Kwa Hili Mimi Ni Thomaso

kinepi_nepi

JF-Expert Member
Aug 16, 2007
869
235
KARUGENDO
Nakala chapishi
Mtumie mwenzio
Jiandikishe utaarifiweKwa hili mimi ni Thomaso

Padri Privatus Karugendo Mei 21, 2008THOMASO aliishi na Yesu. Yeye kama Mitume wengine alimshuhudia Bwana Yesu akifanya miujiza mbali mbali kama ule wa kugeuza maji kuwa divai, kuponya vipofu na kufufua wafu. Yesu, alipomfufua Lazaro, alikuwa na mitume wake.

Ni wazi Thomaso naye alishuhudia muujiza wa Lazaro. Pamoja na kushuhudia miujiza yote hiyo, iliyoonyesha kwamba Bwana Yesu hakuwa mtu wa kawaida, bado Thomaso hakuamini ufufuko ya Yesu, mpaka pale alipougusa mwili ya Yesu na kushuhudia makovu kwenye mikono na ubavuni.

Wanateolojia, wanasema alikuwa na imani haba. Imani ya kuamini baada ya kuona! Tunaambiwa kwamba ana heri mtu yule anayeamini bila ya kuona! Lakini enzi hizi za sayansi na teknolojia, ni vigumu kabisa mtu kuamini bila ya kuona.

Mimi pia kwa hili la kifo cha Dk.Ballali, nina imani haba! Nilipata habari za kifo cha Dk. Daudi Ballali, nikiwa vijijini Karagwe. Nimeshuhudida jinsi watu wanavyofuatilia kwa karibu kila tukio. Kusema ukweli wana uchungu mkubwa juu ya wizi uliotokea Benki Kuu (BoT).

Maisha yanavyozidi kuwa mgumu, ndivyo wanavyolaumu viongozi wanaopora mali ya Taifa. Sasa hivi mafuta ya taa yamepanda bei, ni machungu kwa kila mtu kule vijijini. Hivyo habari za kifo cha Dk. Ballali, wamezipokea kwa uchungu mkubwa. Walitaka arudi akiwa mzima, asaidie kurudisha fedha zao zilizoporwa. Ingawa kule vijijini watu wameonyesha kukiamini kifo cha Dk. Ballali, mimi nimekuwa Thomaso! Rafiki yangu mmoja nilipomtumia ujumbe juu ya imani yangu haba kwa kifo cha Dk. Ballali alinishauri niachane na Uthomaso.

Anataka niamini kwa kusikia na labda kwa vile Serikali imetoa tamko na kututangazia kifo hicho. Lakini kwa hili kwangu inakuwa vigumu kuuvua Uthomaso. Ni lazima nione, nihakikishe ndipo niamini. Hata wakionyesha picha za Dk. Ballali akiwa kwenye jeneza bado sitaamini kifo hiki, hata nikionyeshwa picha za mazishi yake akiingizwa kaburini kule Marekani sitaamini, mpaka pale nitakapoambiwa kwamba DNA imechukuliwa na kupimwa na kuhakikisha kwamba huo ni mwili wa Dk. Ballali. Katika hali hii, inawezekana wakatengeneza kitu tu na kukipachika picha ya Dk. Ballali, ili tuaamini kwamba amekufa, na maisha yakaendelea kama kawaida.

Watanzania tumejijengea utamaduni wa kushangaza kabisa. Utamaduni wa kutofuatilia kitu hadi mwisho wake. Hata kabla ya kutangaza kifo cha Dk. Ballali, tulikuwa tumeliacha hili na kuanza kufukuzia mengine, ambayo nayo ni wazi tungeyaachia njiani! Sasa nguvu zote zimewekwa kwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Kura za maoni kule Zanzibar.

Tunafanana na mbwa anayefukuza gari, likisimama zaidi anachoweza kufanya mbwa ni kulikojolea gari na kuendelea na safari zake. Zile hasira anazokuwa nazo mbwa wakati akilifukuza gari, likisimama zinayeyuka. Kuna orodha ndefu ya mambo yasiyokwenda sawa, lakini wakati ukipita, tunasahau kabisa.

Sasa kwa vile tumetangaziwa kifo basi ndiyo tutazika kila kitu kuhusu kashfa ndani ya BoT.

Uwezekano wa yeye kuendelea kuishi ni mkubwa sana. Fedha zinazongumzwa katika wizi wa BoT ni nyingi. Kama alikuwa na fedha nyingi kiasi hicho, ujumbe ni kwamba anaweza kuendelea kuishi popote hata baada ya “kifo” chake. Baada ya Hitler kushindwa vita, wafuasi wake walitangaza kifo chake. Hakuna aliyeiona maiti ya Hitler wala kaburi lake. Kuna walioendelea kuamini kwamba Hitler, alijificha Marekani Kusini na akaendelea kuishi hadi miaka ya karibuni!

Imani yangu haba juu ya kifo hiki inasababishwa na maswali mengi juu ya kashfa ya BoT ambayo hayana majibu. Huko nyuma tuliambiwa kwamba Serikali, haifahamu kabisa Dk. Ballali amelazwa hospitali gani. Ingawa wakati anaondoka alikuwa Gavana wa BOT, aliaaga na kupewa ruhusa na kuna ushahidi kuonyesha kwamba kabla hajafukuzwa kazi, alikuwa na mawasiliano na ofisi yake.

Tulisikia kwenye vyombo vya habari kwamba alimwandikia Rais Jakaya Kikwete, barua ya kutaka kujiuzulu nafasi yake maana afya yake ilikuwa mbaya. Kama barua hiyo ilimfikia Rais, ni wazi kulikuwa na mawasiliano. Karibuni zaidi Serikali ilisema haimuhitaji, kwamba siku ikimuhitaji kumpata si kazi kubwa. Juzi tu, vyombo vya habari vimetangaza kwamba sasa makachero wa Tanzania, wametumwa kwenda kumtafuta. Hazikupita hata siku tano, tukasikia habari za kifo cha Dk. Ballali na kwamba alikufa Mei 16,2008.

Taarifa ya Serikali ya kifo hicho ilitanguliwa na habari zilizotoka magazetini. Kwa maneno mengine, ni kama Serikali imeshinikizwa na taarifa za magazeti kutangaza kifo cha Dk. Ballali.

Inakuwa vipi mtu kama Dk. Ballali, afe, zipite siku kama nne, bila habari kuvuja? Tuliambiwa alikuwa akitibiwa kwa fedha za Serikali. Hii ina maana hospitali, ilikuwa kiwasiliana na Serikali ya Tanzania. Hivyo kifo chake kingejulikana haraka. Pia sina imani kwamba hospitali hiyo haikuwa na mtu kutoka Tanzania au Afrika. Habari zake zimeandikwa kwenye magazeti mengi ya nje na ziko kwenye mtandao. Picha yake imezagaa kwenye magazeti na kwenye mtandao. Hivyo habari za kufa kwake zisingechukua muda mrefu kujulikana.

Binafsi sikutaka Dk. Ballali afe. Nina imani kwamba Watanzania wenye uchungu na Taifa hawakutaka mtu huyu afe. Tulitaka aje ajibu maswali. Tulitaka kujua jinsi fedha za EPA, zilivyochotwa, tulitaka kufahamu ukweli wa fedha hizi kuingizwa kwenye kampeni ya CCM. Tulitaka kujua mambo mengi yanayohusu BOT, hasa ujenzi wa jengo la BOT, ambao hadi leo hii umeleta utata mkubwa.

Nashawishika kuamini kwamba kuna maelewano ya aina fulani kati ya Serikali na familia ya Dk. Ballali. Wamekubaliana kutangaza kifo, ili Dk. Ballali, aishi kwa amani nje ya nchi bila kusumbuliwa na baadhi ya viongozi wa Serikali walioshiriki kupora fedha za EPA, waishi kwa amani?

Je, wale makachero waliotumwa kumtafuta Dk. Ballali, ndio wamekula njama za kutangaza kifo chake baada ya kukutana naye? Je, Serikali imeamua kufanya mchezo huu mchafu? Hili linawezekana? Ukitafakari kwa undani – unagundua kwamba kama Dk. Ballali, angehojiwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria mambo mengi yangefumuka na kuiweka Serikali kwenye wakati mgumu?

Nimesikia kwenye vyombo vya habari kwamba dada zake wanaomba au wameombewa ulinzi, kwa maana eti wana wosia mzito! Kwamba baadhi ya viongozi wanaohisi kutajwa kwenye wosia huo wanaweza kutishia maisha ya dada hawa.

Sina imani kama kuna wosia mzito kutoka kwa Dk. Ballali. Kama upo, basi huu ni ushahidi kwamba muda wote huo alikuwa na akili timamu, na angeweza kuhojiwa akiwa bado hai. Vinginevyo wosia huo ni mkakati mzima wa familia na Serikali kutaka kutufumba macho.

Mtu anaweza kujiuliza swali ni kwa nini mtuhumiwa aliachiwa kuwa huru wakati wote huo? Kwa nini, hata kama alikuwa hospitalini, hakuwekwa chini ya ulinzi? Kama Rais Kikwete, alifikia hatua ya kutengua uteuzi wake ni kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha juu ya shutuma zilizokuwa zikitajwa juu yake. Na hii ilitosha kwa Rais kutoa agizo la mtu huyu kukamatwa na kurudishwa nchini kwa mahojiano.

Rais, angeagiza mali zake zote zikamatwe. Kwa kifo chake, mali zote zitaendelea kumilikiwa na ndugu na jamaa zake. Kwa nini mali hizi zilizopatikana kwa kupora, ziendelee kuwa chini ya urithi wa Dk. Ballali? Ni vigumu kumshitaki marehemu. Lakini kama angezikwa hapa Tanzania, nina imani vizazi vijavyo wangeifukua mifupa yake na kuishitaki.

Labda wakati makala hii inatoka, tutakuwa tumeonyeshwa picha za mazishi ya Dk. Ballali, lakini kama nilivyosema hapo juu, mimi ni Thomaso. Bila vipimo vya kuhakikisha kwamba aliyekufa ni Dk. Ballali, sintaamini kifo hiki na bado nitaendelea kuiomba Serikali imkamate na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria!
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom