Kinana,Nape wataka waliokula Escrow wang'oke

Donatila

JF-Expert Member
Oct 23, 2014
7,565
21,562
Nape-Nauye--December2-2014.jpg

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.

Sakata la uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Escrow Tegeta iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kuwahusisha vigogo kadhaa wa Serikali, viongozi wa dini na watu binafsi, limeendelea kuwa gumzo kubwa nchini.

Watendaji wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepongeza maamuzi yaliyotolewa na Bunge kuhusiana na tuhuma za uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti hiyo.Pia wameiomba Serikali iharakishe kuchukua hatua stahiki dhidi ya wale wote waliohusika.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Itikani na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, wakati akihutubia mamia ya wakazi wa wilaya ya Mtwara, katika mkutano wa kuhitimisha ziara ya siku 16 ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, katika mikoa ya Lindi na Mtwara ya kukakua, kuhimiza na kusukuma utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010/15.

Alisema chama hicho kinaendelea kudumu kutokana na kufuata maadili ya uongozi na kwamba hakiwezi kudumu kama maadili ya uongozi yatapuuzwa.

“Tunapongeza maamuzi ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kazi waliyoifanya ni nzuri. Wito wetu kwa serikali ni kwamba iharakishe kutoa adhabu stahiki kwa wale wote waliobainika kukiuka kanuni za uongozi,” alisema Nape.

Alifafanua kuwa kama kanuni za chama hicho zinavyoeleza, cheo ni dhamana na kwamba mwanachama hatatatumia cheo chake kwa ajili ya manufaa yake binafsi.Nape alisema hivyo ndivyo viongozi wanavyotakiwa kuwa.

Alisema chama hicho ndio chenye waasisi wa maadili ambao walikemea na kukataza maovu ikiwa ni pamoja na kuwafukuza walioshindwa kufuata maadili.

“Chama hiki ndicho kinachokemea maovu, ndiyo chama chenye maadili, hakiwezi kutetea wanaovunja kanuni na taratibu za uongozi kwa manufaa yao binafsi,” alisema Nape.Kwa Upande wake Kinana, alisema viongozi wasio watendaji ndani ya serikali wanatakiwa kufukuzwa.

Alisema heshima ya CCM itatokana na viongozni na watendaji kuwajibishana pindi wanaposhindwa kutimiza wajibu wao.

“Chama hakiwezi kulea uovu, lazima tuwajibishane, ukishindwa kutimiza wajibu wako achia ngazi, na pindi kiongozi anapofanya vizuri atapewa sifa zake, chama hakiwezi kuendelea kulea maovu,” alisema Kinana.

Alifafanua kuwa viongozi ni lazima wafuate maadili aliyoyasimamia Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

“Mwalimu alikuwa anakemea uovu, na sisi lazima tufuate nyayo zake, CCM ni chama pekee kinachoweza kuiongoza nchi hii kwa amani na ushirikiano, hivyo tusione haya kuwajibishana pindi mtu anapokosea,” alisema Kinana.

MAALIM SEIF: ZANZIBAR IMEATHIRIKA
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema Zanzibar imepata athari kubwa kwa kukosa fedha za wafadhili kutokana na wizi wa fedha hizo katika akaunti hiyo uliohusisha baadhi ya viongozi serikalini.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CUF katika viwanja vya Mkokotoni, jimbo la Tumbatu mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aliitaka baadhi ya miradi inayoathirika kutokana na uamuzi wa wafadhili kusitisha misaada kufuatia kashfa hiyo ni wa Millenium Challenge Corporation (MCC)kutoka Marekani, ambao unasaidia huduma za umeme na ujenzi wa barabara.

Alisema Zanzibar pia inanufaika na misaada ya kibajeti na ile inayotolewa na Mfuko wa Dunia (Global Fund) maeneo ambayo pia yameathirika kutokana na uamuzi wa wafadhili hao ambao hawakuridhishwa na wizi wa fedha hizo.

“Zanzibar tumeathirika sana kuna miradi mingi imesitishwa kwa kashfa hiyo ya Escrow, lakini pia hakuna Mzanzibari hata mmoja aliyetajwa kunufaika na fedha hizo, tungekuwa na mamlaka ya kujiamulia mambo yetu yasingetokea hayo”, alisema.

BAVICHA: PINDA AMELINDWA
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bavicha) Tanzania Bara, Hawa Mwaifungu, amesema wabunge wa CCM wamejaribu kulinda mjadala wa Esrow kwa kuhofia aibu ya kuvunjwa tena kwa baraza la mawaziri. Aliyasema hayo wakati akiwahutubia wanachama wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Magogoni, Zanzibar.

Alisema wabunge hao wamekuwa wakisimama kidete kutetea uchafu unaofanywa na baadhi ya viongozi wao na kuwataka wananchi wasikubaliane na vitendo hivyo.

“Wamejaribu kulinda ili kumlinda waziri Mkuu kwa kuhofia aibu ya kuvunjwa baraza la mawaziri mara mbili huku Rais Jakaya Kikwete akibakiwa na muda mfupi wa kuondoka madarakani,” alisema.

TAKUKURU: TUMEANZA KUCHUNGUZA
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru), imesema imeanza kazi ya kuchunguza sakata hilo na walionufaika na mgawo wa fedha hizo.

Akizungumza na NIPASHE jana, Mkurugenzi wa Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Edward Hoseah, alisema kazi hiyo imeanza, ingawa hakuwa tayari kuzungumzia kwa undani kuhusiana na watu wanaowachunguza.

“Kazi ya kuwachunguza walihusika katika sakata hilo ilishaanza mara moja na tunaendelea na uchunguzi, ”alisema Dk. Hoseah kwa kifupi.
Kwa mujibu wa maazimio ya Bunge yaliyoamuliwa jumamosi iliyopita, Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vinatakiwa kuchunguza na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi.

Miongoni mwa wanaopaswa kuchunguzwa ni mmiliki wa Kampuni ya PAP, Harbinder Singh Sethi na Mkurugenzi wa Kampuni VIP Engineering Ltd, James Rugemalira.

BUNGE: WAHUSIKA WAMESIKIA
Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema haina sababu ya kupeleka serikalini maazimio yaliyofikiwa na Bunge kuhusu sakata hilo kwa sababu viongozi wanaopaswa kutekeleza maagizo hayo wameyasikia.

Katibu wa Bunge hilo, Dk. Thomas Kashililah, alisema hayo katika mahojiano na NIPASHE iliyotaka kujua kama Bunge litawasilisha lini serikalini maazimio yaliyofikiwa na wabunge wakati wa Mkutano wa 16 na 17 uliomalizika jumamosi iliyopita.

“Pamoja na haki ya kupata taarifa sidhani kama tunapaswa kwenda zaidi maazimio yalitangazwa, mmeyaandika na hansard za bunge zimenukuu. Kwa hiyo wanaohusika watakuwa wamesikia maagizo hayo ya Bunge,” alisema.

MAAZIMIO
Bunge lilitoa maazimio manane likiwamo la kutenguliwa kwa nyadhifa za Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa AnnaTibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema.

Wengine waliopendekezwa kuvuliwa yadhifa zao ni wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge hilo, William Ngeleja (Sheria, Katiba na Utawala), Andrew Chenge (Bajeti) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini).

Pia wamo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Viongozi wa umma na maofisa wa ngazi za juu serikalini wanapaswa kuwajibika kwa sababu wamehusishwa na vitendo vya kijinai katika sakata hilo linalohusisha kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL).

Kadhalika, Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kufanya uchunguzi dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na sakata hilo na wale watakaobainika kuhusika kwenye vitendo hivyo vya jinai.

Maazimio mengine ni kumtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji kuhusishwa kwenye kashfa hiyo.
Majaji waliotakiwa kuchunguzwa ni Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Prof. Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Aidha, Bunge lilitaka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika baada ya uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.

Pia, Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.

Serikali imetakiwa kutekeleza azimio la Bunge kuhusu mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na kampuni binafsi ya kufua umeme na hivyo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti.

CWT YATAKA HATUA ZA KISHERIA
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeitaka sSrikali kuwachukulia hatua za kisheria wote wanaotuhumiwa kuhusika katika wizi wa fedha za akaunti ya Escrow kwani kitendo hicho kimelifedhehesha na kulitia doa kubwa taifa na kuichafua serikali iliyo madarakani pamoja na kushusha morali wa kazi kwa watumishi waadilifu.

Rais wa CWT, Gratian Mukoba, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na walimu wa Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa na kusema kitendo cha watu wachache wakiwemo viongozi wenye dhamana kujichotea fedha katika akaunti hiyo huku serikali ikiendelea kukimbizana na wananchi kutaka michango ya ujenzi wa maabara na kushindwa kuwashughulikia mafisadi hao kinawakatisha tamaa watumishi waadilifu nchini.


Chanzo: Nipashe
 
Nape hana jipya,chama chake ni maarufu kwa kuspin mamboz ,kama hajui kutosikilizwa basi bado hajaijua CCM itakuwa anajipendekeza tu ,na huyu Nape ni mwoga sana hawezi kunyanyua wala kufungua mdomo wake kumtaja mtu na kumtolea uvivu ,atabaki kusemea pembeni tufuate maadili haya na yale hana zaidi ya kuwazuga wananchi hasa kwa kuwa mambo yameshafika mitaani ,sasa ile kujichangamsha anaona awadanganye wananchi.

Afahamu tu UKAWA hawakulala wapo macho na watawaeleza wananchi kuwa kila liccm linalopita na kusema huku vichochoroni kuwa maadili ya ccm yatafuatwa huyo atakuwa anawadanganya tena anawadanganya vibaya sana kwani JINAMIZI LA ESCREW bado lipo na litaendelea kuwafichua wengine na hata wale wanaoona wamesalimika wajue bado ,hizi ni hekaheka tu.
 
Back
Top Bottom