Miss Zomboko
JF-Expert Member
- May 18, 2014
- 4,618
- 9,611
OFISA wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Msadizi wa Polisi (ASP), Lydia Ngua (43) amefi kishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka 22 ya kujipatia fedha Sh 489, 615,000 za upatu kutoka kwa watu mbali mbali wakiwamo maofi sa wa jeshi hilo.
Ngua alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mbando.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Ester Martin alidai kuwa katika tarehe isiyofahamika jijini Dar es Salaam, mshitakiwa huyo alijipatia Sh milioni 15.3 kutoka kwa Happy Mhando kwa nia ya kwenda kuziwekeza kwenye vikoba huku akijua kuwa anaenda kuzitumia kwa matumizi yake binafsi.
Martin alidai Septemba 13, mwaka jana jijini Dar es Salaam, Ngua alijipatia Sh milioni 13.2 kutoka kwa Elisia Kisoma. Pia alidai katika tarehe na mahali kusikofahamika jijini Dar es Salaam, mshitakiwa huyo pia alijipatia Sh milioni 7.8.
Katika mashitaka ya nne, inadaiwa kuwa katika tarehe na mahali kusikofahamika ndani ya Jiji la Dar es Salaam, Ngua alijipatia Sh milioni 12.3 kutoka kwa Mariam Yohana. Wakili Martin alidai katika mashitaka ya tano kuwa mshitakiwa huyo alijipatia Sh milioni 3.4 kutoka kwa Jenifa Fokanya. Alidai kuwa mshitakiwa huyo alijipatia Sh milioni 15 kutoka kwa Jane Martin, pia alijipatia Sh milioni 20.8 kutoka kwa WP Mary.
Inadaiwa mshitakiwa huyo pia alijipatia Sh milioni 10.9 kutoka kwa maofisa wa jeshi hilo, ambao ni Mrakibu Msaidizi Imelda Twelve pamoja na kujipatia Sh 9,040,000 kutoka kwa Mrakibu Msaidizi Sarah Komba. Mshitakiwa huyo pia anadaiwa katika tarehe na maeneo yasiyofahamika jijini Dar es Salaam, alijipatia Sh milioni 67 kutoka kwa Inspekta wa Polisi, Richard Ninja na Sh milioni 27 kutoka kwa Shukuru Makaranga.
Ngua anadaiwa kuwa katika tarehe zisizofahamika jijini Dar es Salaam, alijipatia Sh 115,897,000 kutoka kwa Henry Lwiza na katika mashitaka ya 13, inadaiwa alijipatia Sh milioni 75 kutoka kwa Edna Mbeto. Ofisa huyo pia anadaiwa alijipatia Sh milioni 11 kutoka kwa Sabrina Mwakitalu pamoja na kujipatia Sh milioni 23.3 kutoka kwa Lusiana Mwakitalu. Katika mashitaka ya 16, inadaiwa mshitakiwa huyo alijipatia Sh milioni sita kutoka kwa Mwanahamisi Issa, pia alijipatia Sh milioni 3.78 kutoka kwa Mkemimi Abdulkarim na Sh milioni 191.4 kutoka kwa Zidadu Hassan.
Martin aliendelea kudai kuwa, mshitakiwa huyo katika tarehe na maeneo yasiyofahamika ndani ya jiji hilo, alijipatia Sh milioni 4.322 kutoka kwa Innocent Nunuo. Katika mashitaka ya 21, Martin alidai kuwa Ngua alijipatia Sh milioni nane kutoka kwa WP Happy.
Pia anadaiwa alijipatia Sh milioni 37.7 kutoka kwa Halima Nabalanganya inadaiwa kuwa mshitakiwa alijipatia fedha hizo kwa nia ya kwenda kuziwekeza kwenye vikoba huku akijua kuwa anaenda kuzitumia kwa matumizi yake binafsi.
Mshitakiwa huyo alikana mashitaka na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, hivyo aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mbando alimtaka mshitakiwa kuwasilisha mahakamani hapo nusu ya fedha, anazodaiwa au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Pia alimtaka kuwa na wadhamini wawili, wanaotoka kwenye taasisi zinazotambulika au vitambulisho na wadhamini hao pia wametakiwa kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika.
Mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo, hivyo alipelekwa rumande. Hakimu Mbando aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 24, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.