Dr Mathew Togolani Mndeme
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 201
- 808
Maelezo yako marefu mno!View attachment 505420
Mh Waziri Mwijage,
Mapema wiki hii nilimsikiliza Mh Rais Magufuli akiongea na viongozi wa dini aliokutana nao kwenye ikulu ndogo mijini Moshi. Pamoja na mambo mengine aliongelea juu ya tatizo la kuengesha magari katika mji wa Moshi. Wakati akiongelea hili, alichomekea swala la kuegesha magari katika jiji la Dar es Salaam huku akionesha kusikitishwa na kazi hii kufanywa na kampuni ya nje kama wawekezaji. Katika kauli yake alionesha kuchukizwa na jukumu jepesi kama hili kupewa mwekezaji wa nje kama vile hakuna mtanzania ambaye angeweza kutekeleza jukumu hili. Rais alionesha kusikitishwa na aina ya viongozi waliofanya maamuzi ya aina hii.
Juzi nimekutazama bungeni ukijibu hoja za wabunge hasa kuhusu dhana nzima ya uwekezaji wa viwanda. Katika kauli zako ulisisitiza sana umuhim wa wabunge na watanzania kwa ujumla kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda. Maelezo yako na ile kauli ya Mh Rais vilinipa hisia kwamba huenda kuna mambo yanafanyika ndivyosivyo kwa kutokuzingatia mikakati ya uwekezaji tuliyonayo kama taifa. Nimejiuliza maswali matatu:
Mh Waziri, pamoja na kampuni inayosimamia maegesho ya magari aliyoitaja Mh Rais, ninashawishika utakua unafahamu uwepo wa kampuni nyingine ya aina hii nao wakiwa ni wawekezaji toka nje. Hii ni kampuni ya Kimarekani ijulikanayo kama Uber inayofanya biashara ya huduma ya Taxi Dar es Dalaam na ni moja ya uwekezaji wa nje uliofanyika siku za karibuni chini ya uongozi wako. Mh Waziri, dhana ya kukaribisha wawekezaji wa nje kwenye nchi yoyote huwa ina malengo maalumu hasa ya kufanikisha yale ambayo nchi husika haina uwezo nayo. Pamoja na umuhim wa wakezaji w anje, uwekezaji wowote lazima uwe wa kimkakati na uendane na hali ya nchi na changamoto zake huku ukipunguza machungu kwa wananchi wake. Kati ya mambo ambayo nchi mnbalimbali hutazama katika kukaribisha wawekezaji wan je ni pamoja na:
- Hivi sera yetu ya uwekezaji inasema nini kuhusu maeneo ya vipaumbele vya uwekezaji wa nje?
- Ni maeneo gani ya uwekezaji ambayo nchi yetu imeyatenga kama maeneo ya maalum kwa wananchi wake ambayo hatuhitaji uwekezaji wa nje?
- Kama sera ya uwekezaji inayotaja mambo haya ipo, je inajulikana na kutekelezwa kwa kiasi gani na viongozi, watoa vibali vya uwekezaji, na mamlaka za usimamizi?
Mh waziri, mikakati hii na minigne ndio husaidia nchi kutokua soko lisilo na mwenyewe na kujaza kila aina ya uwekezaji hata usio na tija na wenye lengo la kukomba rasilimali za nchi. Nchi nyingi duniani (tajiri na maskini) zimejiridhisha kwamba haziwezi kufikia maendeleo ya kweli ya watu wake kwa kutegemea uwekezaji na wataalamu toka nje ya watu wao. Na kwa minajili hili, wana mikakati ya kitaifa ya kulinda rasilimaliza zao, kudhibiti aina za uwekezaji, kulinda maslahi ya watu wako kutokana na hali za nchi zao, na kubwa zaidi kujenga uwezo wa ndani kwenye maeeno ya kimkakati. Ndio mana China wameamua kutengeneza ndege zao wenyewe pamoja na kwamba kuna makampuni ya nje mengi yanayofanya kazi hii. Ndio mana Ethiopia wanatengeneza vifaru vyao na vifaa vingine vya kijeshi pamoja na kwamba ziko nchi na makampuni yanafanya biashara hii. Pia ndio mana wametengeneza bwawa kubwa la uzalishaji umeme kwa fedha na utalaamu wao bila kukaribisha wawekezaji. Ndio mana Marekani wanazuia/wanadhibiti uwekezaji wa nje kwenye baadhi ya maeneo ya kimkakati. Ndio mana uingereza imefunga migodi yote ya makaa yam awe. Ndio mana Kenya wanawekeza kwa bidii kwenye teknolojia na huduma. Ndio mana Rwanda imewekeza kwenye ICT na sasa wanakazana na elimu na maeneo mengine.
- Moja, wawekezaji wa nje kukaribishwa katika maeneo ambayo tumejiridhisha kwamba sisi kama watanzania tumeshindwa kulifanyi kazi na tunahitaji uwezo wa kutoka nje. Wawekezaji kuleta mitaji (capital) wa fedha na vifaa au teknolojia za kisasa na za gharama kubwa nchi isiokua nayo kama vile kujenga miundombinu ya kisasa na gharama kubwa kama vile reli, mawasiliano, na usafiri wa anga.
- Pili, lazima wawekaji hao waleta kitu (miundombinu, bidhaa, huduma, nk) tofauti na kile kilichoko. Uwekezaji lazima ulenge kutuongezea maarifa, utaalamu na ujuzi ambao nchi haina kwenye maeneo ya kimkakati na vipaumbele kwa taifa na usaidie. Pia uchochee na kukuza elimu ya juu, tafiti, na uvumbuzi kwa watu wake.
- Tatu, Uwekezaji usaidie kuingiza/kuvutia mapato toka nje kutokana na huduma mpya atakayoitoa au bidhaa atakayozalisha.
- Nne, lazima ijiridhishe kwamba pamoja na manufaa ya muda mfupi au ya haraka kwa uwekezaji wa nje, nchi itapata faida ya muda mrefu (kama vile utaalamu – knowledge and technological transfer) ambazo zitasaidia nchi kuendeleza maeneo hayo bila kutegemea wawekezaji na wataalamu toka nchi.
- Tano, kutazama athari ya uwekezaji huo kwa muda mrefu kwa nchi na watu wake kwenye maeneo kama ya uharibifu wa mazingira, makazi, na uhatarishaji wa maisha. Pia nini kitatokea iwapo rasilimali ambayo mwekezaji anaitumia itakwisha na mbadala utakuwa kitu gani.
Mhe Waziri, kwenye biashara ya tozo za kuegesha magari na taxi ambazo tumekaribisha wawekezaji toka nje hakuna kitu cha ziada tunachopata. Mwekezaji anachukua fedha ambazo ziko kwenye mzunguko wetu wa fedha kama faida huku yeye akiwa hajaacha chochote kama sehemu ya uwekezaji wake. Aina hizi za uwekezaji hazimlazimishi mwekezaji kuja na mtaji wala utalaamu wowote wa ajabu ambao watanzania hawana zaidi ya mkakati wa kibiashara na kuvuna faida. Hakuna shilingi toka nje inaingia kwenye soko la Tanzania toka nje kwa mwekezaji kutoza tozo za uegeshaji magari wala huduma ya taxi. Hakuna mtu atakuja Tanzania kutuletea fedha zake kwa sababu kuna kampuni toka nje inatoza maegesho na kukusanya fedha za huduma ya taxi. Zaidi sana wamewekeza kwenye maeneo ambayo tumeshawatengenezea mazingira na miundombinu ya kupata faida.
Mh Waziri, je, sera yetu ya kuvutia uwekezaji toka nje inajumuisha uwekezaji wa biashara ya taxi na tozo za kuegesha magari kama maeneo ya kimakakati na kipaumbele? Je, haya nayo ni maeneo ambayo tunahitaji utaalamu, mitaji na wataalamu kutona nje ya nchi watusaidie maana tumeshaindwa? Uko wapi mkakati wa kitaifa wa uwekezaji? Uko wapi mkakati wa kuwalinda watanzania na kuwawezesha kuboresha baadhi ya huduma rahisi kama hizi kwa utaalamu na miyaji waliyonayo? Je uwekezaji wa aina hii ni semehu ya uwekezaji kwenye uchumi wa viwanda?
Mh Waziri, jambo hili nimeshaliongelea mara mbili kwa kumwandikia mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam maana niliona liko kwenye mkoa wake na nilimsikia akijaribu kusuluhisha mgogoro kati ya kampuni ya Uber na wazawa wanaofanya biashara ya Taxi. Wakati naendelea kusubiri kauli na suluhisho lake, nimeona ni vema tukasikia kutoka kwako ili tusiendelee kushangaa aina zingine za uwekezaji kama huu kwenye maeneo mengine yanayotegemewa na watanzania wa hali ya chini mijini na vijijini. Andiko langu la kwanza kwenda kwa mkuu wa mkoa LIKO HAPA na la pili la ufuatiliaji LIKO HAPA.
Ni matumaini yangu na watanzania wengine tutasikia kauli yako juu ya jambo hili juu ya mwongozo wa kisera na kimkakati katika uwekezaji.
Ni mimi mtanzania mwenzako:
Mathew Mndeme (mwalimu MM)
Barua pepe: mmmwalimu@gmail.com