Sakata la gari la wagonjwa : DC wa Ngorongoro adai Ikulu waliboronga
Katibu wa Rais Prosper Mbenna, akimkabidhi funguo za gari la kubebea wagonjwa (ambulance), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Mkoani Arusha ChristianLaiser kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, kwa ajili ya kituo cha afya cha Engarenaibor wilayani humo, hafla iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam jana.Juzi rais Kikwete aligoma kukabidhi gari hilo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ngorongoro baada ya kubaini kuwa si mlengwa*WASOMI, WANASIASA WAMTAKA RAIS KIKWETE WAWAJIBISHE KWA UZEMBE
Boniface Meena na Freddy Azzah
MKUU wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali amesema kuwa, alimtuma mkurugenzi wake kwenda Ikulu jijini Dar es Salaam kupokea gari la kubebea wagonjwa kutokana na maelezo aliyopewa na ofisi hiyo ya Rais.
Lali alisema hayo jana baada ya juzi Rais Jakaya Kikwete kugeuka mbogo na kumtimua Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro, Kayange Jacob ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kubaini kuwa wasaidizi wake wamemdanganya.
Mbali na kumtimua mkurugenzi huyo, Rais Kikwete ambaye alitakiwa kukabidhi magari ya wagonjwa kwa halmashauri za wilaya za Mbozi na Longido, aliondoka katika hafla hiyo kwa hasira bila kugawa magari hayo.
Lali alitoa ufafanuzi huo kwa kueleza kuwa yeye alipigiwa simu na Ikulu na kutakiwa kumtaarifu mkurugenzi wake kufika Ikulu kwaajili ya kukabidhiwa gari.
"Mimi nilipigiwa simu na Ikulu ikinitaka kumtaarifu mkurugenzi wangu afike Ikulu kukabidhiwa gari, lakini sikujua ni gari la nini hivyo mimi nilimuagiza kama nilivyoagizwa," alisema Lali.
Alisema kuwa baada ya kutakiwa kufanya hivyo alimtaarifu mkurugenzi wake ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya makabidhiano hayo.
Wakati Lali akitoa ufafanuzi huo, wanasiasa na wasomi wamesema kitendo hicho cha kumdanganya Rais ni chakufedhesha na kuwa kilikusudiwa huku CUF kikimtaka Rais kuwawajibisha waliohusika.
Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu wa NCCR Mageuzi Samuel Ruhuza alisema, wasaidizi wa rais walijua kutoka mwanzo kuwa mtu aliyekuja kuchukua gari hilo ni Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro na siyo wa Longido na hivyo kitendo hicho cha kudanganya kilikusudiwa.
"
Huyu jamaa alishatuma madereva wawili kwa ajili ya training (mafunzo) na lazima walikuwa wa Ngorongoro na siyo Longido, kwa hiyo waliamua kumdanganya rais kwa makusudi. Halafu toka ametoka huko akaja mpaka Ikulu akajitambulisha na akaingia mpaka ndani lazima hawa wasaidizi walijua,"
alisema Ruhuza.
Hata hivyo, Ruhuza alisema uongozi kwa ujumla kutoka katika Wilaya aliyotoka ya Ngorongoro aliyotoka Mkurugenzi huyo kulikuwa na uzembe.
"
Kweli inawezekana kuwa Ngorongoro kuna shida ya ambulance (gari la kubeba wagonjwa) kuliko Longodo, lakini bado hiyo siyo sababu, na uongozi wa wilaya hiyo ndiyo iliyompa huyu jamaa access (kumwezesha) mpaka akafika Ikulu, kwa hiyo wote walidhamiria kudanganya Rais,"
alisema Ruhuza.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu alisema kitendo hicho ni ishara ya ukosefu wa nidhamu ya kazi na mmomonyoko wa maadili kwa viongozi.
"
Mimi nadhani ni tukio linaloonyesha dalili kubwa ya vurugu zilizopo serikalini, siyo mara moja yametokea matukio kama haya, kwa hiyo hali hii inaonyesha mmomonyoko wa maadili kwa viongozi na utovu wa nidhamu ya kazi kwasababu maadili ni pamoja na kuhakikisha shughuli zinaenda kama zilivyopangwa,"
alisema Profesa Baregu.
Msomi huyu alisema lawama zisielekezwe kwa wasaidizi wa rais pekee bali hata kwa Wizara ya Utumishi pamoja na Rais mwenyewe kwa kuteua watu wasiokuwa makini na kazi zao.
"
Siyo wasaidizi wake pekee waliomwangusha Rais, kuna utumishi hawa ambao walinisimamisha mimi kazi wakisema kuwa sisitahili kufundisha chuo kikuu, hawa wote wanausika,"
alisisitiza Profesa Baregu.
Naye mwanasheria mkogwe nchini, Bob Makani alisema kuwa kitendo hicho ni kidogo sana na kuwa kimetokana na mkanganyiko mdogo tu.
"
Kama nimesoma vizuri habari hii, suala hili ni dogo sana, rais alikuwa ameahidi mahali pengine na akaja mtu mwingine, kwa hiyo mimi naona ni kitu kidogo sana,"
alisema Bob Makani.
Katika hatua nyingine, CUF kimeelezwa kusikitishwa na tukio hilo huku kikimtaka Rais Kikwete kuchukua hatua kuwawajibisha maofisa waliohusika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa CUF, Ashura Mustapha chama hicho kinaelezea kitendo hicho kuwa ni cha makusudi.
"
Kitendo hiki si cha bahati mbaya kwa kuwa viongozi wengi wa serikali ya CCM wapo madarakani kwa maslahi yao binafsi na kujineemesha kwa kutumia rasilimali za umma ndio maana wasaidizi wa Rais walifanya udanganyifu huo kutaka kupinda ahadi ya Rais Kikwete,"
ilisema sehenu ya taarifa ya CUF. Chama hicho kilimtaka Rais Kikwete kuchukua hatua za haraka za kuwawajibisha wote waliohusika na kashfa hii ya kuidanganya Ikulu.
My Take:
Creating mountains out of mole hills?!
Issue hii sasa imekuwa 'dili' ya kisiasa. Baregu naye kapata mwanya wa kupenyeza dukuduku lake kuhusu uozo wa Idara ya Utumishi!
Kama taarifa hii ni sahihi moja kwa moja Afisa wa Ikulu aliyepiga simu Loliondo ndiye mwenye makosa. Bila shaka ulikuwa ni mkanganyiko wa majina ya Longodi na Loliondo ambayo kidogo yanafanana na yanaweza kumchanganya mtu ambaye hayuko makini. Na kwa afisa wa Ikulu kosa hilo halina mjadala ni uzembe mkubwa.
Bado swali lipo, kwa nini Rais aliteremka kwenda kwenye tukio la kugawa magari hali akijua kuna makosa yaliyotendeka?
Kingine ninachokiona hapa ni dalili za 'fitna' miongoni mwa watendaji wa Ikulu. Huyo aliyekwenda kumwambia ama kumnong'oneza Rais dakika za mwisho kwamba aliyekuja kuchukua gari hatoki Longido bali Loliondo bila kwanza kupeleleza imekuwaje, kujua ukweli na kuweka mambo sawa, naye hafai kuwa karibu na Rais wa nchi!