Kupunguza umaskini: Tujifunze kutoka Thailand

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
KILIMO kina nafasi kubwa katika kupunguza umaskini, hasa kwa nchi maskini kama Tanzania, ambayo idadi kubwa ya watu wake hutegemea kilimo katika kuendesha maisha yao ya kila siku.

Kuongezeka kwa thamani ya mazao ya kilimo kulisaidia sana kupunguza umaskini barani Asia, hasa nchini Thailand katika miaka ya 1970 na 1980. Hata hivyo, kilimo kikiachwa nyuma (bila kuendelezwa), kinaweza kuwa mtego wa umaskini.

Hicho ndicho kinachotokea katika nchi nyingi maskini za kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika, ambako sekta ya kilimo imeachwa nyuma.
Tanzania haina uwekezaji wa kutosha katika miundombinu ya vijijini, teknolojia ya kilimo, zana au vitendea kazi vya msingi.

Kwa matokeo hayo, mafanikio ya kilimo aidha hudumaa au huongezeka kwa taratibu kama si kuanguka kabisa.
Hapa nchini kilimo kimekuwa kikikua kwa asilimia nne katika muongo mmoja uliopita wakati ongezeko la watu likiwa karibu asilimia tatu kwa

mwaka katika mikoa mingi, na katika mikoa mingine ni zaidi ya hapo, hivyo si rahisi kuamini kuwa kilimo kinaweza kusaidia kupunguza umaskini kwa uwiano huu wa uongezeko la watu.

Sambamba na hilo, hakutakuwa na ongezeko lolote la kipato cha wananchi. Hii ndiyo sababu umaskini umeendelea kutamalaki miongoni mwa wananchi hapa Tanzania.

Ni kwa namna gani katika hali hii mtu anaweza kusema kuwa kilimo kitapunguza umaskini miongoni mwa wananchi?
Baadhi ya nchi zinazo majibu ya kueleweka hasa za Asia. Nchi ya Thailand ni mfano maalumu ambao tunaweza kuutumia kujipima na kupata somo zuri ambalo Tanzania inaweza kulitumia.

Thailand imepunguza kwa hakika umaskini tangu miaka ya 1960. Kwa sasa ni msafirishaji mkubwa wa bidhaa za chakula, ikiwamo vyakula vilivyosindikwa. Mchele wa Thailand unanunuliwa sana katika soko la dunia.

Ubora na bei ndogo hufanya bidhaa za chakula za Thailand kuwa bora katika masoko ya dunia. Wanafanikiwaje? Utafiti katika kilimo ndio umewaletea mafanikio makubwa.

Mafanikio ya Thailand kutokana na kilimo hayakuja kwa siku moja. Ni baada ya miongo mingi ya uwekezaji katika kilimo ambako kumezaa matunda. Thailand kwa sasa imekwisha kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia, ikiwamo kupunguza umaskini miongoni mwa wanachi wake kwa kiasi kikubwa.

Katika robo ya mwisho ya karne iliyopita, miundombinu ya vijijini nchini Thailand ilikuwa tayari imeimarishwa kwa kiasi kikubwa, ambapo uchumi wa vijiji tayari ulikuwa umeunganishwa katika masoko.

Urefu wa barabara za vijijini uliongezeka kwa wastani wa asilimia 11 kwa mwaka. Njia za simu vijijini zimeongezeka kwa asilimia 23 kwa mwaka.

Aidha, Thailand usambazaji wa umeme katika vijiji umekuwa ukiongezeka kwa asilimia 17 kwa mwaka. Mwaka 2000, asilimia 97 ya watu wanaoishi vijijini tayari walikuwa wakipata huduma ya umeme. Mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa bidhaa za kilimo.

Upatikanaji mdogo wa umeme katika maeneo ya vijijni hudumaza ukuaji wa kilimo.
Hali ya umeme Thailand tunaweza kuilinganishaje na Tanzania?

Hali yetu ya umeme vijijini bado inatisha, kwani ni vijiji vichache sana vinavyopata huduma hii.
Kuhusu zana za kilimo, Thailand zana za kilimo zimeongezeka kwa kiasi kikubwa kulinganisha na Tanzania ambako upatikanaji wake umekuwa ukidorora mwaka hadi mwaka.

Idadi ya matrekta kwa kila km 100 za mraba za ardhi inayolimika imeshuka kutoka 32 mwaka 1961 hadi 23 mwaka 2005. Hata hivyo wastani wa matrekta yanayomilikiwa na kaya mbalimbali umedorora kutoka asilimia 0.2 mwaka 2000/01 hadi asilimia 0.1 mwaka 2007.

Tangu mwanzoni mwa miaka ya 1980, Thailand iliizidi Tanzania katika pembejeo za kilimo. Idadi ya matrekta kwa kilometa za mraba 100 kwa ardhi inayolimika yaliongezeka kutoka matano tu (dhidi ya 32 ya Tanzania!) mwaka 1961 hadi 261 mwaka 2005.

Katika pato la kila mwananchi wa Tanzania kwa sasa linalingana na ilivyokuwa Thailand mwaka 1963. Ikiwa na maana kwamba pato la mwananchi wa Tanzania kwa sasa ni sawa na pato la mwananchi wa Thailand miaka 49 iliyopita.

Aidha, matumizi ya mbolea pia kimekuwa kikwazo kikubwa miongoni mwa wakulima wengi hapa nchini. Matumizi ya mbolea miongoni mwa mambo mengine ni muhimu sana kwa ongezeko la mazao ya kilimo.

Matumizi ya mbolea nchini Thailand yameongezeka kutoka kilo 1.7 kwa hekta moja mwaka 1961 hadi kilo 120.7 mwaka 2005.
Hapa nchini matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka kilo 0.5 mwaka 1961 hadi kilo 5.8 mwaka 2004, kabla ya kufikia kilo 10.8 mwaka 2005.

Kupunguza umaskini: Tujifunze kutoka Thailand


 
Back
Top Bottom