ushuhudaunaoishi
Member
- Dec 1, 2025
- 7
- 3
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, chama hicho kimeendelea kuwa madarakani, hali inayoendelea kuzua mjadala mpana ndani na nje ya Mitandao ya Kijamii kuhusu nafasi yake kama chama dola.
Wakati takwimu rasmi zikionesha ushindi, maoni ya wananchi, hususan mjini Dodoma, yanaonesha simulizi tofauti inayouliza si nani alishinda, bali kwa nini hamasa ya kisiasa imeendelea kupungua.
Mtazamo huu, iwe ni wa kweli au la, umejenga imani kwamba mabadiliko ya kisiasa ni magumu kupatikana kupitia sanduku la kura pekee.
Kwanini sio sanduku la Kura pekee?
Kwa miaka mingi au Awamu tofauti za Kiserikali kumekuwa na malalamiko kwamba kile kinachopigwa kwenye sanduku la Kura na kupatikanana matokeo yake ama siyo halali au kulikuwa na upungufu mwingi na wengine wanasema kulikuwa na kura hewa.
Hali hiyo inaonesha licha ya kuwa upigaji kura ni sehemu ya demokrasia lakini kiuhalisia katika siasa zetu inaonesha wazi hakuna uhalisia wa demokrasia inayotajwa na kile kinachofanyika.
Hivyo basi inatakiwa elimu kubwa itolewe kabla ya kujisifu kuwa sanduku la kura pekee ndio demokrasia, Wananchi wanatakiwa kufahamu thamani ya kura yao, jinsi inavyotakiwa kutumika, wasimamizi wa Uchaguzi nao wanatakiwa Kutenda haki, mifumo ya kutambua kura zilizopigwa na uhalisia wake.
Hayo tote yakifanyika kutakuwa na wingi wa Wapiga Kura halali kujitokeza na mwisho wake uchaguzi ukifanyika washindi halali watapatikana, hayo yote yanatakiwa kufanyika ili thamani ya Sanduku la Kura iwe halisi na siyo kama ilivyo sasa ambapo malalamiko ni mengi kuliko kile kinachoelezwa kuwa kuna demokrasia.
Mtazamo wa Mtandaoni
Uchunguzi wangu mijadala katika Mitandao ya Kijamii unaonesha kuwa CCM hukosolewa zaidi kuliko kusifiwa.
Katika majukwaa ya X, Facebook na TikTok, wananchi wengi hujadili CCM kama chama kisichohitaji tena kushawishi kwa hoja, bali kinachotegemea muundo na dola ambao ndani yake kuna mfumo dhaifu.
“CCM haishindi kwa sababu watu wanakipenda, inashinda kwa sababu ya ubabe,” anasema Moses Jumaa, Mchambuzi huru wa siasa anayefuatilia mijadala ya kisiasa mtandaoni.
Kauli kama hizi zimekuwa za kawaida, zikionesha mabadiliko ya namna wananchi wanavyokichukulia chama hicho.
Noel Lyoba, Mkazi wa Mailimbili Dodoma anasema CCM ni chama kinachotetewa na Wachache, Kinachopingwa na Wengi huku akitolea mfano kuwa,"Ukizunguka kwenye mitandao ya kijamii—X (zamani Twitter), Facebook, Instagram na TikTok taswira ya CCM ni tofauti kabisa na ile ya majukwaa rasmi,imepoteza mvuto haionekani kama chama cha matumaini mapya," amesema.
Maoni mengi ya wananchi mtandaoni hayapingi ushindi wa CCM kwa hoja za kisheria, bali yanapinga uhalali wa kihisia wa ushindi huo.
Kauli kama “walishinda kama kawaida”, “ilikuwa wazi tangu mwanzo” au “kura yangu haibadilishi chochote” zimekuwa kauli za kawaida zaidi kuliko pongezi.
Hili linaashiria jambo moja muhimu: Kwamba CCM inaendelea kuweppo madarakani lakini inapoteza Ushawishi kwa nguvu ya umma.
Jamii na Mtaani
Tofauti na maoni na malalamiko ya Mitandaoni, mitaani hali ni ya ukimya unaobeba ujumbe mzito.
Maeneo ya masoko, vijiweni na vituo vya daladala jijini Dodoma, Wananchi wengi hawazungumzi siasa kwa hamasa kama ilivyokuwa zamani kuhofia usalama wao.
“Siasa zipo juu juu, lakini maisha ni magumu nchini, tunaogopa kusema ukweli kwa kuhofia kukamatwa na kuswekwa ndani,” amesema Mama Asha Abdalah, mfanyabiashara ya mboga mboga soko la Sabasaba.
Kauli hii inaakisi hisia ya wananchi wengi wanaoona CCM kama sehemu ya mfumo usiobadilika, si kama chombo cha matumaini mapya.
Licha ya hao, Wafanya biashara wengine wa Soko hilo la Sabasaba jijini Dodoma wamelalamikia kile wanachodai kuwa ni ugumu wa kufanyika kwa mabadiliko ya mifumo mibovu chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakisema changamoto zao zimekuwa zikijirudia bila ufumbuzi wa kudumu.
Wamesema licha ya ahadi mbalimbali zinazotolewa katika vipindi vya uchaguzi na mikutano ya kisiasa, bado mifumo ya ukusanyaji wa tozo, upangaji wa maeneo ya biashara na urasimu wa vibali imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo yao ya kiuchumi.
Yusuf Hamza anasema mifumo ya sasa imekuwa ikiwabana zaidi wajasiriamali wadogo, huku ikionekana kuwanufaisha wachache wenye uwezo au ukaribu na mamlaka.
Anasema mara kadhaa wamewasilisha malalamiko yao kupitia viongozi wa soko na mamlaka za Serikali za Mitaa, lakini hakuna mabadiliko ya msingi yaliyofanyika, hali inayowafanya kupoteza imani na utayari wa CCM kusimamia mageuzi ya kweli yanayogusa maisha ya wananchi wa kawaida.
Aidan Magesa ameeleza kuwa wanahitaji uongozi unaothubutu kuvunja mifumo kandamizi na kusikiliza sauti za walio chini, badala ya kulinda mifumo wanayoiona kuwa imepitwa na wakati.
Amesisitiza kuwa mabadiliko wanayoyataka si ya kisiasa pekee, bali ni ya kiutendaji na kimfumo, yatakayowezesha biashara kukua, kuongeza ajira na kuboresha ustawi wa jamii kwa ujumla.
Anasema Wengi wanachukulia CCM kama sehemu ya maisha yao ya kisiasa isiyobadilika,Si kwa sababu wanakipenda, bali kwa sababu:
“ndicho kilichopo”
“hakuna cha kufanya”
“maamuzi makubwa hayafanyiki kwa kupiga kura .
Huu ni mtazamo hatari kwa chama chochote cha siasa, kwa sababu unaashiria kupotea kwa uhusiano wa kihisia kati ya chama na wananchi.
Nguvu ya Ushindi dhidi ya Ushawishi
Ushindi wa CCM katika Uchaguzi wa 2025 unaonesha bado kina nguvu ya kimuundo na kiutawala, hata hivyo, nguvu hiyo haifanani na ushawishi wa kijamii.
Wataalam wa siasa wanaeleza kuwa kuna tofauti kubwa kati ya kushinda uchaguzi na kupendwa na wananchi.
“Chama kinaweza kushinda bila kushinda mioyo ya watu,” anaeleza Dk. Conrad Masabo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dodoma, akisisitiza kuwa hali hiyo hujenga demokrasia dhaifu.
Mhadhiri huyo amesisitiza kuwa bila mageuzi ya kina ya kimfumo ikiwemo mifumo ya uchaguzi, utawala wa ndani ya chama na ushiriki wa wananchi demokrasia itaendelea kuwa ya juu juu na isiyogusa maisha halisi ya watu.
Viongozi wa Ngazi za Chini
Katika jamii, taswira ya CCM mara nyingi huamuliwa na viongozi wa ngazi za chini wenyeviti wa mitaa, kata na matawi.
Hata hivyo baadhi ya viongozi hao wamepoteza ushawishi wa kijamii kutokana na tuhuma za upendeleo na kutojibu kero za wananchi.
“Ukimuona mwenyekiti wako hafanyi kazi, unakichukia chama chote,” amesema Saida Kusaja mkazi wa Nzuguni, Dodoma hali inayoonesha dhahiri na moja kwa moja namna CCM inavyoonekana katika jamii.
Amedai kuwa kutowajibika kwa viongozi hao kunachochewa na mifumo iliyowekwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba mifumo hiyo imewapa kinga viongozi wa ngazi ya chini kwa kuwafanya wawajibike zaidi kwa chama kuliko kwa wananchi waliowachagua.
"Hali hii inasababisha malalamiko yetu kupuuzwa bila hatua za maana kuchukuliwa, kumekuwa na tabia ya viongozi wa mitaa kutokutoa majibu ya wazi kuhusu matumizi ya rasilimali, ukusanyaji wa michango na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, " Amesema.
Naye Mtemi Nzowa anasema hata wanapojaribu kuhoji au kuwasilisha malalamiko yao, huonekana kama wanapinga chama tawala badala ya kutafuta haki zao za msingi, jambo linalodhoofisha ushiriki wa wananchi katika maamuzi yanayowahusu moja kwa moja.
Kwa ujumla Wananchi wameeleza kuwa mifumo ya uongozi inayolinda maslahi ya kisiasa kuliko uwajibikaji wa kijamii imekuwa chanzo cha kuporomoka kwa imani yao kwa viongozi wa mitaa.
Wamesisitiza kuwa bila kuvunjwa kwa mifumo hiyo na kuwepo kwa uwajibikaji wa kweli, wananchi wataendelea kukosa sauti, huku maendeleo yakibaki kuwa ahadi zisizotekelezwa katika ngazi ya chini ya jamii.
Mabadiliko ya Ndani ya Chama Tawala
Ndani ya CCM yenyewe, kumekuwepo mijadala kuhusu mabadiliko ya uongozi na demokrasia ya ndani.
Baadhi ya wanachama wanaona chama kimekuwa kikubwa kiasi cha kupoteza uwezo wa kusikiliza sauti za chini.
“Maamuzi mengi yanatoka juu, sisi wanachama wa kawaida tunabaki watazamaji,” amesema mwanachama wa CCM aliyeomba hifadhi ya jina lake .
"Hata haya mazungumzo nahofia huenda nikachukuliwa hatua, Chama chetu kimekuwa kikitishia uhai wa watu kila siku, tunaogopa Sana,tukiwa nje wengi wetu tunajinasibu kuwa wana CCM lakini ki ukweli kwenye mioyo yetu inavuja damu, demokrasia ya ndani ya chama imekufa muda Sana, "anaeleza.
Vijana na Siasa
Vijana kwenye siasa wanatazamwa kama ni Kizazi Kisicho na Denii ndani ya historia kwa CCM kwa sababu Kizazi cha vijana wa sasa hakina kumbukumbu ya TANU, Azimio la Arusha wala mapambano ya awali ya uhuru.
Kwao, CCM si chama cha historia, bali ni chama cha ajira ngumu kupatikana, maisha ghali, ahadi zisizogusa maisha yao moja kwa moja.
Vijana, ambao ndio kundi kubwa la wapiga kura, wana mtazamo tofauti kabisa,kwao, CCM si chama cha historia bali ni chama cha sasa kinachopimwa kwa ajira, gharama za maisha na fursa.
Nje ya takwimu za Tume ya Uchaguzi na hotuba za ushindi, kuna simulizi nyingine simulizi ya Vijana inayoishi mitandaoni, mitaani, vijiweni na kwenye mazungumzo ya siri .
Ni simulizi ambayo haiulizi nani alishinda, bali inauliza:
“Kwa nini watu hawashangai tena maajabu ya CCM?”
“Kwanini hamasa imepungua?”
“Kwanini ushindi hauleti shangwe?”
Haya ni maswali yanayoifanya CCM baada ya 2025 ionekane si kama chama kinachopendwa kwa mapenzi ya Vijana bali kama chama kinachokubalika kwa mazoea, hofu au kukosa mbadala unaoaminika.
Teknolojia na Simulizi Mpya:
Mitandao ya kijamii imebadilisha kabisa uwanja wa ushawishi wa kisiasa. CCM, kama vyama vingine, imejikuta ikikabiliana na simulizi ambazo haiwezi kuzidhibiti kikamilifu.
Memes, video fupi na mijadala ya moja kwa moja vimekuwa silaha za wananchi kueleza kutoridhika kwao.
"Maridhiano ya kisiasa yenye afya yanapaswa kuwezesha uwazi, uwajibikaji na mjadala wa wazi, hata pale ambapo hoja zinakosoa chama tawala, endapo CCM itaendelea kudumisha mifumo ya mawasiliano inayodhibiti mjadala na kuua sauti mbadala, demokrasia itaendelea kuwa dhaifu, na wananchi watazidi kupoteza imani yao kwa taasisi za uongozi na siasa kwa ujumla,” anaeleza mtafiti mmoja wa mawasiliano ya kisiasa.
Aidha, ameonya kuwa demokrasia dhaifu huzaa uongozi usio na presha ya kuwajibika, huku akihimiza mijadala ya wazi na mageuzi ya kimsingi kama njia pekee ya kuijenga Tanzania yenye ushindani wa kisiasa na utawala bora.
Kwa jumla, baada ya Uchaguzi wa 2025, CCM bado kina nguvu ya kisiasa na kimuundo, lakini ushawishi wake wa kijamii umebadilika kwa kiasi kikubwa.
Mitandaoni na mitaani, chama hicho hakichukuliwi tena kama chama cha matumaini mapya bali kama sehemu ya mfumo uliopo. Changamoto kubwa kwa CCM si kushinda uchaguzi unaofuata, bali kushinda tena imani ya wananchi.
Kwa sababu katika siasa za kisasa, chama kinaweza kutawala kwa muda mrefu, lakini bila uhalali wa kijamii, nguvu hiyo hubaki kuwa dhaifu na ya muda.