Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 34,175
- 43,936
Ya'rabi miye nalia
Haya n'nashuhudia
Ya shari twajitakia
Ya mambo ya kuchukia
Kabebwa asobebeka!
Twaona yanatukia
Kama giza latujia
Wenyewe twashingilia
Totoro twaliingia
Kabebwa asobebeka!
Kwa mbwembwe wametujia
Ahadi watumwagia
Tabasamu za udhia
Nazo wanatupatia
Kabebwa asobebeka!
Ati kura watakia
Zamu tena walilia
"Zaidi" waaahidia
Wabongo twashingilia!
Kabebwa asobebeka!
Kasi zaidi zajia
Nguvu zaidi walia
Ari zaidi mamia
Na uzembe zidia!
Kabebwa asobebeka!
Nikisema wachukia
Eti ninapandizia
Chuki isiyoishia
Kwa wale wenye nia
Kabebwa asobebeka!
Sasa nawaulizia
Ni vipi tutafikia
Yale tunayotakia
Kwa mwendo wa kurudia
Kabebwa asobebeka!
Ubovu ukirudia
Kwa kasi ya kuzidia
Fisadi ukimpatia
Nguvu ya kumzidia
Kabebwa asobebeka!
Vipi mtaifikia
Njozi mnayotakia
Mazuri mnayolilia
Si kwamba mmefulia
Kabebwa asobebeka!
Zaidi mwaitakia
Hiyo mtajipatia
Na zaidi mtalia
Huku mnashangilia
Kabebwa asobebeka
Mwenye akili sikia
Ubongo wako tumia
Usifuatie hisia
"zaidi" kukumbatia
Kabebwa asobebeka!
Lazima kuulizia
Ni vipi walishindwia
Zaidi kutupatia
Miaka iloishia?
Kabebwa asobebeka!
Mbona waliwaachia
Mafisadi kutambia
Kamati kuwaundia
Na kesi kuwatungia?
Kabebwa asobebeka!
Mbona hawakutupatia
Ubora wa kuzidia
Elimu ikazidia
Maisha kushangazia?
Kabebwa asobebeka?
Majambazi wazidia
"zaidi" wamejazia
Ni vipi watazidia
Ya zaidi kuzidia?
Kabebwa asobebeka?
Barabara twapitia
Mahandaki yazidia
Na magonjwa pindukia
"zaidi" twajitakia?
Kabebwa asobebeka
Zaidi mwajizidia
Mmezidi twachukia
Mmbwembwe mmetuzidia
Twazidi kuwakimbia!
Kabebwa asobebeka!
Natamati natamia
Beti ninazifungia
Wazo nimewapatia
Ya nini cha kuchukia
Kabebwa asobebeka!
ZAIDI NTAZIDIA
WAKIZIDIA NAZIDIA
NIKIZIDI NAZIDIA
ZAIDIA YA KUZIDIA!
Na. M. M. Mwanakijiji (Ngurumo ya Ushindi a.k.a Sauti ya Kijiji)
shairi lako zuri sana ndugu mwanakijiji lakini ukumbuke kasema mzee Sadan Abdul Kandoro ya kuwa
Mtu chake apendacho,hakina hila machoni
huridhika kuwa nacho, japo hakina thamani
mapenzi hayana kicho, yaamkapo moyoni
mwenye mapenzi, haoni ingawa macho anayo
kwa maana hiyo hata iweje atabebwa hivyo hivyo kwa kuwa tumempenda
Tutapingana, tutatofautiana lakini wote tukiipenda nchi tunaweza kuikomboa!
utakapojua tunapatana zaidi kuliko kupingana na kutofautiana tutabakia tunashangaana.. LOL
shairi lako zuri sana ndugu mwanakijiji lakini ukumbuke kasema mzee Sadan Abdul Kandoro ya kuwa
Mtu chake apendacho,hakina hila machoni
huridhika kuwa nacho, japo hakina thamani
mapenzi hayana kicho, yaamkapo moyoni
mwenye mapenzi, haoni ingawa macho anayo
kwa maana hiyo hata iweje atabebwa hivyo hivyo kwa kuwa tumempenda
Aliyasema Sadani, Abdul bin Kandoro,
Alilighani zamani, Wakati giza totoro
Zile Zama ujanani, elimu yetu totoro,
Kwa nini bado tubebe, kitu kiso na thamani?
Mapenzi hayana kificho, hiyo kweli nakubali,
Chochote nilichonacho, thamaniye ni halali,
watu kutolea macho, thamani yake dalili,
Katu tusiridhike, na kitu kiso thamani.
Mtu chake apendacho, budi kupendwa na wengi,
kuonwa na kila jicho, kusemwa na walio wengi
Umma ukisema hicho, pasipo kujali rangi
Kitu chenye thamani, ni kinachopendwa na wengi