NASUBIRI
Member
- May 18, 2012
- 10
- 5
KWA NINI WAISLAMU WANAKUSUDIA KUSUSIA SENSA 2012? Ni nini kilichotokea? Ni jazba au wana hoja?Katika gazeti la Tanzania Daima la 16 Juni 2012, mwandishi mmoja aiitwaye Ratifa Baranyikwa aliandika na ninanukuu Mfano mwingine ni huu wa juzi, ambako Waislamu wametangaza kuisusia sensa na sababu wanayoitoa ni kutoridhishwa na majibu ya Wassira, kadhalika ubabe aliowaonesha. Inawezekana kabisa ndugu zangu Waislamu hoja zao zikawa si za msingi, lakini katika kujibiwa, kuna mambo ambayo Wassira alitakiwa kuyaangalia kwa makini.Nimenukuuu mawazo hayo ya mwandishi si kwa nia ya kumjibu bali kuonesha kwamba habari zinazowahusu waislamu huandikwa kwa lengo la kusaidia hoja potofu ya mwandishi au kupotoshwa kabisa. Ni kweli waislamu tunaazimia kususia sensa ifikapo tarehe 20 Juni, 2012 lakini si kutokana na majibu ya Wassira wala ubabe wake aliouonesha kwa waislamu katika mkutano wa Dodoma. Tumeeleza wazi hata kabla ya mkutano wa Dodoma kwamba kutokushiriki au kushiriki kwetu kutategemea kutekelezwa kwa madai yetu ambayo ni kwanza, kutia kipengele cha dini katika dodoso la sensa; pili, kuwepo uangalizi wa pamoja wa wanadini katika zoezi zima la sensa tangu kuhesabu, kujumlisha hadi kutoa matokeo. Jingine la kuundwa upya idara ya takwimu kwa uwiano wa waislamu na wakristo lingeweza kusubiri likafanyika hata baada ya sensa.Mwandishi anatilia anadai hoja za waislamu kwamba hazina msingi. Hivi ili hoja iwe na msingi inatakiwa iweje au itolewe na nani? Inaelekea kuna mazoea kwamba hoja zote zinazotolewa na waislamu hapa Tanzania hazina msingi bali zile za Wakristo au za ma-Padri, Maaskofu na Wachungaji. Waislamu wanadai kurejeshwa kwa Mahakama za Kadhi, hoja zao hazina msingi!. Wanadai Tanzania ijiunge na OIC kwa faida ya watanzania wote kama ilivyo kwa Uganda, Msumbiji na hata Urusi ambayo ina hadhi ya mwanachama mwangalizi (observer membership), hoja zao si za msingi!. Sasa wanataka kiwekwe kipengele kitakachowezesha dini ya mtu ijulikane katika dodoso za sensa, nako pia hoja zao hazina msingi!.Hili linatulazimisha kuandika kuelezea hoja za waislamu katika madai yetu ya kurejeshwa kipengele cha dini katika maswali dodoso (questionnaire) ya sensa. Lakini ili kupata picha nzima, ni vema kuelewa chimbuko la waislamu kudai madai haya katika sensa ya mwaka huu kwani Tanzania huru imeshafanya sensa mwaka 1967, 1978, 1988 na 2002 lakini mbona waislamu hatukudai kipengele cha dini kitiwe katika dodoso za sensa hizo? Madai haya yameibukaje katika sensa ya mwaka huu?Chimbuko la madai ya waislamu kudai kipengele cha dini kitiwe katika dodoso la sensa mwaka huu ni kule kuonekana wakristo wamehodhi nafasi mbali mbali za madaraka nchini kuanzia serikali na idara zake, mashirika ya umma, bunge, elimu n.k kwa madai kwamba wao wako wengi kuliko waislamu. Awali madai ya kuhalalisha dhulma hii yalikuwa wakristo wamesoma kuliko waislamu lakini hivi sasa wanadai wao wako wengi kuliko waislamu. Hii ni kufuatia kutolewa kwa takwimu feki na TBC1 tarehe 26 Aprili, 2012. Hivi leo waislamu wasomi hata kwa daraja za Phd (U-profesa) wako wengi tu lakini bado dhulma hii ya uwakilishi mdogo wa waislamu iko pale pale.Mara ikaibuka hoja kwamba wakristo wanashika madaraka na wana maendeleo makubwa kwa sababu si tu ya kuwa na elimu bali kwa sababu wao ni wengi kuliko waislamu. Hapo wengine tukaanza kufuatilia takwimu za idadi ya waislamu na wakristo nchini. Tulipochunguza takwimu hizo idara ya takwimu tukagundua kwamba sensa ya mwisho iliyokuwa na kipengele cha dini nchini ni ile ya mwaka 1967 ambayo matokeo yake yalichakachuliwa na kuonesha wakristo ni wengi kuliko waislamu kwa kuzidisha idadi ya wapagani (Wapagani 34.3%, Wakristo 33.5% na Waislamu 31.4%).Na hili la kupikwa takwimu, katika kipindi Hamza Kasongo Hour kinachoendeshwa na kituo cha Channel Ten tarehe 17 Juni, 2012 Sharifu Mohamed Yahya wa Tanga, akihojiwa na Bw. Hamza Kasongo, alieleza kwamba katika sensa ya mwaka 1988 idadi ya wakazi wa Tanga iliripotiwa kuwa 1,500,000 na idadi hiyo hiyo ikaripotiwa tena katika sensa ya 2002. Wakazi wa Tanga walihoji iweje hakuna watu walioongezeka lakini hawakupewa majibu yoyote kuelezea usanii huu. Bila shaka wakazi wa Tanga ambao wengi ni waislamu hawakutakiwa kuonekana wameongezeka ili wakristo wawe wengi katika mji huo kiidadi.Ni mambo kama haya ya kuchakachua takwimu kwa maslahi ya wakristo ndiyo yanayowafanya waislamu kutokuwa na imani na idara ya takwimu ya taifa ambayo inafanya kazi kwa maslahi ya kanisa badala ya nchi. Hata takwimu zinazotolewa na makanisa kuonesha idadi yao kwamba wako wengi (mfano tovuti ya Kanisa Katoloki katika RCNet inaonesha wakristo 44%, waislamu 34%) takwimu hizo wanazipata kutoka idara ya takwimu ingawa hakuna kipengele cha dini moja kwa moja bali wameweka kipengele cha kuuliza idadi ya misikiti na makanisa katika eneo ambacho kinawawezesha kupanua (extrapolate) takwimu na kuonesha wakristo wako wengi. Na kwa kutumia idadi ya misikiti na makanisa kama kigezo, wakristo wataonekana kama wako wengi maana kwa waislamu msikiti mmoja tu unawatosha wote kuswali hapo pamoja na tofauti zao ndogo ndogo lakini wakristo watahitaji makanisa zaidi ya moja kwa kuwa wafuasi wa kanisa moja hawaruhusiwii kufanya ibada katika kanisa jingine hivyo lazima kila dhehebu wajenge kanisa lao.Kuweko kipengele cha Dini ni kwa mujibu wa Umoja wa MataifaTukirudi katika hoja za waislamu kutaka kipengele cha dini kiwepo katika dodoso la sensa mwaka huu ni kwamba kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, sensa ya watu inatakiwa kujumlisha si tu idadi yao bali makabila yao, utaifa wao (kama Marekani ambako wakazi wake wanatoka mataifa mengine, dini zao (kwa madhehebu), lugha zao na hata rangi zao (races), angalia www.unstats.un.org. kipengele cha dini kipo katika para ya 2.109 hadi 2.111 ya maelekezo ya Umoja wa Mataifa juu ya sensa ya watu kwa mataifa mbali mbali. Lengo lake ni kuuwezesha umoja wa Mataifa kuwa na takwimu za idadi ya watu zenye mfumo mmoja kutoka mataifa mbali mbali ili kulinganisha (for purposes of international comparability)Kutolewa Takwimu za Uongo za Idadi ya Wakristo na Waislamu hapa nchiniKwa kuwa kunatolewa takwimu za uongo za idadi ya Waislamu na Wakristo nchini ambazo hazitokani rasmi na idara ya takwimu ya taifa, basi pawekwe kipengele cha dini katika dodoso ili takwimu zitakazotolewa sasa ziwe takwimu rasmi. Siku ya Muungano Aprili 26, 2012 TBC1 walitoa takwimu za uongo kuhusu idadi ya wakristo na waislamu kwamba wakristo ni 52% na waislamu 32%. Kalenda zilizotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu na hata kugawiwa mabalozi wa nchi za nje zinaonesha wakristo 45% waislamu 35%. Tovuti ya Kanisa Wakristo 44% waislamu 34%, Tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani 2011 wakristo 62% waislamu 32% na vivyo hivyo vyanzo vingine wakristo ni wengi kuliko waislamu. Mantiki inatwambia haiwezekani watu ambao mwaka 1957 walikuwa idadi yao ilikuwa kubwa kuliko wakristo kwa watu wawili kati ya watatu idadi hiyo ipunguwe ghafla mwaka 1967 (Wapagani 34.3%, Wakristo 33.5% na Waislamu 31.4%).Mwanahistoria bobezi Mohamed Said aliandika Vyanzo tofauti vya takwimu vinatoa takwimu tofauti zinazopingana kuhusu hesabu ya Waislam na Wakristo katika Tanzania. Hii inatokana na ukweli kuwa somo hili ni nyeti. Katika nchi za Kiafrika ambazo zina wafuasi wengi wa dini hizi mbili, kwa mfano Tanzania na Nigeria, uchunguzi wa kuwa ni dini gani ina wafuasi wengi kupita mwenzake ni chanzo cha mgongano na mzozo. (M. Said, Mwalimu Julius K. Nyerere, Kanisa Katoliki na Uislam -Dola na Tatizo la Udini Tanzania).Kinachotokea sasa ni uthibitisho wa maneno haya ya ndugu yangu Mohamed Said kwani kwa nini kipengele cha idadi ya majumba ya ibada kiruhusiwe kuwepo katika dodoso la sensa mwaka huu lakini kipengele cha kumuuliza mtanzania dini yake kisiruhusiwe? Kwa maneno mengine, kwa nini majumba ya ibada yahesabiwe lakini wale wafanyao ibada katika majumba hayo iwe marufuku kuwahesabu? Ni nini kimekusudiwa hapa? Kwa nini serikali inaungana na msimamo wa Makanisa kupinga kuingizwa kipengele cha dini katika dodoso la sensa mwaka huu? Katika dodoso la mwaka huu makanisa yameoneshwa kwa alama ya jengo na msalaba na misikiti alama ya jengo na mwezi na nyota. Kwa kuwa serikali inakubali kuhesabiwa majumba hayo ya ibada, ndiyo maana waislamu tunadai kipengele cha dini kirejeshwe katika dodoso la sensa ili si tu idadi ya majumba ya ibada ijulikane bali pia idadi ya waumini wafanyao ibada katika majumba hayo ijulikane rasmi na sio takwimu za uongo au makisio ya uongo kama ilivyozoeleka.Waislamu hawatoshiriki zoezi la sensa hadi madai yao yatekelezweViongozi wa Kiislamu wamekuwa wakiitaka serikali kupitia idara ya takwimu kurejesha kipengele cha dini katika dodoso la sensa (si kuweka maana bali kuerejesha maana kilikuwepo) kwa hatua mbali mbali na wala hawakukurupuka kama watu wanavyodhani. Kwanza, katika mkutano uliofanyika White Sands Hotel Dar es Salaam kati ya idara ya takwimu na viongozi wa dini. Pili, kupitia barua yao kwa idara hiyo ya tarehe 4 Juni, 2012 ambayo ilieleza wazi kwamba kama hilo halitafanyika hadi tarehe 20 Juni, 2012 waislamu hawatoshiriki sensa. Hatimaye serikali ikaitisha mkutano wa viongozi wa dini mjini Dodoma tarehe 10 Juni, 2012 na ndipo Waziri Wasira alipotoa kauli ya serikali kwamba haitorejesha kipengele hicho kwa madai eti serikali haipangi mipango ya maendeleo kwa kutumia takwimu za dini. Kama maneno hayo ni kweli, kwa nini wameweka kipengele cha majumba ya ibada?Serikali isidhani waislamu ni wajinga. Kama serikali haipangi mipango ya maendeleo kwa kuzingatia dini basi dini hiyo itakuwa ni Uislamu tu kwa sababu tangu serikali za kikoloni mipango ya maendeleo ya serikali inazingatia sana dini ya Kikristo. Mkataba wa Maridhiano kati ya Serikali na Makanisa (MoU) wa mwaka 1992, ni ushahidi wa hili. Kwa mujibu wa mkataba huo, serikali na makanisa huunda tume mbili Tume ya Elimu ya Kanisa ambayo hushughulika na masala ya huduma za elimu chini ya Kanisa na Tume ya Huduma za Afya za Kanisa. Tume hizi zina wataalamu kutoka makanisa na serikalini na kwa pamoja huunda sera za elimu na afya za taifa na mipango ya maendeleo. Haiwezekani mwaka 2008-9 serikali iwe imetoka bilioni 170.1 kwa makanisa pasina mipango ya maendeleo. Kwa hiyo kama serikali haipangi mipango yake kwa kuzingatia dini maneno hayo ni kweli tu kwa Uislamu na si dini ya Kikristo. Tunaamini hii ndiyo sababu serikali haitaki kusikiliza madai ya waislamu kwa sababu kwake ni kupoteza muda tu kwani kilal kitu kinakwenda kama kilivyopangwa kwa mkataba wa serikali na wakristo sasa kuna haja gani ya kujua idadi ya waislamu? Ndiyo maana waislamu tunakataa kushiriki sensa hii kwa kuwa ni kuidhinisha dhulma hizi dhidi yetu tu.Umefika wakati kwa waislamu kujitambua wafanye nini katika kila linalotokea hapa nchini. Hii itatusaidia kupambana na dhulma mbali mbali zinazotokea iwe ni wanafunzi waislamu kudhulumiwa kwenye mitihani yao, kunyanyaswa au ni hili la sensa. Mshikamano wetu ni silaha muhimu sana kwetu. Bila shaka siku iliyowekwa na waislamu itapita pasina kutekelezwa madai yetu ili waone kama tutashika msimamo wetu na pia wapate muda wa kutugawa ili tuanze kupingana na nguvu zetu zidhoofike. Waislamu endeleeni kushikamana kama mlivyoonesha kwa taasisi na jumuiya zenu bali masheikh na viongozi mbali mbali na waislamu kwa ujumla. Mkifanya hivyo wanaweza kuweka kipengele hicho kabla ya siku ya sensa na kama hawakufanya hivyo, msimamo wetu uko pale pale, hatutoshiriki sensa ijayo.