Kwanini mawaziri wanazomewa, wapinzani wanafagiliwa?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,820
287,886
Kwanini mawaziri wanazomewa, wapinzani wanafagiliwa?

Mwandishi Wetu


KWA mtu anayefuatilia taarifa za mikutano ya mawaziri mikoani, walikokwenda kutetea ufisadi, bila shaka atakubaliana nami kuwa wamechemsha na kutia aibu.
Kwanza wanasema uongo wazi wazi. Hebu soma nukuu hii ya mtu mwenye shahada ya uzamili, PhD, Juma Ngasongwa na mwingine kadhalika mwenye shahada hiyo hiyo, Emmanuel Nchimbi.

”Hao wanaosema serikali ilisaini haraka ikasahau masilahi ya nchi, jambo hili ni propaganda. Hili nalikanusha mbele yenu, si kweli. Hawa watu walijuaje jambo hilo wakati hawakuwa London? Tulioingia nao mkataba ni wakazi wa Canada. Kusainiwa London ilikuwa rahisi, kwa sababu waziri na rais walikuwa London.” alisema Dk. Juma Ngasongwa.

Nimeshuku usomi wa mtu huyu kutokana na nukuu hii na sababu isiyo na mashiko anayoitoa. Anashangaa watu walijuaje mambo ya mkataba iwapo hawakuwa London! Anashangaza na kusikitisha.

Watu wanajua mambo ya mwezini hata kwenye sayari ya Mars, yeye anashangaa ya London ambapo ni mwendo wa saa tisa tu! Kukanusha si kusema nakanusha, bali kueleza ukweli pale wenzio waliposema uongo.

”Ilikuwa rahisi kusaini katika ubalozi wetu pale London. Pale ni kwetu, hakuna tofauti na hapa nchini na si hotelini kama wanavyopakaza.”

Anaendelea kusema daktari huyu kuwa wapinzani wanawahadaa watu kuwa mkataba ulisainiwa hotelini wakati ni kwenye ubalozi wetu. Hivi waziri huyo alijiandaa kuongea au aliamua kujisemea kama kina Kindunge, Marumaru na Mgosi?

Je, anadhani Watanzania walioko mikoani ni mabung’a, hawajui kuwa mkataba ulisainiwa hotelini hata kama ni London? Je, mtu kama huyu anayetumia kodi yetu kutudanganya na kutufanya mataahira, si fisadi wa kimawazo?

Kwanini serikali inafuja pesa yetu kugharimia jinai ya uongo na kuungana kutetea ufisadi? Je, kwa uongo mwepesi kama huu CCM itaweza kuondoa sumu ya wapinzani? Je, wananchi wakijua wanageuzwa majuha watalaumiwa wakiamua kuwatimua hata kwa mawe?

Hebu soma mauzauza mengine haya kutoka kwa mtu mwenye shahada ya udaktari na uwaziri juu yake.

“Huyu Slaa si mzalendo kwani haiwezekani mtu wa familia moja uende nyumba ya pili kusema nduguzo wasipewe chumvi,” alisema.

Kwanza huyu anaonekana kuwa na mawazo ya utegemezi. Kwake serikali omba omba inayomiliki watu, wanyama, mito, madini na kila utajiri ni sawa! Je, huyu kweli kaelimika au kapitia madarasani tu na anaweza kuchangia chochote kwenye kumkomboa Mtanzania? Je, huyu si msomi wa karatasi sawa na chui wa karatasi wa mwenyekiti Mao? Kwake uzalendo ni kufuga madhambi na kulindana! Kwanini iwe vibaya kumtahadharisha jirani yako na mtu anayemjua kuwa ni kibaka?

Daktari huyu anayetia shaka ithibati ya elimu yake, siku moja kabla ya kutoa kauli hii, alikaririwa akidai kuwa kila mmbea nchini anaitwa Slaa, akimaanisha Dk. Willibrod Slaa.

Kwanini hawa watu wanashindwa kutumia busara? Kwanini hawajiulizi ni kwanini wanazomewa na kugunwa ilhali kina Slaa kila wanapokwenda wanapokewa vizuri hadi kumfanya Katibu Mkuu wa CCM Yusuf Makamba, kuona kijicho na kuwahimiza watu wasiwapokee kishujaa?

Kwanini wanakuwa wagumu wa kujifunza? Hivi hawajishangai wananchi wanavyowashangaa kwa kuunguza pesa yao kwenda kutetea kikundi cha watu wanaojulikana kwa ufisadi wao ambapo kama wangekuwa wanasingiziwa wangeachia ngazi na kusafishwa na vyombo husika? Wanadhani wananchi hawajui kuwa wakati wao wakitumia kisingizio cha kuondoa sumu ya wapinzani kuwaibia wananchi kwa kujilipa nights na posho nyingine, kina Slaa wanatumia kidogo walichonacho?

Ukipitia upuuzi unaofanywa chini ya dhana ya kuondoa sumu ya wapinzani, unagundua aina nyingine ya ushirika katika jinai (conspiracy) nzima ya ufisadi. Kwanini mawaziri ambao hawakutuhumiwa wawe na uchungu wa kutetea visivyotetewa kiasi cha kuongea vitu visivyoingia hata kwenye akili ya kuku? Ndiyo. Kwanini muda na rasilimali zinazochezewa kwenye usanii huu zisielekezwe kwenye kutoa huduma muhimu za jamii ambapo kwa nchi yetu ni mbovu na sehemu nyingine hakuna?

Je, kwanini CCM isiitwe chama cha mafisidi? Maana wanapotuhumiwa watu binafsi badala ya kuwabana hata kuwawajibisha, kiko tayari hata kuhatarisha usalama wa nchi kwa kuchota pesa na kuzitumia kuwatetea bila kufanikiwa?

Je, huku ndiyo kuishiwa kwa CCM? Maana kwa mtu anayeona na kusikia wanayosema hawa “Watetezi njaa” yasivyoondoa sumu bali kuishindilia kwenye nyoyo za waathirika, anashangaa busara inayotumika kuendelea kufanya ziara hizo!

Kwanini CCM imeshindwa kumsaidia Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete jinsi ya kuendesha nchi na kutatua matatizo ya nchi yetu ambayo amekiri hivi karibuni kuwa hajui chanzo cha umaskini wala afanye nini?

Alikaririwa mjini Paris akisema: “Hata mimi sielewi. Hili ni swali ambalo hata mimi huwa najiuliza kila siku, ni nini ambacho hatujafanya? Nafikiri tunaongoza barani Afrika katika kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini,” alisema Jakaya Kikwete.

Je, kwa mtu mwenye mawazo namna hii anaweza kukushawishi kuwa kuna anachojua katika kutatua matatizo ya nchi, ukiachia mbali ule utani wa kwenda Kanani? Kama mkuu wa serikali hajui sababu wala la kufanya, anaendeshaje nchi?

Anakiri kuwa Tanzania inaongoza kuvutia wawekezaji. Anashindwa kufahamu kuwa kuvutia wawekezaji pekee bila ya kuwapo usimamizi bora na uadilifu, haviwezi kufua dafu, zaidi zaidi vitaongeza matatizo kama ilivyo sasa.

Amekuwa akipewe mfano wa Botswana ambayo haitufikii kwa wingi wa madini hata wawekezaji. Lakini anashindwa kujifunza kuwa Botswana wamefika walipofikia kutokana na uzalendo na uadilifu, tofauti na upanya na ufisi unaoendelea nchini mwetu.

Tuzidi kudurusu nukuu ya Kikwete.

Je, licha ya kubabaisha mtu wa namna hii hawadanganyi wananchi? Maana ukimsikia majukwaani, anasema maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezakana. Lakini akitoka anakuja na nukuu ya kukata tamaa na ya kutojua kitu kama hiyo hapo juu! Huyu hajachanganyikiwa na kuzidiwa kweli?

Ukisoma nukuu hiyo ukaunganisha na alivyowaita watendaji wake kule kwenye semina elekezi Ngurdoto, unapata jibu kuwa kumbe CCM imeamua kutumia matukio kutumalizia pesa.

Maana kama hajui anachopaswa kufanya huku akituaminisha kuwa kule Ngurdoto alikuwa na mkakati wa kutukwamua, inatia shaka kama anaelewa anachosema. Hili linahitaji makala nzima.

Tukirejea kwenye ziara ya kikosi cha maangamizi cha kutetea ufisadi cha CCM, kusema ukweli hakuna la maana ambalo kimeishafanya, zaidi ya kuchochea hasira za umma. Kwanini CCM haisomi maoni ya wananchi na nyuso za wauliza maswali, hata maswali yenyewe yanayoulizwa?

Je, CCM inajua na kuona ukweli kuwa haina bao, inaamua kuendelea kuvuruga kwa vile uwezo wake wa kufikiria unazidi kupungua kutokana na kuwa na viongozi wanaotokana na mifuko yao badala ya ithibati na uwezo wao?
Kuna haja ya kuisaidia CCM kuelewa kuwa kama itaendelea kuwa kokoro la kukumba kila vinyama vya baharini, vingine vitaiozesha zaidi ya ilivyooza kiasi cha kuimaliza kabisa.

Loe mtu mwenye akili timamu unashangaa kwanini CCM inachelewa kujirekebisha, hata kujitutumua kutetea ufisadi. Unashangaa kama kweli chama kimebaki na ‘think tunk’ badala ya ‘think junk!’ Maana wakati wa Mwalimu uvumi kidogo kuhusu mkakati wa chama ulitosha kubadili uelekeo haraka. Na hii ndiyo siri ya ufanisi wa mwalimu kisiasa.

Tuhitimishe kwa kulaani ufujaji wa pesa na muda wetu kwa kutulisha uchafu na uongo vinavyofanywa na wanaoitwa mawaziri.


Nkwazigatsha@yahoo.com
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom