Kwa kipindi kirefu, Tanzania imekuwa inatoa taarifa ya pato la taifa kutumia aina moja ya uwasilisha | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kwa kipindi kirefu, Tanzania imekuwa inatoa taarifa ya pato la taifa kutumia aina moja ya uwasilisha

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, May 5, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  May 5, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Kwa kipindi kirefu, Tanzania imekuwa inatoa taarifa ya pato la taifa kutumia aina moja ya uwasilishaji wa taarifa hiyo licha ya kuwa imetoka katika mfumo wa uchumi hodi kwenda uchumi wa soko. Njia hiyo pekee ni ile ya Pato la Taifa (Gross Domestic Product by Industry Origin) kama jumla ya Pato la kila sekta au Kiwanda. Takwimu hizo ndizo zinatumika kuonesha kiwango cha ukuaji wa uchumi kila mwaka.

  Hakuna atakayebisha kuhusu ugumu wa ukokotoaji wa takwimu za Pato la Taifa. Lakini, hakuna atakayebisha kuhusu hatari zitakazotokana na ukokotoaji “usio sahihi” wa takwimu za Pato la Taifa.

  Takwimu sahihi za Pato la Taifa ni muhimu katika upangaji wa mipango ya maendeleo ya nchi, kwa wawekezaji katika kutanabaisha sekta zinazolipa, ambazo ziko nyuma au mbele kiuendelezaji au kiuwekezaji.

  Pia huitahadharisha serikali kuhusu matumizi bora ya rasilimali zake katika kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijamii.Takwimu hizo ni muhimu kwa mashirika ya fedha ya kimataifa kama Benki ya Dunia na IMF, ambayo ni wafadhili wakubwa wa miradi ya maendeleo nchini.Takwimu pia ni muhimu kwa wawekezaji wa ndani na taasisi za fedha.

  Pamoja na kuwasilishwa kwa taarifa hizo za Pato la Taifa kwa “Mtazamo Mmoja tu wa Kisekta” kwa kipindi kirefu, hakuna aliyehoji kuhusu “usahihi” wa takwimu hizo. Nyakati zote tumekuwa tukizichukulia takwimu hizo kwa moyo safi kabisa kwamba ni sahihi, kwa sababu zimekuwa zikitolewa na serikali.

  Hivi sasa uchumi wetu umeondokana na mfumo wa hodhi ambao serikali ilikuwa mwajiri mkuu na mfanyabiashara zote. Kwa kuingia katika mfumo wa uchumi wa soko, sekta binafsi ndiyo yenye nafasi kubwa zaidi ya kuendesha na kumiliki shughuli za uzalishaji mali na biashara, serikali ikiwa na jukumu la uwezeshaji na uratibu kwa maslahi ya Taifa. Serikali lazima sasa iache kuwasilisha takwimu za Pato la Taifa kwa kutumia mtazamo mmoja wa uzalishaji kisekta.

  Ni rahisi sana kucheza na takwimu za Pato la Taifa iwapo zitawasilishwa katika mtazamo mmoja tu wa uzalishaji kisekta. Mchumi yeyote analitambua hilo.Lazima serikali ikubali kuanza kutoa takwimu za Pato la Taifa katika mitazamo yote mitatu, kama ilivyo katika nchi za wenzetu. Na utaratibu huo umeonyesha mafanikio makubwa katika kudhibiti kwa usahihi mwenendo wa ukuaji uchumi na uwekezaji ulio na tija zaidi.

  Mitazamo hiyo, kwanza, Pato la Taifa Kisekta au Kiviwanda (The Output Approach). Kwa kawaida uchumi hugawanywa katika sekta zipatazo kati ya 12 na 15 hivi. Uzalishaji unatazamwa na kupimwa katika kila sekta na jumla ya uzalishaji katika sekta zote ili kupata takwimu za Pato la Taifa kiuzalishaji kisekta.

  Mtazamo wa pili, ni kwa kuangalia matumizi ya serikali na sekta binafsi pamoja kiwango cha uwekezaji nchini (The Expenditure Approach).

  Jumla ya matumizi ya ndani ya nchi (Binafsi na ya Serikali na Uwekezaji) yakijumlishwa mauzo ya bidhaa na huduma zetu nchi za nje (exports of goods and services minus imports of goods and services) na kutoa manunuzi yetu ya bidhaa na huduma kutoka nchi za nje, ndipo utakapo pata takwimu za Pato la Taifa kwa bei za soko (GDP at market prices).


  Mtazamo wa tatu, ni kwa kuangalia vyanzo mbalimbali vya mapato (The Income Approach). Vipo vyanzo sita katika kukokotoa takwimu hizo za Pato la Taifa Kimapato. Mapato yatokanayo na ajira, ajira binafsi, faida za makampuni, faida za makampuni ya umma, mapato yatokanayo na kodi (Rent) na mapato yatokanayo na nyenzo au rasilimali za uzalishaji mali (Factor Incomes).

  Uwasilishaji wa takwimu za pato la taifa katika mitazamo yote mitatu kwa wakati mmoja ni muhimu sana katika kuhakiki usahihi wa takwimu hizo. Na wala kisitafutwe kisingizio chochote kwamba kazi hiyo ni ngumu sana au haina umuhimu au ulazima wowote.

  Kwa bahati mbaya sana Tanzania hajajenga kada ya wahakiki au wakaguzi wa mahesabu au takwimu za kiuchumi zinazotolewa na serikali na taasisi zake (Economic Auditors).

  Benki Kuu haiwezi kuwa wakaguzi wa mahesabu au takwimu za kiuchumi zitolewazo na serikali, kwa sababu yenyewe ni taasisi ya serikali. Ni msemaji mkuu wa serikali katika masuala yote ya uchumi. Lazima pawepo na chombo au vyombo huru vitakavyo tambulika kisheria.

  Hili ni jambo muhimu sana katika kudhibiti mwenendo sahihi wa ukuaji wa uchumi na katika kudhibiti ubadhirifu katika mgawanyo wa rasilimali za nchi katika uwekezaji wa ndani na toka nje ya nchi. Taifa limeshasomesha vijana wengi katika uchumi na uhasibu lakini serikali imeshindwa kuwatumia ipasavyo.

  Tutazungumziaje mipango sahihi ya kutokomeza umaskini na kukuza uchumi wakati taaluma za wachumi na watakwimu zinapuuzwa?
  Ukuaji wa uchumi sio uzuri wa takwimu tu za Pato la Taifa.

  Takwimu zinaweza kupikwa. Takwimu lazima ziakisi uhalisi wa hali ya maisha katika kaya au kwa mtu mmoja mmoja.Mfumuko wa Bei, ukosefu wa ajira, kiwango cha tija na ufanisi katika uzalishaji mali ni baadhi ya viashira vya hali bora ya kukua kwa uchumi.

  Mambo hayo pia yanagusa masuala mengine kama viwango vya riba za mabenki na ugumu wa upatikanaji wa mikopo kutoka benki, thamani ya sarafu, uwezo wa kununua (Purchasing Power), uwezo kitaifa katika kujitosheleza katika mahitaji bila kutegemea bidhaa kutoka nje, uimara wa miundo mbinu ya uchukuzi na usafirishaji na nishati.

  Tusidanganyike kwamba uchumi wetu unakua kwa kasi. Hapana, sio kweli. Tujipapase upya.

  Mwandishi ni mchambuzi wa uchumi na siasa
   
Loading...