Kalamu Yangu
JF-Expert Member
- Dec 21, 2016
- 1,094
- 1,031
(Aibu Kusimulia)
‘’Ni aibu kufikiria, itakuwa kusimulia?’’ Sauti ya Latifa ilisikika kupitia simu, ni dhahili alikuwa akilia.
‘’Pole sana ndugu yangu lakini aibu hadi simuni, tena ukitumia jila la kificho?’’Nilijaribu kumpooza kwa kuingiza utani kwenye maongezi yetu kumbe nilikuwa kama nimechochea kilio chake.
Akakohoa na kuonesha kapaliwa mate, kisha akatulia na kuendelea kuongea safari hii sauti yake ilionesha huzuni na uchungu aliokuwa nao achana na aibu aliyokuwa nayo tangu awali.
‘’Jina feki ni kwako Michael, kwa Mungu na wahusika tunaolijua tukio hili ni jina halisi hata ningejiita kiumbe wa kutoka sayari ya mbali kuna watu duniani, Mungu na malaika zake wanalijua hili’’
Alimeza mate na kutulia kwa muda (nadhani alikuwa akijaribu kufuta machozi yaliyokuwa hayakomi) kamasi zilisikika zikirudishwa zilikotoka.Kisha akaendelea.
‘’Michael ni aibu, aibu ambayo kama si ile hadithi ya ‘Siri Yenye Mateso’ ambayo ilinionesha kuwa kuna mambo ya aibu na kuumiza duniani basi nisingethubutu kukuambia suala hili’’ Nilikumbuka kile kisa kilichoandikwa na ndugu yangu Moringe Jonasy ingawa sikuona kama kulikuwa na kisa cha kutaajabisha na kuonewa aibu kwa binadamu wa zama hizi.
‘’Ile hadithi ilikuwaje?’’
‘’Umesahau Michael au unataka kunichora tuu?’’
‘’Hujakisoma?’’ Sauti yake sasa ilikuwa ni ya kulaumu.
‘’Nini, mtu kuzaa na shemeji yake? Daktari kuzaa na mgonjwa wake? Au familia kupata watoto wa jinsia moja?’’ Nilijaribu kukumbuka visa vya kile kitabu ambacho nilikuwa mmoja wa wahariri wake.
‘’Na kisa cha fumanizi la mwalimu?’’ Alinikumbusha akionekana kurejea kwenye ule ukawaida wake, sauti za kwikwi na kamasi kupandishwa kila muda zilikuwa zimekoma.
‘’Ahh sasa waogopa fumanizi, Latifa? comeon Latifa hiyo imekuwa kawaida sasa au ni fumanizi la baba na mwana?’’ Nilijaribu kumfanya aone tatizo lake lilikuwa la kawaida hiyo yote ilikuwa katika kumrejesha kwenye hali ya kuona tatizo lake si la kiwango cha juu sana duniani ,kama alivyokuwa amenitumia ujumbe mchana wa siku ile, ujumbe ambao niliupuuza baada ya kuona ulitoka kwenye namba nisiyoielewa, namba ya nje ya nchi, ilikuwa ni Vatcan.
‘’Bora ingekuwa hivyo Michael, si fumanizi la baba na mwana lakini ni fumanizi la rafiki’’Aliongea na kutulia akitaka lile aliloliongea liniingie lakini ni kama alivyotegemea niliangua kicheko ambacho kilinifanya nitokwe na chozi.
‘’Nilijua utacheka Michael, na yeyote ambaye ningempigia simu hii na kumweleza hili’’Aliongea kwa sauti ya kumaanisha na kunifanya nitafakari zaidi nikimuua mbu aliyekuwa akiifaidi damu yangu kwenye bega langu la kushoto.
‘’Lazima nicheke Tiffah kwani ajabu kwa marafiki kufumaniana?’’ Nilimuuliza nikimalizia kicheko changu kilichonitoa chozi pale kwenye ufukwe pweke wa ziwa, kwa mbali nikiona mwanga wa taa za wavuvi na zile za magari machache ng’ambo ya ziwa lile nchini Malawi.
‘’Mie siyo punguani wa kuogopa fumanizi la rafiki yangu na kuyatamani mauti Michael, kisa hiki ni tofauti na visa ulivyozoea kuviandika kwenye hadithi zako ni kisa cha ajabu ambacho nafsi yangu inaamini ni vyema kuufikishia ulimwengu jambo hili’’
‘’Naam nieleze hicho kisa nami nilie kama uliavyo maana najikuta nazidi kuchekeshwa’’
‘’Hujui Michael ni kisa kirefu kilichojaa mambo ya kustaajabisha ngoja nikusimulie tuu kama utalia ama utacheka ni uamuzi wako kwani ni kawaida watu kuchekeshwa na yanayoliza na kulizwa na yachekeshayo, cha msingi na cha lazima nakuomba uuandikie ulimwengu juu ya jambo hili ukikiweka kisa katika hadithi na uhalisi wake’’
Hiyo ilikuwa ni sehemu ya maongezi kati ya rafiki yangu Michael na binti aliyejitambulisha kwa jina la Latifa, Michael ni rafiki yangu kipenzi ambaye alikuwa na kisa cha kweli cha ‘’Meseji kutoka kwa Marehemu Mchungaji’’ lakini kwa bahati mbaya alikutwa na matatizo yaliyomweka kitandani hadi leo.Matatizo mwendelezo wa kisa kile cha ajabu ambacho Valentine ya mwaka jana nilipoenda kumtembelea na kumweleza lengo langu la kuandika hadithi ya ‘’Chozi langu Valentine’’ akanipa simu yake na kunionesha sehemu ya kisa chake alichoanza kuandika juu ya binti huyo akikipa jina la K ilio cha Valentine na kunipa rekodi ya mazungumzo yake ambayo yeye aliyaandika kama yalivyokuwa lakini baada ya kuyasikiliza nikaamua kuandika kisa hiki kwa namna ninayoiweza zaidi kwani kuandika hadithi kwa mtindo wa Daiolojia huwa kunanipa tabu sana.
Michael alininisisitiza Valentine ya mwaka huu kisa hiki kiwafikie wasomaji na iwe zawadi kwao nami nimeamua kukileta kwa namna niliyoona itamvutia hata Latifa kama yu hai kuko Ulaya.
_______________
Tarehe kumi na nne ya mwezi wa pili mwaka 2010 ilikuwa ni siku muhimu na ya kuvutia sana kwa vijana wawili wapenzi Sarah na Credo waliokuwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Tumaini Iringa.Si tuu kwa kuwa ilikuwa ni siku ya wapendanao duniani kwote lakini siku hiyo ilikuwa ni siku ya kuzaliwa ya wapenzi hao.Wakiwa na furaha ya kuadhimisha siku hiyo kwa pamoja kwa mara ya pili kwani mara ya kwanza ilikuwa mwaka uliopita wakiwa si wapenzi ingawa tukio hilo liliwaunganisha na kuwafanya wawe wapenzi.
Baada ya sherehe hiyo kufanyika kwenye ukumbi mdogo uliokuwa ng’ambo ya chuo cha Ruaha, Sarah na Credo waliachana na rafiki zao na kuelekea nyumbani ama tuseme vyumbani kwao walikokuwa wamepanga.Walipoachana na rafiki zao waliopanda daladala ama kutembea kwenda kwao kwa miguu kama walivyofanya akina Sarah, walikumbatiana na kupena mabusu kabla ya kuendelea na safari yao kuelekea nyuma ya Chuo cha Ruaha palipokuwa na makazi ama tuseme malazi yao huku wakiwa wameshikana mikono kimahaba.
Kitu ambacho hawakukijua ama walikijua na kukisahau ama kukipuuza kutokana na vipombe walivyorashia vinywani mwao kuitoa ile aibu ya kusherekea na kuchangamka kunogesha sherehe yao iliyofana kutokana kuwa katika siku ambayo kwa waanzilishi ilikuwa ni ya wapendanao ila kwa sie wanamapokeo ni siku ya zinaa na ngono.Walipita kwenye kichaka kidogo kilichokuwa kikikaribia kona ya ukuta wa chuo na kuwakuta watu watatu waliokuwa wamekaa kwenye mawe wawili upande huu mmoja upande wa pili wa barabara ile iliyokuwa na majani mabichi yaliyonyeshewa na kimvua kidogo kilichokuwa kimenyesha jioni ya siku ile, kichaka kilichojulikana kwa uhatari wake kutokana na uwepo wa mateja.
Ilikuwa ni saa saba usiku, na akili zao zikawaambia kuwa wale walikuuwa ni wavuta bangi tuu walioamua kuutumia usiku ule kwa kuwa na kitu wakipendacho, bangi.
Naam hawakukosea watatu wale walikuwa wakivuta bangi na walianza kuzivuta muda mrefu tangu kile kimvua kilipoacha kunyesha na sasa walikuwa wamependana na bangi na bangi ilikuwa imeuzidi upendo wao na kuziteka akili zao.Walitenda akili zilivyowaambia na kwa bahati mbaya kila mmoja alizifuata, huyu alipowaza kuimba pambio waliimba wote, huyu alipowaza kulia walilia wote na mengine mengi waliyoyatoa waliyafanya kwa umoja wao.
Sauti za wapenzi wale wakiimbiana nyimbo za mapenzi na kucheka kimahaba kutoka mbali ziliwafanya watulie kuwasikiliza, ulikuwa ni wimbo mmoja wa Kenny Rodgers aliokuwa akiuimba Credo ndio uliomfanya Sarah ajikute ajisahau kabisa kama walikuwa barabarani kwenye usiku ule uliokuwa na giza zito.Joto la huba lilijidhihirisha kupitia kiganja kilichofumbatiwa na kile cha mpenziwe.
‘’Simameni’’Sauti nzito ya kilevi iliyojaa amri ilisikika kutoka kwa mmoja wa wale waliokaa upande mmoja wa barabara wawili.
‘’Habari zenu mabraza’’
‘’Shikamooni’’ Sauti zao zilisikika kwa zamu huku Sarah akionekana mwenye uoga.
Nywele zilimsimama kwa woga akizidi kujisogeza kwenye mwili wa mpenziwe ambaye naye alianza kuiona ile hatari waliyokuwa wameisogelea.
‘’Kaeni’’ Sauti ilitoka upande wa pili wa ile barabara.
Waligwaya, na hilo ndilo walilolitaka wale wavuta bangi kwani waliwavamia na kuwaweka kwenye himaya yao, wawili wakimdhibiti Credo na mmoja akimdhibiti Sarah aliyekuwa akiomba msamaha kwa wale wahuni ambao hawakutaka kumsikia wa kumjali zaidi ya kumtaka anyamaze.
Waliwaongoza hadi kwenye kichaka kikubwa kilichokuwa kilimani ambako huko walikutana na wahuni wengine ambao wao walikuwa wabwia unga.Hapo wakalazimishwa kuvuta bangi kitu ambacho Credo hakukikubali na kutaka kupambana nao kitu ambacho kilikuwa kosa kubwa sana kwani aliwafanya wale mabwana wachane na mpenziwe na kuanza kumpiga.
‘’Sarah kimbia’’ alimwambia mpenziwe huku akiendelea kupokea kipigo kizito kutoka kwa wale mateja na wavuta bangi wenye nguvu lakini kabla Sarah hajafanikiwa kuunyanyua mguu akimbie kutokana na hofu na ule upendo aliokuwa nao kwa mpenziwe alikamatwa na mmoja wa wale wavuta bangi wenye nguvu na kudhibitiwa kikamilifu akishuhudia kitu kilichomuumiza moyo wake.
Kitu ambacho hakuweza kustahimili kukitazama kwani mpenziwe alivuliwa suruali yake na kuingiliwa kimwili na vijana wawili wavuta bangi waliowakuta pale barabarani na wakawaleta pale.
Alifumba macho asiuone ule unyama lakini masikio yake yalizisikia sauti za kilio cha maumivu alichokitoa mpenziwe huku maneno ya kashfa , dhihaka na ya kukolea utamu kutoka kwa wale vijana wawili waokuwa wakipokezana kwa zamu yakimuumiza nafsi yake na kujikuta akitokwa na machozi na kilio ambacho kilizuiwa na yule mvutaji aliyemdhibiti kwa kumziba mdomo wake.
Dakika ishirini za mateso na maumivu ya mwili na akili kwa wapenzi wale wawili zilikuwa kama muongo wa mateso mfululizo.Waliachiwa na kutakiwa kukimbia bila kugeuka huku wale walevi wa bangi na unga walipotelea kilimani wakikimbia na kucheka vicheko vilivyozidi kuzikata nyoyo za wapenzi wale ambao sasa badala ya mwanaume kumsaidia mwanamke safari hii mwanamke akawa akimsaidia mpenziwe kutembea kwani alikuwa akishindwa kutembea vyema.
Waliofika walipopanga , ambapo Credo alikuwa akikaa peke yake na Sarah akikaa na rafiki yake na kwa Credo kukiwa kama kwake hivyo waliingia moja kwa moja kwa Credo na akachemsha maji na kumwogesha akimkanda.Baada ya hapo akampa dawa ya kutuliza maumivu iliyopunguza maumivu ya mwili lakini nafsi zao ziliumia sana kuliko hata maumivu ya mwili.
Palipokucha palikucha na taarifa za Credo kuwa na homa ambayo wengi walijua ilitokana na uchovu wa kushereheka usiku uliopita.Walifanya siri ya wawili , siri iliyowaumiza peke yao kwani walijua kuvuja kwa siri hiyo ni aibu na mateso ya nafsi zao.
Walifanikiwa kuifanya siri hiyo ikadumu hadi pale Credo alipopona na kuendelea na masomo kama kawaida .Kupona kwa Credo kulikuwa faraja kwao ingawa ile aibu haikukoma mioyoni mwao lakini ambacho hawakukijua kupona kwake ulikuwa ni mwanzo wa aibu nyingine kubwa iliyotisha.
Wiki mbili baada ya Credo kupona Sarah alitamani tunda, tunda alilolipenda akalila na kulitamani zaidi kabla ya tukio lile la aibu lakini siku walipoamua kulila tunda ilikuwa ni msiba mwingine kwani Credo akahakikisha kile alichokuwa akikiwaza wakati akijiuguza.Aliwaza kwani licha ya kushikwa na kuguswa hapa na pale katika kuugua kwake alijikuta akili ikishtuka lakini mwili uligoma, siku zote uligoma katika usiri lakini siku ile uligoma kwenye usiri wa wawili ambao walianza kuuzoea ingawa usiri huo kwa Credo ulikuwa ni kama utumwa kwake kwani alijua lazima kulikuwa na siku ambayo usiri huo utapotea hasa siku akija kumkosea mwenye siri yake.
Tofauti na alivyotegemea jambo lile lilimuumiza na kuonesha kumuumiza sana Sarah ambaye licha ya kuona kwa macho yake, hakuwa tayari kukubaliana na hali ile na kuwa mvumilivu akijaribu kila siku kwa mwezi mzima, kimya miezi miwili kimya mitatu hadi mwaka ulipoisha bado mwili wa Credo ulikataa kufanya kile akili yake ilitaka.
Hadi walipohitimu Sarah aliondoka akiwa mnyonge na mwenye hofu sana, kitu ambacho kwa Credo ni kama alikuwa amekisahau, alijiweka mbali na Sarah na kumtaka atafute mwanaume asiye na tatizo kama lake.Sarah hakutaka kukubalina na jambo hilo akitaka kumsaidia mpenziwe kwa kutafuta tiba hospitalini jambo ambalo Credo hakulitaka akimwambia kuwa ule ulikuwa ni mwisho wake kuwa mwanaume sahihi kwani hakukuwa na matarajio ya kupona.
Walipoachana chuoni ulikuwa ni mwisho wa mawasiliano yao kwani Credo alibadili namba za simu huku akiacha kuwasilina na marafiki ambao aliamini kuwa Sarah angehangaika kutafuta mawasiliano yake kupitia kwao.
Huo ukawa mwisho wa Credo na Sarah, Sarah akiachiwa maumivu makali hadi pale alipopelekwa na wazazi wake nchini Afrika ya kusini alipobadili mazingira na marafiki kidogo kidogo yale maumivu yalipungua na kujikuta akisahau kumbukumbu za tukio lile zikija mara chache tofauti na hapo awali.
Credo alipotoka Mjini Iringa aliingia jijini Arusha ambako ndiko kwao kabla ya kujizamisha jijini Dar es salaam ambako na huko alikutana na rafiki yake wa siku nyingi ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye kampuni moja kubwa. Akipokea mshahara mnono ambao uliweza kumsitiri yeye na rafiki yake wa siku nyingi ambaye aliingia pale jijini kwa minajili ya kutafuta ajira akiwa na shahada yake ya Uandishi wa habari.
Rafiki yake alikuwa amepanga nyumba ya vyumba vitatu na sebule, chumba kimoja wakikifanya ofisi yao na viwili vya kulala kila mmoja na cha kwake.Mara kwa mara rafiki yake alikuwa akitembelewa na nduguze hali iliyowafanya wakawa wanalala pamoja wakimpisha mgeni.
Katika siku walizokuwa wakikaa pamoja waliburudika kwa kile rafiki yake alichokikusanya akimsaiidia kuendeleza ofisi ambayo Credo aliitumia kuandaa vipindi vingi ambavyo aliamini siku moja angekuja kuviuza kwenye vyombo mbalimbali vya habari.Kuna nyakati rafiki yake alikuwa akitembelewa na mpenzi wake aliyekuwa akifanya kazi nje ya nchi wakati mwingine rafikiye akija na vimada wengine alikuwa akiokota katika ulevi.
Pombe ina mengi ya kushangaza na kustaajabisha lakini inapowekwa vingine huleta vioja vilivyo na hatari kubwa, ndivyo ilivyokuwa usiku mmoja walipokuwa wakinywa pombe Credo alifanikiwa kuitia pombe hiyo kitu kilichoamsha hisia za ajabu kwao kabla ya kuwaingiza kwenye ulimwengu wa ajabu.
Huo ukawa mwanzo wa tendo chafu lichukizalo mbingu na nchi, tendo ambalo walilifanya kila walipopata nafasi.Credo akawa mke na rafikiye mume, pale walipofika wapenzi wa rafikiye Credo alibaki kuwa rafiki wa kweli akiwaita hao wanawake ni shemeji zake huku moyo wake ukiumia.Hali ilindelea hivyo hadi siku binti aliyejipa jina la Latifa alipoingia nchini kimya kimya siku ya Valentine ,ilikuwa ni usiku uliofanana na ule wa miaka kadhaa iliyopita pale Iringa kwani kijimvua kilikuwa kimetoka kunyesha na kutengeneza umande palipokuwa na nyasi na kuweka vidimbwi pale palipokuwa na bonde.
Saa kama zile za tukio lile la kuaibisha pale Iringa , siku hiyo tukio hilo la kuaibisha lilifanyia chumbani kwa rafiki yake Credo na hakuonekana kulionea aibu hadi pale waliposhtushwa na kilio cha Latifa pale dirishani na kukurupuka , lakini walikuwa wamechelewa.
Latifa aliumia sana , mtu aliyemwita shemeji alikuwa mke mwenzake si kwa kusikia bali kwa kuona kwa macho yake.Aliwaita na kuwauliza kulikoni huku akitokwa machozi Credo alieleza kila kitu akiomba msamaha kuwa ndiye mkosaji na alianza mchezo ule baada ya tukio lile pale Iringa kuumaliza uanaume wake akifanya tendo hilo na watu mbalimbali pale Iringa.Siku ile alikuwa amemtilia madawa kwenye kileo na kumsisimua mwili rafiki yake na amekuwa akifanya hivyo mara nyingi hadi alipoona tukio lile limezoeleka kwenye kichwa chake.Dawa hiyo alikuwa ameipata kwa shoga mwenzake mmoja pale Iringa na alikuwa akiitumia mara nyingi aliomba msamaha na kuhitaji msaada wa kutoka kwenye uchafu huo.
Ndipo Latifa alipovaa ujasiri wa kuondoka nao hadi Italia kwenye hospitali moja wakipata matibabu ya kimwili na kiakili.Na baadaye akaelekea kwenye mji/nchi ya Vatican na kupiga simu ile kwa Michael mwandishi mwenzangu wa hadithi ambaye bado yupo kitandani akipigania uhai.
Naam hiki ndicho kilio cha Valentine ambacho leo nimetimiza ahadi yangu kwa Michael kukileta kiwe funzo kwenu wasomaji wangu.
Mwisho.