Hussein Massanza
JF-Expert Member
- Dec 26, 2012
- 1,016
- 2,195
Rais John Magufuli leo amemteua Prof Kitila Mkumbo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Kitila pia ni mshauri, vilevile mwanachama wa ACT-Wazalendo.
Uteuzi wa Kitila una athari nyingi kutokana na uhusika ambao yeye mwenyewe amekuwa akiuonesha kwa umma. Kitila ni msomi, mwana mageuzi, mchambuzi wa siasa, jamii na taaluma. Kitila ni mkosoaji wa Serikali kwa sera na mifumo yake mbalimbali. Huyo ndiye Kitila.
Eneo la Kitila kuwa mwana mageuzi, mchambuzi na mkosoaji kisha kutambulika kuwa mmoja wa waasisi na mwanachama mwenye daraja kubwa ACT-Wazalendo, hapo ndipo kunakosababisha maneno yawepo. Je, ni sahihi Kitila kupokea uteuzi? Huo ndiyo mzizi!
KITILA NI MTANZANIA
MOSI; Unapokuwa Mtanzania wa kweli, lazima uwe na tamaa ya kuijenga nchi yako kwa uwezo wote unaokuwa nao. Ukipewa nafasi ya kuitumikia nchi yako hiyo ni baraka, huo ni uteule, hupaswi kulaza damu.
PILI; Dhana hii ifahamike, kwamba vyama pinzani na tawala, vyote malengo ni kujenga nchi, isipokuwa chama tawala kina nyenzo (Serikali), wapinzani wao hupaswa kuwa macho kuhakikisha nyenzo (Serikali), inatumika vizuri kwa ajili ya nchi. Ndiyo maana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni huitwa Serikali Kivui.
Kama ujenzi wa nyumba, mpinzani ni fundi mtazamaji, akiona tofali linapindishwa anatakiwa kusema “hilo tofali halipo sawa”, ukiwa chama tawala, maana yake wewe ndiye mjenzi mtendaji, kwa hiyo unatazamwa. Mjenzi mtendaji na mjenzi mkosoaji, wote lengo ni kuhakikisha nyumba inakuwa bora.
TATU; Kitila ameteuliwa na Rais Magufuli, huyu ni Mkuu wa Nchi, hivyo si adabu kumkatalia. Hata kama hataki kwa kuona hawezi kufanya naye kazi, vema kumheshimu kwa nafasi yake, nyakati zijazo akiona kazi haziwezi kwenda, atakuwa huru kuachia ngazi.
Tunahitaji kuwa na upinzani wa kisiasa wenye mizizi ya upendo na kuheshimiana. Viongozi wawe na angalizo baina yao kwa nafasi zao. Kukataa uteuzi wa Rais kwenye kadamnasi, inaweza kutafsiriwa kuwa kuna chuki kati ya anayeteua na aliyeteuliwa au chuki ya vyama vyao, vilevile kukataa uteuzi ni twezo kwa mteuzi.
NNE; Je, unakuwa mpinzani kwa sababu unapenda kubisha na kukosoa au unaona yapo mambo yanakosewa? Kama msingi ni kuona mambo hayapo sawa, Kitila amepewa kazi kubwa mno, kazi ya kuwa mtendaji mkuu wa wizara, kwa hiyo ni matarajio kuona mabadiliko chanya kwenye wizara hiyo. Alichokuwa anakikosoa tukione wizarani kwa vitendo.
Katibu Mkuu wa wizara ni mtumishi wa umma namba moja kwenye wizara husika. Waziri na naibu wake wanakuwepo kuhakikisha uwajibikaji wa kisiasa unakuwepo, hii ni kwa sababu Serikali inasimamiwa na wanasiasa.
Waziri na naibu wake wanakuwepo kuhakikisha ule utashi wa kisiasa unatimia. Ilani ya chama tawala inatekelezwa, mipango ya wanasiasa waliopewa hatamu ya kuongoza Serikali inapata usimamizi. Hata hivyo, mtendaji mkuu wa kila kitu kwenye kila wizara ni Katibu Mkuu. Basi Kitila aende akatende na utofauti uonekane!
NADHARIA ZA UTEUZI WA KITILA
MOSI; Rais Magufuli anamkubali Kitila kwa uwezo wake wa kutazama mambo na kujenga hoja, kwa hiyo ameamua kuweka kando tofauti za kisiasa na ukosoaji wake, hivyo kuamua kumtumia ili kujenga nchi moja?
PILI; Rais Magufuli ameona ndani ya chama chake (CCM), katika idara za Serikali na kwenye mashirika ya umma, hakuna mtu mwenye kuweza kuimudu kazi ya kuwa mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku za Wizara ya Maji na Umwagiliaji, hivyo Kitila pekee ndiye anafaa?
TATU; Prof Kitila alikuwa muwania ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), akiwa na tiketi ya ACT. Hali hiyo ilisababisha mvutano wa kuwania nafasi za upinzani na Chadema ambao mwishoni kanuni ziliwabeba, kwamba ndiyo wenye kustahili kuwa na wabunge wawili EALA pamoja na Cuf mmoja.
Je, Rais Magufuli ameamua kuikomoa Chadema, kwamba amekosa EALA kisha yeye anampa majukumu makubwa zaidi serikalini?
NNE; ACT ni chama kichanga, Kitila amekuwa mmoja wa vichwa visafi katika uchakataji wa fikra za ujenzi wa chama. Kitendo cha Kitila kuwa Katibu Mkuu wa wizara, maana yake ACT kitakosa huduma yake. Je, Rais Magufuli ameona akiue ACT kwa kuchomoa moja ya nguzo zake? Kitila ni nguzo ACT.
TANO; Prof Kitila ni mkosoaji wa Serikali, siyo mwoga, tena hukosoa kisomi, bila jazba wala matusi. Na ukosoaji wa hoja bila jazba hupenya zaidi kwenye fikra za watu. Je, Rais Magufuli amemwona Kitila ni mwiba wa fikra za Watanzani dhidi ya Serikali yake, kwa hiyo amemteua ili kumfunga mdomo?
Maana ni juzi tu Kitila alihoji uhusiano wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Rais Magufuli, hasa baada ya Magufuli kumtengua aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akimkingia kifua Makonda.
Hoja ilikuwa Makonda kufanya uvamizi kwenye kituo binafsi cha matangazo ya televisheni, cha Clouds TV na kulazimisha kurusha kipindi alichokitaka yeye. Nape alisimamia sheria lakini Magufuli alimwachisha kazi kumlinda Makonda. Kitila alihoji kuna nini kati ya Rais na RC wa Dar?
HASARA ILIPO
Kuna msemo kwamba mtu anapooa, tunasema kambi ya mabachela imepata pigo. Hivyo, jamii ya wachambuzi, wakosoaji, wasahihishaji wa mambo, ni pigo kwao kwa Kitila kuwa sehemu ya Serikali, maana maadili ya kazi hayatampa fursa ya kukosoa, itabidi awe anamezea.
Hasara hii ipo pia kwake binafsi, kwamba yapo mambo ambayo atatamani kujenga hoja na kushauri tofauti, lakini hataweza. Majukumu ambayo Kitila amepewa, pamoja na nguvu kubwa ya kiutendaji anayopata katika wizara yake, upande wa pili, analazimisha awe kipofu kwa madudu mengine serikalini, na hata akiona basi awe bubu.
Hasara kwa wasomi, Kitila angeendelea kufundisha chuo ili kukifaa zaidi kizazi kipya cha wasomi, angeendelea kufanya utafiti na kushauri mambo mbalimbali ya kitaalamu, hasa eneo la Elimu na Saikolojia ambako amebobea zaidi.
Hasara kwa upinzani, maana pamoja na tofauti za vyama, zipo nyakati ambazo wapinzani waliposimama pamoja, mawazo ya Prof Kitila yalikuwa mbolea yenye kustawisha hoja na misimamo ya kambi. Nasisitiza; hasara kubwa zaidi ipo ACT kwa uchanga wao, maana walimhitaji mno Kitila kwa uzoefu na maarifa yake.
NIA NI NJEMA
Hivyo ndivyo naamini, kwamba uteuzi wa Kitila umefanyika kwa nia njema kwa nchi, hivyo pongezi kwa kila upande. Rais Magufuli kwa kuona tofauti za kisiasa siyo muhimu mbele ya maslahi ya nchi. Pongezi kwa Kitila kutokana na sifa zake nyingi ambazo zimemvutia Rais Magufuli.
Hivi ndivyo inapaswa kuwa, maana upinzani wa kisiasa siyo uadui, bali ni ushindani wa hoja za namna bora ya kuongoza dola. Ni ushindani wa itikadi, falsafa na nadharia sahihi za ujenzi wa dola. Siyo vita.
Hata wakati mwingine, itakuwa afya kwa nchi kama Rais Magufuli ataonesha nia ya kufanya kazi na Rais wa Jamii ya Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, kisha Lissu naye akubali.
Itapendeza zaidi kama Rais Magufuli ataonesha nia ya kufanya kazi na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kisha Mbowe aridhie. Na kufanya kazi siyo mpaka kumteua katika nafasi fulani, la hasha! Hata kuketi meza moja na kunywa kahawa kisha kubadilishana mawazo ya kujenga nchi, hivyo pia ni kufanya kazi pamoja.
Rais Magufuli kuazima mawazo ya wapinzani katika Serikali anayoongoza ni jambo jema. Wapinzani pia kumshirikisha Rais Magufuli mawazo yao kwa ajili ya nchi ni afya.
ACT pia hawapaswi kuchukulia uteuzi wa Kitila katika sura hasi kwamba Rais Magufuli amebomoa chama chao, bali upande mwingine wajipongeze kuwa walikuwa kwenye timu moja na mtu bora ambaye Rais wa Nchi ameona anafaa amepewe majukumu makubwa ya kiserikali.
Kama chama, wanapaswa kumpa kila la heri na kumuaga kwa heshima, pengine nyakati zijazo wakawa pamoja tena kwenye timu. Kikubwa ni uhai, lakini maisha ya binadamu na safari zao, husababisha dunia ionekane inazunguka sana. Ipo kesho!
Mungu Ibariki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Imeandikwa na Mchambuzi Luqman Maloto