kwa matamshi yangu ya sasa nilipokuwa kijana niliitwa Chaupele nilipokuwa mtu mzima niliitwa manywele nilipokuwa mwalimu niliitwa BURE.
Huu utakuwa wimbo wako utakapostaafu urudipo nyumbani umelewa kangara na nyayo zako zikishindwa kulenga njia nyembamba vijijini. utakuwa kichekesho kwa watoto watapokuita, ticha! popote upitapo.
kumbuka mwalimu utakapostaafu. mijusi watataga mayai ndani ya viatu vyako vilivyokwisha visigino na ndani ya sidiria chakavu zilizoshikizwa kamba kwa pini. mende watazaliana ndani ya chupa tupu za marashi na za bia.
na manyigu yatajenga ndani ya kofia zilizosahaulika kutani. utakapokufa nge watazaliana chini ya jiwe juu ya kaburi lako, na mlevi fulani akipita atapenga na kupangusa vidole kwenye jiwe pweke. mwanzo na mwisho wako ndio huo.
lakini wakati ungali hai unaweza kubadili mkondo wa maji. lakini kwanza tuzungumze. wewe na mimi. acha mioyo yetu izungumze. baada ya kunyanyaswa na kisha nusu mshahara,
utafundisha tena nyimbo za kusifu viongozi? utafundisha tena ngonjera? utapeleka tena wanafunzi asubuhi wakajipange barabarani kusubiri mgeni afikaye saa kumi, an apitapo apunga tu mkono kuwatia kichaa cha shangwe na huku nyuma mwasambaa na njaa?
tazama rundo la daftari mezani utalimaliza kwa mshahara wa mkia wa mbuzi? tuzungumze. ninyi na mimi. acha mioyo yetu izungumze. mkiwa waoga na kujikunya kama jongoo mtawekwa kwenye kijiti na kutupwa nje ya ua, na ndani mtawaacha wacheza ngoma wakitunga nyimbo mpya.
sikilizeni walimu. anzeni kufundisha hesabu mpya: mjinga mmoja kujumlisha wezi ishirini ni sawa na sifuri. fundisheni historia mpya: hapo zamani za sasa hapakuwa na serikali.
sikilizeni kwa makini. umoja hatuna: twasambaratika kama nyumbu. tulichonacho ni woga, na kinachotuangusha ni unafiki. lakini tusikate tamaa kama mbuni. tukiupata umoja bado tunayo silaha. KURA. SHAIRI HILI LINAPATIKANA KATIKA KITABU CHA "DHIFA"