Kifo cha TANU na ASP na kuzaliwa CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kifo cha TANU na ASP na kuzaliwa CCM

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by KIM KARDASH, Feb 23, 2012.

 1. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #1
  Feb 23, 2012
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Na Joseph Mihangwa,Raia Mwema,Toleo 226.

  WAKATI alipokubali kuunganisha chama chake cha Afro-Shirazi (ASP) na chama cha Tanganyika African Union, Oktoba 1976, Rais wa Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, hakujua kwamba kwa kufanya hivyo, alikuwa anajitia kitanzi cha kupoteza urais wa Zanzibar miaka minane baadaye.


  Tangu mwanzo, chale zilimcheza Jumbe, pale Mwalimu Julius Nyerere, Septemba 5, 1975, alipopendekeza kwenye kikao cha pamoja cha Halmashauri Kuu [NEC] za TANU na ASP, kwamba vyama hivyo viungane. Lakini Jumbe, kwa kusita, na kwa hofu na shaka iliyofichika, alitaka chama chake kipewe muda zaidi kuweza kufikiria pendekezo hilo.


  Hatimaye, makubaliano ya Oktoba 1976 yalizaa chama kipya kilichoitwa Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichozinduliwa Februari 5, 1977. Ni CCM kilichompiga buti Jumbe, Januari 1984, kwa tuhuma za kuthubutu kuhoji muundo wa Muungano, akapoteza nafasi zote za uongozi – urais wa Zanzibar, umakamu mwenyekiti wa CCM Taifa, na umakamu wa rais wa Muungano. Ilikuwaje?


  Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi aliongoza Zanzibar kuanzia Aprili 1972 baada ya kifo kwa kupigwa risasi cha Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume. Alirithi nafasi hiyo kwa msaada mkubwa wa Mwalimu Nyerere dhidi ya matakwa ya baadhi ya Wazanzibari ambao walitaka mtu mwenye kuenzi na kuendeleza fikra na utawala wa kibabe wa Karume, arithi nafasi hiyo. Walimtaka Kanali Seif Bakari.


  Mwalimu hakukubaliana na maoni ya Wazanzibari ya kumteua Kanali Seif Bakari, mwanajeshi, kuwa Rais wa Serikali ya awamu ya pili, Zanzibar. Alijenga hoja kwamba, kwa kuwa Karume aliuawa na mwanajeshi, Luteni Hamud Hamud, kumteua mwanajeshi mwingine (Bakari) kuwa Rais, kungeleta picha na hisia kwamba, kuuawa kwa Karume yalikuwa ni mapinduzi ya kijeshi.


  Nyerere akampendekeza aliyekuwa Waziri katika Ofisi ya Rais (mambo ya Muungano), Aboud Jumbe, kuchukua nafasi hiyo. Hoja yake ikapita.


  Jumbe na Nyerere walifanana kwa mengi: wote walikuwa wasomi waliosoma pamoja Chuo Kikuu Makerere; kisha wote wakawa waalimu. Jumbe alilegeza mengi yenye ukakasi yaliyokithiri wakati wa utawala wa Karume. Hata ile misuguano iliyotia fora kabla ya hapo, kati ya Karume na Nyerere juu ya Muungano na kutishia kuvunjika kwa Serikali ya Muungano, ilitoweka.


  Hatimaye Jumbe alianza kukubalika Visiwani na Bara; akawa kipenzi cha Rais wa Muungano, Mwalimu Nyerere. Mara nyingi alialikwa Bara na baadaye akapaona kama nyumbani kwake.


  Lakini kadri alivyozidisha ziara za kirais Bara na nje ya nchi kumwakilisha Nyerere, ndivyo alivyozidi kujitenga na siasa pamoja na mambo mengi ya Visiwani. Hatimaye alipaona Dar es Salaam kuwa kwake zaidi kuliko Zanzibar. Aliweza kuruka kwa ndege kwenda Zanzibar mchana kwa ziara fupi, na kurejea Dar jioni.


  Kutokuwepo kwake Zanzibar kwa muda mrefu kulizua pengo na ombwe la kiuongozi kwa kuwa hakuna miongoni mwa wasaidizi wake aliyethubutu kumfuata Dar Es Salaam kwa mashauriano. Kwa sababu hii kila kitu kilisubiri arudi Zanzibar kwa "ziara" fupi, hata kama ni idhini ya kukata mti.


  Nyerere alifurahishwa na utendaji wa Jumbe na kuingiwa hamu ya kutaka Muungano zaidi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuviunganisha TANU na ASP, kama tulivyoona mwanzo.


  Ili kumfurahisha Mwalimu Nyerere juu ya Muungano, mara nyingi hotuba zake zilianza hivi: "Tunataka umoja; ni kwa njia hii pekee kwamba tunaweza kubadili mambo mengi, ili kwamba palipo na kukata tamaa pawe na matumaini, penye chuki pawe na upendo na amani……".


  Muungano ulivyozidi kuimarika, ulifika wakati Jumbe akajiona kama mrithi halali mtarajiwa wa Rais Nyerere, na hivyo kujimwaga zaidi roho na mwili kwa mambo ya Muungano, badala ya kushughulikia utawala wa Visiwani. Ni matarajio hayo ya kurithi nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, yaliyomfanya akubali kirahisi kuungana kwa ASP na TANU. Ingekuwa enzi za Karume, na kwa jinsi tofauti kati yake na Nyerere zilivyokuwa dhahiri na kubwa, huenda TANU na ASP visingeungana.


  Kuanzia Februari 1972 hadi Aprili 1983, Chama kipya – CCM kilifurahia ndoa mpya kwa utulivu; lakini pale Nyerere alipopendekeza marekebisho zaidi ya "kuimarisha Muungano", mlipuko mpya wa malalamiko ulitokea Zanzibar, moja ya hayo ni hofu ya nchi hiyo kumezwa na "Tanganyika".


  Hofu ya Wazanzibari iliongezeka pale Watanzania Bara walivyozidi kupendekeza kuwa na Serikali moja ya Muungano, badala ya muundo wa Serikali mbili ndani ya Muungano. Hofu hizi za Wazanzibari zilianza kumweka pabaya Jumbe juu ya uswahiba wake na Nyerere; alianza kuitwa "msaliti" wa Wazanzibari na Zanzibar, naye akaanza kugeuka nyuma, lakini kwa kukanganyikiwa; alikuwa njia panda.


  Ili kurejesha imani ya Wazanzibari kwake, lakini kwa chukizo kwa Nyerere, Jumbe aliomba mawazo ya kiserikali kutoka kwa makatibu wakuu wote wa wizara na watendaji wakuu wengine wa Serikali ya Zanzibar.

  Wote walikataa muundo wa Muungano wenye Serikali moja, wakapendekeza kuwe na Serikali tatu – Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano tu. Lakini kubwa lililomchanganya akili Jumbe lilikuwa njiani, likimnyemelea.

  Mwaka 1983, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Muungano, Edward Moringe Sokoine, aliteuliwa kuwa waziri mkuu. Sokoine alikuwa kiongozi makini, shupavu, mnyoofu na mwenye mvuto mkubwa kwa watu. Na katika kipindi kifupi tu, alijidhihirisha kuwa "chaguo la watu" na mrithi halali wa Nyerere ambaye naye alimkubali kwa ishara na kwa vitendo. Akawa anaonyesha upendeleo dhahiri kwa Sokoine. Kuna sababu nyingi kwa hilo; lakini itoshe kutaja tatu tu kati ya hizo.


  Moja ni kwamba, Nyerere alianza kumwona Jumbe kama kiongozi mpweke, asiyeungwa mkono na watu wa chini (umma) Visiwani. Alimwona pia kama dikteta mkimya, asiyeweza kushauriwa akashaurika na watu wa chini yake.

  Nyerere aligundua pia kile pekee kilichomsukuma "ang'are" kwake na kwa Wabara: kiu ya kurithi nafasi ya Rais baada ya Nyerere.

  Baya zaidi lililomuudhi Mwalimu ni kwa Jumbe kugeuka mhafidhina wa kidini na mpambanaji wa Kiislamu katika Taifa lisilo na dini. Jumbe alizuru nchi nzima akitoa mihadhara kwenye misikiti hata Serikali ikalazimika kutoa waraka mkali wa Rais (presidential circular), kuwakumbusha viongozi wa kitaifa kutojitambulisha na mambo ya kidini. Hata hivyo, Jumbe alipuuza waraka huo, akaendelea kivyake.


  Habari zikamfikia Jumbe juu ya kuanza kupoteza upendeleo wa Nyerere na kuchuja; zikauma, zikamvunja moyo; uhasama kati ya Jumbe na Nyerere ukazuka. Katika hali hiyo Muungano ukaanza kutikiswa.


  Hatua ya kwanza iliyoanza kutikisa Muungano ilikuwa ni kumrejesha Tanzania Bara, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Damian Lubuva; badala yake akamteua raia wa Ghana, Alhaj Bashir K. Swanzy na kumpa uraia.


  Kuanzia hapo, madai ya Wazanzibari kutaka mabadiliko ya Katiba, kupitia mihadhara, magazeti na redio, yalipamba moto. Wengi watakumbuka matangazo ya redio ya mafichoni, maarufu kama "Kiroboto tapes", ya kudai Wazanzibari warejeshewe visiwa vyao, yalivyopamba moto hadi ilipogunduliwa msituni na wanajeshi kutoka Bara na kuzimwa.


  Kwa kupitia Jaji Bashir Swanzy, iliandaliwa hati ya mashtaka kuhoji muundo na uhalali wa Muungano kwenye Mahakama Maalumu ya Kikatiba ya Jamhuri ya Muungano, ambayo kazi yake pekee, kwa mujibu wa ibara ya 126 ya Katiba ya Muungano ya 1977, "ni kusikiliza shauri lililoletwa mbele yake na kutoa usuluhishi juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba, iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar".


  Hati hiyo ya mashitaka ilipotea mezani kwa Jumbe katika mazingira ya kutatanisha, na hatimaye kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere. Taarifa za uhakika zinaonyesha kuwa waliofanikisha kazi hiyo ni pamoja na wakubwa wa sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wakati ule wakiwa SMZ.


  Haraka haraka na hima, kikaitishwa kikao cha NEC ya CCM mjini Dodoma, Januari 1984 na Jumbe akawekwa kiti moto kwa dhambi ya kujaribu kutua mahali malaika wanapopaogopa kutua, kwa maana ya kuhoji Muungano; kisha ikatangazwa "kuchafuka kwa hali ya siasa Zanzibar".


  Bila kumeza maneno, Jumbe alikiri kuandaa hati hiyo kama moja ya haki zake za kikatiba.

  Mbali na hati ya mashitaka, Jumbe aliandaa pia barua ndefu kumkumbusha Nyerere jinsi Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano zilivyokuwa zikikiukwa. Alihoji pamoja na mambo mengine, mantiki ya kuunganishwa kwa TANU na ASP kuunda CCM na mamlaka chama hicho kiliyojipa, ya kutunga Katiba ya kudumu ya 1977.

  Kwa msaada wa Mwanasheria Mkuu Swanzy, Jumbe alifanya rejea Sheria ya kuahirisha na kusogeza mbele muda wa kuitisha Bunge la Katiba, Namba 18 ya 1965, Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya 1965, na ubatili wa Katiba ya kudumu ya 1977 kwa namna ilivyobuniwa na kutungwa.


  Kwa kuwa barua hiyo ndefu ilikuwa imeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, alimtaka Waziri Kiongozi, Ramadhan Haji, ahakikishe imetafsiriwa kwa Kiswahili iweze kujadiliwa na Baraza la Mapinduzi.


  Kama ilivyotokea kwa hati ya mashitaka, barua hiyo nayo ilitoweka mezani kwa Jumbe katika mazingira ya kutatanisha na kumfikia Nyerere. Kwa kuwa alikuwa hajaitia sahihi ilibidi kikao cha NEC kimtake Jumbe aseme kama hayo ndiyo yalikuwa mawazo yake; naye kwa mara nyingine, na bila ya kutafuna maneno, alikiri, na hivyo mvua ya mawe ikazidi kumnyea.


  Awali, Januari 12, 1984, Jumbe alihutubia wananchi kwenye kilele cha sherehe za Mapinduzi, siku chache tu kabla ya kuitwa Dodoma. Katika hotuba hiyo, hakuficha kukerwa kwa Serikali yake namna Muungano ulivyotekelezwa kinyume na matakwa asilia. Aliwataka wananchi wawe wavumilivu na wenye subira wakati tatizo hili likiendelea kushughulikiwa.

  Bila kumeza maneno, na Mwalimu Nyerere akisikia; Jumbe alisema, kama pasingepatikana mwafaka na maridhiano kati ya Zanzibar na Serikali ya Muungano juu ya jambo hilo, angelipeleka kwenye Mahakama Maalumu ya Katiba kupata ufumbuzi kwa yote haya.

  Katika kikao cha NEC cha Dodoma, Jumbe alielezewa kama "kiongozi dhaifu na msaliti wa Muungano". Alipinduliwa sawia na kupoteza nafasi zote, kisha akasindikizwa nyumbani kwake na kuwekwa chini ya ulinzi wakati harakati za kusafisha hewa ya kisiasa zikiendelea.


  Tetemeko likawakumba wasaidizi wake wakuu, wakiwamo Waziri Kiongozi, Ramadhan Haji, Waziri wa Nchi, Aboud Talib, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Wolfango Dourado wakati Swanzy alirejeshwa kwao Ghana.


  Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ulinzi wa Muungano na Mjumbe wa NEC, Kanali Seif Bakari, alipigana kiume kikaoni kujaribu kumwokoa Jumbe, lakini aliishia kuwekwa chini ya ulinzi wa nyumba yake na hatimaye kizuizini Tanzania Bara.

  Nafasi ya Jumbe ilichukuliwa na Alhaj Ali Hassan Mwinyi, na Seif Sharrif Hamad akaukwaa Uwaziri Kiongozi.

  Je, hayo yalikuwa Mapinduzi dhidi ya Jumbe, kutekwa nyara au zilikuwa hatua za kinidhamu za chama?.

  Jumbe alikuwa Rais wa "nchi" ya Zanzibar kwa mujibu na kwa misingi ya Katiba ya Zanzibar ya 1979. Na kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano [Articles of Union] wa 1964, ambao ndio unaosimamia na kutawala Katiba zote mbili – Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar, suala la Vyama vya Siasa halikuwa, halijawa na halipashwi kuwa jambo la Muungano.

  Kwa mantiki hii, kitendo cha chama cha siasa kumwondoa madarakani Rais wa "nchi" yenye Katiba yake, yenye Serikali yake na Bunge lisilotawaliwa na Katiba ya Muungano, ni dhahiri kilikuwa kimevuka mipaka ya uwezo wake. Kwa sababu hii, hayo yalikuwa Mapinduzi ya kutumia nguvu ya kisiasa).


  Baada ya kazi ya kumpindua Jumbe kukamilika, na ili kuhakikisha "vituko" vya kuhoji Muungano vimedhibitiwa Visiwani, suala la Usalama wa Taifa, ambalo kabla ya hapo halikuwa jambo la Muungano (ilikuwa ni Ulinzi tu), liliingizwa kwenye Muungano kusomeka "Ulinzi na Usalama".
   
 2. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #2
  Feb 23, 2012
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Huu mkasa mzito sana,kiufupi hiyo hati ya mashitaka "haikupotea",kitapoteaje kitu muhimu kama hicho tena ofisini kwa rais mezani kwake???hiyo hati ilinyofolewa na msaliti wa kweli wa wazanzibari maalim seif shariff hamad ambae alikua akitumiwa kama mtu wa usalama wa taifa wa mwalimu nyerere aliyepandikizwa ofisi ya rais wa zanzibar kuchunguza na kuripoti mwenendo mzima wa rais wa zanzibar,na maalim seif baada ya "kukwiba" hati hiyo alimpelekea boss wake ambae ni Julius Nyerere.

  Lakini ikumbukwe pia Jumbe ndio alimtoa seif kusikojulikana na kumfanya ajulikane kabla ya kukata kona na kuutumikia usalama wa taifa.Nyerere alikua anawapatia sana wazanzibari.
   
 3. Kimbunga

  Kimbunga Platinum Member

  #3
  Feb 23, 2012
  Joined: Oct 4, 2007
  Messages: 13,011
  Likes Received: 1,816
  Trophy Points: 280
  Mkuu Kim acknowledge basi source yako! Nadhani ni Nasaha za Mihangwa hizi.
   
Loading...