Kujivua gamba CCM hatihati

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
[h=3]Kujivua gamba CCM hatihati [/h]

*Makamanda wa shughuli waanza kurudi nyuma
*Siku 90 zayeyuka, kikao NEC maswali magumu


Na Tumaini Makene
Majira

WAKATI Watanzania wakisubiri kwa hamu kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho
kinatarajiwa kufanya maamuzi magumu, ikiwemo kuwachukulia hatua makada wake wanaotuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali za ufisadi, imebainika mpaka sasa chama hicho hakijapangwa kitafanyika lini licha ya siku 90 zilizoahidiwa awali kukamilika.

Katika maamuzi yake ya kikao kilichopita, hasa juu ya tathmini ya uchaguzi mkuu wa 2010, iliamuriwa kuwa CCM kiongeze kasi ya mapambano dhidi ya viongozi na wanachama wanaojihusisha na rushwa, wakitakiwa wawajibike wenyewe kwa maslahi ya chama na wasipofanya hivyo chama kiwawajibishe kwa maslahi ya chama na nchi.

Kwa mujibu wa taratibu za CCM, vikao vya NEC vya kawaida hufanyika mara moja kila baada ya miezi minne, ingawa pia inaweza kufanya mkutano usiokuwa wa kawaida wakati wowote kunapotokea haja au kunapokuwa na maelekezo ya kikao cha juu kufanya hivyo.

Kwa kufuata utaratibu huo na kuzingatia kuwa NEC ya CCM ilifanya kikao chake cha mwisho Aprili 10, mwaka huu, ilitarajiwa kuwa chombo hicho cha juu katika kufanya maamuzi ya chama kitakutana wakati wowote Julai, au mwanzoni mwa Agosti mwaka huu.

Utaratibu wa kuitisha kikao cha dharura ulitarajiwa pia kutumika kwa sababu mojawapo ya maamuzi yaliyopaswa kutekelezwa ni pamoja na umuhimu wa suala lenyewe la kuwabana makada wanaodaiwa kukisababisha kupoteza mvuto mbele ya jamii.

Kutokana na kauli mbalimbali za viongozi waandamizi wa CCM, makada ambao wanaonekana kulengwa na maamuzi hayo ya kujivua gamba ni pamoja na Mbunge wa Monduli, Bw. Edward Lowassa, Mbunge wa Bariadi Magharibi Bw. Andrew Chenge na Mbunge wa Igunga, Bw. Rostam Aziz.

Awali ilielezwa kuwa shughuli ya kuvuana gamba ndani ya chama ingefanyika siku 90 baada ya kikao cha Aprili, baadaye kauli hiyo ikabadilishwa kuwa hazikutajwa siku, bali ingetegemea kikao cha NEC kinachofuata.

Akizungumza jana kwa njia ya simu na Majira, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye ambaye amekaririwa mara kadhaa akisisitiza kuwa hatua dhidi ya makda hao haikwepeki, alisema jana kuwa mpaka sasa sekretarieti ya chama hicho haijapanga ratiba ya kikao kijacho cha NEC na haijulikani itapangwa lini.

Kwa kawaida moja ya majukumu ya sekretarieti ya CCM, ambayo mwenyekiti wake ni Katibu Mkuu, ikiwa na wajumbe wakiwemo Manaibu Katibu Mkuu wa CCM, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Oganaizesheni, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Itikadi na Uenezi, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Uchumi na Fedha, Makatibu Wakuu wa Jumuiya za CCM, ni pamoja na kusimamia shughuli zote za utendaji na kuandaa shughuli za vikao vya chama katika ngazi ya taifa.

Majira lilitaka kujua kutoka kwa Bw. Nnauye ukweli wa habari kuwa sekretarieti ya CCM imeshakutana kupanga ratiba ya kikao kijacho cha NEC, lakini pia kutaka kujua kitafanyika lini hasa ikizangatiwa kuwa kumekuwepo na mshawasha mkubwa katika jamii juu ya kikao hicho, hasa juu ya maamuzi kinachotarajiwa kuyafanya.

"Hatuna ratiba...hatujapanga ratiba ya kikao hicho cha NEC na haijulikani kitafanyika lini...hizo habari kuwa sekretarieti imekutana kupanga kikao cha NEC si za kweli. Hakuna document zinazoonesha hivyo. Kwa kweli sijui sekretarieti itakutana lini na kikao cha NEC kitafanyika lini. Hatujapanga vikao hivyo, hivyo siwezi kupanga wala kubuni hapa

Akizungumzia juu ya maamuzi 26 ya NEC iliyopita ambayo yanahusu mabadiliko makubwa, alisema "tatizo waandishi mmeamua kufuatilia moja tu la kuwavua watu...lakini hata hilo tulisema wazi kuwa tunawavua watu nafasi zao katika vikao vya maamuzi ya chama... sisi kama chama hatuna haja ya kuwawajibisha kisheria, bali tutawawajibisha kisiasa, kwani hatuna ushahidi wa kisheria kama wengine wanavyotaka.

Uchunguzi wa Majira umebaini kuwa baadhi ya watuhumiwa waliotarajiwa kujiuzulu kutoka katika uongozi hakuna ambaye yuko tayari kufanya hivyo, na kwamba hata uongozi wa CCM wameanza kurudi nyuma katika kutekeleza azma yao.

Hivi karibuni ilielezwa kwenye vyombo vya habari kuwa watuhumiwa watatu ambao majina yao yalitajwa na wajumbe kwenye NEC ya Aprili waliitwa na kuhojiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Bw. Pius Msekwa kuhusiana na tuhuma dhidi yao lakini hakuna taarifa yoyote rasmi iliyotolewa na chama hicho kuhusu mahojiano hayo.

Hivi karibuni akizungumza na wanachama wa CCM, mkoani Morogoro, Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Wilson Mukama alinukuliwa akisema kuwa 'lazima wavue gamba' ambapo alifafanua kuwa yeye ni sawa na mtu aliyeteuliwa kufanya kazi ya kunyonga baada ya mahakama kupitisha hukumu, hivyo hataogopa kutekeleza hukumu hiyo.

Alinukuliwa zaidi akisema kuwa uamuzi wa ngazi za juu wa CCM ukishatolewa kuhusu kuvua gamba watuhumiwa wa ufisadi, hakuna kiongozi atakayepuuza kuutekeleza.

"Ufisadi unasemwa dhahiri na wananchi kwa kuwataja watuhumiwa hadharani wakiwahusisha na EPA (Akaunti ya Malipo ya Nje ya Benki Kuu), Dowans, ununuzi wa rada na Richmond, na vikao vya chama vimetoa uamuzi. Kilichobaki ni utekelezaji tu, na hukumu ikishatolewa na mahakama hakuna njia nyingine isipokuwa kutekeleza agizo hilo," alisema Bw. Mkama akinukuliwa katika moja ya magazeti ya kila siku.

Katika nukuu hiyo, Bw. Mkama aliongeza kusema kuwa hakuna mwananchi asiyejua kuwa ndani ya CCM wapo viongozi wenye nyadhifa kubwa wanaotuhumiwa kwa ufisadi kuanzia wa EPA, Richmond, Dowans, Rada na kashfa nyingine.
 
Hawana mpya hao magamba,kihama chao kinakuja,watajuta na hiyo danganya toto ya magamba
 
Wanatuzingua tu hao! Wamezidiwa nguvu na magamba na hawana la kutuambia tena. Kwa ninavyowajua ccm, sioni dalili yoyote ya kusikia tamko kwamba Lowasa amevuliwa ubunge wa Monduli na amebaki mwanachama tu!
Ukisikia Nape anasema wanawawajibisha kwenye ngazi ya chama ujue hakuna jipya maana huko kwenye chama hawana vyeo vya maana tena, labda ujumbe wa mkutano mkuu ambao hata Kopa, Banji, Asha nao wamo!
 
Inakuaje CCM wanakiri kuna mafisadi ambao lazima wavuliwe gamba wakati huo huo serikali waliounda wenyewe haioni kuna ufisadi na tena inamsafisha Chenge? Hiki ni kiini macho...
 
Ndio matatizo ya kuwa na Kiongozi wa nchi ambaye ameingia madarakani kimazabemazabe. Siku zote anakuwa muoga kuchukua hatua madhubuti katika kuongoza chama chake au kuiongoza nchi. Sasa hivi CCM na Tanzania zote ziko njia moja zikididimia kutokana na kuwa na kiongozi dhaifu na muoga wa kutimiza wajibu wake kama kiongozi.
 
kwanza hapo mwanzo hakukuwa na magamba, hata sasa ccm hakina magamba, mambo ya kujivua ilikuwa ni kiburudisho tu.
 
Back
Top Bottom