Kifo cha Sajenti Kinyogoli: Mke wa marehemu, wengine 14 watiwa nguvuni

real G

JF-Expert Member
Feb 7, 2013
5,227
5,292
ASKARI.jpg


Watu 15 akiwamo mke wa marehemu, Sajenti Ally Salum Kinyogoli wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na tukio la kuuawa kwa askari huyo wa kikosi cha usalama barabarani usiku wa kuamkia jana.

Kinyogoli aliyezikwa jana saa 10 jioni kwenye Makaburi ya Mzambarauni, Kitunda, Dar es Salaam alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kutoa taarifa kuhusu hali ya usalama barabarani katika vyombo vya habari.

Kinyogoli aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake, Chatembo Kata ya Mwandege, Mkuranga mkoani hapa mbele ya mtoto wake, mwenye umri wa miaka kumi na moja.

Akizungumzia kukamatwa kwa mjane huyo, Kamanda wa Kipolisi Temeke, Gilles Muloto alisema: “Sidhani kama mnaweza kuzungumza naye kwa sababu hao waliomshikilia ni polisi na wanakwenda naye kituoni. Hata hivyo, mimi siyo msemaji wa hili anayeweza kulizungumzia ni Kamanda wa Mkoa wa Pwani.”

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi ambaye hakuwapo msibani alipopigiwa simu ilipokewa na mpambe wake ambaye alisema: “Mkuu leo amebanwa na vikao vingi kuna Mwenge mkoani kwake na hili tukio la kusikitisha.”

Mgogoro wa kifamilia

Mama mlezi wa marehemu, Coletha Ndima alisema mara ya mwisho kuonana na Kinyogoli ni juzi wakati marehemu alipopeleka baadhi ya samani zake kwa kile alichodai mke wake mkubwa alikuwa akiziuza.

“Hatujui kama kuna mgogoro lakini Kinyogoli aliwahi kutuambia kuwa anataka kuoa mke wa pili, sijui alishaoa, kwa sababu alisema atakuja kumtambulisha mchumba lakini hakufanya hivyo,” alisema.

Ndima alisema marehemu aliwahi kumwambia kuwa ana mgogoro na mkewe mkubwa lakini hajui ni wa nini.

Mmoja wa polisi ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema polisi wanamshikilia mama huyo kwa kuwa yeye ndiye aliyemuita Kinyogoli aende nyumbani kwake na mauti kumfika.

“Marehemu alitengana na mke wake mkubwa, lakini siku moja kabla ya kifo, mama huyo alimuita akimwambia watoto wamemkumbuka, usiku huohuo, ndipo walipomuua,” alisema.

Mtoto asimulia mauaji yalivyotokea

Mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Ebenezer iliyopo Mwandege alieleza kuwa watu wawili walifika nyumbani hapo na kumtaka amuite baba yake.

“Nilipoingia ndani kumuita baba, nilimkuta anatandika kitanda, baba akaniambia waambie nakuja, wakati natoka, baba naye alikuwa nyuma yangu, lakini niliwakuta wale watu safari hii wamevaa ninja (mask) lakini kabla ya hapo walikuwa hawajavaa,” alisema.

Alisema watu wale walianza kumkaripia baba yake wakimtaka awape funguo ya gari lakini alikuwa akibishana nao na kisha kuanza kupambana nao lakini walimpiga bastola ya kichwani na mbavuni.

“Wakati baba anapambana nao alikuwa anawauliza nimefanya nini, lakini hawakumjibu, alianza kupiga kelele, wanangu nakufa, wanangu nakufa,” alisimulia kuongeza:

“Ujue baba alishawaweza wale, lakini walivyoona anawashinda nguvu waliamua kumpiga bastola.”

Baba wa marehemu, Salum Kinyogoli aliwataka polisi kufuatilia suala hilo ili wahalifu hao wapatikane.

Dada wa marehemu, Zainab Kinyogoli aliyeonekana kuchanganyikiwa kutokana na msiba huo alikuwa akilia mfululizo huku akisema: “Ally aje nimbebe, nimemuachia ziwa, nimembeba.”

Maelezo ya polisi

Awali, Kamanda Mushongi aliwaambia waandishi wa habari mjini Kibaha kwamba wauaji hao walifika nyumbani kwa askari huyo wakitumia pikipiki aina ya Boxer na waliingia ndani kwa kuruka uzio.

Hata hivyo, wauaji hao walipofika kwenye gari hilo hawakufanya lolote bali walitelekeza ufunguo huo na kutokomea.

“Naweza kusema ni tukio la kushtukiza kwa kweli kwa sababu ilikua ni muda mfupi tu toka askari aliporudi nyumbani kwake akitokea kazini na hawa wauaji hawakuchukua kitu maana hata ufunguo wa gari waliouchukua pale nyumbani walitoka nao nje na kuuacha,” alisema Mushongi.


Chanzo: Mwananchi
 
Unawezaje kujihusisha na mauaji ya mzazi mwenzako? Sasa watoto wanabaki wakitaabika. Hasira hasara.
Mkuu hii kitu ipo sana...kama unakumbuka Arusha pia kuna mwanamke alikamatwa kupanga mauaji ya mmewe ambae ni mfanyabiashara mkubwa ila bahati nzuri habari za wauaji zikavuja..na yule mama akakiri kabisa...na mmewe akasema kamsamehe.. Mungu atunusuru
 
hapo ukiunganisha doti utaona kuwa mke ndio anahusika, japokuwa anaweza akapatikana hana hatia kutokana na techinicality, ila ndio yeye
kinachohuzunisha zaidi watoto wamekuwa exposed kwenye mambo ya ukatili wa mapenzi wakiwa na umri mdogo mno, kitu kitakchokuja kuwaathiri sana
 
Hili lina funzo flani kidogo, Mwanaume ukiona huelewani na Mke wako, na njia zote za kidiplomasia zimeshindikana, kabla ya kutangaza kuoa tena lazima ufanye risk assessment ya hali ya juu sana, sababu usipoletewa majambazi unaweza kurogwa ukawa chizi, kwa vile mkeo utakuwa umeish nae mda mrefu unaweza kuwa umeshamfahamu, kama ni mtu wa waganga au vip.
Kama ishu ni mali nadhan ni kuandika urithi ambao ni conditional will kwa watoto, yan labda mali haitauzwa mpaka kitu flani kifanyike.
 
Back
Top Bottom