data hizi hapa chache
Kwa mujibu wa Dk Slaa, ambaye pia ni katibu mkuu wa Chadema, chama chake kimekuwa kikifuatilia kwa makini matokeo hayo na kugundua wizi mkubwa wa kura kwenye nafasi za urais na ubunge.
Mgombea huyo wa urais, ambaye mara nyingi hujenga hoja kwa kutumia ushahidi, alisema moja ya maeneo waliyogundua kuwepo kwa wizi wa kura ni matokeo ya Jimbo la Geita lililo mkoani Mwanza ambako alidai Nec ilitangaza kuwa kwenye uchaguzi wa rais, CCM imepata kura 17,792 na Chadema kura 3,789.
Lakini akasema kwa mujibu wa fomu walizonazo ambazo zilisainiwa na mawakala wao kwenye kata 20 za jimbo hilo, CCM ilipata kura 30,960 na Chadema 15,736.
"Nashangaa Nec wanatangaza matokeo haya kutoka wapi? Hayo ya Geita ni moja tu. Kule Hai, fomu zinaonyesha kwenye urais CCM ina kura 20,120 na Chadema 26,724, lakini Nec imetangaza kuwa CCM ina kura 35,910 na Chadema kura 18,513," alisema Dk Slaa huku akionyesha baadhi ya fomu kwa waandishi wa habari.
Dk Slaa pia alitoa mfano aliodai kuwa wizi wa kura katika kituo namba 00070103 cha Ubungo jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa fomu 24A inaonyesha CCM wamepata kura 68,727 na Chadema 65,450, lakini matokeo ya kata za Ubungo yanaonyesha CCM ina kura 70,472 na Chadema 72,252.
Dk Slaa alisema mbali na Ubungo, tatizo hilo pia alidai liko Kigoma Mjini ambako Chadema imeshinda kwa zaidi ya kura 500, lakini "matokeo yalichakachuliwa na kusababisha vurugu hadi askari wakawapiga mabomu wafuasi wa Chadema".
Pia alisema kwenye Jimbo la Segerea, ambako matokeo yalicheleweshwa kwa siku mbili na kutangazwa usiku wa manane juzi, mambo ni mabaya zaidi kwa kuwa fomu 21 A na B hazikuwepo na wasimamizi walikwenda nazo majumbani kulala.
"Kiwalani fomu hazikuwepo na matokeo hayakuonekana. Kipawa vituo vinne matokeo hayakuonekana na Vingunguti kuna vituo saba na Tabata vituo viwili ambako matokeo hayakuonekana," alisema Dk Slaa.
Aliongeza kusema: "Hali kama hiyo pia imetokea Morogoro Mjini. Matokeo hayajaonekana na yametangazwa tu. Kibakwe na Kiteto mgombea hakushirikishwa katika kutangaza matokeo.
"Hayo ni majimbo ya mifano tu. Yapo majimbo mengi na kutokana na hali hiyo, Chadema imetoa tahadhari kwa Tume na vyombo vya ulinzi na usalama kuwa taratibu hazijafuatwa na nyingi zimevunjwa."
Dk Slaa alisema kuwa ni muhimu waangalizi wote wa uchaguzi wakatoa taarifa zao hadharani ili kusaidia nchi na kumtaka mkuu wa Jeshi la Polisi kuendesha chombo hicho cha dola kwa haki na maadili waliyosaini.
Baadaye mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa kauli hiyo ya Dk Slaa ni tamko rasmi la Chadema.
Kutoka Mwananchi la leo