Kupiga kidaku

Idd Ninga

JF-Expert Member
Nov 18, 2012
5,136
4,298
1)Mimi nataka kujua,kuuliza si ujinga

Swali nalipambanua,kusikiza najipanga

Masikio nainua,Leo nitoke na mwanga

Eti kupiga kidaku,ilikuwa ni haramu ?


2)Daku walituhamsha,kwa qaswida wakiimba

Mtaa kachangamsha,dini kaoneka simba

Nani amewafurusha,tuwaoni wakitamba

Eti kupiga kidaku,ilikuwa ni haramu ?


3)Usiku walizunguka,ni mola aliwachunga

Kwa mbali walisikika,kwa qaswid walotunga

Mtani wametoweka,ni Nani alowadunga

Eti kupiga kidaku,ilikuwa ni haramu ?


4)Wale wahamsha daku,so kwamba ninawafumba

Siwaoni tena huku,ama wameenda Pemba

Au kupiga usiku,wanawaogopa mamba

Eti kupiga kidaku,ilikuwa ni haramu ?


5)Ama shida ni madufu,ndo yaloleta majanga

Hapo wakafua dafu,Kule ikatupwa nanga

Kapoteza maarufu,kidaku wakamfunga

Eti kupiga kidaku,ilikuwa ni haramu ?


6)Au hivi ni haramu,nogopa sije nizomba

Nahamu niifahamu,ili mambo yawe bomba

Nauliza kinidhamu,na majibu nayaomba

Eti kupiga kidaku,ilikuwa ni haramu ?


SHAIRI- KUPIGA KIDAKU

MTUNZI-Idd Ninga,Arusha

+255624010160

iddyallyninga@gmail.com
 
Back
Top Bottom