Kosa Langu - 5

Kosa Langu - 5

plan z

JF-Expert Member
Joined
Jun 10, 2019
Posts
1,395
Reaction score
1,439
SIMU/WHATSAPP: 0768571786

Leyra Lacena alikua msichana wa kipekee sana, alikua na uvumilivu wa ajabu hakutaka kunichoka mapema kiasi kile, alipoona jitihada zake hazijazaa matunda aliamua kunipeleka nyumbani kwao, alinitambulisha kwa wazazi wake na ndugu zake wawili wa kike ambao wote kwa pamoja walinipokea kwa uchangamfu mkubwa sana jambo lililozidi kuniaminisha kua hakika Leyra Lacena alikua ni mali yangu licha ya kwamba sikua nimemtamkia neno lolote la nakupenda.
Maisha yao yalikua ya kizungu familia yake ilinifurahia sana, hawakujali kuhusu dini yangu, walikua wakarimu sana bila shaka waliupenda uchangamfu wangu jambo lililofanya niwazoee mapema. Mimi pia nilimpelekea nyumbani kwetu kama alivyofanya yeye hapo awali, wazazi wangu na wadogo zangu walimpokea kwa furaha, wote waliushangaa uzuri wake. Nilimtambulisha Leyra kama rafiki yangu, niliogopa kuharibu mambo sababu kwanza sikua nimemwambia Leyra kua nampenda, pili niliwaogopa sana wazazi wangu hasa baba yangu ambaye siku zote alinisihi niachane na habari za wanawake mpaka muda sahihi utakapofika.

Furaha yote ilidumu kwa muda mfupi kwani baada tu ya kurudi chuo habari za Lucyra ziliwafikia wazazi wangu, waliniita nyumbani, bila hatia yoyote walinigombeza kama mtoto mdogo. Hukumu ya mateso yote ya Lucyra ilikua juu yangu, waliogopa kuvunja ujirani mkubwa wa familia zetu ambao ulikua umedumu kwa muda mrefu. Sikuwafanyia jeuri niliheshimu mawazo yao lakini sikuyaunga mkono, ilikua ni too late tayari, kwangu ilikua ni rahisi kwa Tanzania kuchukua kombe la dunia kuliko mimi kumuacha Leyra.
Wakati maradhi ya aibu yakiendelea kunitesa maradhi ya mapenzi nayo hayakua nyuma kumtesa Lucyra, ilikua afadhali yangu kwa sababu maradhi yake yeye yalizidi kuongezeka siku hadi siku. Kwake hospitali iligeuka kua kama chooni sababu ya kwenda mara kwa mara, kulazwa kwake ilikua ni kama dozi, badala ya saa mipira ya plastiki ilining’inia mikononi mwake, aliongezewa maji mara kwa mara sababu ya kupungua kwake.

Jambo hili liliwaumiza sana wazazi wake, hawakunisemesha neno lakini nyuso zao zilionyesha wazi chuki yao iliyokua juu yangu, waliniona kama msaliti niliyemsaliti binti yao na kumuacha awe mtu wa kuteseka kila siku kwa sababu ya mapenzi. Kutojali kwangu wala kuogopa kitu chochote kulizidi kuwakasirisha, kwa kinyongo na chuki nyingi juu yangu waliamua kuhama Dar es salaam, walihamia Arusha, walimuhamisha na binti yao Lucyra pia hawakutaka anione tena kama ilivyokua kwao.

Kuvuja kwa pakacha nafuu kwa mchukuzi, kuhama chuo kwa Lucyra ilikua ahueni kwangu sababu nilipata uhuru wa kua na Leyra muda wote. Furaha yangu hiyo kwa Daniel ilikua msiba kuhama chuo kwa Lucyra lilikua pigo kubwa sana moyoni mwake, kwake kumuona Lucyra ana kwa ana kila siku ilikua ni furaha tosha licha ya kwamba hakua amekubaliwa.
Katika moja ya nyimbo zake Marehemu Remy Ongala aliwahi kuimba kua kipenda roho hula nyama mbichi, kipenda roho haoni wala hasikii, hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Daniel, kwake kukaa mbali na Lucyra ilikua ni mateso makali, wiki moja tu toka Lucyra ahame chuo, Daniel alianza kukonda.
Mapenzi ni kitu cha ajabu sana, yaone tu kwa mwenzako akiteseka, unaweza kumuona kama chizi lakini hujui kile anachokihisi moyoni mwake. Hata uwe gaidi kama Osama na misuli mikubwa kama The Rock mbele ya mapenzi utakua mdogo kama panado za Kenya. Hata anko Magu pamoja na kutumbua kote akifika kwa mama Janeth anakua mpole kama kifaranga cha njiwa.

Hivyo ndivyo ilivyokua kwa Daniel wiki moja bila kumuona Lucyra ilitosha kumtesa, kama mwanzo alijua asipofanya kitu lazima atateseka zaidi kama sio kufa kabisa. Katika mazingira ya kushtukiza Daniel nae alihama chuo bila hata kuaga.
Kuhama kwake kulihashiria uchaguzi, uchaguzi mdogo wa Cr ulifanyika kwa bahati nzuri nilichaguliwa kushika mahala pake. Nilikua Cr mpya, nilijiona kua miongoni mwa vijana wachache wenye bahati, kua Cr ni jambo la kawaida lakini kwangu lilinisaidia sana, ufaulu wangu ulianza kuongezeka sababu kiongozi yoyote lazima uongoze kwa mifano.
Bado naendelea kuyashangaa mapenzi, mapenzi ni kitu cha ajabu sana sababu kuhama kwa chuo kwa Daniel na kumfuata Lucyra alipo bado haikumzuia Lucyra kunikumbuka. Licha ya kwamba nae alihamishwa chuo lakini bado aliendelea kunikumbuka.

Mwanamke akipenda amependa kweli, Lucyra alikua kama kupe hakuchoka kunikumbuka hata mara moja. Mara kwa mara alinitafuta WhatsApp, huko alinitumia picha nyingi za utotoni tulizopiga wote wakati tukikua na kuifurahia michezo yetu ya kitoto pamoja. Kila muda aliomba nimtumie picha zangu.Lucyra hakunichukia alizidi kuniambia kua bado ananipenda sana na kila dakika kila saa hua ananifikiria. Kila siku aliponitafuta aliuliza kuhusu hali yangu pia alinijuza kuhusu maendeleo ya afya yake ambapo kutokana na maelezo yake bado alikua akisumbuliwa na maradhi ya mapenzi juu yangu.

Kadri maradhi ya mapenzi yalivyodhidi kumtafuna Lucyra na kumfanya azidi kudhoofika ndivyo maradhi ya aibu nayo yalivyozidi kunitafuna na mimi. Kuhama kwake chuo hakukunisaidia chochote zaidi ya kunipa ukaribu mkubwa na Leyra ambapo licha ya ukaribu huo bado nilishindwa kumueleza Leyra hisia zangu mpaka muda huo.
Dar es salaam jua lilizidi kua kali, watu wengi mitaani waliendelea kutafuta pesa kwa udi na uvumba. Chuoni nako masomo yalizidi kua magumu kila mwanafunzi alikua bize kusoma kwa bidii kuhakikisha anafaulu mitihani yake yote.
Sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi, miezi, mwaka, hatimaye miaka ilikatika, polepole kama mwendo wa kinyonga mjane email, simu na meseji za Lucyra zilianza kupungua. Ilianza kupita siku moja bila kupata simu wala ujumbe wowote kutoka kwake hatimaye wiki hadi miezi ikawa inapita bila kupata simu wala ujumbe wowote kutoka kwake. Kwangu kilikua sawa sikujali chochote kwa sababu sikua nikimpenda.

Tulikua mbioni kumaliza mwaka wa pili, mpaka wakati huo sikua nimemtamkia Leyra neno nakupenda. Tulikua na ukaribu mkubwa sana kila mtu alidhani tulikua wapenzi lakini haikua, kitu pekee nilichoambulia kwa Leyra mpaka wakati huo ilikua ni kuyabusu mashavu yake na kumkumbatia sababu ya ule ukaribu wetu.Muda wa mitihani ulifika, chuoni kila mwanafunzi alikua bize kusoma. Tulikua tunamaliza mwaka wa pili wa masomo. Tulifanya mitihani ya kumaliza semista, mitihani ilikua migumu sana lakini kwa neema za Mungu tulimaliza salama. Baada ya kumaliza mitihani tulifunga chuo na kwend likizo ndefu ya field muda wa miezi mitano.

Muda wa likizo miezi mitano kwangu ilikua ni kama mwaka, kama ilivyokua kwa Daniel mimi pia sikuweza kukaa mbali na Leyra, hali hii ilinitesa sana lakini sikua na jinsi zaidi ya kukabiliana nayo. Nilijitahidi sana mara kwa mara tukawa tunawasiliana, muda mwingi wa likizo ya field tulitumia ku chat na kuongea kwa video call kila siku.
Hali hii ilidumu kwa miezi kadhaa ya mwanzo lakini ghafla ilianza kubadilika polepole. Leyra aliacha kujibu meseji zangu, mwanzo nilidhani bahati mbaya lakini haikua, kila meseji niliyotuma WhatsApp aliisoma lakini hakunijibu, sikutaka kukata tamaa kwa sababu nilikua nampenda, niliendelea kumtafuta lakini cha ajabu hata nilipompigia simu hakupokea tena wakati mwingine alikata kabisa.


......... Itaendelea .........
 
Back
Top Bottom