Kiso chako hakishikiki

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,284
1463371184210.jpg

Ufanye uende mbio, kaskazi mashariki,
Ubebe na kuku kwio, kwa ndumba unihiliki,
Yote yawa kifagio, kwa uwezo wa Maliki,
Jalali sio babio, elewa sihadhiriki.
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Mja kalisha kalio, hazina pato shiriki,
Fanya uweke fungio, huta zuia riziki
Waja angua kilio, useme na hizo chuki,
Mola wangu kimbilio, wallahi sifedheheki,
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Nimegundua mwenzio, tabasamu lako feki,
Watia kinukajio, kwa chips na mishikaki,
Umepaka kipambio, sumu nipate fariki,
Rabi kahuluku "sio" ndio mana sianguki
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Ulo nalo kusudio, fahamu halisomeki,
Uweke na kikingio, kiso chako hukishiki,
Ingia kwa kitubio, umrudie Razaki,
Jalali kaumba "ndio" kwahivyo sitetereki.
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Wanisema kwa wenzio, vile isivyo stahiki,
Mithili ya kisusio, mdomoni sikutoki,
Neno mwenziwe sikio, halichomi si mkuki,
Mungu tanipa tulio, hakika sibabaiki.
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Umeshika mchinjio, na bado haushutuki,
Chakughuri kilalio, kiumbe hauzinduki,
Punguza matamanio, dunia haibebeki,
Rabi nipe kifutio, nifute zako falaki
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Alokupa mtwangio, na kinu simdhihaki,
Kuna siku ya chungio, kiumbe huiepuki,
Hivyo situpe dekio, kesho haitabiriki,
Hapa pana zingatio, wajibu nduguye haki,
Kiso chako hukishiki, hata kwa lake shikio.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
0622845394 Morogoro
 
Back
Top Bottom