nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,860
- 5,803
Na Farida Ramadhani
MWANASIASA mkongwe nchini, Kingunge Ngombare Mwiru amesema waliharibu mwanzoni kabisa walipochanganya miiko ya viongozi na miiko ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi hicho, kwani kumekuwa na tatizo la ufuatiliaji ambalo linawaachia viongozi kujinufaisha badala ya kufanya kazi kwa ajili ya nchi.
Alisema kuwa tatizo la maendeleo ya sasa ni kutokana na kuacha misingi ya Azimio la Arusha ambalo lilikuwa linaeleza wazi misingi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na miiko ya viongozi iliyowataka kutotumia madaraka yao kujinufaisha.
Kingunge alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika kilele cha maadhimisho ya tano ya Tamasha la Kigoda cha Mwalimu Nyerere ambapo mjadala ulikuwa ni Maendeleo ni Mapambano ya Ukombozi uliozungumzia Azimio la Arusha na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Tuliiweka miiko ya viongozi kwenye katiba ya chama, lakini hakuna ufuatiliaji wa hiyo ibara ya 18 ya katiba, tunasaini fomu za mali tulizonazo kabla ya
uongozi, lakini nani anafuatilia unapoacha uongozi? Hamna, alisema.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) alisema kuwa njia pekee ya kuiinua nchi kiuchumi ni kufuata misingi ya Azimio la Arusha ambalo lilikuwa linasisitiza kupinga unyonyaji kwa kujikwamua, hususani katika masuala ya kilimo.
Alisema kuwa ingawa Azimio lilikuwa na upungufu wake, lakini liliweza kufanya vizuri katika maendeleo ya nchi huku akitolea mfano jinsi lilivyoinua biashara ya zao la korosho pamoja na tumbaku.
Zitto alisema kuwa Azimio lilikuwa na lengo la kuleta maendeleo endelevu, lakini limepuuzwa na nchi kuingizwa kwenye dira ya maendeleo ambayo inaangalia maendeleo ya nchi hadi 2025, hali inayomuwia vigumu kuelewa kama kweli mwaka huo ni mwisho wa maendeleo.
Alisema kuwa azimio lilijikita zaidi kwenye maendeleo vijijini, lakini dira hiyo imetilia msisitizo zaidi kwenye viwanda ambavyo vinaaminika kukuza uchumi kwa haraka bila kujali masuala ya kilimo wakati katika nchi masikini kama Tanzania kilimo ndiyo uti wa mgango.
Mwalimu Nyerere alisema kuwa ujinga ni kudhani kuwa fedha ni chanzo cha maendeleo. Na mimi nasema ujinga ni kufikiria kuwa uchumi utakuwa wakati tumekitupa kilimo. Asilimia 75 ya Watanzania ni watu wa vijijini na maendeleo ya kweli yanatoka vijijini inabidi tuinue kilimo, alisema.
Baadhi ya wanazuoni walioshiriki tamasha hilo walisema kuwa maendeleo ya taifa yanazidi kuzorota huku wananchi wachache wakifaidika na uchumi wa taifa kutokana na viongozi kuogopa kirusi cha Azimio la Arusha ambacho ni ujamaa.
Walifafanua kuwa woga wa kirusi hicho umesababisha nchi kukisahau kilimo kuwa ndicho chanzo cha maendeleo ya kiuchumi badala yake imekuwa ikitilia msisitizo maendeleo ya viwanda pamoja na ubinafsishaji ambao unawafaidisha wachache.