile wanachokiona kuwa ni udhaifu katika uongozi tuliona na sisi tukawapuuza kila mara na kuona ni wasaliti, ni mpaka nani aseme ndio tutaona ni sawa wanachosema? Kwa nini kila mara tumekuwa wepesi sana kuwarushia madongo hata pale wanapokujaribu kufanya ulio wajibu wao? Hivi ni mpaka Slaa na Zitto waseme jambo ndipo linakuwa la kusikilizwa? Hebu tuwe wakweli kidogo lets think with our brains and not our hearts here.

  Prof. Lipumba akisema jambo na Hamad vile vile ooooh walowezi...wanatumia wananchi kupata something wakinyamaza ooooh wako wapi hao wanaojiita wapinzani. Sisi tunaposema sana humu ndani je? hatufanyi hilo hilo? Hatuwatumii wananchi kupata maneno marefu yasiyowafikia wasiomo humu? Tumetimizaje wajibu wetu? Tumewafikia watanzania wangapi kuwaeleza maana halisi ya mfumuko wa bei na adhari za uongozi huu wa kishkaji. Lets play our part! Tuwape nafasi na kama hatuwaamini basi tujitokeze tuanzishe mijadala kama hiyo kwa uwazi zaidi tukutane na wananchi tuzungumzie hatima ya nchi yetu. Otherwise hata sisi ni walowezi tena walowezi wenye woga
   
 8. Mwiba

  Mwiba JF-Expert Member

  #8
  Aug 30, 2008
  Joined: Oct 23, 2007
  Messages: 7,606
  Likes Received: 215
  Trophy Points: 160
  Ni sawa kabisa unayosema ,kama wao wamekubali kuwa viongozi wa kuongoza vyama vya upinzani basi wawe ni wapinzani tu ,hakuna kuunga mkono wala mguu Chama tawala na hiyo ndio kasi ya gurudumu la upinzani unatakiwa kwa kila hali utoe pumba katika Chama tawala ,yaani ni upinzani tu ila hakuna kurushiana ngumi ndivyo vyama vya upinzani vinavyofanya kazi huko maulaya, husikii kuunga mkono wala miguu ,ni upinzani mbele kwa mbele.
  Kwani kuunga mkono Chama Tawala ni kuwayumbisha wananchi ,nionavyo matarajio ya wananchi ni kuona msimamo wa vyama vya upinzani hauonyeshi huruma kwa Chama tawala.

  Leo CCM ni chama tawala lakini siku kikianguka basi ndio siku nitakapo kuwa nao pamoja na kukikuna chama kitakachofanikiwa kuwepo madarakani.
  Mkae na kufahamu kuwa mimi sitakuwa mpiga kofi wa Chama tawala chochote kile na hii haimaanishi kwamba sieleweki hapana wandugu ,nipo nao katika ujenzi wa taifa kwa kasi na ari mpya. Sitokubali kuwa mfano wa wabunge hawa tulionao baada ya kumaliza kikao na kupewa posho yao wanakaa pamoja na kushereheka kwa muziki ,yaani utafikiri wamefanikiwa kumkwamua Mtanzania na maisha yanayozidi makali.

  Wanachokifanya wabunge ni dharau kwa wananchi haswa na wale wa upinzani wanaposhiriki katika diskobunge ambalo mafisadi na wapokea posho hukusanyika na kufurahia kwa kumalizika msimu wa mavuno.

  Chama tawala kimefanikiwa kuliteka bunge kwa kuwawekea mradi wa posho nono ,hii ndugu zangu WaTanzania ni rushwa kwa style fulani na ndio inayowanyamazisha wabunge wengi pale bungeni ,si mnasikia kuna wabunge kazi yao kucheka na kupiga makofi kama haitoshi wanaongeza na kugonga meza , hivyomnategemea watu hawa kuwakoromea wala rushwa wakati Serikali na Chama chake tawala kinawapa rushwa kupitia mgongo wa posho.
  Hivi mnaelewa kikao cha siku moja tu posho ya mbunge ni kiasi gani halafu uliza yule polisi anaewekwa pale benki kulinda kwa siku anapokea kiasi gani ?
  Mlinzi yule yupo pale na roho yake mkononi au sio ,fikirieni mnapojaribu kuwajadili hawa wabunge na wabunge wa kundi la upinzani.
  Sasa hebu waondoleeni posho nono (Posho iwe calculated ,chai ya asubuhi ,chakula cha mchana na chakula cha usiku na gharama ya nyumba ya kulala ambayo watalipwa baada ya kuwasilisha risiti zenye mhuri wa hoteli aliyolala) ,mishahara ilingane na wafanyakazi wengine ,iwepo heshima au ruzuku ya kuwa yeye ni mbunge labda isizidi kiwango cha chini cha Mshahara ambacho kitakuwa fixed kwa wabunge wote. Yaani uwepo uwiano fulani na kima cha mshahara cha waajiriwa wengine.
  Sikwambii baada ya kumaliza tamu ya kuwepo bungeni eti anachotewa mamilioni hayo yaliopo eti kiinua mgongo ,kuna watu wamemaliza kazi sehemu nyengine kiinua mgongo chao imekuwa mbinde kukipata ,wabunge kila usiku wanajimwaga kwa disco siku tu kikao kinapomalizika au kufungwa.
   
 9. Liz Senior

  Liz Senior JF-Expert Member

  #9
  Aug 30, 2008
  Joined: Apr 19, 2007
  Messages: 485
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33

  Mwiba: Hayo hapo juu ndio yanayonichanganya! Na hapo najiuliza Je sisi tumefanya nini? Je tumetimiza wajibu wetu? Kwani haki ya wewe kupishwa kufanya mambo tofauti na wanayoyafanya viongozi hao wa upinzani imeshikiliwa nao? Kwanini kusubiri wageuke Raila wakati wewe unaweza kuwa Raila km unaamini hilo ndilo sahihi? Kwani wao wakifanya hivyo wafanyavyo na wewe ukaanzisha mchakato tofauti nao kufikia lile lengo ambalo unaamini tunalitarajia itakuwa vipi? Mimi nafikiri wao wamefanya kwa namna yao nawe kama mtanzania mkerwa na hali hii ya maisha "bora kwa kila mtazania" unapaswa kutimiza wajibu wako. Kama leo viongozi wapinzani wameonekana fisi na wapo hadharani je sisi tuliopo hapa kijiweni tutakuwa nini? au ndio tutakuwa viumbe wale wanaoficha mikia wakishtuliwa? Hata hivyo bado sijamsikia Lipumba akipongeza kazi ya Mkulu.

  By the way wenye hasira wa kupishwa wapo wapi? Kweli mwenye hasira anauliza njia ya kupishwa? Unadhani Kenya waliomba kupishwa? Wangeombwa kupishwa wasingekuwa walipo leo. Haya ni maoni yangu
   
 10. Mwiba

  Mwiba JF-Expert Member

  #10
  Aug 30, 2008
  Joined: Oct 23, 2007
  Messages: 7,606
  Likes Received: 215
  Trophy Points: 160
  [​IMG] Ni baada ya posho.
   
Loading...