Kulikoni Makanisa ya Tanzania yanakengeuka? Tuanze na Tamko la KKKT

Unseen

Member
Feb 27, 2018
35
46
AMANI YETU, TAIFA LETU,

A. UTANGULIZI

Amani Ya Mungu Iwe Kwenu Ndugu zangu Watanzania, awali ya yote naanza kwa maneno Matakatifu yatokayo ndani ya Biblia yapatikanayo katika Mithali31:8-9 yanayosema "Fumbua Kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao; Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; uwapatie maskini na wahitaji haki yao" .

Maandiko yaliyonukuliwa hapo juu kwa hakika yanasadifu Matendo na aina ya Uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Kiongozi Mkuu wa nchi na Serikali ya Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa muda mfupi aliokaa madarakani amefumbua kinywa chake kuwasemea Wanyonge waliofanywa mabubu kwa miaka mingi, akawatetea waliotelekezwa na akahukumu kwa haki watu wote waliohukumiwa kwa hila na ounevu na zaidi ya yote akawafungulia maskini dunia yao, akawapatia elimu bure akawarahisishia kupata huduma za afya na kuwaimarishia taasisi za kushughulika na shida zao kwa kusisitiza uadilifu na kupiga vita Rushwa na Ufisadi.

Kwa Masikitiko Makubwa jitihada za Mhe. Dkt. John Magufuli zimekuwa zikikumbana na vikwazo kadhaa, vikubwa kwa vidogo kutoka kwa aina mbalimbali za Watu na Taasis. Katika hali hii imekuwa ikieleweka kwa kila Mtanzania mwenye Utashi sababu ya mambo hayo, wengi katika wakosoaji wa Mhe. Dkt. Magufuli wamekuwa ni waathirika wa Utendaji haki wenye ukali na uchungu dhidi ya Upotofu wa maadili mema, Rushwa na ufisadi, wizi wa Mali na Rasilimali za nchi, ukosefu wa uwajibikaji, biashara haramu za nyara za nchi, madawa ya kulevya na Ujangili, wafanyabishara na watumishi wa Umma waliojizolea mali nyingi kwa njia za Ujanjaujanja, wahujumu uchumi nk. nk...

Katika hali ya kustaajabisha kabisa Mhe. Dkt. John Magufuli ameanza kupata Upinzani Mkali kutoka kwa viongozi wa Dini, hususan wa Kikristo na Madhehebu yake. Walianza baadhi ya Wachungaji wakiongozwa na J. Gwajima, kutokana na aina yake ya uchungaji hakuwa na athari kubwa kwani Watanzania wengi walichukulia maneno na matendo yake kama burudani kupitia mitandao ya kijamii, na kwa Watanzania wanaojitambua vyema waliyachukulia kama maoni ya Mtu aliyejizolea Umaarufu Mkubwa kutokana na mapungufu ya uelewa wa Watu.

Baadae hali hii imekuwa ikienea kwa kasi hadi ikawafikia Ndugu zangu Wakatoliki na hivi Sasa Waprotestanti wa KKKT nao wanapita katika mapito hayohayo. Swali la kujiuliza kwa nini Makanisa yanafanya hivi ? Kwa nini wanafanya mambo hayo sasa ? Kumeharibika jambo gani hadi Makanisa yanaonyesha taharuki ya Waziwazi ?

Ili kupata uchambuzi usio na upendeleo wa Upande wowote, nimeamua niandike makala yangu hii kwa Vipengele kama vile vya UJUMBE WA PASAKA KUTOKA BARAZA LA MAASKOFU WA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA (KKKT) ingawa kinyume na Wao nimeanza kwa Kuandika AMANI YETU, TAIFA LETU badala ya TAIFA LETU, AMANI YETU kutokana na ukweli kwamba Taifa linakuwa taifa kama Amani ipo na hivyo Amani inatangulia kabla ya Taifa, na hapo huenda ndipo ninapotofautiana vikali na hawa viongozi wa Makanisa.

B. AMANI YETU NA TAIFA LETU

Ndugu zangu Watanzania Amani ni zaidi ya kuishi bila ya kusikia sauti za Risasi, milio ya Makombora au kukatwa Mapanga, kutokana na tafsiri ya neno Amani kuwa pana sana yafaa tukasema Amani ni hali ya binaadamu kuwa na Utulivu wa Nafsi na kuwa na Matarajio ya kuwa na kesho bora zaidi kuliko leo yake, hata hivyo hii siyo tafsiri ya neno bali ni maana ya Mafuhumu ya neno husika.

Amani ya nchi yetu ambayo imelipamba taifa letu kwa miaka yote ni Matunda ya Wananchi Wastaarabu, wenye kuvumiliana na kustahamiliana, wenye kupendana na kuhurumiana, wanaofikiria nchi yao kwanza kabla ya maslahi yao binafsi na wakweli wa kauli na matendo. Amani yetu siyo zao la Chama chochote cha siasa, taasisi ya kiraia au dhehebu lolote la dini. Kwa hali hiyo watanzania wenyewe nje ya itikadi zao za vyama, dini, makabila na makundi mbalimbali ndio wenye mamlaka ya kuzungumzia Amani ya nchi Yao. Hata hivyo haizuii kanisa kama taasisi yenye watu na kama kiunganishi cha Watu wenye imani fulani kuzungumzia amani ya nchi, ingawa kauli ya kanisa inabaki kuwa kama ushauri kwani kanisa halina uwezo wa kuleta au kuondoa amani kama Wananchi wako kinyume na Matakwa hayo.

KKKT kupitia nakala ya SALAMU ZAO ZA PASAKA imedai kufikisha miaka 500, cha kustaajabisha ni kwamba kama kanisa lina Historia ndefu kiasi hicho kwa nini limesahau yaliyotokea miaka minne iliyopita ? Je Makanisa yamesahau kwamba miaka minne tu iliyopita katika funga kama hii ya kuelekea Pasaka waumini wao walikuwa wakiogopa kwenda makanisani na kwenye maeneo ya mikesha na kusherehekea sikukuu kwa kuhofia kushambuliwa na magaidi ? Je ni kweli ndani ya miaka hii minne kanisa limesahau kushambuliwa kwa viongozi wa kanisa huko Zanzibar, Arusha n.k ? Je hivi sasa kuna hofu kiasi cha Mtu kutamani asitambulike ni wa dhehebu gani au hata kwenda kwenye nyumba yake ya Ibada ? Je hofu ya sasa ya Watu inaathari kubwa kwa Kanisa kuliko ile iliyowafanya watu wakimbie nyumba zao za Ibada ? Je, ni kweli Kanisa lenye Historia ya kurekodiwa ya zaidi ya miaka 500 linakosa historia ya ya kukumbuka tu ya miaka tisa iliyopita, wakati Majambazi walipopora Mabenki mchana kweupe, barabara zilipofungwa na majambazi wenye silaha na Magari kutekwa na Watu kuuliwa Mchana kweupe ? Kanisa mbona halikutoa Salamu kama Hizi ? Je ni kweli Watanzania Amani ya nchi hivi sasa inashuka kuliko nyakati hizi ? Tumesahau maduka ya Mtaani yakiporwa saa 12 za jioni na milio ya Risasi juu ?

Ukweli ni kwamba kuna aina ya Uhalifu wa watu kupotea kama tunavyoona, hata hivyo haimaanishi kwamba Watu kupotea kumeanza leo. Miaka michache iliyopita Watanzania wenye asili ya ALBINO wamekuwa wakipotea kabisa na wengine kuokotwa wakiwa wamekufa au wamekatwa baadhi ya viungo vya miili yao, kwa bahati mbaya Kanisa limechukua historia ya Miaka 500 lakini likachana ukurasa wa Matukio hayo yanayoendana kinyume na Mpango wa Mungu kwa Mwanadamu na kufufuka kwa bwana wetu na mwokozi Yesu Kristo.

Miaka michache iliyopita, chini ya hiyo 500 ya KKKT ajali zilikuwa zikiua kuliko hata Ugonjwa wa UKIMWI, njaa pia iliua watu kadhaa kutokana na Ukame na Wananchi kukosa kulima na kuweka akiba wakitegemea chakula cha serikali cha Msaada. Kutokana na msimamo wa Mhe. Magufuli juu ya chakula cha Msaada na ubanaji wa Watumiaji wa barabara kumekuwa na upungufu mkubwa wa ajali za barabarani na vifo vitokanavyo na njaa. KKKT hawana hesabu ya mambo haya katika amani na hivyo kwao amani iko mashakani zaidi kuliko kipindi chochote cha kanisa hilo nchini hapa kiasi cha kutolea Salamu Mahsusi za Pasaka juu ya Amani ya nchi tena kwa mawazo hasi kabisa utadhani kanisa hilo ni tawi la Chama pinzani kinachowania madaraka dhidi ya Chama kinachotawala.

  1. JAMII NA UCHUMI
Ni ukweli uliowazi kwamba, Sekta binafsi na mashirika ya dini ni wadau wa maendeleo, si washindani wa serikali katika kuchangia maendeleo ya taifa, huu ni ukweli usiopingika, tatizo linakuja kwamaba Imani ya KKKT linaamini kwamba Serikali imekuwa mshindani wa sekta binafsi kutokana na maelezo ya ibara katika nakala ya Salam zao za Pasaka. Swali la kujiuliza, kama kanisa ni kwa ajili ya Ustawi wa binadamu katika nyanja zote za maisha ikiwemo imani yake, Serikali inapotoa huduma ambayo Sekta binafsi illihodhi na kuitoa kwa hila, Serikali inakuwa Upande wa Mungu au wa Shetani ? Je Sekta binafsi ikinufaika na wananchi wakaadhirika katika maisha yao, KKKT linafaidika kwa namna gani ?

Katika historia ya KKKT kwa nini mmechana Ukurasa wa Wafanyabiashara, Wawekezaji na Tasisi mbalimbali kukwepa kodi na kuingia mikataba ya hovyo kabisa isiyo na Maslahi kwa Taifa ? Kwa nini ndani ya Miaka yenu 500 hamjawahi kutoa Salam za Pasaka za kuwakemea wakwepa kodi ila mnatoa Salam za Kulalamika kwa wakusanya kodi pale tu wanapokosea, kwani KKKT lilikuwa linafaidika vipi na Ukwepaji Kodi ?

Vijana ni hazina ya nchi hii, taifa halitakiwi kuwa na hofu kwa kuwa na vijana wengi ambao wananguvu ya kuzalisha na kulinda taifa lao, badala yake taifa lazima lijipange kutumia vijana hao kwa kiwango cha juu kabisa. Kazi ya kanisa ilitakiwa iwe ni kuishauri Serikali na kuwafunda vijana kuwa na Uzalendo na Uaminifu kwa taifa lao na kuwajenga katika maadili mema na ucha Mungu, na kufanya kazi kama anavyosisitiza Mungu kupitia Biblia na kama anavyohimiza Mhe. Magufuli.

Sina Uhakika na namna KKKT wanavyowafikia wananchi, ila Kuhusu Kilimo kwa Mara ya kwanza baada ya miaka mingi wananchi wameuza mazao yao kwa bei nzuri zaidi. Angalia mifano ya bei za Korosho, Kahawa na Pamba na ulinganishe na miaka michache tu iliyopita. Naomba kanisa liwaulize waumini wao wa Lindi, Mtwara na Singida kama tokea Uhuru waliwahi kupata mashamba, mbolea na pembejeo zingine na Ardhi bure ili wazalishe Korosho tafauti na Uongozi wa Mhe. Magufuli? Waulizeni Waumini wenu wa Morogoro n.k kuna Migogoro mingapi ya Ardhi kati ya Wakulima na wafugaji ambayo inaendelea sasa kulinganisha na miaka mitano iliyopita ?

  1. Maisha ya Siasa
katika Unafiki wa Wazi kabisa kufanywa na KKKT kwa mwaka 2018 ni pale wanapodai “Kupungua na hatimaye kutoweka kwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari ”. Hivi hicho KKKT mnachokidai kama kipo nyie mmewezaje kueleza Salamu hizi kwa Watanzania ? Mmewewzaje kukusanyika na hizi habari mimi nimezipataje ? Kila Mtu mwenye utashi atagundua ukosefu wa uadilifu na ukweli kwa Salam hizi za KKKT

KKKT wameongea sawa na Vyama vya siasa vya kiafrika vinaposhindwa Uchaguzi kwamba “Kukosekana kwa mazingira ya haki na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi zote zimeghubikwa na ubabe, vurugu, hila, na vitisho ” kana kwamba KKKT walikuwa wamesimamisha mgombea Mahala. Labda nyie KKKT siku nyingine mtoe muongozo kwa mujibu wa kanisa lenu Uchaguzi huru na wa haki ni wa namna gani ? Au ni ule ambao ameshinda mgombea wa Chama gani ?

Kuhusu “Utekelezaji wa mipango ya maendeleo wenye mwelekeo wa kiitikadi ” kwani awamu hii imeacha kuwapendelea nyie ? Je imewapendelea wakina nani ? Au akiingia Muadilifu wa kuacha kuwapendelea ndo anaonekana kuwa na Mwelekeo wa kiitikadi ?

Mnaposema “Udhalilishaji wa kauli njema isemayo "Maendeleo hayana chama". Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia fedha nyingi katika chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili kuleta maendeleo ” kwani wanaotoka CHADEMA kwenda CCM wanalipwa kiasi gani na wanaotoka CCM kwenda CHADEMA wanalipwa kiasi kwa sababu naona uhamiaji ni kwa kila Chama na sijajua bei ya kuhama. Je KKKT mmeona katika awamu hii ndio watu wanahama Vyama, je hiyo katiba yenu Mpya itazuia watu kuhama ? Neno Katiba mpya katika Salam zenu limerudiwa mara 11 ila neno Biblia limetajwa mara moja. Nashangaa kwa vile sisi Tanzania tuna Katiba ya kuandikwa, kwenu nyie kitabu cha katiba kina nguvu kuliko Biblia, nadhani kwenye Salam zenu zenye Pumzi ya Mungu ilitakiwa Biblia Itajwe kuliko Katiba kama sijakosea.


  1. KWA NINI MAKANISA YANAKENGEUKA ?
Ndugu zangu Watanzania, kila Mtanzania mwenye Utashi anaelewa Mchango wenye Historia ndefu wa Makanisa katika kutoa huduma kwa Wananchi, Makanisa yamekuwa yakimiliki Mashule, Vyuo vya Elimu ya ufundi, kati na ya juu, mahospitali, nyumba za kulala wageni, magari na mashamba.

Hali hii Iliipelekea Serikali kulazimika kuanzisha Hospitali teule ambazo ni za makanisa pale serikali Iliposhindwa kuanzisha na kuendesha Hospitali zenye hadhi husika kama vile za Wilaya, mikoa na Rufaa, katika Hospitali hizi Serikali ilipeleka Madaktari, wauguzi na Watumishi wengine ambao serikali iliwalipia, ikawanunulia vifaa tiba na kutoa Ruzuku kwa Hospitali hizo, kwa bahati mbaya Mhe. Magufuli alipoingia tu akaja na Sera ya Kuimarisha huduma za jamii kwa kuwa na Zahanati za serikali kila kijiji, kituo cha Afya kila kata na Hospitali ya Serikali kila Wilaya, kwa tafsiri ya haraka, makanisa yanakosa keki kama yalivyozoea tangu dahari.

Mhe. Magufuli kaleta Elimu ya Sekondari hadi kidato cha nne bure, vyuo vijae vya umma vyenye hadhi Kwanza, TCU iache kupanga wanafunzi kwenye vyuo binafsi kwa kushirikiana na Uongozi wa vyuo kwa lengo la kujichotea fedha kutoka bodi ya mikopo. Kumbuka Makanisa ndiyo yanayomiliki vyuo na mashule hayo ambako kwa sasa kuna upungufu mkubwa sana wa wanafunzi.

Kutokana na mifumo iliyokuwepo wakati, taasisi ikiongozwa na Mlokole na Watumishi wote wanakuwa Walokole na Kama kiongozi ni Muislam halikadhalika, Mhe. Magufuli amejenga nidhamu ambapo tume ya ajira imeanza kuajiri kwa kupima uwezo wa Mtu na siyo vimemo vya Wachungaji na Maaskofu, kukosekana upendeleo huo kumeanza kusababisha vijana kwenda kanisani kuombewa kupata kazi bila Mrejesho wa ushuhuda wa wanaopata kazi kwani vimemo hakuna tena. Hali hii inatishia umaarufu wa Maaskofu na Wachungaji waliojizolea umaarufu kwa kuombea Wahitimu kisha wakapata kazi na kurejesha shukurani. Shukurani hazipo tena kwani Wahitimu hawapati kazi kwa maombi tena bali kwa kufaulu Mtihani wa Tume ya Ajira. Hali hii inalitia hofu kanisa kutokana na Ongezeko kubwa la hawa vijana.

Kutokana na Mhe. Dkt John Magufuli kuleta nidhamu ya fedha, vijana waliokuwa wanapata fedha kwa njia haramu na kutoa Sadaka za Mamilioni kanisani hadi wakaitwa Wazee wa kanisa ilihali wazee wapo lakini kwa vile hawana fedha wakawa wanaonekana kama Mabarobaro hivi sasa hawatoi tena sadaka kubwa na Wengine hawahudhurii kabisa kanisani kwa kukimbizana na maisha. Hii imefanya wazee ndo wawe Wazee wa Makanisa huku mapato yakishuka kwa kasi.

HITIMISHO

Ndugu zangu viongozi wa dini, anzeni kufundisha na kueneza dini badala ya kuweka Maslahi yenu binafsi mbele, Mtangulize Mungu mbele kama anavyokuombeni Mhe.Dkt John Magufuli, raha yenu mtaipata kwa Mungu huko peponi kama mnavyotufundisha sisi na tukawaamini. Tunawaheshimu sana viongozi wetu wa dini, lakini mkichupa mipaka tutawakosoeni vikali mno kwa sababu pamoja na Uongozi mliopewa na Mungu bado nyie ni wanadamu na Mna mapungufu mengi. Msipende kusema mnaongozwa na Mungu katika kutetea maslahi yenu. Mungu aliyeumba Mbingu na Ardhi hawezi kushindwa kuona tofauti ya Utawala huu na mafaniko yake dhidi ya tawala zilizopita na badala yake akakosoa.

KKKT na wengine, jueni kwamba kinacho wakutanisha waumini wenu ni Imani ya dini tu, lakini upenzi wa Siasa, Ushabiki wa michezo nk ni nje ya hayo yanayo waunganisha, matendo mliyoanza kuyafanya yanawagawa baadhi ya waumini kwa wengine, itafika siku Mtahubiri na kugawa Makanisa yenu na Mtasikia waumini wenu wanaanza kupigana vijembe vya kisiasa kanisani.

Ni vyema Mtoe tamko kwamba huu ni msimamo wa Maaskofu na sio wa Waumini wa KKKT kwani ndani ya kanisa hilo siyo wote wanakubaliana na upotoshaji uliofanywa.

Kanisa lijue linachochea na kukuza hali ya Chuki ya wananchi dhidi ya serikali yao, badala ya kufundisha Upendo na maridhiano hususan katika kipindi hiki ambacho kama kanisa lilivyofanya kusambaza Salam zake za Pasaka kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii, kundi jingine linatumia njia hiyohiyo kushawishi wananchi kufanya maandamano yasiyohalali dhidi ya Serikali yao.

NB: Hata hivyo nimeshangazwa na Salam za KKKT, neno Yesu Kristo limetajwa mara 8, katiba mara 20, Sekta binafsi mara 4, amani mara 21,siasa mara 12,shetani mara 0, hadi sasa najiuliza kinacholeta Taabu duniani ni kukosa katiba Mpya au ni Shetani ? Mi naona Mngesema Wazi kwamba Mnaunga Mkono Maandamano yanayopangwa kwani Mtizamo wenu na Wanaopanga Maandamano ni sawa kabisa
 
Kwani hao viongozi wa makanisa hawana haki ya kusema lilote lenye ushauri mzuri? Hawapewi mlaka na vifungu vya biblia hiyo inayoamru watu wasifumbe kinywa? Ndugu yangu,rudi ukasome uoya hiyo biblia ndio uje uwakosoe hawa watu. Kwa kifupi, hakuna uongizi uliokamilika kwa 100% sasa wanawzae wakawa wanazungumzia hayo kutokana na mapungufu yao au ya upande wapili
 
Kuna Makanisa mengi ni Matawi ya Vyama vya Siasa. Viongozi wa Makanisa hayo Wanatumia Migongo ya Waumini, Madhabahu na nguvu ya Msalaba kama sehemu ya kufikia Maslahi na tamaa zao binafsi.

Huu uliouandika ni uongo wenye nia ya kupotosha. Hawa viongozi wa makanisa hawafaidiki na chocolate kutoka kwenye vyama vya siasa na waliyoyasema yote yana ukweli.
 
Unapaswa kufahamu walikutana maaskofu 27 wakajadili mambo mbalimbali na kisha kuja na ukweli tuliouona...sasa mjinga mmoja unakaa na kujitia msomi na mwelewa saana na kuanza kujibu!! Labda kwakuwa unaongozwa na mapepo mengi.
Ujinga mchache ni unaposema wasitetee maisha ya watu wanaotekwa na kuuawa bila ufumbuzi kupatikana kisa eti miaka 4 ilopita kunavitu kadhaa vilitokea pia! Jinga sana wewe.
Upuuzi mwingine ni unaposema amani ni kuwa na utulivu wa nafsi...na matarajio ya kesho bora?? Huna akili we hats kusiko na amani panaweza pakawa na utulivu! Watu wanatekwa,wanafungwa kiholela,wananyimwa kukutana hats misibani wanavamiwa na kupigwa mabomu halo unaiona amani ewe mjinga?
Eti mbona wao wamekusanyika na kusema,unajisahaulisha kilichomtokea mwenzao wa Moshi aliyeshikwa na kuhojiwa polisi? Nchi hii tuliambiwa unaruhusiwa kwenda popote na kufanya shughuli yoyote mradi usivunje sheria sasa iweje kiongozi akitaka kwenda mahali kukutana na wenzake na kufanya kikao azuiwe MF. Zitto kwenye ziara sake??
Kutetea dhambi/uovu ni kutetea shetani na kuwa wakala wake...kukaa kimya ni kumwogopa na kuruhusu ashamiri zaidi!! Sooote tukemee mabaya na kumsifu Mungu wetu.
HONGERA KKKT. Japo ni dhahiri wapo watakaopinga na kudharau neno lenu kuu lakini tupo tunaolithamini neno lenu na kesho tutakua viti vya mbele kusikiliza neno hili adhimu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom