30 Juni, 2019
Nakuandikia nikiwa nimeguswa sana na hatua zilizochukuliwa dhidi yako za kukuondolea ubunge.
Imeniuma kama ilivyowauma Watanzania wengine ambao wanakumbuka kupigwa kwako risasi nyingi mwilini tarehe 07 Septemba, 2017. Maumivu na uchungu wa unyama ule sio jambo ambalo linatarajiwa binadamu kumfanyia binadamu mwenzake.
Wapo wanaoshambuliwa na kufa papo hapo na wengine kufa baadaye, lakini kwa Tundu Lissu, Mwenyezi Mungu amenyoosha mkono wake upo hai mpaka leo ukiwa umepitia matibabu makubwa ya upasuaji mara kadhaa ili kutengeneza viungo vyako vya mwili.
Napomshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai wako, pia nawashukuru Madaktari wote kuanzia wa Tanzania, Kenya na Ubelgiji ambao wamefanya juhudi kubwa kunusuru maisha yako na kwa upendo wa Mungu upo hai mpaka leo na tunakusikia tena ukinena.
Kwa sisi wacha Mungu uhai wako mpaka leo ni zawadi kutoka kwa Mungu na ni upendeleo mkubwa kwako na kwa sisi tunaokupenda. Kwa sababu wapo waliopigwa risasi na sasa wapo ardhini wamezikwa.
Juzi Spika wa Bunge Job Ndugai ametangaza kufutwa kwa Ubunge wako, hii ilikuwa inahitimisha majibizano ya mara kwa mara yaliyoanza tangu ulipopata nafuu na kukuwezesha kuzungumza. Ilikuwa ni hatua ya uchungu mwingine mkubwa kwetu tulioona dhahiri inakuumiza zaidi. Kwamba kwa kutokuwa Mbunge sasa hata stahiki za ubunge hutopata tena.
Jambo hili ni chungu sana.
Ninalo neno la kukwambia na ninaomba ikikupendeza na wote wanaonisikiliza ikiwapendeza tulisome.
Haina mashaka kwamba jambo ulilofanyiwa halikupaswa kabisa kufanyiwa siasa, ni uhalifu dhidi ya uhai wa binadamu, lakini kwa bahati mbaya sana, narudia kwa bahati mbaya sana wewe mwenyewe na jamaa zako wa chama chako cha siasa mkaanza kutumia mashambulizi dhidi yako kama ajenda ya kujijenga kisiasa dhidi ya wapinzani wenu wakubwa ambao ni chama cha mapinduzi CCM ambacho ni chama tawala.
Nasema tena ni bahati mbaya sana kosa hili ulikubali kulianzisha wewe mwenyewe na wenzako wa CHADEMA. Kwa hesabu za kawaida kuanzia pale binafsi nilijua kwa sababu mmelipeleka huko basi CCM wasingeweza kukaa kimya ili muwamalize hasa wakati huu tunapoelekea chaguzi.
Kauli zako ulizokuwa unazitoa ukiwa kitandani zilivumiliwa kidogo na mara kadhaa CCM wenyewe walisikika wakisema hawawezi kujibizana na mgonjwa. Hata jamaa zako wa CHADEMA walipojaribu kuchokonoa walivumiliwa kwa mazingira hayo hayo.
Kana kwamba hiyo haitoshi ukaamua kufanya ziara ya nchi za Ulaya na Amerika ukifanya jambo hilo hilo la kuwasulubu CCM na Serikali kimataifa kwa mahojiano yaliyojaa mbwembwe nyingi na kashfa nzito dhidi ya Rais, Spika na CCM kwa ndio waliokushambulia kwa sababu walitaka kukudhibiti usiwaseme. Uliapa kuwa utawamaliza kwa kueleza walichokufanyia.
Kwa wenye akili tukaona hapa sasa ajenda imehama kutoka mgonjwa kwenda mpambanaji.
Wewe mwenyewe na wenzako wa CHADEMA mkaendelea kushinikiza taasisi mbalimbali za kimataifa ziinyime ushirikiano Tanzania ikiwemo fedha za miradi ya maendeleo na mkafanikiwa kwa kiasi fulani. Kwa wenye akili tukajua hapa mtawapoteza wafuasi wengi wanaoelewa madhara ya kampeni hii.
Wewe mwenyewe na wenzako CHADEMA mkatamka mara kadhaa kuwa hamjali kuhusu gharama za matibabu yako, kwamba mtalipa na mkaitisha harambee Watanzania na wengine wachange fedha za matibabu yako. Wenye akili tukajua hapa mnakwenda kupoteza nguvu muhimu ambayo ni fedha kwa matibabu na ustawi wa siasa zenu.
Na mengine mengi mengi.
Yote haya mlikuwa mnafanya juhudi ya kuishughulikia Serikali, Spika, Rais na vyombo vya dola vya Tanzania ambavyo mmevichafua sana kimataifa.
Umefanya yote hayo ukiwa unafahamu kuwa pako mahali ambapo unaowashughulikia wanaweza kulipa kisasi. Ukiwa unajua kuwa unabanwa na sheria za mwajiri wako ambaye ni Bunge, ukiwa unajua kuwa unamchafua anayetoa fedha za matibabu yako, ukiwa unajua unaowachafua wanao uwezo wa kukuondoa katika kiti chako cha ubunge na wakatangaza jimbo lipo wazi na litagombewa na wengine ili wananchi wa Singida Mashariki wasikose mwakilishi.
Katika mazingira hayo, ulitarajia nini?
Kwa mawazo yangu kilichosababisha uondolewe Ubunge ni wewe mwenyewe na wenzako ndani ya CHADEMA. Mnadanganyana sana na mmekosa kabisa ubunifu wa kufanya siasa katika mazingira ya sasa. CCM inawashinda na mnamalizika kwa kukosa maarifa.
Leo umefukuzwa Ubunge, muda mfupi ujao atapatikana Mbunge mwingine wa Singida Mashariki na kwa muda wa mwaka mmoja na miezi kadhaa atajijenga kisiasa na kiuchumi, maana yake ni moja tu mwakani kwenye uchaguzi mkuu kama utaamua kuomba tena Ubunge tayari utakuwa una mpinzani anayetetea kiti chake. Haitakuwa kazi rahisi. Hapa umepigwa vibaya sana na sidhani akina Mbowe kama wanakushauri vizuri na nina mashaka kama hawatakutelekeza. Siamini kama wataendelea kukugawia fedha bila kazi ya kufanya na siamini Watakubali kukupisha kwenye nafasi zao ama matarajio yao ya kisiasa.
Najua wapo watakaobeza mawazo haya lakini huo ndio ukweli. Hapa hesabu za kisiasa hazijakaa sawa na sasa ndugu yangu Tundu Lissu umeshaondolewa kwenye ajenda, itakulazimu uanze kupambania kuondolewa kwako na kutafuta huruma ya wananchi wakati jamaa wanasonga mbele.
Na ni kujidanganya sana kwamba katika dunia ya leo utajenga siasa yako kwa kutegemea watu wale wale ambao walitutawala na leo bado wametukalia kiuchumi. Kwamba unalofanyiwa utasema Ulaya na Amerika, ni kupoteza muda, mwisho wa siku Tanzania ni nchi huru inayojiamulia mambo yake yenyewe. Unaweza ukadhani uanasheria wako utakusaidia lakini kumbuka mahakama utakazozitegemea ni za Tanzania, Majaji wanateuliwa na Rais na vyombo vya ulinzi na usalama vipo chini yake.
Labda kama unaamini kwamba Tanzania inaweza kuingia kwenye vita na Taifa fulani kwa ajili yako. Au unaamini kuwa wewe ni mtu bora kuliko mtu mwingine yeyote Tanzania kwamba suala lako ni la kufa na kupona. Mimi siamini hayo yote.
Ninachokiona ni kutaka kukutumia kama mtaji wa kisiasa. Kwamba uendelee kuisema CCM, Serikali, Spika na vyombo vya dola ili ionekane CHADEMA inaonewa. Very poor strategy.
Katika mazingira haya ambayo Serikali ya Rais Magufuli inafanya miradi mikubwa ya maendeleo iliyoshindikana tangu nchi ipate uhuru, inatetea wanyonge na kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii ambayo ndio mahitaji makubwa ya wananchi, siasa hizo zina nafasi finyu sana. Ni kuumizana na mwisho wa siku unaanguka.
Kosa kama hili wamefanya wanasiasa wengi na hawakufanikiwa. Akina Kiiza Besigye, Morgan Tshivhangilai na wengine wengi. Fight against the ruling regime must be smart and productive. Any miscalculation is a serious loss.
Niishie hapo nawatakia Jumapili njema.
H.M Kituta
Mtanzania Mpendahaki.