Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
Kivuko cha Mv Magogoni kinachotoa huduma kwa wananchi kutoka upande wa bahari eneo la Magogoni kuelekea Kigamboni Jiji la Dar es Salaam kimesitisha kutoa huduma kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo makubwa.
Katika taarifa iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme(TEMESA) Mhandisi Manase Ole Kujan kwa niaba ya Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano imesema kuwa kuanzia Mei 5 2016 kivuko hicho kitakuwa katika matengenezo makubwa ambayo yatafanya kusitisha huduma zake kwa muda.
Taarifa hiyo imesema kuwa huduma za kivuko zitaendelea kama kawaida kwani wananchi watatumia huduma ya kivuko cha Mv Kigamboni pamoja na kivuko kilichokodishwa na Serikali kutoka kampuni ya Azam Marine vitavyokuwa vinasaidia kutoa huduma kwa wananchi kwa muda wote ambao Mv Magogoni itakuwa katika matengenezo.
“ Muda wake wa matengenezo umefika na ni wakati muafaka kwa kivuko kwenda kwenye matengenezo ni muda mrefu kimetumika na kusimama kwa kivuko hiki hakutaleta madhara makubwa kwani mara baada ya kuzinduliwa kwa daraja la Nyerere hivi karibuni tuna imani wananchi watatumia daraja hili ili kendelea na shughuli zao za kila siku” imesema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo wananchi wenye magari wanaotumia vivuko hivyo wameshauriwa kutumia daraja jipya la Nyerere ili kuepukana na usumbufu wa kusubiri kivuko pekee cha Mv Kigamboni chenye uwezo wa kubeba magari na kufafanua kuwa kivuko kutoka Azam Marine kina uwezo wa kubeba watu peke yake.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa matengenezo ya kivuko cha Mv Magogoni yatafanyika Jijini Dar es Salaam chini ya usimamizi wa Temesa katika matengenezo ya mitambo na ukarabati na ujenzi utafanywa na kampuni ya kizawa ya na Songoro Marine Transport Yard yenye makao makuu yake Jijini Mwanza.
Aidha kivuko cha Mv Magogoni kitakabidhiwa kesho kwa kampuni ya Songoro Marine Transport Yard kwa ajili ya matengenzo hayo na mara baada ya mkandarasi kuangalia hali ya kivuko atatoa muda kamili wa kumalizika kwa matengenezo ya kivuko hicho.
Serikali katika katika jitihada za kupunguza msongamano katika vivuko hivyo imeamua kwenda kukifanyia ukarabati mkubwa ili kukiongezea uwezo na ufanisi wa kuhudumia wananchi kwa kusaidiana na daraja jipya la Nyerere lililozinduliwa na Mhe. Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt john Pombe Magufuli hivi karibuni ili kuondoka na tatizo la msongamono kwenye vivuko vya Kigamboni.
Source: Michuzi