SoC03 Kilimo biashara na ustawi wa jamii za wakulima: Jitihada wezeshi kumtua jembe la mkono mkulima wakitanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Jerry Farms

Member
Jul 18, 2022
30
29
Katika zama hizi za vijana tujiajiri! Dhana korofi na swali tatanishi limekua ni kwa jinsi gani serekali inaweza kukabiliana na suala tambuka la ukosefu wa ajira. Kwa kurahisisha wengi huishia kusema, " ardhi ni kubwa vijana kwa nini msijiajiri..." wengi (wasomi na vijana wasio na ajira) huhisi ni dharau na wengineo huhisi ni kejeri kwao, haya yote yanakuja kwa kuangalia wazee vijijini waliolima miaka nenda rudi na kuishia kupiga mzunguko wa lima -vuna-kula!! Lakini je ni kweli kwa miaka nenda rudi hali hii yapaswa kuwa kama ilivyo?

La hasha! mfumo huu unapaswa kufumuliwa na ni wakati sahihi wa serikali na jamii ya wakulima kuja na mpango kabambe wa uboreshaji wa kilimo. Sekta ya Kilimo nchini imetoa ajira ya zaidi ya asilimia 65 ya wananchi, hivyo jamii ya wakulima haina budi kufumua mfumo na kujikita katika dhana ya kilimo biashara.

Mabadiliko haya yote yatawezekana tu kama patakua na ari na utayari wa mabadiliko kuanzia wizarani hadi kwa mkulima mwenyewe.

Pamoja na jitihada kubwa za serikali katika kuboresha kilimo hali bado inahitaji jitihada zaidi na zaidi. Kuifikia kauli mbiu ya "KILIMO NI UTI WA MGONGO WA TAIFA" mambo yafuatayo hayana budi kufatwa;

ELIMU YA KILIMO
"Mwanangu mshike sana elimu usimuache aende zake"ni kauli kidogo ya zamani lakini yenye maana kubwa. Elimu kabla ya kilimo ndio kila kitu. Mkulima kabla ya kujikita katika shughuli za kilimo hana budi kulijua kwa undani zao tarajiwa shambani. Mkulima awezeshwe kujua nini hitaji la zao kabla, wakati limepandwa na baada ya kuvunwa. Elimu katika nyaja ya kilimo ni hitaji la msingi kwa wakulima. Vikundi vidogo vidogo vya wakulima havina budi kuanzishwa na mpango mahsusi wa kuvipatia elimu ufuate. Elimu isiishie katika vikundi tu bali ofisi za kata ziwe na taratibu ya kutoa na kubandika vipeperushi vitoavyo elimu juu ya zao stahimilivu kulimwa katika maeneo yao, kwa kufanya hivyo Umma utafikiwa kwa ukubwa hivyo mabadiliko chanya katika kilimo.

MPANGO WEZESHI WA UPIMAJI WA AFYA YA UDONGO
"Kilimo sio kukariri"! Hii ni sentensi inayoweza kukushangaza kidogo msomaji. Lakini huu ndio ukweli, wakulima wengi wamekariri kua nikianza na mbolea X itafata mbolea Z na ntamalizia na mbolea K nakuja kuvuna! Lahaula! kilimo hakiendeshwi hivyo. Kuijua afya ya udongo ni jambo la msingi kabla ya kuingia katika kilimo. Hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau haina budi kuja na mpango mkakati wa upimaji wa afya ya udongo mashambani kata kwa kata, tarafa kwa tarafa. Mpango huu unaweza kufanywa kama ilivyo katika programu ya shughuli za urasimishaji ardhi. Hapa serikali kwa kushirikiana na wadau inaweza toa vifaa na wataalamu katika kila kata na jamii ya wakulima kuombwa kuchangia gharama kidogo za upimaji.

KUREJEA HISTORIA YA HALI YA MVUA NA USTAWI WA MAZAO
Njia hii itakua ni sehemu ya suruhisho kwa maeneo yale ambayo zoezi la upimaji wa afya ya udongo litakua halijafikiwa. Mkulima awe na utaratibu wa kukagua na kukusanya taarifa juu ya hali ya mmea taarifa hizi aziwasilishe moja kwa moja ofisi ya kijiji au kata anakoishi nakusaidiwa.

MATUMIZI YA TEHAMA KATIKA KILIMO
Kufuatia ukuaji wa sayansi na teknolojia, serikali inaweza kuja na programu wezeshi na mfumo wa utumaji na ujibiwaji wa maswali yote yahusuyo kilimo kwa jumbe za simu. Kwa kushirikiana na kampuni za mawasiliano serikali inaweza kuja na mpango wa kumwezesha mkulima kurusha swali na kujibiwa bure na mtaalamu wa kilimo pasi na gharama. Vilevile wataalamu wa tehama wanaweza buni programu zitakazo wasaidia wakulima wenye simu janja kufungua na kupiga picha kisha kutafuta jibu la jambo lenye utata shambani kupitia simu janja.

SEREKALI KWA KUSHIRIKIANA NA WADAU WAKILIMO KUAGIZA DHANA BORA ZA KILIMO NA KUGAWA BURE KWA VIKUNDI VYA WAKULIMA
Kwa kua kilimo kimeajiri umma mkubwa wa watanzania na zana duni za kilimo ni jambo mtambuka miaka nenda rudi, serikali haina budi kuja na mfumo wezeshi utakao mfanya mkulima aachane na jembe la mkono. Kwa kushirikiana na wahisani serikali inaweza anza na ugawaji wa zana za upandaji, umwagiliaji na utunzaji wa mashamba ama kwa gharama nafuu au bure. Ni wakati muafaka wa mkulima kuachana na jembe "chapa jogoo" sasa. Kilimo kiwe ni kazi rasmi sasa, dhama hii ndio iwe mwisho wa kulima kwa jembe la mkono! inawezekana.
UANZISHWAJI WA MAABARA ZA KI WILAYA/KANDA KWA AJILI YA KUPIMA UBORA WA MBOLEA ASILIA
Viambata lishe muhimu vipatikanavyo katika mbolea zetu za asili vinaweza kupimwa katika maabara hizi na kumrahisishia mkulima kujua ni yapi mapungufu yaliyomo katika mbolea anayotumia. Viambata kama Nitrojeni, Patashiamu na Phosiforasi ni mahitaji muhimu kwa mimea, hivyo taratibu za upimaji kwa gharama nafuu zinaweza kupangwa na wataalamu wa kilimo katika ngazi za wilaya hadi kata.


ELIMU YA JINSI YA KUBORESHA MBOLEA ASILIA KATIKA KILIMO
Matumizi ya mbolea organia yameshika hatamu katika maeneo mengi nnchini. Hili limetokana na unafuu wa gharama na upatikanaji kwa urahisi wa mbolea hizi mfano mbolea ya kuku, ng'ombe, nguruwe, punda nakadhalika. Tunarudi pale pale kwenye dhana ya "kilimo sio kukariri", juhudi inapaswa kuwekwa katika kutoa elimu juu ya jinsi ya kuipa thamani mbolea yetu hii. Mfano katika nchi ya Kenya wakulima huelekezwa jinsi ya kuongeza vitu katika mbolea ili kuifanya iwe na viambata lishe vingi kwa mmea, mfano uongezaji wa majivu katika mbolea. Uwekaji sahihi wa mbolea kwa kuzingatia hali ya afya ya udongo ni kitu cha muhimu katika kilimo.

HITIMISHO
Wakulima shime kwetu kujikita katika kupenda kujifunza zaidi kabla ya kuingia katika kilimo. Tufanye juu chini kulijua zao tarajiwa kupandwa shambani kabla ya kuingia shamba. Serikali na wadau wa kilimo wawekeze zaidi katika kumuwezesha mkulima.
 
Back
Top Bottom