MLANGO WA 9
NGUVU ZA WAGANGA KATIKA NCHI
Waganga walikuwa na nguvu katika nchi, na kupewa heshima nyingi. Walikuwako waganga wa namna nyingi; kama wale wa kuleta na kukomesha mvua, wa kutibu wagonjwa na wale waliokuwa na ujuzi wa kutazama utumbo wa ng'ombe au mbuzi na kondoo. Kila Mchagga aliamini kuwa maisha yake yalikuwa mikononi mwa waganga ambao walijua habari zote za miili yao. "Wamangi" waliwaheshimu waganga pia kwa sababu kila kitu waganga walichosema Wamangi" walifuata. Kama “wamangi" walitaka kitu fulani kifanyike waliwaita kwanza waganga na kuwauliza kama ilikuwa vizuri kitu hicho kitendeke au sivyo. Kama waganga walisema kisitendeke, "wamangi" hawakukifanya
kitu hicho.
Waganga walikuwa na maarifa mengi. Walipewa heshima na watu kwa sababu walikuwa na kazi ya kutunza afya ya watu. Walikuwa na madawa mengi ya majani na maganda ya miti yaliyoponya magonjwa mengi. Ni ajabu kwamba magonjwa mengine yaliyoponywa na madawa haya wakati Wazungu walipofika, hawakuweza kuyaponya kwa madawa ya Kizungu. Mpaka leo hivi yako magonjwa fulani ambayo huponywa na madawa haya lakini madawa ya Kizungu hushindwa.
Waganga hawa walijidai kuelewa na matumbo ya ng'ombe na mbuzi na kondoo; wakati mbuzi wa kutambika alipochinjwa, waganga walikuja kutazama utumbo wake Kama utumbo huo ulikuwa namna fulani, vitu vingi vibaya vilitokea katika nchi.
Waganga walijidai kujua mzunguko wa jua na mwezi. Walitoka nje usiku na kuangalia rangi yake. Kama ulikuwa na rangi nyekundu katika mawingu yaliyouzunguka, walihesabu vitu vingi vilivyotokea mwaka ule. Kama mwezi ulikuwa na rangi nyeupe tu, hii ilikuwa dalili nzuri. Waganga hawa walikuwa wamejifunza kuwa mwezi ulikuwa na rangi fulani saa fulani usiku. Saa zile zilipofika waliwaambia watu waende kutazama mwezi. Walipoona kuwa mwezi ulikuwa na rangi zile walizosema waliamini kuwa waganga walisema kweli.
Wakati “mangi” fulani alipotaka kwenda kupigana na "mangi" mwingine, alimwita mganga na kumwuliza kama watu wake watashindwa au hapana. Kama alisema watashinda "mangi" alimwuliza siku nzuri ya mapigano. Baada ya kutafuta sababu nyingi za kupendelea siku fulani kwa kuanza kupigana mganga alikwenda kwa "mangi" na ku- mwambia siku yenyewe, na siku ile ile vita ilianza.
Waganga walitunga maarifa mengi ya hila ambayo karibu yote yalikuwa ya kujipatia chakula na mali kutoka kwa watu. Kama mbuzi ilichinjwa kwa tambiko, lile tambiko halikutokea vema kama watu wa nyumba ya yule mtu aliyetambikiwa walikula nyama ya yule mbuzi. Nyama karibu zote zilichukuliwa na yule mganga. Watu waliamini kuwa ikiwa mganga hakupewa ujira wake wa kutosha hata kama alitengeneza tambiko la mtu, tambiko lile halikutokea; kwa sababu hii mganga alipewa hata zaidi ya ujira wake ili afurahiwe na kufanya kazi yake vizuri.
Watu maskini katika nchi hawakuweza kulipa ujira wa waganga ijapokuwa walijua iliwabidi kufanya hivyo ili taabu zao ziishe, iliwalazimu kukopa mbuzi na kondoo na kuwalipa waganga. Madeni haya yalizidi hata mwishowe walishindwa kuyalipa. Umaskini siku zile ulikuwa kitu kibaya kwa watu ambao hawakuweza kujisaidia. Watu hawa hawakupenda kuwa maskini bali maisha yao yaliwafanya hivyo. Wachawi waliroga watu na walikuwa na maarifa mengi ya udanganyifu mtupu. Hawakupewa heshima yo yote katika nchi, na walipopatikana kama wanaroga watu walishtakiwa na kuteswa sana hata kuuawa. Makusudi ya wachawi yalikuwa mabaya kwa sababu walitaka kuwaua watu na Wachawi walikuwa na madawa yaliyowekwa katika vibuyu na pembe. Waliwadanganya watu kuwa madawa haya yaliweza kuponya magonjwa. Walipowatibu watu walipigapiga vibuyu na pembe na kuwaambia watu kuwa madawa yaliweza kuponya magonjwa yao. Walipowatibu na kusema hivyo walitazama mbinguni na kutema mate, na huu ulikuwa udanganyifu mtupu.
Wachawi walizika vitu walivyopaka madawa karibu na nyumba za watu. Watu walisadiki vitu hivi viliweza kuwaletea magonjwa. Ilisadikiwa kuwa hakuna mtu aliyeweza kutibu magonjwa yaliyoletwa na vitu vile isipokuwa wachawi. Mara wachawi waliitwa na kuondoa vitu vile, na baada ya kazi yao wakapewa mbuzi au kondoo. Wakati mwingine kama mchawi alimchukia mtu au mwanamke fulani, alimnyemelea usiku na kumzikia vitu vya madawa chini ya kitanda chake.
Maisha ya Wachagga yalitawaliwa na nguvu za waganga ambao waliwatendea mema na walipewa heshima. Lakini wachawi walikuwa watenda maovu na walilaaniwa. Maisha yalikuwa ya taabu kwa mambo haya, na Wachagga wengi waliona kuwa ni nguvu za ajabu ambazo hawakuwa nazo.