Kweli, mikopo elimu ya juu inakwenda kusiko

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
269
Jana gazeti hili lilichapisha habari iliyomkariri Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa akiiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kubadilisha mfumo wa utoaji mikopo, kwani mfumo uliopo hivi sasa unawanufaisha watoto wa vigogo na matajiri.


Yamekuwapo malalamiko mengi kutoka kwa wanafunzi wa elimu ya juu kuhusu suala hilo kwa muda mrefu sasa, kiasi kwamba imefika wakati wadau wa masuala ya elimu wakawa na dhana kwamba suluhisho la tatizo hilo haliwezi kupatikana kwa sababu hakuna utashi wa kisiasa. Malalamiko ambayo yameikuza dhana hiyo yanatoka kwa wanafunzi wanaotoka katika familia maskini ambao wanadai kwamba bodi hiyo ya mikopo haiwatendei haki kwa vile watoto wa vigogo na matajiri ndio hasa wanapewa mikopo ya asilimia 100.

Madai hayo sasa yanaonekana kuungwa mkono na Waziri Kawambwa ambaye aliwaambia wajumbe wa bodi hiyo ya mikopo katika kikao chao juzi kuwa ni kweli kwamba wanafunzi wengi wanaopata mikopo ya asilimia 100 ni watoto wa matajiri, vigogo, maprofesa na madaktari.

Alisema kuwa kwa mujibu wa mfumo wa mikopo uliopo hivi sasa, ili mwanafunzi awe na sifa ya kupata mkopo wa asilimia 100, lazima apate daraja la kwanza au la pili, na akaongeza kwamba wanafunzi wenye mazingira ya kufaulu kwa viwango hivyo ni watoto wa mawaziri, matajiri, maprofesa na madaktari, lakini sio watoto wa wafugaji, wakulima na walalahoi.

Sisi tunakubaliana na Waziri Kawambwa kwa asilimia 100 kwa sababu amesema kile ambacho viongozi wengi, wakiwamo waliomtangulia katika wizara hiyo, walikuwa wanashikwa kigugumizi kukizungumzia. Ni kweli kwamba mtoto wa mlalahoi au wa mfugaji na mkulima, hata kama atakuwa na akili za kuzaliwa, hawezi katika mazingira anayoishi kupata nyenzo za kumuwezesha kufaulu katika viwango vilivyoainishwa hapo juu. Pamoja na kwamba hutokea hapa na pale mtoto wa mlalahoi akafaulu katika viwango hivyo, hilo huwa jambo ambalo ni nadra sana na sababu zake zinaweza kuelezwa kirahisi.

Ni kweli kuwa mtoto wa mlalahoi hana chake katika mfumo hasi wa elimu tulionao katika nchi yetu. Ni mtoto wa kigogo, yaani mtoto wa waziri au wa rafiki yake, mtoto wa tajiri na watu wenye kipato cha juu na maisha bora, wakiwamo maprofesa, madaktari, wabunge, viongozi wa juu serikalini na wengineo wenye ushawishi mkubwa katika jamii, ndio anayewezeshwa na kuweza kufaulu kwa viwango vya daraja la kwanza na la pili.


Baada ya kufutwa kwa Azimio la Arusha, mfumo wa elimu -- kama ulivyo wa uchumi -- ulibadilika kutoka kwenye miliki ya umma na ukaangukia kwenye miliki ya wenye fedha, kwa maana ya kutumia ukwasi kuhakikisha kwamba mifumo hiyo inafuata dira na matakwa ya wenye fedha. Mtanzania wa kawaida alibaki hana chake.

Ni katika muktadha huo suala la mikopo kwa watoto wa walala hoi linapaswa kuangaliwa, kwani kama tulivyosema hapo juu, mifumo ya elimu na utoaji mikopo inawapendelea watoto wa vigogo ambao ndio wanashinda mitihani kwa viwango vya juu, hivyo kustahili kupewa mikopo ya asilimia 100. Ni watoto hao ndio wanaopata tuisheni, usafiri wa uhakika, lishe bora, walimu bora, shule nzuri na nyenzo muhimu kama vitabu na madaftari. Ndio hao wanaopata nafasi katika hosteli za vyuo vikuu kwani wana uwezo wa kutoa rushwa ya Sh 300,000 kwa chumba.

Sisi tunasema kuwa agizo la Waziri Kawambwa la kuitaka bodi hiyo ya mikopo kubadili mfumo wa utoaji mikopo litekelezwe haraka kwani ndilo suluhisho la tatizo la mikopo kwa watoto wanaotoka katika familia masikini. Tunampongeza tena waziri huyo kwa kubuni wazo zuri ambalo litaufanya mchakato mzima wa utoaji mikopo kwa wanafunzi uwe endelevu.
 
Back
Top Bottom