Magazetini
JF-Expert Member
- Aug 16, 2014
- 593
- 1,713
Mwenyekiti wa CUF Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi wa gazeti hili. Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Elias Msuya, Mwananchi
Jumatatu,Agosti 18 2014 saa 7:56 AM
Kwa ufupi
Sisi tunao wabunge na wawakilishi kutoka Zanzibar wa vyama vyetu na hawakwenda hata kwenye vikao, tukiwajumlisha tunahitaji watu 14 kutokana na wale wajumbe 77 (wa Zanzibar) wa Kundi la 201 na kule tuna uhakika wa watu kama 21
Dar es Salaam
Wakati mchakato wa Katiba mpya unaendelea mjini Dodoma na suala la theluthi mbili likisumbua vichwa vya wengi, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kuwa kura za wajumbe 14 kutoka Zanzibar ndizo zitauokoa au kuukwamisha mchakato huo.
Profesa Lipumba alikuwa kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kuhusu mustakabali wa mchakato wa Katiba baada ya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia kuhudhuria vikao.
Kundi hilo lilisusia vikao Aprili 16 kwa madai kuwa Bunge lilipoteza mwelekeo kwa kuacha kujadili Rasimu ya Katiba, hasa katika suala la muundo wa serikali ya Muungano na kwamba chama tawala, CCM kiliingiza suala la serikali mbili ambalo halimo kwenye rasimu hiyo badala ya serikali tatu.
Kutokana na uamuzi wa Ukawa, ambayo inaundwa na wajumbe kutoka CUF, Chadema, NCCR Mageuzi na baadhi wa kundi la 201 kutoka taasisi mbalimbali za kijamii, kuna shaka kwamba mchakato huo huenda usifanikiwe kutokana na ukweli kuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inataka uamuzi upitishwe na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara na idadi kama hiyo kutoka Zanzibar.
Kutokana na utashi huo wa kisheria, Profesa Lipumba alisema wana uhakika kuwa Katiba haitapita kwa kuwa wanao wajumbe 14 kutoka kundi la 201 ambao ndiyo tegemeo lao.
"Sisi tunao wabunge na wawakilishi kutoka Zanzibar wa vyama vyetu ambao hawakwenda hata kwenye vikao. Tukiwajumlisha, tunahitaji watu 14 kutokana na wale wajumbe 77 (wa Zanzibar) wa Kundi la 201 na kule tuna uhakika wa watu kama 21," alisema.
"Wapo baadhi waliokwenda kuhudhuria vikao, lakini tunajua misimamo yao. Tunajua kuna mbinu zinafanyika kuwarubuni, lakini tunawafuatilia kwa karibu."
Alisema kuwa Ukawa wana uhakika pia wa kuungwa mkono na wabunge na wawakilishi wa CCM kutoka Zanzibar katika kutetea mamlaka ya Zanzibar.
"Kama mnafuatilia mazungumzo ya Baraza la Wawakilishi, katika malalamiko ya suala la Muungano, mazungumzo ya CUF na CCM yalikuwa yanafanana na hata ule waraka uliopelekwa bungeni kutoka CCM Zanzibar ambao sasa wanaukana, unataka mamlaka tatu. Maana yake nini? Mamlaka ni Serikali," alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
"Hata kura zitakapopigwa, CCM hawawezi kupata theluthi mbili za upande wa Zanzibar. Suala la Katiba ni suala la maridhiano."
Aitetea Tume ya Jaji Warioba
Huku akitetea uamuzi wa Ukawa kutoka nje ya Bunge la Katiba, Profesa Lipumba ametaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na rasimu iheshimiwe kwa kuwa imefanya kazi kubwa.
"Pamoja na kwamba kila kundi lilikuwa na mambo yake katika Katiba, yale mambo ya msingi yaliyoletwa na Jaji (mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph)Warioba na Tume yake tuyasimamie na yaongoze mchakato wa Katiba. Ukiisoma rasimu ile kwa kweli utaona Tume hiyo imefanya kazi kubwa," alisema Profesa Lipumba.
Amewataja makamishna wa iliyokuwa Tume hiyo ya Mabadiliko ya Katiba akisema kuwa utaalamu wao ndiyo umezingatia umuhimu wa muundo wa serikali tatu.
"Kati ya wataalamu waliobobea katika Katiba ni pamoja na marehemu Dk Sengondo Mvungi na Profesa Palamagamba Kabudi. Siyo Profesa Issa Shivji (namheshimu sana huyo, kwani ameandika mengi kuhusu Zanzibar kwamba imebanwa sana)," alisema.
"Lakini, utaalamu wa Profesa Shivji ni sheria za kazi. Ni msomi mwenye uelewa mpana… lakini wanafunzi wake ni wataalamu wa masuala ya Katiba ambao ni Dk Mvungi na Profesa Kabudi ndiyo wameona hivyo.
"Hawa ni wazalendo. Huwezi ukahoji uzalendo wa Jaji Warioba, Jaji Augustino Ramadhani, Joseph Butiku, Dk Salim Ahmed Salim na wengineo."
Utata Bunge la Katiba, NEC
Lipumba amesisitiza kuwa hata Bunge hilo likiendelea na vikao vyake, bado Katiba ya wananchi haitapatikana kwani haitakuwa na maridhiano ya kisiasa.
"Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar, Abubakar Bakari hayumo katika Bunge Maalumu, unajadili vipi Katiba? Huwezi kupata Katiba bila maridhiano ya kisiasa ya Wazanzibari, hakuna maridhiano ya kisiasa. Kwa hiyo, tunataka mchakato usitishwe," alisema.
Kwa upande mwingine, Profesa Lipumba alisema kuna mikanganyiko mingi katika Bunge hilo pia kukiwa na utata wa kufanyika kwa kura ya maoni kutokana na maandalizi hafifu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
"Tume ya Uchaguzi ilivyo sasa, hata Daftari la Wapigakura wanasema hawana, wameshafuta vitambulisho vya kupigia kura. Wanasema wataliandaa ifikapo Septemba wakati hadi tufikie kwenye Uchaguzi Mkuu 2015 tuna mwaka mmoja," alisema.
Aliongeza: "Halafu wanachanganya mambo, leo utasikia mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta anakutana na jamii ya wafugaji. Kwamba wafugaji hawamo kwenye rasimu?
"Tunafahamu Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeeleza katika ripoti zao kwamba mambo hayo yote walikuwa nayo, lakini hawakuyaweka kwa kuwa hii ni Katiba ya Muungano.
"Mambo ya ardhi, serikali za mitaa hayakuwekwa. Sasa, utaletaje mambo ya Tanzania Bara yaamuliwe na Wazanzibari wakati wana Katiba yao? Hata ile mantiki iko wazi tu," alisema Profesa Lipumba.
CHANZO: Mwananchi