Kila mmoja ashiriki tutokomeze Kifua Kikuu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kila mmoja ashiriki tutokomeze Kifua Kikuu

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Mar 27, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Mar 27, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  Ugonjwa wa Kifua Kikuu bado ni tishio kubwa duniani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon katika ujumbe wake wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kifua kikuu, ambayo kimataifa hufanyika Machi 24 kila mwaka, amebainisha hali hiyo.

  Akasema kwamba ugonjwa huo unashika namba mbili kwa kuambukiza na kuua duniani na kwamba takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2010 watu milioni tisa walipatwa na maradi ya kifua kikuu ambapo milioni 1.4 miongoni mwao walifariki dunia katika nchi zinazoendelea.

  Akasema kifua kikuu husababisha pigo kubwa kwa familia na jumuiya mbalimbali. Mamilioni ya watoto wamepoteza wazazi.
  Watoto waishio na wanafamilia walioathirika wana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na ugonjwa huo. “Kwa vile si rahisi kuthibitisha uwepo wa maradhi hayo kwenye mwili wa mgonjwa. Kwa hiyo, mwaka huu tunakusudia kupanua uelewa wa jinsi ambavyo watoto huathiriwa na ugonjwa huu," alisema.

  Anakiri kwamba juhudi za pamoja zimesaidia kupunguza vifo kwa asilimia 40 tangu mwaka 1990. Watu milioni 46 wameponywa kuanzia mwaka 1995 kutokana na juhudi za Umoja wa Mataifa, serikali mbalimbali, wafadhili, makundi ya kijamii, washirika binafsi,

  wataalamu wa afya, na makumi ya maelfu ya watumishi wa idara za afya pamoja na familia na jumuiya zilizoathirika.
  Hii inadhihirisha jinsi ugonjwa huo unavyoendelea kuitesa dunia, hivyo kama alivyotoa rai Ban Ki-moon, juhudi za pamoja za mataifa

  zinahitajika zaidi katika kuutokomeza. Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayosumbuliwa sana na ugonjwa huo.
  Taarifa kuhusu ugonjwa huo inaonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya 18 kati ya nchi 22 duniani zenye idadi kubwa ya wagonjwa. Aidha inakadiriwa kuwa kila mwaka hugundulika zaidi ya watu milioni tisa wana ugonjwa huo na zaidi ya milioni mbili hufariki duniani.

  Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii, Dk. Hadji Mponda, wiki hii, ugonjwa wa Kifua Kikuu umekuwa ukiongezeka siku hadi siku nchini kutoka takriban wagonjwa 11,000 waliogundulika mwaka 1980 hadi kufikia 63,453 mwaka 2010.

  Hata hivyo, waziri anasema utafiti uliofanywa na wizara yake kwa kushirikiana na shirika la Afya Duniani(WHO) mwaka 2003 na 2004 ulibaini kuwa ugonjwa wa ukimwi unachangia kwa asilimia 60 ya ongezeko la ugonjwa wa kifua kikuu nchini. Ongezeko hilo linaelezwa kusababishwa na misongamano ya watu hasa mijini, makazi duni na kuchelewa kupatikana huduma za tiba.

  Mwaka 2009 kwa mara ya kwanza Tanzania ilianza kutoa matibabu ya kifua Kikuu sugu (MDR-TB) katika hospitali ya Kibong’oto Wilayani Siha, Kilimanjaro na zaidi yaasilimia 70 ya wagonjwa walipona. Huduma hii imesaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi ambao walikuwa wanakufa pasipo msaada wa tiba ya uhakika.
  Kwanza tunapongeza juhudi za serikali katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali yanayosumbua wananchi ikiwa ni pamoja na kifua

  Kikuu na Ukimwi. Nguvu na msukumo mkubwa umewekwa katika kukakikisha kwamba maradhi hayo yanadhibitiwa kikamilifu.
  Na katika kupunguza gharama katika matibabu ya maradhi hayo mawili ambayo yanaoneana kunyemeleana, serikali imeweka utaratibu katika hospitali zote ziwe za serikali au binafsi kuhakikisha kuwa dawa za Kifua Kikuu na Ukimwi zinapatikana kwa wagonjwa bure.

  Kwa mantiki hiyo, wanatakiwa kuhakikisha kuwa wagonjwa wao wanapelekwa hospitali mapema ili waweze kupata tiba haraka wapone na kuendelea na ujenzi wa taifa. Siyo busara kuona watu wakificha wagonjwa au mtu kuona dalili za ugonjwa, kisha kuona aibu kujitokeza kupima ili apate tiba.

  Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa mkoani Mtwara ni “Nitatokomeza Kifua Kikuu kipindi chote cha uhai wangu”. Ni ujumbe ambao unamnyooshea kidole kila mmoja wetu kwamba anao wajibu wa kuhakikisha kuwa tunashiriki katika kuutokomeza ugonjwa huu.

  Wapo watu ambao wamekuwa na dalili za kifua kikuu lakini wanaogopa kwenda kupima wakidhani wana virusi vya ukimwi. Kumbe watu wa aina hii endapo wangekwenda kupima na kugundulika kifua kikuu, zipo dawa za kutibu kabisa maradhi hayo, tofauti na ukimwi ambao dawa zake ni za kurefusha maisha tu kwani tiba na chanjo bado.

  Jamii yetu yafaa ibadilike na kuzingatia elimu inayotolewa na serikali kupitia vituo vya huduma za afya na mahospitalini pamoja na asasi mbalimbali yakiwemo mashirika ya dini ili kutokomeza kabisa magonjwa haya.

  Kikubwa na cha kuzingatia ni wagonjwa kwenda hospitali kupatiwa tiba na pia wale wanaowahudumia wafuate maelekezo na tahadhari kuzuia maambukizi.
  Kama kanuni zote za afya zitatiliwa maanani, tunaamini kuwa idadi ya wagonjwa wa kifua kikuu nchini mwetu itapungua kwa kiwango kikubwa na pengine hatimaye kuutokomeza kabisa. Inawezekana, kila mmoja wetu ashiriki katika mapambano haya.  CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

   
Loading...