Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,478
39,997
Vipo vingi vya kuiga, vinavyopaswa kuigwa,
Hivyo mtu akiiga, hata yeye ataigwa,
Ubaya siyo kuiga, ni vile vinavyoigwa,
Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?

Mashindano ya urembo, tumeiga asilani,
Wanatao kwa mapambo, wandele majukwaani,
Wanasa kama urimbo, na nusu nguo mwilini,
Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?

Hilo tumelikubali, tukasema ni modeni,
Vichupi na suluali, na mavazi ya fukweni,
Wakiyajibu maswali, kwa lafudhi za kigeni,
Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?

Twashindanisha watoto, kwenye urembo jamani,
Urembo huo ni ndoto, kwa watoto wa shuleni,
Watoto wawe watoto, twadhulumu jamani,
Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?

Hebu pita kijiweni, mwangalie Solomoni,
Suruali matakoni, na kofia kisogoni,
Aimba Kimarekani, kakulia Kiwalani,
Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?

Tunaporudi nyumbani, twatoka ughaibuni,
Twajifanya ni wageni, tumesahau kingoni,
Ndoo ya maji bafuni, twataka ya mvua jamani,
Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?

Tuige vilivyo bora, vyenye tunu na thamani,
Tusiwe tunajichora, kwa kuiga vya kihuni,
Tuige bila papara, vya kutupa ahueni,
Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
 
Laiti ningejaliwa ustadi wa kutunga shairi ningejibu kishari hii hoja yako. Kaa ukijua kuwa nakuunga mkono, uigaji tunaochukuwa saa hakika ni wa kiafkani.
Hao watoto wa miaka sita na nane wanajua nini kuhusu urembo? si tunawaharibia self esteem zao? Na kuwafanya wafikiri kuwa urembo ndiyo kitu cha maana kuliko kuchapa kazi na kuwa na nidhamu katika kila tufanyacho?

Nawaagiza wasichana kuwa mrembo hakufanya chochote ili awe mrembo, kajaliwa sura kutokana na waliomzaa kuwa na sura na umbile zuri. ( najua najua mtasema kufanya mazoezi, kujua kuvaa, kupakaa poda, na mengineyo) lakini uzuri wa sura ni wa kuzaliwa. mazoezi na poda vyahitaji kipato kikubwa hivyo mabinti wetu kazaneni shule na kuchapa kazi.

Shukrani mwanakijiji.
 
.......
Tuige vilivyo bora, vyenye tunu na thamani,
Tusiwe tunajichora, kwa kuiga vya kihuni,
Tuige bila papara, vya kutupa ahueni,
Kuiga tunakoiga, twaiga na vya kijinga?
Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)

Papara kweli uleke, nimekumbuka msemo
Kuiga hata upweke, ujuha uso kikomo!
Mageti na kuta zake, twaiga bila kisomo
Pokea tano wakwetu, umeyanena maneno!

Utadhani zumbukuku, vichwani kama hazimo
Ni lazima ya kikuku, twaiga bila vipimo?
Usomi wetu mabuku, vichwani mbona hazimo?
Pokea tano wakwetu, uliyonena maneno!

Uliyonena maneno, kimekolea kisomo
Umeonesha muono, uhodari uso kimo
Tuige yalo manono, machafu yawe kikomo
Pokea tano wa kwetu, umeyanena maneno!
 
Hodi malenga nabisha,nami nipate sikika.
Dodoma mpaka Arusha,kwa sauti nasikika
Wino wangu nadondosha,hili jambo lanishika
Kuiga ni jambo pana,Sijui kipi cha kufanya

Wakati watupeleka, Vya ungerezani vya tuvuta
Zamani ninakumbuka,Merekani litushika
Tulijivika kaboka,sarawili na bukuta
Kuiga ni jambo pana,sijui kipi cha kufanya

Kuna swali najiuliza,sipati jibu hakika
Hipu Hopu tunacheza,mdundiko umetupika
Kizuri kinajiuza,kibaya cha paparika?
Kuiga ni jambo pana,sijui kipi cha kufanya

Kuiga kipi nambieni,Kati ya hivi jamani?
Kichupi cha bushimeni,au vithong'i vya marekani?
Baikoko duarani,Au raga sitejini?
Kuiga ni jambo pana,sijui kipi cha kufanya
 
Papara kweli uleke, nimekumbuka msemo
Kuiga hata upweke, ujuha uso kikomo!
Mageti na kuta zake, twaiga bila kisomo
Pokea tano wakwetu, umeyanena maneno!

Utadhani zumbukuku, vichwani kama hazimo
Ni lazima ya kikuku, twaiga bila vipimo?
Usomi wetu mabuku, vichwani mbona hazimo?
Pokea tano wakwetu, uliyonena maneno!

Uliyonena maneno, kimekolea kisomo
Umeonesha muono, uhodari uso kimo
Tuige yalo manono, machafu yawe kikomo
Pokea tano wa kwetu, umeyanena maneno!


Choveki nimekukubali
 
Kuiga kipi nambieni,Kati ya hivi jamani?
Kichupi cha bushimeni,au vithong'i vya marekani?
Baikoko duarani,Au raga sitejini?
Kuiga ni jambo pana,sijui kipi cha kufanya

Du! Kweli umo! Humo kuna falsafa nzito ya utamaduni! Pata na hizi:

1. Tatuu ya Kimarikani, au Chale za Umakondeni?

2. Kujipiasi kwa Uzunguni, au kujitoga kwa Umasaini?

P.S: Hiyo ya 2 nimeitohoa kutoka kwa mwanafalsafa mmoja wa utamaduni!
 
Back
Top Bottom